Featured Post

WARAKA WA CHACHA ZAKAYO WANGWE KWA HALMASHAURI KUU YA CHADEMA 2008



Pichani ni aliyekuwa Katibu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia Dk. Wilbroad Slaa akiangalia gari lililosababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime Chacha Wangwe katika eneo la Pandambili, wilayani Kongwa mkoani Dodoma ambapo Mheshimiwa Wangwe alikuwa anatokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam siku ya Jumapili, Julai 27, 2008.

 
HUU ni Waraka ulioandikwa na Chacha Zakayo Wangwe (marehemu) mwaka 2008 kabla ya kifo chake ambao alikuwa ausome kwenye Halmashauri Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kama sehemu ya utetezi wake baada ya kusimamishwa nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.
Hata hivyo, Chacha Wangwe, aliyekuwa Mbunge wa Tarime, hakufanikiwa kuusoma waraka huo, kwani mauti yalimfika wakati akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kuwahi kikao hicho.
Chacha alikufa katika ajali ya gari iliyozua utata katika eneo la Pandambili, Dodoma Jumapili saa 2:55 usiku, Julai 27, 2008, ambapo alikuwa akiwahi mazishi ya Bhoke Munanka kabla ya kikao cha Halmashauri Kuu.

UTANGULIZI.

Jumamosi, June 28 mwaka huu wajumbe kadhaa wa Kamati Kuu ya CHADEMA walidai kuwa wamesitisha Umakamu uenyekiti wangu katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma siku hiyo. Kesho yake Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mhe. FREEMAN MBOWE akaitisha mkutano wa waandishi wa habari na kutaja sababu za kunisimamisha uongozi.

Inatosha tu kusema kuwa sababu zote alizotoa ni za uzushi kama ile inayodai kuwa mimi navujisha siri za chama kwa viongozi wa CCM bila hata kutaja siri hizo, au kusema nimezitoa lini, wapi, na kwa kiongozi yupi?Kikao hicho kinachosemekana kunisimamisha uongozi, kilikuwa na wajumbe 31 ambao takribani nusu hawakuwa na uhalali wa kupiga kura kinyume cha katiba na kanuni za CHADEMA kwa vile walikuwa wameandaliwa kwa kazi hiyo.

 Wajumbe 7 walikataa kushiriki njama hizo.
Kufuatia jaribio hilo la kunivua uongozi kutokubalika kwa wanachama walio wengi wa CHADEMA , Mwenyekiti MBOWE na wafuasi wake wameendelea kuhaha kwa kuongeza sababu nyingine mbalimbali ili kuhalalisha njama zao. Sasa hivi wameingia hatua ya kuwashawishi wanachama wa Tarime eti wanifukuze uanachama.Kwa kuzingatia katiba, kanuni na taratibu za CHADEMA, nilichokifanya mimi baada ya kubaini njama zao ni kukata rufaa kwa Baraza Kuu la Chama, kupinga upotoshaji unaofanywa chini ya uongozi wa Mhe. MBOWE anayeonekana kutaka kuendesha chama kinyume na matarajio ya wanachama walio wengi.

Hivyo basi zipo habari za uhakika kuwa kikao hicho cha Baraza Kuu hakitaitishwa ama kabisa, au kitacheleweshwa kwa makusudi, kwa visingizio mbalimbali ikiwemo kutokuwa na fedha za kukidhi gharama za kikao hicho.

Naomba nikiri kuwa ninakerwa sana na mtiririko mzima wa sakata hili linalozua mgogoro unaokiyumbisha chama. Ukweli ni kwamba mimi niligombea Umakamu Mwenyekiti nikiwa na agenda ya kufufua uhai wa chama kwa kukaripia vitendo visivyostahili katika kuendesha chama. Agenda yangu haijabadilika. Yote niliyoyasema wakati nagombea nafasi hii yanafahamika kwa wana CHADEMA wote.

