- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Kijana Jacob Louis 'Kaparata' (38) akimwelekeza mmiliki wa blogu ya Taifa Kwanza! jinsi alivyolitengeneza gari lake la kifahari aina ya 'Kaparata' kwa kipindi cha miezi mitatu tu.
Jacob Louis 'Kaparata' akiingia kwenye gari lake alilolitengeneza mwenyewe kwa miezi mitatu.
Wananchi wakipigana vikumbo kulishangaa gari la 'Kaparata' katika viwanja vya maonyesho ya Biashara ya Kimataifa (Saba Saba) jijini Dar es Salaam.
Na Daniel Mbega
SIYO Jeep la Mmarekani wala Korando la Mkorea. Hili ni gari
aina ya Kaparata ambalo limebuniwa na kutengenezwa na kijana Mtanzania, Jacob
Louis ‘Kaparata’ (38), mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam ambaye
ametumia vifaa vingi vinavyopatikana hapa hapa nchini.
Waliobahatika kuliona gari hili katika Maonyesho ya Biashara
ya Kimataifa – Saba Saba wamekiri kwamba huu ni ubunifu mkubwa ambao unastahili
kuungwa mkono na serikali na mamlaka nyingine.
“Nimetumia vifaa vingi vinavyopatikana hapa nchini. Chassis
nimeitengeneza kwa kutumia square pipe, bodi nimelisuka kwa kutumia brake pipes
zinazotumika kutengenezea vitanda na nikatumia mabati ya gauge 18 ambayo
yanatumika kutengenezea mageti,” anafafanua Kaparata.
Anaongeza: “Nilipomaliza kutengeneza chassis nikaenda kununua
injini, diff, gear box na matairi, ambavyo vyote ni vya gari aina ya Suzuki
Carry. Unajua Suzuki Carry ni fupi ina futi 10, lakini nilichokifanya ni kuongeza
chassis hadi futi 12. Injini ina nguvu sana ila kigari kile kimenyimwa bodi.
Sasa gari yangu hii imeonekana kuwa na nguvu, ina kasi.”
Kaparata anasema kwamba, gari yake ina muundo wa kipekee
tofauti na gari lolote duniani na ameitengeneza kwa kipindi cha miezi mitatu tu
kabla ya maonyesho ya mwaka huu ya Saba Saba ambapo limemgharimu kiasi cha Shs.
12,850,000.
“Nilipokuwa mdogo nilikuwa mtundu sana nikitengeneza magari na
vitu mbalimbali kwa kuiga nilivyoviona, ndipo watoto wenzangu wakanipachika
jina la ‘Kaparata’, ambalo nimelizowea na kuamua kuiita kampuni yangu kwa jina
hilo.
“Tangu mdogo nilipenda kuangalia filamu na nilivutiwa na gari
moja nililoliona kwenye filamu ya Delta Force ya Chuck Norris (The Flyer 72
Advanced Light Strike Vehicle) nikaapa kwamba lazima nije nitengeneze gari la
aina hiyo,” anasema Kaparata.
Hata hivyo, anasema kwamba, alitumia muda wa wiki mbili
kutengeneza chassis ambayo alihakikisha inanyooka na kukaa sawa kabla ya
kuendelea na utundu mwingine.
“Hivi sasa nikitembea na gari yangu, hata kama tumeongozana na
magari mengine ya kifahari, watu wataitazama gari yangu mitaani na wamevutiwa
nayo huku wengine wakinitaka nitengeneze mengine niyauze,” anasema.
Anasema wakati anaanza kuitengeneza gari hiyo vifaa pekee
alivyokuwa navyo ni drill machine, grander na welding machine – vifaa vitatu
tu, ambapo mabati na vifaa vingine alivinunua.
Kwa kuwa yeye si fundi mchundo, mabati na vifaa vingine
aliyapeleka kwa mafundi mchundo ambao walimkunjia kwa muundo na vipimo
alivyovitaka yeye.
“Lakini nimeingia hasara kubwa kwa sababu wakati mwingine
unampelekea mtu akukunjie bomba au bati, lakini anakosea, inabidi kulitupa na
kutafuta jingine.
“Nilipokuwa nayabeba mabati kupeleka kwenye viwanda kwa ajili
ya kukunja wengi waliniona kama mwendawazimu, wengine wakanikatisha tamaa na
kusema magari wanatengeneza Wazungu miye Mswahili maskini wapi na wapi!”
anasema.
Hata hivyo, anamshukuru mkewe Elizabeth William aliyemzalia
watoto Beatrice (14), William (10) na Neema (2) ambaye alikuwa akimtia moyo
kila wakati aendelee na ubunifu wake.
“Unajua hata kule kwenye viwanda nilikokuwa napeleka
hawakuamini, kwa sababu nilipoyabeba mabati wengine walidhani nakwenda
kutengeneza ndoo, lakini baada ya mabati hayo kukunjwa kama nilivyotaka, wote
walishangaa,” anasema.
Ukilitazama gari hilo kwa mbali unaweza kudhani ni aina mpya
ya Jeep ingawa muundo ni tofauti kabisa, na kama utalikaribia utashangaa kuona
vikorombwezo vingi.
