- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
KWA
miaka mingi ndizi ndilo zao kuu la chakula mkoani Kagera, na sasa limekuwa zao
la biashara kwa baadhi ya wilaya kama Karagwe na Muleba.
Ndizi
zinasafirishwa kwa wingi kwenda mikoa mingine ndani na nje ya Kanda ya Ziwa na
zinaonekana kupendwa na walaji wengi, hasa ‘Ndizi Bukoba’. Ndizi zinatokana na
migomba.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba,
japokuwa kuna mazao mengine yanayolimwa Kagera kama kahawa, mahindi, maharage,
mikunde, viazi vitamu, viazi mviringo, viazi vikuu, njugu mawe, karanga,
nyanya, machungwa, mapera na mananasi, lakini migomba
ndilo zao linaloongoza kwa chakula.
Mbali
ya Kagera, migomba hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha,
Morogoro, Tanga, Mbeya, Kigoma na Mara.
Taarifa
ambazo MaendeleoVijijini inazo zinaonyesha kwamba, wastani wa uzalishaji wa
ndizi nchini Tanzania ni tani 665,000 kwa mwaka.
Matumizi:
Matumizi
makuu ya ndizi ni chakula – wenyeji wa Kagera hutumia ndizi kama chakula chao
kikuu. Ndizi aina ya kisukari pamoja na jamii nyingine huliwa zikiwa mbivu. Zipo
jamii nyingine za ndizi ambazo hutumika kutengeneza jamu, pombe, juisi na mvinyo.
Ndizi
mbichi huliwa kama chakula baada ya kupikwa, kuchomwa au kukaangwa. Pia
hutengenezwa unga ambao unafaa kwa chakula ambapo wengine hupika ugali,
hutengeneza maandazi, keki, bajia na kadhalika.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba,
majani, maua, maganda na shina la mgomba ni chakula cha wanyama wafugwao hasa
ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Shina
hutumika kuezekea nyumba na hutoa kamba ambazo hutumika kufungia mizigo, kusuka
vikapu na mikeka.
Aidha,
shina na majani makavu yaliyooza hutumika kama mbolea. Pia hutandazwa shambani
kuhifadhi unyevu na kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Majani
mabichi hutumika kama mwamvuli na sahani za kupakulia au kufungia chakula.
Hali ya hewa:
Migomba
hustawi vyema kwenye udongo wenye rutuba na unyevu wa kutosha. Hupendelea
mwinuko wa kuanzia usawa wa bahari mpaka meta 1,800 na hali ya joto kiasi cha
nyuzijoto 27 za Sentigredi.
Migomba
inahitaji mvua kiasi cha milimeta 760 hadi 2,200 kwa mwaka. Iwapo kilimo cha
umwagiliaji kinatumika basi umwagiliaji ufanyike kila wiki.
Upepo
mkali unaweza kuiangusha migomba au kuchanachana majani, hivyo, iwapo sehemu
kilimo hicho kinafanyika kwenye sehemu yenye upepo mkali, inashauriwa sehemu
hiyo ipandwe pembeni mwa shamba ili kuzuia upepo.
Aina za migomba:
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, kuna
aina zaidi ya 100 za migomba zinazolimwa ulimwenguni.
Hata
hivyo, zimegawanywa kwenye makundi kadhaa ambapo zipo ndizi za kupika; ndizi za
kutengeneza pombe; ndizi za kula mbivu; na ndizi za kuchoma au kukaanga. (Hii
inaweza kuwa mada yake inayojitegemea).
Aina
za jumla za migomba inayostawishwa ulimwenguni ni: Mshale, Kiguruwe au
Kimalindi, Mkono wa Tembo, Mzuzu, Matoke, Mtwike, Bokoboko au Mkojosi, Jamaica
na Kitarasa.
Aina
nyingine ni Kisukari cha Kamba, Paka, Sikuzani, Mbwailuma, Mnanambo, Mlelembo,
Williams, Grand Nine, Green Uganda na Pazz.
