Featured Post

WABEMBE – 2: HUMTULIZA CHIFU MFU KWA KUMFUKUA

Kinyago kilichochongwa na Wabembe

Na Innocent Nganyagwa
LEO nawakaribisha kwenye safu yetu maridhawa ya kijadi, tujumuike pamoja na kutopea kwenye ujadi wetu ambapo tunawatembelea ndugu zetu Wabembe kwa mara ya pili.
Basi kabla hatujaendelea kufahamu mambo yao, niwakumbushe tena kuwa, tukitoka kwa Wabembe tutawatembelea Waha, halafu tutatua kwa Wakimbu.
Tukitoka kwa Wakimbu, tunatarajia kuyatembelea kwa zamu makabila ya Wanyisanzu, Wanyiramba, Warangi na Wasi.

Nikukumbushe kwa ufupi tu kwamba, jana tulionakuwa, ndugu zetu hawa wanaoongea lugha yao ya Kibembe, ambao wakati mwingine jina lao hutamkwa ‘Wabeembe’ wanapatikana mkoani Kigoma.
Huko kwenye wilaya ya Kigoma Vijijini, wanatangamana na makabila mengine ya Wamanyema, Wabangubangu, Wagenye, Wagoma, Wakusu, Warege, Wahoholo na Wambwari.
Lakini hawa Wabembe na hayo makabila jirani zao, wanatokea Kongo, nchi tunayopakana nayo upande uliopo mkoa wa Kigoma. Tuliona kuwa, kule Kongo wanapatikana kwenye nchi zote mbili zenye jina hilo, yaani Jamhuri ya Kongo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Huko waliishi kwenye uwanda wa kaskazini mwa Mto Zaire, ndugu yangu, nadhani unafahamu kuwa Kongo ya DRC, wakati wa utawala wa Mobutu ilikuwa inaitwa Zaire. Basi jina hilo lilitokana na mto huo, ambao hao Wabeembe waliishi kwenye uwanda ulio pembezoni yake kwa upande wa kaskazini.
Jina la Kongo lilirudishwa tena na Hayati Laurent Kabila, aliyekuwa rais wa nchi hiyo baada ya kumpindua Mobutu. Kabila aliuawa, kisha nafasi yake ilichukuliwa na rais wa sasa wa nchi hiyo, mwanaye, Joseph Kabila.
Mauaji hayo ni katika vurumai za kunyang’anyana madaraka, ambazo kwa kawaida haziishi kwenye nchi hiyo. Nadhani hata sasa unafahamu mapigano yanayoendelea huko, baina ya makundi makubwa na madogo ya wapiganaji, yakiwemo majeshi ya serikali ya Jenerali muasi, Laurent Nkunda, Mai Mai na makundi mengine.
Tatizo kubwa la Kongo hii tunayoizungumzia, ni ukubwa wenyewe wa nchi na muingiliano wa makabila, yanayotaka kudhibiti madaraka. Tena kwa bahati mbaya, makabila hayo yako kuanzia ile Kongo ya Brazaville, kupitia hii ya Kinshasa, hadi Rwanda na Burundi.
Makala iliyopita, tuliona baadhi ya makabila hayo yaliyojazana huko Kongo, ambapo nilijaribu kuwatajia machache. Maana huko inasemekana kuna idadi ya makabila yapatayo 420 hivi, jaribu kulinganisha na makabila yetu.
Licha ya takwimu za kutatanisha, kuwa tuna makabila 120, lakini ni machache mno kulinganisha na yaliyoko huko walikotokea Wabembe.
Utamaduni wa Wabembe una mfumo ulioelemea maeneo yao ya asili, wakiwa na jamii zenye kutunza vyema kumbukumbu za chimbuko lao la asili.
Kwa mfumo huo, watu wa familia moja wanaweza kutawanyikia maeneo ya mbali, lakini huweza kutambuana hata kwa vizazi vitatu kabla au baada. Pia tuliona kuwa wanaongozwa na machifu wao, ambapo ‘ngaluba’ yaani chifu husika, huwasiliana na mizimu.
Wao wanaamini katika mizimu, hata katika baadhi ya shughuli zao kama vile uwindaji, hufanya kwanza ibada zao za kijadi kabla ya kwenda kuwinda.
Wabembe ni mahodari kwa utamaduni wa uchongaji, hutumia vinyago vilivyochongwa kwa mambo mahususi ya kiimani.
Mathalan, huomba mbele ya vinyago hivyo vinavyowakilisha taswira ya mizimu yao. Licha ya kuamini mizimu, lakini pia wanamuamini Mungu muumba ‘Nzambi’ ambaye wanamuabudu.
Kutokana na imani yao kwake, hawana taswira ya kitu chochote kinachomuwakilisha. Huyo Nzambi, ndiye anayedhibiti maisha na kifo, kwa mujibu wa imani yao. Japo kuna wachawi ‘ndoki’ ambao wanaweza kusababisha kifo kutokana na ulozi kwa kutumia ujuzi wa kishirikina. Kutokana na kuamini mizimu ya mababu zao, kuwa inahusiana kwa karibu na watu walio hai, basi huitolea sadaka.
Hilo hufanyika kwa ibada inayoongozwa na kuhani, ambaye huomba mbele ya vinyago vinavyoitwa ‘kitebi’ au ‘bimbi’. Vinyago hivyo vilivyochongwa na waganga, huvishwa mavazi kama ya wawindaji au waganga.
Kusujudu mbele ya vinyago vya kimizimu, kulianzia kwa waganga hapo zamani, ambao awali walitumia vinyago vyao vya kupigia ramli ‘nkisi’.
Hayo ndiyo tuliyoyaona kwa ufupi jumamosi iliyopita, tulipoanza kuwatembelea hawa ndugu zetu Wabeembe.