“Hiki kioo cha mbele ni cha Land Cruiser ila nimekata mashavu
ya pembeni. Indicator ni za Bajaj aina ya TVS, shoo ni za vifaa mbalimbali vya
magari. Nimeweka vent kama za Ranger za kuingizia hewa kwenye air cleaner na
mengine kibao,” anasema.
Kaparata anasema kwamba, ubunifu ni gharama kubwa, lakini
mahali alipofikia kwa sasa anajiona kama ni mhandisi aliyebobea ingawa kikwazo
ni mtaji pamoja na kutambulika na mamlaka zinazohusika.
“Mheshimiwa Rais Magufuli amesema anataka kuona Tanzania yenye
viwanda ambayo ndiyo nia pekee ya kutengeneza aira kwa sisi vijana, sasa mimi
nimeamua kuanza bila kupata msaada wa mtu yeyote mpaka nimekamilisha,
ninachokihitaji kwa sasa kwanza ni kutambuliwa na serikali kwa ubunifu wangu,
halafu niweze kupatiwa mtaji na mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi.
“Kama leo nitaamua kutengeneza gari nyingine kama hii,
ninaamini ndani ya mwezi mmoja nitakuwa nimeitengeneza na itakuwa bora kuliko
hii kwa sababu nimejifunza makossa yote wakati nahangaika na hii hapa,”
anaongeza.
Gari la kifahari la Kaparata limeacha gumzo kwa wageni
wanaoshiriki na wanaotembelea maonyesho ya biashara ya kimataifa – Saba Saba,
hususan Banda la SIDO.
“Kwani linauzwa kiasi gani? Hili linafaa sana kwenda nalo
shamba,” alisema mwananchi mmoja. Mwingine akasema: “Hili ni zuri kama gari
aina ya Jeep, la kutokea na familia kwenda kupunga upepo.”
Naam. Walikuwa ni wananchi waliotembelea Banda la SIDO
alikoliegesha gari hilo kwa maonyesho pamoja na bidhaa zake nyingine, kwa kuwa
yeye ni miongoni mwa vijana wanaonufaika na fursa za Shirika hilo la Viwanda
Vidogo ambalo linawakusanya wajasiriamali na wabunifu pamoja ili kuonyesha kazi
zao.
Yeye anafanyia shughuli zake katika eneo la SIDO Vingunguti na
hata gari hilo ndiko lilikotengenezewa.
“Sikubahatika kusoma hata darasa moja kutokana na matatizo ya
kifamilia, huu ni utundu wangu ambao nimekuwa nao tangu nikiwa mdogo. Nilianza
kutengeneza magari ya kuchezea kwa kutumia mabati, lakini daima ndoto zangu
zilikuwa kutengeneza gari langu mwenyewe, nashukuru Mungu ndoto hizo
zimetimia,” anasema Jacob ambaye alizaliwa Mpanda mkoani Katavi kabla ya
kuhamia Kigoma ambako baba yake Mzee Louis Jacob alikuwa dereva katika Mamlaka
ya Pamba.
Akiwa mtoto wa saba kati ya watoto nane, Jacob anasema kwamba
ni wawili tu kati yao waliowahi kuingia katika vyumba vya madarasa ambao ni
dada yake wa pili kuzaliwa ambaye aliishia darasa la nne na kaka yake wa tatu
kuzaliwa aliyemaliza darasa la saba.
Anasema, baada ya wazazi wao kutengana mwaka 1993, mama yao
aliamua kuwachukua yeye na ndugu zake na kurudi Mpanda ambako maisha
yaliendelea kuwa magumu mno.
“Elimu ya zamani, hasa ya darasa la sababu, haikuweza
kumfikisha popote hata yule kaka yangu, kwa hiyo tulijikita katika shughuli za
shamba tu,” anaeleza.
Hata hivyo, anasema kwamba licha ya kutoingia darasani, hivi
sasa anajua kusoma baada ya kufundishwa kusoma a, e, i, o, u na mpwawe Sarah
William mwaka 1993 na yeye akaziunganisha herufi hizo.
Kaparata anasema kwamba, mpaka anakamilisha kutengeneza gari
lake hakuchukua hata senti tano ya mtu bali ni fedha zake mwenyewe kutoka
katika vyanzo vingine.
Anasema kwamba, wengi walimcheka na kusema kama anazo fedha za
kuchezea bora akawape maskini kwa vile asingeweza kufanikiwa kutengeneza gari,
lakini kwa kuwa alikuwa na ndoto zake akaamua kuyapuuza maneno yao na kukwangua
kila akiba aliyokuwa nayo kutimiza hayo malengo.
“Mimi ninafanyia kazi zangu pale SIDO Vingunguti, zaidi
natengeneza mashine za kutotolesha vifaranga ambazo kidogo kidogo ndizo
zinazoniingizia fedha, hivyo hata fedha za kutengenezea gari hili zimetokana na
kazi hizo,” anasema.
Anaongeza kwamba, licha ya kutokusoma, lakini utundu na
ubunifu wake vinamwezesha kuendesha maisha yake na amekuwa tegemeo kubwa kwa
ndugu zake wote.
Amewaasa vijana wengine waliosoma na hawana ajira pamoja na
wale ambao hawakubahatika kupata elimu kutokukata tamaa, bali wanaweza kutumia
vipaji na nguvu walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu kufanya maendeleo.
Comments
Post a Comment