Featured Post

WABEMBE: WATU WA ENEO LENYE MAKABILA MENGI

Bango linaloonyesha tamasha la sanaa za Wabembe lililofanyika kwama 2017 huko Marekani

Na Innocent Nganyagwa

NDUGU zangu, karibuni kwenye safu yetu ya kijadi inayoangalia Asili na Fasili yetu, inayotufanya tujivunie ujadi wetu wenye asili ya Kiafrika.
Baada ya kutoka kwa Wairaqw, sasa tunatua mkoani Kigoma, tunapiga hodi kwa ndugu zetu Wabembe, ambao kwa asili wanatokea kwenye eneo lenye msongamano wa makabila.

Kabla hatujaanza kuwatembelea ndugu zetu hawa, nikufahamishe tena dira ya ramani yetu.
Tukitoka kwa Wabembe tutapiga hodi kwa Waha, ambao watafuatiwa na Wakimbu, lakini hadi kuwafikia hao Wakimbu, tutakuwa tumeshaanza mwendo wa taratibu kuelekea tena kaskazini mashariki, tukipitia eneo la katikati mwa nchi yetu.
Katika njia hiyo tutakayopitia, kuna ziara za kuyatembelea makabila ya Wanyisanzu, Wanyiramba, Warangi na Wasi.
Safu hii ni kwa ajili yetu sote, hivyo basi unapowasilisha ombi la kutembelewa kabila lako kimakala, huwa nalijumuisha kwenye orodha ya maombi ninayoyapokea awali.
Nikufahamishe kuwa, nilianza kupokea maombi siku nyingi sana zilizopita, kiasi kwamba kuna muda yalikuwa mengi mno, ikabidi nisitishe kwa muda kupokea maombi hayo. Nilifanya hivyo, ili nipate nafasi ya kupunguza mzigo mkubwa wa maombi niliokuwa nao.
Lakini, kuna ombi moja kwenu ndugu zangu, nawasihi mfuatilie kwa karibu ziara zetu na kusoma kwa makini uchambuzi wetu.
Ndugu zetu hawa Wabembe wanaoongea lugha yao ya Kibembe ambao wakati mwingine jina lao hutamkwa ‘Wabeembe’, wanapatikana mkoani Kigoma, huko wapo zaidi kwenye Wilaya ya Kigoma Vijijini.
Ndugu zetu hawa wanawiana na idadi kadhaa ya makabila. Wanatangamana na Wamanyema, Wabangubangu, Wagenya, Wagoma, Wakusu, Warege, Wahoholo, Wambwari nakadhalika.
Lakini hawa ndugu zetu Wabembe huko wanakotokea, wanatangamana na makabila mengi mno kuliko unavyoweza kufikiria.
Takwimu za mwisho za idadi ya makabila hapa nchini, ziliainisha kuwa tuna makabila yapatayo 120. Lakini, tarakimu hizo za makabila zinatatanisha kutokana na ukweli kwamba kuna makabila yaliyopoteza utambulisho kwa kumezwa na mengine, yapo pia yanayojitambulisha kwa majina ya makabila mengine yakiwa mbali na maeneo yao ya asili.
Yapo pia makabila yanayopotea kutokana na mbari kuingiliana, au makabila ya ‘mbari’ tofauti yanayochanganyika na kuzalisha jamii nyingine ya watu, ambao huamua kujitambua kama kabila.
Pia usisahau makabila yaliyotengwa au kujitenga na makabila yao ya asili, kwa namna hiyo si rahisi kuwa na idadi ya makabila 120 tu hapa nchini.
Pengine inabidi tufanye kazi ya ziada kuanza kuorodhesha makabila yetu, kazi ambayo tukiianza hatujui tutaimaliza lini, hiyo ni kama tukiamua kufanya hivyo.
Maana ya kukueleza yote hayo ni kwamba, kuna makabila ya maeneo ya pembezoni mwa mipaka ya nchi yetu yanayotokea nchi jirani. Makabila mengine yamesababishwa yaonekane yanatokea nchi jirani, kutokana na mgawanyiko uliosababishwa na mipaka iliyochorwa na wakoloni.