Tukiendelea kutoka hapo, ni kwamba, kwa Wabembe, uchongaji vinyago unahusika sana na imani, si kuchonga alimradi kuchonga tu.
Kama ambavyo tumeona, wao huvitumia vinyago hivyo kuwasiliana na mizimu.
Maumbile ya vinyago hivyo hutofautisha mzimu mmoja na mwingine, kwa jinsi vinavyochongwa, hasa kwa eneo la kifuani hadi tumboni. Eneo hilo la mwili wa kinyago wa kimizimu, huwa na aina ya mapambo ambayo hutofautisha aina na hadhi ya mzimu mmoja na mwingine.
Pia, vinyago hivyo huwa na maumbo, ukubwa na jinsia tofauti, kutegemeana na mzimu husika. Mzimu unaoishi ndani ya kinyago huwaangalia wale wanaomhusu, pia huwaadhibu wale wanaoenda kinyume na taratibu zao za kimila.
Vinyago hivyo vya kimizimu huvishwa nguo na mikufu ya ngozi shingoni, vinyago vya kiume huwa na ndevu. Mara nyingi huwa vimeshikilia silaha kwa mikono miwili, au kisu mkono mmoja na kibuyu mkono wa pili.
Mitindo ya nywele ya vinyago hivyo hutegemea maumbo, lakini mara nyingi huwa wima huku magoti yamekunjwa kiasi na miguu imesimama kwenye kitako maalum.
Vinyago vya jinsia ya kike huwa tofauti kimaumbile, vikiwa na videvu vikubwa, midomo na pua kubwa zaidi, huku masikio na nywele zake zikichongwa kwa unadhifu zaidi.
Licha ya vinyago hivi vya kimizimu, lakini pia, Wabembe wana kinyago kikubwa zaidi kilichotengenezwa kwa ngozi na vitambaa.
Kinyago hiki kinachoitwa ‘Muziri’ huwa hakiwekwi ndani ya nyumba au kaya kama vile vinyago vya kimizimu, bali huwekwa kwenye eneo la kuingilia kwenye kijiji husika.
Muziri alitengenezwa kwa sababu mahsusi, mathalan, endapo ‘ngabula’ alisababisha matatizo ili kuonesha dhamira yake, ya kutaka kufukuliwa kutoka kwenye kaburi alilozikwa.
Basi akishafukuliwa, mifupa yake huwekwa ndani ya Muziri ili kutuliza matatizo anayoyasababisha.
Pia Muziri alitumika kwenye matambiko mengine mbalimbali, akiwekwa sehemu mahususi kwa madhumuni husika.
Mjadi mwenzangu, najua huenda unashangazwa na mambo haya, lakini tutakutana nayo sana siku za usoni, hasa tutakapoanza kutoka hapa nchini na kuyatembelea makabila ya nchi nyingine za Kiafrika. Basi nikiendelea kukuelezea kuhusu yule Muziri, ni kwamba, hutengenezewa kibanda na kuwekwa humo. Akishakaa kwenye kibanda chake, hutolewa sadaka za vyakula na pombe, mara nyingi huwa pombe ya mnazi.
Hawa ndugu zetu Wabeembe, huchonga pia vitu vingine kwa matumizi ya kawaida, kama vile vifaa mbalimbali vya ngoma na muziki wao vikiwemo zeze, filimbi, hata mapambo kama hereni.
Lakini, tofauti ya vitu vya kawaida na vile vinyago, si matumizi yake tu, bali pia vitu vya ziada vinavyotumika kukamilishia maumbo yake. Vile vinyago vya kimizimu huwekwa ‘bilango’ yaani dawa za mitishamba, au wakati mwingine nywele, kucha na mifupa ya wafu wanaoaminika kugeuka mizimu.
Mafundi wa kutengeneza vinyago hivyo ni wale waganga, ambao hutegemewa katika kutambua walozi hasa inapotokea mtu akifa ghafla bila kuugua au kuuawa, au kudhurika. Wajadi wenzangu, msije kudhania kuwa hawa Wabembe wana mambo hayo tu, kwa kuwa nimeelezea kwa kina simulizi zao za vinyago vyao vya kimizimu. Licha ya uwindaji, lakini pia wanalima, jukumu ambalo kwa utaratibu wao wameachiwa zaidi akina mama.
Wao hulima mpunga, mahindi, karanga, maharagwe na migomba, wanaume ndiyo wenye jukumu la kuleta mboga za kuliwa na vyakula hivyo, kwa kuwinda wanyama.
Miaka ya hivi karibuni walianza kuwa wajasiriamali, wakikodisha maeneo yao ya kilimo, pia wakijiingiza kwenye uchimbaji dhahabu na chuma. Watu muhimu kwenye jamii yao huunda ‘bwami’ yaani aina ya baraza au jumuiya ya wanaume watu wazima, inayohusika na maamuzi muhimu ya kijamii.
Mambo ya imani kwao ni ya kimafungu, kutokana na mizimu ya koo husika kama tulivyoona mfumo wao wa kutambuana, hata vizazi vitatu kabla na baada. Lakini pia, kutokana na kutangamana na makabila mengine, wameiga baadhi ya mambo ya kiimani ya makabila hayo.
Wanaamini pia katika mizimu mikuu inayohusika na masuala tofauti tofauti, kuna mzimu wa mambo ya asili ‘bahomba’ pia kuna mzimu wa ardhi ‘m’ma’ na mzimu wa ziwani Tanganyika ‘mkangualukulu’ na mizimu mingineyo.
Naam, basi kwa haya machache niliyoweza kukuletea kuhusu Wabembe, tuhitimishie hapa ziara yetu kwao.
Tukutane tena kesho kwa mambo zaidi ya kijadi.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Desemba 06, 2008.

Comments