Walikuwepo walioyalalamikia na walikuwepo walioyapongeza matamshi yangu hayo.Mwisho wa yote wana CHADEMA waliridhika kuwa ajenda yangu ilikuwa sahihi na hivyo wakanichagua kuwa Makamu Mwenyekiti. Hivyo basi hata kama ni kweli kuwa ulikuwepo mvutano wakati wa kampeni ile, lakini hilo ni jambo la kawaida katika uchaguzi. Nijuavyo mimi hayo yalitakiwa yawe si ndwele nasi tugange yajayo kwani wanachama walikwisha fanya uamuzi halali kupitia kura zao.

Baada ya kuingia kwenye wadhifa wa Makamu Mwenyekiti Taifa, nilifanikiwa kuzungumza na Mhe. MBOWE kuhusu mambo, hususan yale, niliyoyapigania wakati wa kinyang?anyiro kile na kumuomba tukae chini na kutafuta jinsi ya kufanikisha azma hiyo.Ni imani yangu kuwa waraka huu utawasaidia wanaCHADEMA wenzangu na watanzania wote kwa ujumla, kuelewa vizuri ukweli wa mambo niliyoyapigania kabla ya kuwa Makamu Mwenyekiti, na ninayoendelea kuyasimamia hivi sasa nikiwa Makamu Mwenyekiti, na inshallah nitakayoyatekeleza baadae kama Taifa Mwenyekiti wa CHADEMA.

Kimsingi mambo tunayotofautiana na Mhe. MBOWE ni haya yafuatayo:-

MATUMIZI YA RUZUKU

CHADEMA hupata ruzuku ya Tshs. 66,000,000 kwa mwezi (Milioni sitini na sita). Mimi nasema si haba hasa tukizingatia chama kilikotoka. Naamini kuwa kiasi hiki cha fedha kikisimamiwa vizuri kinaweza kukirahisishia chama kujieneza katika ngazi zote toka Tawi, Wilaya, Mkoa na Taifa.

Si kweli kwamba matatizo yote yatamalizwa na fedha hizi lakini basi hata ofisi za chama zinaweza kuwa hai nchi nzima kitu ambacho kwa sasa hakipo. Mahesabu yanaonesha kuwa mtaji wa laki moja (Tshs.100,000/=) kwa wilaya moja nchini inatosha, hivyo kwa Wilaya 126 kwa mwezi jumla yake ni Tshs. milioni 12 (Tshs. 12,600,000/= ) zinahitajika ( Wilaya 126 x 100,000 kila wilaya = 12,000,000/=)Hata tukisema tupeleke kiasi hicho kwa kila jimbo la uchaguzi jumla yake ni Tshs. Milioni 23 (Tshs. 23,000,000/=) kwa maana ya majimbo 213 x 100,000 = 23,000,000/=.

Mhe. MBOWE anasema hizo ni pesa nyingi sana kwa uimarishaji wa chama. Mimi nasema hapana, kiwango hiki kwa kila Wilaya au Jimbo la uchaguzi ni muafaka kwani haba na haba hujaza kibaba.Chini ya uongozi wa Mhe. MBOWE na wafuasi wake hawastaajabu kuwa kati ya Tshs. 374,144,000.40 zilizopatikana kama ruzuku katika ya Januari 1 na Juni, 30, 2008, Tshs. 350,000,000/= zilitumika Makao Makuu ya CHADEMA na Tshs. 25,000,000/= tu ndizo zilikwenda Wilayani kuimarisha chama.Mimi naona mgao huu unayatukuza Makao Makuu ya CHADEMA isivyostahili wakati huo huo ukidhalilisha chama nchi nzima.

MADENI YA UCHAGUZI

Kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Mhe. MBOWE alitufahamisha wanachama kuwa alikuwa anakidai chama US $ 181,949.00 sawa na Tshs. 218,338,546. Mpaka sasa chama kimekwisha mlipa Tshs. 175,000,000/=Baada ya kupata wadhifa wa Makamu Mwenyekiti, na kwa kuzingatia takwimu zionekanazo hapo juu katika kulinganisha matumizi ya fedha Wilayani na Makao Makuu niliamua kumshauri MBOWE asitishe kujilipa deni kutokana na fedha za ruzuku kwani siamini kuwa kulipa madeni yaliyopita kunaendana na utaratibu wa usimamizi wa fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa toka serikalini.