Utayarishaji wa shamba:
Shamba
kwa ajjili ya kupanda migomba ni lazima litayarishwe mwezi mmoja kabla ya
kuipandikiza migomba. Tayarisha shamba kwa kung’oa visiki na kupunguza miti
mikubwa. Katua ardhi katika kina cha kutosha ili kuiwezesha mizizi kupenda
kwenye udongo kwa urahisi.
Chimba
mashimo yenye ukubwa wa sentimeta 60 hadi 90 kina, urefu na upana. Lakini kumbuka
pia kwamba ukubwa wa shimo hutegemea hali ya mvua. Katika sehemu zenye mvua
kidogo, migomba ipandwe kwenye mashimo makubwa ili kuhifadhi unyevu. Mashimo makubwa
yasitumike sehemu zenye mvua nyingi kwani huozesha migomba.
MaendeleoVijijini inatambua kwamba,
kitaalam nafasi kati ya shimo na shimo na kutoka mstari hadi mstari hutegemea
aina ya migomba. Kwa mfano, aina fupi ya migomba hupandwa katika nafasi ya meta
tatu kati yam mea na mmea na meta tatu kutoka mstari hadi mstari.
Aina
ndefu hupandwa katika nafasi ya meta nne hadi tano kati ya mstari na mstari na
meta nne hadi tano kati yam mea na mmea.
Kumbuka
tu kwamba, wakati wa kuchimba mashimo, tenganisha udongo wa juu na wa chini. Changanya
udongo wa juu na mbolea ya samadi au takataka zilizooza vizuri, yaani
matamahuluku (organic matter) kiasi cha debe mbili hadi tano.
Pia
unaweza kuongeza gramu 60 za dawa aina ya Furadan 5G au gramu 30 za Miral 30G
kwenye mchanganyiko huo. Dawa hizo hudhibiti mashambulizi ya wadudu aina ya
fukusi wa migomba (Banana weevil) au minyoo ya mizizi.
Weka
mchanganyiko huo kwenye shimo. Jazia shimo kwa tabaka la pili la udongo (udongo
wa chini). Shimo likijaa weka mambo katikati ya shimo kwa urahisi wa kulitambua
wakati wa kupandikiza miche. Mchanganyiko huo uachwe shimoni kwa muda wa mwezi
mmoja hadi miwili kabla ya kupandikiza miche ili kuiwezesha mbolea kuendelea
kuoza na kupoa.
Mbegu/Miche ya kupanda:
Migomba
inaweza kustawishwa kwa kupanda machipukizi au vipande vya shina vyenye mizizi
(tunguu) au miche iliyozalishwa kwa njia ya chupa kwenye maabara.
a)
Machipukizi (Banana Sucker)
Machipukizi ni migomba
inayojitokeza kando kando ya mgomba mkubwa. Kuna aina mbili za machipukizi nayo
ni mmachipukizi madogo na machipukizi makubwa.
Mchipukizi madogo ni
yale yenye majani membamba na mamchache. Machipukizi ya aina hii yanayofaa
kupandikizwa ni yale yenye urefu wa sentimeta 100 hadi 150 na unene wa
sentimeta 15. Mamchipukizi hayo huzaa katika kipindi cha miezi 12 hadi 18
kuanzia wakati yalipopandikizwa shambani.
Machipukizi makubwa ni
yale yenye majani mapana. Machipukizi ya aina hii yanayofaa kupandikizwa nay
ale yenye urefu wa sentimeta 150 hadi 200 na unene wa sentimeta 25. Urefu huo
ni kwa aina ndefu ya migomba. Kwa aina fupi ya migomba urefu uwe sentimeta 60
hadi 90. Machipukizi hayo huzaa kuanzia miezi tisa hadi 10 tangu kupandikizwa
shambani.
