UNAIKUMBUKA HII? “GWAJIMA HUKODI WATU WAJIFANYE MISUKULE!”http://rumaafrica.blogspot.com/2013/10/watu-zaidi-ya-20-warudishwa-kutoka.html 
Baadhi ya watu waliorudishwa na Askofu Gwajima kutoka kwenye Misukule Oktoba 2013.
 
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
KATKA maktaba ya MaendeleoVijijini tunaendelea kuwaletea kumbukumbu mbalimbali zinazomhusu Askofu machachari nchini, Josephat Gwajima, ambapo leo tunakuja nah ii iliyotolewa mahakamani na Mchungaji (R.I.P.) Christopher Mtikila.

Jana MaendeleoVijijini iliwaletea kumbukumbu kuhusu ‘misukule’ ambayo inadaiwa kumuumbua Askofu Gwajima huku mmoja wa wahusika katika kadhia hiyo akitaka alipwe fidia ya Shs. 1 bilioni kwa kudhalilishwa na kugombanishwa na familia yake kiasi cha mkewe kuamua kukimbia.
Mhusika huyo alimpelekea Askofu Gwajima Hati Mashtaka (Demand Note) kupitia kwa taasisi ya Liberty International Foundation (LIF) iliyokuwa ikiongozwa na Mchungaji Mtikila.
Hata hivyo, katika kumbukizi ya leo, inaonyesha kwamba Mchungaji Mtikila, ambaye alikuwa ameshtakiwa na Jamhuri kwa uchochezi mwaka 2012, alitoa ushahidi mahakamani na kumtuhumu Askofu Gwajima kwamba ndiye aliyesababisha yeye akashtakiwa kwa kuwa tu alimtaka aache kuipotosha jamii kwa kutumia Neno la Mungu kwamba anafufua wafu.
 Mchungaji (R.I.P.) Christopher Mtikila akipunga mkono kizimbani baada ya kushinda kesi ya uchochezi dhidi yake.

Ni katika maelezo hayo ya mahakamani ambapo Mchungaji Mtikila alisema Gwajima huwa anawakodi watu na kuwalipa fedha ili wajifanye kwamba walikufa kichawi na kuchukiwa misukule na yeye amewafufua, jambo ambalo siyo kweli.
Wachunguzi wa masuala ya kijamii pia wanahoji iweje kati ya misukule wote hakuna hata mmoja ambaye aliwahi kuthibitika kwa kuwa na Cheti cha Kifo (Death Certificate), bali wote walikuwa ‘watu wasiojulikana’.
Habari kamili hii hapa chini:
Gwajima na msukule wake Mohammed Mustapha