Mhe. MBOWE alichachamaa na ndipo nilipomshauri kuwa kama ni hivyo basi atuthibishie pesa hizo anazodai alikikopesha chama ziliingia kwenye akaunti gani ya CHADEMA, kupitia hundi ipi, na lini? Nilimuomba pia kutaja ni kikao gani cha chama kiliidhinisha matumizi ya fedha hizo kwani kama hakuna ushahidi wa maidhinisho, ni dhahiri kuwa matumizi hayo hayakudhibitiwa na chama na kwa mantiki hiyo kuyafanya kuwa matumizi binafsi ya Mhe. MBOWE.Vilevile, nilimueleza kuwa matumizi ya fedha hizo alizodai alikikopesha chama yalikuwa yakinuka harufu ya UFISADI.

Stakabadhi zote kuhusiana na matumizi hayo zilionesha kuwa gharama za aidha ununuzi na / au ukodishaji wa vifaa hivyo, hazikutofautiana na viwango wanavyolipishwa watalii kwa huduma kama hizo, kwa maana ya gharama ya juu sana.Na kwa kuwa hata baada ya kuwa Mhe. MBOWE amekwisha lipwa zaidi ya nusu ya deni alilodai kuikopehsa CHADEMA, vifaa vyote yakiwemo magari, vipaza sauti na kadhalika vimebakia kuwa mali yake binafsi, basi bila kumficha nilimueleza kuwa huko ni kukinyonya chama kwa kukigeuza kitega uchumi cha watu binafsi.Kuhusu suala la kulipa madeni kupitia ruzuku ya serikali, nilimuomba Mhe. MBOWE afuatilie kwa Msajili wa Vyama vya siasa ili tupate ufafanuzi kama kweli fedha za ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa, inaweza kutumika kulipia madeni ya viongozi wa vyama hivyo yatokanayo na uchaguzi ili CHADEMA isiathirike kisheria.

Niseme kweli hapa kwamba, kwa vile wanaCHADEMA wengi walinichagua kuwa Makamu Mwenyekiti, na hata mimi mwenyewe tulikuwa wagombea wa nafasi za ubunge, udiwani n.k katika uchaguzi wa mwaka 2005 ningefarijika sana iwapo na sisi tungerejeshewa angalau chochote cha kufidia gharama zetu, kwa maana kwamba kama chama kimeamua kurudisha gharama hizo kiwalipe wote badala ya kulipa madeni kwa wateule wachache.

UTEUZI WA WABUNGE WA VITI MAALUM

Naamini ukweli wa suala hili hauna mjadala. Kwamba Mhe. MBOWE na wafuasi wake walighushi orodha ya majina ya viti Maalum badala ya kupeleka yaliyopendekezwa na Kamati Kuu sio siri.

Naamini hata Mhe. MBOWE anakubaliana nami kuwa suala hili si moja ya siri anazodai nimevujisha! Yamesemwa mengi juu ya mtafaruku uliojitokeza kuhusu viti maalum hadi baadhi ya waasisi wa chama wakataka kujitoa na hivyo kumlazimisha Mwenyekiti Taifa ( FREEMN MBOWE) na Katibu Mkuu (DR WILBROAD SLAA) kukiomba radhi kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kwa kukiuka katiba, kanuni na maadili ya chama katika suala hili la kugushi viti maalum.

Ni ukweli ulio wazi kuwa kitendo hicho cha upendeleo bado kina iumiza taswira ya CHADEMA. Chama kinaonekana kuendekeza ujanja ujanja kiasi kwamba watu na binti zao, wakwe zao, shemeji zao, waume wenzao, wachumba wa shemeji zao, wake wenza na kwa kiwango kikubwa watu wa kabila moja ndiyo wamekuwa sura ya CHADEMA bungeni.Katika hili nilichoweza kumueleza Mhe. MBOWE ni kuwa chaguzi mbalimbali tangu za Mitaa, Ubunge na Urais zinakaribia ni vizuri tufanye bidii kusambaza nguvu zetu nchi nzima tuwe na mtaji wa kura maeneo mengi ili kashfa kama hii isijirudie. Hii ni kwa msingi kuwa chama kikijitanua kutakuwa hakuna sababu ya kuwaona watu wa eneo fulani tu kuwa ndiyo mhimili wa CHADEMA na hivyo zikitokea fursa itakuwa rahisi chama kuwakilishwa na mtandao wake mpana badala ya koo au kabila fulani.Sasa kwa kuwa kuimarisha chama kitaifa maana yake ni matumizi ya fedha, nalo hili likawa nongwa ingawa kwa mtazamo wa Makao Makuu kulipa madeni kwa wateule wachache si nongwa.