Machipukizi hayo yote ni
lazima yachukuliwe kwenye migomba inayozaa mikungu mikubwa, yenye afya na
isiyokuwa na magonjwa au wadudu waharibifu kama vile minyoo wa mizizi au fukusi
wa migomba.
Lazima yatoke kwenye
migomba inayovumilia mashambulizi ya magonjwa au wadudu waharibifu.
Kipenyo cha sehemu ya
chini ya shina kiwe kati ya sentimeta 15 hadi 25.
Yawe na afya na yasiwe
na dalili zozote za magonjwa au wadudu waharibifu.
b)
Vipande vya shina lenye
mizizi (Tunguu - Banana rhizome or corm)
Hii ni sehemu ya chini
ya mgomba yenye mizizi na mamcho. Shina hung’olewa kutoka kwenye mgomba
uliokwishavunwa kasha hukatwa katwa katika vipande viwili au zaidi ili kupata
miche mingi.
Kipande kimoja
kinatakiwa kiwe na uzito usiopungua kilo mbili na nusu na macho mawili ya
katikati. Ni muhimu kuzingatia uzito huo kwa kuwa kipande hicho kitakuwa na
chakula cha kutosha kulisha mche mchanga.
Faida ya kutumia tunguu
ni kwamba, ni rahisi kudhibiti fukusi wa migomba na minyoo ya mizizi kwa kuwa
vipande hivi huweza kutumbukizwa kwenye dawa ya kkuzuia fukusi wa migomba na
minyoo wa mizizi kwa urahisi kuliko machipukizi. Vile vile dawa huenea vizuri.
Katika sehemu zenye
uhaba wa mbegu ni njia pekee ya kupata mbegu za kutosha kwani tunguu
hukatwakatwa katika vipande vingi.
c)
Kupanda miche
iliyozalishwa kwenye maabara (Tissue cultures)
Miche huzalishwa kwenye
maabara kwa kutumia utaalam mamalum.
Faida kubwa za kutumia
miche hiyo ni kwamba, haina magonjwa au wadudu waharibifu kama vile minyoofundo
(Nematodes) na fukusi wa migomba.
Kwa kutumia njia hii,
miche mingi ambayo haipatikani inaweza kuzalishwa kwa wakati mmoja. Ni rahisi
kusafirisha.
Tena kwa kutumia
teknolojia hiyo, miche haipotezi sifa za mgombamama.
Upandaji:
Wakati
mzuri wa kupanda migomba ni mwanzoni mwa msimu wa mvua. Kabla ya kupanda,
punguza majani na ondoa mizizi yote. Ondoa mambo kwenye shimo kasha tengeneza
shimo dogo katikati ya shimo kubwa.
Pandikiza
mche kwenye shimo hilo na shindilia sehemu yote kuzunguka shina na mwisho weka
matandazo kama vile nyasi au majani makavu ya migomba.
Kutunza shamba:
Ni
muhimu kutunza shamba la migomba vizuri ili kupata mavuno mengi na bora. Matunzo
hayo ni kama yafuatayo:
-
Baada
ya migomba kuchipua hakikisha shamba ni safi kwa kulipalilia wakati wote.
-
Migomba
yote ing’olewe wakati wa kupunguza au baada ya kuvuna ikatwe na kuweka
matandazo kuzunguka shina ili ioze na kuwa mbolea. Ikiwezekana ongeza nyasi
kavu juu ya takataka hizo. Matandazo huzuia uotaji wa magugu, huhifadhi unyevu
ardhini, huongeza mboji na hupunguza kazi ya kupalilia.
-
Punguza
machipukizi na bakiza migomba mitatu katika kila shina. Bakiza mgomba wenye
ndizi (mama), unaoendelea kukua (mtoto) na unaoanza kuchipua au kuota (mjukuu).
-
Upunguzaji
wa machipukizi hufanya migomba istawi vizuri na kutoa mavuno mengi na bora.
