KILIMO BORA CHA MIEMBENa Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
MIEMBE hulimwa karibu katika nchi zote zilizoko kwenye ukanda wa joto, na hasa tropiki. Nchini Tanzania miembe hulimwa zaidi kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya (wilayani Kyela), Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Tabora na Tanga, MaendeleoVijijini inakuletea ripoti kamili ya kilimo hicho.
Taarifa za Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi zinaonyesha kwamba, uzalishaji wa maembe nchini ni wastani wa tani 159,472 kwa mwaka na kwa kawaida maembe ni miongoni mwa matunda ya bustani yanayochangia Pato la Taifa (GDP).

Waswahili huwa wanasema; “Usidharau dafu, embe tunda la msimu!” Wako sahihi kwa sababu dafu linapatikana wakati wote, lakini embe hupatikana kwa msimu.
Lakini japokuwa ni tunda la msimu, lakini embe linafahamika kama mfalme wa matunda kutokana na ladha na harufu yake. Msimu wa embe unajulikana kwa harufu ambayo hutamalaki.
Rangi ya nyama ya embe iliyo ya njano huvutia walaji na asilimia 60 mpaka 70 ya tunda lililoiva huliwa. Linaweza kuliwa kama tunda, lakini pia hukamuliwa kupata maji ya matunda, hutengenezwa jamu, saladi, siki na achali.
Embe mbivu ina sukari, vitamin A, B na C kwa wingi, hivyo ni tunda muhimu kwa lishe na afya ya binadamu.

Mazingira mazuri
Miembe hupendelea kipindi kirefu cha jua, joto la wastani ambalo ni nyuzi joto 25 za Sentigredi na mwinuko wa kuanzia meta 0 hadi 600 kutoka usawa wa bahari.
Miembe hustawi zaidi katika maeneo yanayopata wastani wa mvua kati ya milimeta 650 hadi 1,800 kwa mwaka na udongo wenye kina kirefu, unaopitisha maji kwa urahisi na wenye uwezo wa kushika unyevu kwa muda mrefu.
Kwa kawaida, miembe hupendelea uchachu wa udongo (soil pH) kati ya 5.5 na 7. Udongo wenye uchachu zaidi ya 7 huwa na upungufu wa madini aina ya zinki na chuma.

Aina za miembe
Zipo aina nyingi za miembe, hata hivyo, zinaweza kugawanywa katika makundi matatu kulingana na sifa zifuatazo:
a)  Umbile la Mti, Maua na Majani
Katika kundi hili kuna aina fupi na ndefu. Aina fupi ni kama vile miembe Chotara, Sabre, Kent, Keith, Tommy Atkins na Alphonso. Aina ndefu ni kama vile Sindano na Boribo.
b)  Umbo, Ukubwa, Uzito, Ladha na Ubora wa Tunda
Aina za miembe yenye matunda makubwa ni Dodo na Sabre. Aina zenye matunda madogo ni Sindano na Mawazo.
c)   Mazingira yanayofaa kwa kilimo chake
Mazingira hayo ni kama vile; hali ya hewa, ubebaji wa matunda, msimu wa kuvuna na ustahimilivu wa magonjwa na mashambulizi ya wadudu. Aina zinazopendelea mwinuko wa juu ni kama vile Sabre na zinazopendelea mwinuko wa chini ni Boribo, Sindano na Dodo.

Njia za kuzalisha miembe
MaendeleoVijijini inaelewa kwamba, njia kuu zinazotumika kuzalisha miembe ni kupanda mbegu halisi moja kwa moja shambani au kupandikiza miche iliyobebeshwa (Graft Method).
a)  Kupanda mbegu moja kwa moja shambani
-         Shamba ni lazima litayarishwe mwezi mmoja hadi miwli kabla ya kupanda mbegu. Tayarisha shamba kwa kuchimba mashimo yenye ukubwa wa sentimeta 90 upana na urefu. Kina kiwe na sentimeta 60.
-         Mashimo yenye ukubwa huo yatumike sehemu zenye ukame. Sehemu zinazopata mvua nyingi tumia mashimo yenye ukubwa wa sentimeta 60 upana, urefu na kina.
-         Nafasi kutoka shimo hadi shimo ni meta 10 mpaka 15 na kati ya mstari na mstari ni meta 10 hadi 15. Hata hivyo, nafasi ya kupanda hutegemea aina ya miembe.
-         Mashimo yakishakuwa tayari, jaza mbolea za asili kama vile samadi au mbolea vunde zilizooza vizuri kiasi cha debe mbili hadi tatu kwa kila shimo.
-         Changanya mbolea na udongo wa juu pamoja na gramu 250 za mbole ya chokaa (Triple Super Phosphate – TSP).
-         Wakati mzuri wa kupanda ni mwanzoni mwa msimu wa mvua.
-         Panda mbegu zilizokomaa vizuri mara baada ya kuzitoa kwenye kokwa. Mbegu zipandwe katika kina cha sentimeta tano. Mwagilia baada ya kupanda na endelea kumwagilia hadi mbegu zitakapoota. Mbegu huota baada ya siku 20.
b)  Njia ya Kubebesha (Graft Method)
Miche kwa ajili ya kubebesha hukuzwa kwanza kitaluni na baadaye huhamishiwa shambani baada ya kubebeshwa.
Katika kitalu, mbegu hupandwa kwenye mistari yenye nafasi ya sentimeta 30 mstari hadi mstari. Nafasi kati ya shimo na shimo ni sentimeta 15. Mbegu pia zinaweza kupandwa kwenye vifaa kama vile mifuko ya plastiki, vikapu vya majani au viriba vya majani ya migomba vyenye urefu wa sentimeta 30. Vifaa hivyo hujazwa udongo uliochanganywa na mbolea za asili zilizooza vizuri.