Cha ajabu ni kwamba Mhe. MBOWE hakukana kuwa hili la viti maalum na hata upangaji wa ajira kwa ukabila una leta athari mbaya kwa mustakabali wa CHADEMA
Katika maongezi yangu nae nilikuwa wazi nilipotahadharisha kuwa:

1. Watanzania wakiendelea kuona kwamba CHADEMA inaendeshwa kwa misingi ya kikabila hawatajiunga na chama chetu na tutakosa wafuasi.

2. Watanzania wakiona kuwa sisi tumeweka mbele ukabila kuliko utaifa hawatatupa madaraka na kutawala kwa kuhofia yale yanayotokea nchi jirani kama Rwanda, Burundi, Kenya na kadhalika ambako nafasi za raia wote zimehodhiwa na kabila moja na hatma yake watu wamechinjana kama kuku kwa kupinga hilo.

Pia nilimwambia kwamba, kwa jinsi sura ya uteuzi wa Wakurugenzi na watendaji wengine wa Makao Makuu inavyoonekana, sasa tayari chama chetu kimebatizwa jina la CHAMA CHA WACHAGA, na hii si kuwatendea haki raia wengine na makabila yao ambao wataonekana kama punguani kujihusisha na chama na ukabila.Yote haya ninayosema kuhusu ukabila, upendeleo na kadhalika sio dhana tu. Kufuatia malalamiko mengi yaliyokuwa yakisikika nchi nzima kuhusu masuala haya, Kamati Kuu ya CHADEMA ilikwisha unda Tume kutafuta ukweli wa mambo hayo. Tume hiyo ya watu watano iliongozwa na Mhe. Merky Lugendo Mziray ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA nayo imekwisha toa taarifa yake kwamba Makao Makuu ya CHADEMA yanatawaliwa na ubaguzi wa kikabila, kidini na kielimu.

UTENDAJI WA KIBABE

CHADEMA ni chama kilicho njia panda kwa sasa kutokana na utendaji wa kibabe wa Mhe. MBOWE. Ninafahamu jinsi vyama vingine vya upinzani hapa nchini kama vile NCCR ? Mageuzi vilivyoporomoka haraka haraka mithili ya nyumba ya mabua. Chama NCCR ? Mageuzi kilifikia mahali pazuri tu hadi watu wakaanza kufikiria kuwa kingekuwa chama mbadala kwa CCM.

kwa bahati mbaya uchu wa madaraka, ulafi wa ruzuku, na tabia za kimangimeza kwa pamoja vikakiathiri hadi kupoteza umaarufu wake.Na hata vyama vingine vya upinzani vina dalili hizo hizo japo kwa viwango vinavyotofautiana. Ila badala ya kujichunguza na kujua kasoro zetu, kila siku vyama vyetu, vimekuwa vikidai kuwa ni chama tawala ndicho kinachoviroga, kama ambavyo Mhe. MBOWE ameanza kuweweseka kupitia vyombo vya habari.Napenda kuthibitisha kuwa katika mgogoro unaopaliliwa sasa na Mhe. MBOWE ndani ya CHADEMA kutokana na ufisadi, ufuska, ulevi wa madaraka na umangimeza chanzo chake ni tabia yake ya kuendesha chama kibabe. Mathalan kumzuia Martin Mung?ong?o Mkurugenzi aliyechaguliwa kwa kura kutofanya kazi zake ndani ya chama, madai ya kupigana na watendaji wa chama ndani ya baa na vitendo vingine vya aina hiyo ni ushahidi tosha wa hulka hii.