-
Kila
mwaka weka mbolea ya samadi kiasi cha debe mbili kwa kila shimo. Kama una
uwezo, unaweza pia kuweka gramu 300 za mbolea ya mchanganyiko aina ya N.P.K.
yenye uwiano wa 20: 10: 10 kwa kila shina. Mbolea hii iwekwe mara moja wakati
wa mvua za vuli na mara mbili wakati wa masika.
-
Mbolea
ya samadi iwekwe mara moja kwa mwaka na iwekwe kwa kuisambaza kuzunguka shina
usawa wa majani yalivyofikia na ifukiwe.
-
Migomba
ikikosa maji ya kutosha huzaa mikungu midogo. Ili kuzuia hali hiyo isitokee
hakikisha shamba lina unyevu wa kutosha wakati wote.
-
Migomba
inaweza kuanguka kutokana na upepo mkali au kulemewa na uzito wa mkungu. Ili kuzuia
hali hiyo, simika mti wenye panda (mwega) karibu na shina.
-
Kamba
pia inaweza kutumika kwa kufunga kikonyo cha mkungu kwa juu na kufungiwa sehemu
ya chini ya shina la mgomba mwingine ulio karibu.
-
Migomba
kishaanza kutoa maua inashauriwa kuweka alama katika kila mgomba ili kuwa na
uhakika wa idadi ya mikungu itakayokomaa kwa wakati mmoja. Alama iwekwe juu
kwenye kikonyo cha ua. Kamba, kitambaa au riboni zenye rangi tofauti vinaweza
kutumika kama alama. Hakikisha kila unapoweka alama, mikungu hiyo irekodiwe
kwenye daftari. Zoezi hili lirudiwe kila wiki.
Kuzuia
wadudu waharibifu na magonjwa:
a)
Wadudu waharibifu
Fukusi wa Migomba (Banana Weevil)
Fukusi wa migomba ni
mdudu mwenye rangi nyeusi na midomo iliyochongoka. Mdudu huyu hushambulia shina
la migomba na huleta hasara kubwa.
Fukusi huyu hutaga mayai
kwenye shina usawa wa ardhi. Mayai huanguliwa na kuwa funza ambao hutoboa shina
na kutengeneza matundu. Wanapokuwa wengi na matundu huwa mengi mpaka yanakutana
ndani kwa ndani.
Dalili
-
Majani
hubadilika rangi na kuwa njano.
-
Mmea
hudumaa na unapoanguka shina hukatika.
-
Mgomba
huzaa mkungu dhaifu na mdogo.
-
Mgomba
huangushwa kirahisi na upepo.
-
Machipukizi
yaliyoshambuliwa hudumaa, hunyauka, na hatimaye hufa.
-
Shina
hutobolewa sehemu za chini na likipasuliwa katikati kwa urefu matundu mamdogo
meusi, viwavi na fukusi wapevu huonekana.
Kuzuia
-
Kupalilia
mara magugu yanapoota.
-
Kupunguza
mashina.
-
Kukata,
kupasua na kutandaza shambani vipande vya shina mara baada ya kuvuna.
-
Kukata
majani yaliyokauka.
-
Kuweka
matandazo.
-
Kuweka
mbolea ya kutosha ili migomba iwe na afya.
-
Kutumia
mzunguko wa mazao kwa kuanda mahindi, muhogo au mtama kwa muda wa miezi 12 hadi
18 baada ya kung’oa migomba iliyoathirika.
-
Kupanda
aina za migomba zinazostahimili mashambulizi ya wadudu hao.
-
Kuwatega
na kuwaua wadudu kwa kutumia vipande vya shina vilivyopasuliwa na kuwekwa
karibu na shina la mgomba.
-
Kutumia
dawa kama vile Furadan 5G na Miral kiasi cha gramu 60 kwa kila shina. Dawa iwekwe
kwa utaratibu ufuatao: Toa takataka zote a majani sentimeta 30 kuzunguka shina.