Posted on November 7, 2012 by New Hope Ministry
MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amemtuhumu mchungaji Josephat Gwajima wa kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe Tanganyika Packers, kuwaahidi watu fedha wajifanye misukule awafufue.
Mtikila alidai hayo mahakamani mwishoni mwa wiki mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ilvin Mgeta wakati akitoa ushahidi wake katika kesi inayomkabili ya kuchapisha na kusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.
Akitoa ushahidi wake alidai kuwa chanzo cha kesi hiyo kinatokana na yeye kumfuata Mchungaji Gwajima akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya muda ya Ukristo ya kutetea amani mwaka 2010, kumweleza tabia hiyo anayofanya sio nzuri.
Alidai Gwajima hakufurahia kitendo hicho akamuahidi kumshitaki kwa Rais Jakaya Kikwete kuhusu waraka aliokuwa akiusambaza (Mtikila) ili afungwe.
Alidai aliamua kumfuata mchungaji huyo baada ya watu kumweleza kwamba Mchungaji Gwajima aliwaahidi Sh 300,000 ili wajipake vumbi na kuvaa magunia wapigwe picha na kujitangaza kuwa walikuwa wamekufa halafu Gwajima ajifanye amewafufua.
“… tena mmojawapo ni mtumishi wako wa mahakamani hapa ila nimesikia amehama, walinifuata na kunieleza kuwa waliahidiwa fedha ili mtoto wake ajifanye alikuwa amefichwa chini ya ziwa Victoria kwa miaka saba na wakatangaza kuwa aliuawa na baba yake mzazi kumbe ni mbinu ya Gwajima ajifanye amemfufua,” alidai Mtikila. Aidai kuwa baadaye alifuatilia na kugundua mtu huyo alikuwepo na hakuwahi kufa.
Aliendelea kudai kuwa anaamini kushitakiwa kwake katika kesi hiyo kunatokana na Mchungaji Gwajima kwa sababu baada ya kupokea malalamiko hayo kutoka kwa waumini wa kanisa lake la Ufufuo na Uzima, aliambatana nao pamoja na wachungaji wengine kumfuata akidai kuwa nia yao wamkemee kama neno la Mungu linavyosema.
“Hatukufanikiwa, Gwajima alibadilika akasema anaongea na Rais nifungwe kutokana na waraka niliouandika, akasema kabisa anaweza kumpigia simu wakati huo huo. Hivyo naamini kabisa msingi wa kesi hii ni Gwajima,” alidai Mtikila.
Mtikila alidai kuwa alimpa Rais Kikwete waraka huo aliouandaa ambao ulikuwa ukisambazwa nchi nzima lakini hakufikishwa mahakamani na kuhoji kuwa iweje aburuzwe mahakamani baada ya kwenda kwa mchungaji Gwajima.
Alidai kuwa siku moja alfajiri nyumba yake ilizingirwa na askari kama 12 wakimtaka afungue mlango akidai kuwa kutokana na yeye kuwa mzoefu wa kupekuliwa na askari, alipofungua alipekuliwa na kutakiwa kwenda kituo kikuu cha polisi.
Alidai alipowauliza askari sababu ya kupelekwa polisi kuwa ni kwa ajili ya waraka ule, walikiri na ndipo aliwatolea nakala kila mmoja na yake akawapa wasome na akakumbuka maneno ya mchungaji Gwajima kuwa atamfunga.
Aliendelea kudai kuwa aliwaomba askari wale wamsubiri atoe nakala 70 zaidi ili awapatie watu waliokuwa wakisubiri kwa sababu alitakiwa kwenda na kompyuta yake polisi. Alipofika huko aliwakuta watu 14 ambao walikuwa wakimhoji na wanne kati yao walimhoji kama alikuwa na tofauti na Gwajima.
Aidha, Mtikila alidai kuwa mchungaji Gwajima alikuwa ni miongoni mwa mashahidi wa upande wa Jamhuri lakini hakutokea mahakamani akidai kuwa alijua amemkosea Mungu na kanisa badala yake walikuja watu wake ambao hawakuwepo siku alipokwenda kwa Mchungaji huyo.
Katika ushahidi wake Mtikila alidai kuwa alialikwa kuhubiri Agosti mosi hadi 3, 2009 Mwanza kwenye kongamano, yale aliyohutubia wakamuomba ayaweke kwenye maandishi ili ujumbe uwafikie viongozi wote Wakristo nchini ambapo zilizalishwa nakala 1,000, ziligawiwa 700 akabaki na 300 kwa ajili ya kusambaza.
Mtikila alikiri maelezo yake ya polisi Aprili 15, 2010 yaliyosomwa na kutolewa mahakamani kama kielelezo katika ushahidi wa Jamhuri. Alikiri kuwa kweli aliuandaa waraka huo na kuusambaza mwaka 2009, lakini alikanusha kwamba haukuwa wa uchochezi kwani unahusu maneno ya Mungu.
Mtikila alikiri zilikuwa nakala 100,000 ambazo zilisema kwamba Rais Kikwete anaangamiza Ukristo na amekuwa jasiri kuingiza Uislamu katika Katiba ya Jamhuri, wakristo waungane kuweka mtu Ikulu’.
Kesi hiyo itaendelea Juni 25 mwaka huu kwa ajili ya Mtikila kuendelea kutoa ushahidi wake. Alidai kuwa kesi hiyo imekusudiwa ifungwe kwa sababu ni mtakatifu hana dhambi anatetea Ukristo.