Jinsi ya kubebesha

-         Miche hubebeshwa inapofikia umri wa miezi sita hadi 18. Kata kikonyo kutoka kwenye miti inayozaa matunda bora na ambayo haina magonjwa wala wadudu waharibifu.
-         Chagua kikonyo chenye unene ulio sawa na ule wa mchemama na urefu wa sentimeta 20.
-         Kikonyo kiwe na vichomozo viwili hadi vitatu.
-         Chonga pande mbili za kikonyo kwa urefu kiasi cha sentimeta mbili hadi tano. Wakati wa kuchonga hakikisha mamcho yanaangalia juu.
-         Kata sehemu ya juu ya mchemama sentimeta 25 kutoka usawa wa ardhi.
-         Pasua mchemama katikati sentimeta mbili hadi tatu kuanzia juu kwenda chini.
-         Chomeka kikonyo kwenye mkato huo.
-         Funga kwa kutumia uutepe wenye urefu wa sentimeta 25 na upana wa sentimeta moja.
-         Baada ya siku 30 hadi 45, fungua utepe kuangalia kama kikonyo kimeunga. Kama kimeunga, legeza utepe na acha mpaka mche utoe majani.
-         Miche huwa tayari kupandikizwa shambani ifikiapo umri wa miezi 12 kuanzia ilipobebeshwa.

Kupandikiza michezo shambani
Mashimo yatayarishwe mwezi mmoja kabla ya kupandikiza. Tayarisha kwa kuweka mbolea za asili kama vile samadi kiasi cha madebe mawili hadi matatu kwa kila shimo. Pandikiza miche mwanzoni mwa msimu wa mvua au wakati wowote kama unatumia kilimo cha umwagiliaji.
Miti iliyobebeshwa huwa na umbile dogo hivyo huhitaji nafasi ndogo ambayo ni meta nane hadi 10 kati ya mstari na mstari na kati ya shimo na shimo.

Changanya na mazao mengine
Miembe inaweza kuchanganywa na mazao mengine kwa miaka mitano hadi sita ya mwanzo.
Mazao ambayo yanaweza kuchanganywa ni kama vile mananasi, migomba na aina mbalimbali za mboga.

Utunzaji wa shamba
MaendeleoVijijini inasisitiza kwamba, jambo la muhimu kabisa ni palizi. Katika shamba la miembe, palizi hufanyika kwa kufyeka majani yote na kutengeneza kisahani kuzunguka shina.
Weka madebe mawili hadi matatu ya mbolea za asili kama vile samadi kwa mti kila mwaka.
Mbole ya N.P.K. pia inaweza kuwekwa ambapo kiasi kinachotakiwa ni kilo moja kwa mti kila mwaka.
Mbolea inapaswa kuwekwa mwanzoni mwa msimu wa mvua.

Magonjwa yanayoshambulia miembe
Miembe, kama mimea mingine, hushambuliwa na magonjwa mbalimbali, lakini yaliyo makubwa ni haya yafuatayo:

Chule (Anthracnose)
Huu ni ugonjwa wa ukungu unaoshambulia majani na matunda.

Dalili zake
-         Majani huwa na madoadoa meusi ambayo baadaye huwa makubwa na makavu.
-         Maua pia huwa na madoa madogo meusi yaliyosambaa.
-         Maua hupukutika.
-         Matunda huwa na mabaka madogo meusi ambayo baadaye huwa makubwa na yenye rangi ya kikahawia iliyochanganyika na nyeusi.
-         Kukiwa na unyevu mwingi, ukungu wa rangi ya pinki huonekana katikati ya baka. Hali hiyo husababisha maembe mamchanga kudondoka.