Sambaza dawa katika eneo hilo, kisha ichanganye na udongo. Ifukie kwa
kutifuatifua udongo na mwisho weka matandazo.
-
Weka
dawa mara tatu kwa mwaka; mwanzoni mwa mvua za vuli, mwanzoni na mwishoni mwa
mvua za masika. Katika sehemu zenye msimu mmoja wa mvua, dawa iwekwe mwanzoni,
katikati na mwishoni mwa msimu kablla ya mvua kwisha.
Minyoo wa Mizizi/Minyoofundo (Nematodes)
Wadudu hawa hushambulia
mizizi. Mimea iliyoshambuliwa huonyesha dalili zifuatazo:
-
Migomba
hudumaa.
-
Idadi
ya machipukizi hupungua.
-
Majani
hubadilika rangi na kuwa njano.
-
Mikungu
ya ndizi huwa midogo na vichane vyake hupungua.
-
Migomba
huanguka bila shina kukatika.
-
Mizizi
huwa na vidonda na huoza. Iwapo minyoofundo wanahusika, mizizi huwa na
mafundofundo.
Kuzuia
-
Kupanda
migomba katika eneo ambalo halina minyoo.
-
Kutumia
mbegu bora zinazotokana na mashinamama ambayo hayajashambuliwa.
-
Kukwangua
na kuondoa mizizi yote kabla ya kupanda.
-
Kutumbukiza
miche katika maji ya uvuguvugu yaliyo na joto la nyuzi 55 za Sentigredi kwa
muda wa dakika 20 kabla ya kupanda.
-
Kuweka
shamba katika hali ya usafi wakati wote.
-
Kuzuia
usambazaji wa minyoo kutoka shamba hadi shamba.
-
Kuweka
dawa ya Furadan 5G au Miral kiasi cha gramu 60 (vijiko 12 vya chai) kwa kila
shina. Dawa iwekwe umbali wa sentimeta 30 kutoka kwenye shina na iwekwe mara
tatu kwa mwaka.
b)
Magonjwa
Panama
Huu ni ugonjwa
unaosababishwa na aina ya ukungu ambao unaweza kuishi ardhini hata kama hakuna
mimea iliyopandwa. Kwa hali hiyo ni vigumu sana kuuzuia ugonjwa huo mahali
ulipokwishaenea.
Panama hupendelea udongo
wenye majimaji na huingia kwenye mimea kupitia kwenye mizizi iliyojeruhiwa. Huenezwa
kwa kuchukua mimea kutoka mahali penye ugonjwa hadi pengine. Vile vile miguu,
vifaa vya kulimia na maji vinaweza kueneza ugonjwa huo.
Dalili
-
Kingo
za majani huonyesha rangi ya manjano. Baada ya muda rangi huenea hadi katikati
ya jani. Baadaye rangi ya njano hubadilika na kuwa ya hudhurungi na majani
hukauka.
-
Dalili
nyingine ni kupasuka kwa shina. Mpasuko huo hufanya ufa upatao urefu wa
sentimeta 15 hadi 30 na kina cha sentimeta mbili hadi tano. Wakati mwingine
urefu hufikia meta mbili.
-
Hata
hivyo, mgomba unaweza kupasuka kutokana na magonjwa mengine au sababu zingine. Lakini
ukipasua mgomba ulioshambuliwa na panama sehemu za ndani huwa na rangi ya
zambarao.
Kuzuia
-
Usichukue
micheo kutoka shamba lililoshambuliwa na ugonjwa huo.
-
Ng’oa
migomba yote yenye ugonjwa na kufukia au choma moto.
-
Panda
aina ya migomba inayostahimili mashambulizi ya ugonjwa huo kama vile Kiguruwe.
Madoa Jani (Sigatoka Leafspot)
Huu pia ni ugonjwa
unaosababishwa na ukungu. Hupendelea hali ya unyevunyevu na kushambulia zaidi
majani machanga. Huenezwa na upepo au kwa kupanda miche iliyoshambuliwa.