Hadi sasa Mhe. MBOWE amefanikiwa kukizuia chama hiki kisifanye kazi ya siasa mkoa wa Dar es salaam kwa miaka minne.Ninavyoongea hivi sasa CHADEMA imekuwa ikikimbia vikao vya Democratic Union of Afrika (DUA), Muungano wa Vyama Vya Upinzani, uliofanikisha CHADEMA kujuana na Conservative Party ya Uingereza na Republican ya Marekani. Vyama dada hivi vyote vinaulalamikia uongozi wa CHADEMA kwa kufuja fedha ya misaada na kuwasilisha kwao risiti za kugushi, kama ilivyofanyiwa Conservative Party baada ya kutoa msaada wa Tshs. 78,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa baiskeli na pikipiki ambazo hazikununuliwa.Katika mkutano wa Kamati Kuu ya CHADEMA huko Dodoma hivi majuzi tu, Mhe. MBOWE kwa kauli yake aliwatisha wajumbe kuwa alikuwa amethibiti uwezekano wowote wa wajumbe kujisikia huru kwa kutoa mawazo ambayo yangepingana na ajenda yake aliyoitoa ghafla kikaoni kunisimamisha Umakamu Mwenyekiti.

Mhe. MBOWE Alikifahamisha kikao kuwa alitoa taarifa kwa IGP, SAID MWEMA kuwa kuna wahuni ambao walitaka kuuchafua mkutano wake, naye IGP akahakikisha kuwa mkutano ule unalindwa kwa kiwango cha kushtua kama ambavyo hata vyombo vya habari vimethibitisha.Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayobainisha Mhe. MBOWE ni kiongozi wa aina gani.

HITIMISHO

Kama nilivyokwisha sema hapo awali, sijaacha na sintoacha ajenda yangu ya kufufua uhai wa CHADEMA kwani ndiyo ahadi iliyofanikisha kuchaguliwa kwangu kuwa Makamu Mwenyekiti Taifa. Nilipopata wadhifa huo nilianza kuitekeleza ajenda hiyo kupitia mahojiano na Mwenyekiti MBOWE kuhusu matumizi ya ruzuku, madeni ya uchaguzi, uteuzi wa wabunge wa viti maalum, nafasi za ajira Makao Makuu, na kuhusu mwenendo wa chama Mkoa wa Dar es salaam.

Nilijikuta katika mvutano mkubwa kila nilipogusa eneo lolote katika haya. Nakiri kuwa kwa kiwango kikubwa sikuwa na uwezo wa kubadili mambo hayo yaliyokuwa yakiratibiwa kwa ukaribu na Mhe. MBOWE na wafuasi wake kwani sikupewa ushirikiano wa aina yoyote na chama pale Makao Makuu.

Ni vigumu kuamini, lakini ni kweli kuwa sikuwa na ofisi Makao Makuu, sikupewa vitendea kazi kama magari, vipaza sauti na/au vyombo vya habari, na sikuwahi kupata taarifa yoyote ya kiutendaji toka Makao Makuu.Kwa kuzingatia yote hayo, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru kwa dhati wanachama wa CHADEMA mkoa wa Dar es salaam ambao kwa pamoja tulisimama kidete kufufua uhai wa chama hapa jijini. Niseme tu ushirikiano wao wa hali na mali uliniwezesha kushughulikia masuala muhimu ya kitaifa na kimataifa.

Rai yangu kwa wana CHADEMA na wale wote wanaokitakia mema chama chetu na nchi yetu kwa ujumla ni kwamba kazi ya kupigania demokrasia ya kweli ndani na nje ya chama, kukiepusha chama na vitendo vya ukabila, migogoro, ubadhirifu, umangimeza, ufisadi na ubaguzi wa aina yoyote bado inaendelea na nawaombeni mniunge mkono kwa hali na mali katika vita hii. Naamini tutashinda.

Mungu Ibariki CHADEMA,
 Mungu Ibariki TANZANIA.....

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA.

Comments