Kuzuia
-         Nyunyizia dawa za ukungu kama vile Dithane M-45
-         Ondoa matawi yote yaliyozeeka kabla ya maua kutoka.

Ubwirijivu (Powdery Mildew)
Huu pia ni ugonjwa unaosababishwa na kuvu au ukungu. Hushambulia zaidi maua, majani na matunda.

Dalili
-         Maembe machanga huanguka kabla ya kukomaa.
-         Matunda yaliyokomaa huwa na ranggi ya kahawia.

Kuzuia
Nyunyizia dawa za ukungu aina ya Sulphur Dust au Baylaton.


Wadudu Waharibifu
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, miembe hushambuliwa na wadudu wengi. Baadhi ya wadudu hao ni vijasidi, vidugamba, vidung’ata na nzi wa tunda aliyezoeleka na nzi wa tunda mgeni (Bactrocera evadens).

Nzi wa Tunda Mgeni (Bactrocera evadens)
 Nzi huyu ni hatari zaidi katika uzalishaji wa maembe. Nadhani unafahamu ule wimbo wa “Mdudu kaingiaje ndani ya kokwa la embe”! Basi huyu nzi ndiye kisababishi kikubwa.

Dalili
-         Kuanguka kwa maembe kiasi cha asilimia 50 hadi 80.
-         Maembe yakikatwa huwa yameoza na mara nyingi yanakuwa na funza wengi.

Kuzuia
-         Fukia maembe yaliyoanguka katika kina cha futi tatu.
-         Palilia mara kwa mara eneo lililo chini ya miembe ili kuwaacha wazi funza na buu waweze kushambuliwa na wadudu walawangi au kuathiriwa na hali mbaya ya hewa katika ukuaji wake.
-         Ondoa au fyeka miti ya matunda ya porini ambayo iko karibu na shamba la miembe ili kupunguza mazalio ya nzi nje ya msimu wa embe.
-         Vuna maembe ambayo hayajashambuliwa yakiwa bado juu ya mti. Hali hiyo inapunguza ongezeko la idadi ya nzi katika shamba.
-         Tumia vivutio vilivyochanganywa na dawa aina ya Decis au dawa yoyote ya wadudu ili kuua majike ya nzi huyo.
-         Tumia dawa ya kuvutia dume (Pheromone) aina ya Methly eugenol iliyochanganywa na dawa ya Dichlorovos ili kuua nzi dume.
-         Nyunyiza dawa aina ya Dimethoate.
-         Tumia mbinu husishi.

Tahadhari
-         Wakulima ambao mashamba yao yanapakana wanashauriwa kufanya zoezi la kudhibiti kwa pamoja ili kuzuia uwezekano wa wadudu hao kuhamia shamba linguine ambalo hatua za kmdhibiti hazijachukuliwa.
-         Wadudu wengine wanaweza kuzuiwa kwa kunyunyizia dawa aina ya Selectron au Sevin. Dawa zinyunyiziwe wakati miembe imetoa maua. Kwa ushauri zaidi muone mtaalam wa kilimo.

Uvunaji wa maembe
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, miembe ambayo haikubebeshwa huanza kuzaa inapofikia umri wa miaka sita hadi saba tangu kupanda mbegu. Lakini ile iliyobebeshwa huzaa inapofikia umri wa miaka miwili mpaka mitatu tangu kupandikiza miche.
Uvunaji wa maembe hutegemea matumizi yaliyokusudiwa. Mfano, maembe kwa ajili ya matumizi ya nyumbani huvunwa baada ya kkuanza kubadilika rangi kutoka kijani kibichi na kuwa njano. Maembe kwa ajili ya kusafirisha huvunwa yangali bado na rangi ya kijani kibichi lakini yamekomaa.
Njia bora ya kuvuna maembe ni kuchuma kwa mikono ambapo matunda huchumwa pamoja na vikonyo vyake. Acha kikonyo chenye urefu wa sentimeta tatu hadi nne ili kuzuia utomvu. Utomvu huchafua matunda na hushusha ubora wake. Embe lililovunwa bila kikonyo huingiliwa na vimelea vya magonjwa kwa urahisi.
Vuna maembe wakati wa asubuhi au jioni ili kuepuka jua kali linaloweza kuharibu matunda. Wakati wa kuvuna hakikisha maembe hayadondoshwi chini ili kuepuka uharibifu.
Mavuno hutegemea aina na umri wa mti. Mti wenye umri mdogo unaweza kuzaa wastani wa matunda 4000 hadi 600 kwa msimu. Mti mkubwa unaweza kuzaa matunda 10,000 na zaidi. Wastani wa mavuno ni tan inane kwa hekta moja.