Dalili
-
Majani
huwa na madoa ya rangi ya njano, kahawia au nyeusi ambayo huunganika na kufanya
mistari.
-
Ndizi
hushindwa kukomaa kama mashambulizi yakizidi.
-
Mgomba
huzaa mkungu wenye vichane vidogo.
Kuzuia
-
Panda
migomba katika sehemu isiyotuamisha maji.
-
Daima
weka shamba katika hali ya usafi.
-
Punguza
mamchipukizi yasiyotakiwa.
-
Ondoa
majani yote yaliyoshambuliwa na yachome moto.
-
Panda
kwa nafasi inayopendekezwa ili kuepuka msongamano.
-
Kama
italazimu tumia dawa ya Bayfidan
Kuzuia wadudu na
magonjwa
Katika
kuzuia wadudu wahalifu pamoja na magonjwa, daima zingatia kanuni hizi:
-
Kulima
na kutayarisha mashimo mapema kwa kuzingatia ukubwa na nafasi zinazotakiwa.
-
Kuweka
mbolea ya samadi au ya chumvi chumvi kwa kiasi kinachotakiwa.
-
Kupanda
aina ya migomba inayostahimili magonjwa na wadudu waharibifu.
-
Kupalilia
na kupunguza machipukizi.
-
Kuondoa
na kukatakata majani yote yaliyokauka na yasiyotakiwa.
-
Kuweka
matandazo kuzunguka mashina ili kuhifadhi unyevu na kuongeza rutuba.
-
Kukata,
kupasua na kutandaza shambani vipande vya shina mara baada ya kuvuna.
-
Kutumia
kwa uangalifu dawa za kuzuia au kuangamiza wadudu na magonjwa endapo italazimu.
Uvunaji:
Migomba
huanza kuzaa katika kipindi cha kati ya miezi tisa mpaka 18 tangu kupandikiza
miche shambani.
Hata
hivyo, muda wa kuzaa hutegemea hali ya hewa, utunzaji wa shamba, aina ya
migomba na aina ya micheo iliyopandikizwa.
Kwa
mfano, ndizi aina ya Matoke, Mnanambo na Mlelembo huchukua muda mfupi kuliko
ndizi aina ya Mshale, Kimalindi, Kiguruwe, Ndizi Ng’ombe na Kitarasa. Hali kadhalika,
migomba iliyopandwa kwa kutumia machipukizi makubwa huanza kuzaa mapema kuliko
iliyopandwa kwa kutumia machipukizi madogo.
Ndizi
huwa tayari kuvunwa katika kipindi cha siku 80 hadi 120 tangu kutoa maua. Hata hivyo,
kipindi cha kukomaa kwa ndizi hutegemea aina ya mgomba, hali ya hewa na
kuzingatiwa kwa kanuni za kilimo bora cha migomba.
Ii
mkungu usianguke chini, watu wawili wahusishwe wakati wa kuvuna. Mmoja awe
anakata shina na mwingine anapokea mkungu ili usianguke chini. Baada ya mkungu
kukatwa, kikonyo kikatwe kwa kutumia kisu kikali.
Ndizi
za kupeleka kwenye soko la mbali zivunwe wakati ndizi moja katika mkungu
imekomaa kwa asilimia 75. Wakati huo ndizi huwa bado za kijani na pembe
zinaonekana kidogo.
Ndizi
kwa ajili ya matumizi ya nyumbani zivunwe baada ya vichane vyote katika mkungu
kukomaa. Mkungu uliokatwa uning’inizwe kwenye kamba au waya ili kuepuka
uharibifu.
Wastani
wa mavuno kwa hekta moja ni tani 15 mpaka 20. Kwa migomba iliyotunzwa vizuri ni
tani 38 mpaka 50 kwa hekta.
Comments
Post a Comment