Mipaka ya kijadi ni ile ya himaya za kichifu za makabila mbalimbali, kwa maeneo yao husika waliyoyatumia kuendeshea maisha yao ya kila siku.
Basi hawa Wabembe nao wana hali kama hiyo, kwa asili wanatokea huko Kongo, ndiyo maana wanapatikana zaidi kule Kigoma.
Kama unaifahamu vyema jiografia kwa jinsi ramani ya nchi yetu ilivyo, sina shaka unanielewa nikikutaarifu hivyo.
Hata baadhi ya makabila mengine yanayowiana nao kwenye maeneo waliyopo, yanatokea huko, mfano mzuri ni Wamanyema, Wahoholo na Warege.
Huko wanakotokea, Wabembe ni kundi dogo, yaani si kabila kubwa kulinganisha na makabila mengine ya Kongo.
Najua utakuwa unajiuliza mbona nataja Kongo tu bila kuainisha ni Kongo ipi kati ya zile mbili? Ile ambayo ni Jamhuri ya Kongo au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo wakati wa Mobutu iliitwa Zaire?
Wabembe wanapatikana kwenye Kongo zote mbili, ile yenye mji wake mkuu Brazzaville na ile yenye mji mkuu wa Kinshasa, ambazo hapo zamani zilikuwa himaya moja.
Wabembe waliishi kwenye uwanda ulio kaskazini mwa Mto Zaire, ambapo majirani zao walikuwa Wateke na makabila mengine.
Ndugu zetu hawa wenye utajiri mkubwa wa utamaduni, hasa wa uchongaji, kama tutakavyoona hapo baadaye, huko walikotoka kuna makabila mengi kwa kweli kulinganisha na hapa kwetu.
Inasemakana Kongo ya DRC ambayo ni kubwa kwa eneo, ina makabila makubwa na madogo yanayokaribia 420 kwa idadi.
Nikutajie baadhi tu ya makabila ya huko Kongo (ya Brazaville) kuna makabila kama vile ya Wateke, ambao ni majirani wa Wabembe. Makabila mengine ni pamoja na Wababochi, Wakuyu, Wakongo, Wakwele, Wavili, Wamboshi, Wasanga na Wasundi.
Inavyoelekea, katika ule mgawanyiko uliozalisha nchi mbili za Kongo, DRC ilibakiwa na makabila mengi zaidi. Huko kuna makabila ya Wayaka, Walar, Wapakibeti, Wazande, Wabaali, Wababyeru, Wakongo, Wabakuba, Wabushongo, Wambuti, Walega, Wali, Walwalwa, Wambole, Wangba, Wango, Wapende, Warambo, Warambu, Wasala, Wasalampasu, Wasongye, Wasuku na Wateke wapo huko pia.
Makabila mengine ni Wati, Watsioko, Watchokwe, Wabeke, Wabemba, Wabena Wiembe, Wabena Luluwa, Wawila, Wawinja, Wawinza ambao moja ya jamii zake tanzu ilizalisha Wasukuma na Wanyamwezi waliopo hapa nchini.
Wawira, Waboa, Wabobangi, Wabodo, Waboenga, Wabolia, Waboloki, Wabombo, Wabopgandi, Waboyela, Wabua, Wabudu, Wabuja, Washongo, Wawuyu, Wawaka, Wayeru.
Hayajaisha, pia kuna Wandengese, Wadongo, Wakonda, Wagenya, Wagoma, Wagyeli, Wahamba, Wahemba, Wahoholo, Wahungana, Wahutu, Wajonaam, Wakanu, Wakela, Wakomo, Wakusu, Wakwame, Waleka, Waleku, Walengola na Walese.
Mengine ni Walibinza, Walikao, Waliko, Walobala, Walobo, Waloi, Walokele, Walombi, Walombo, Walomotwa, Waluba, Waluba Upemba, Walunda na Wamakere.
Pia kuna Wamalele, Wamamvu, Wamangbetu, Wamanja, Wamayogo, Wamayombe, Wammba, Wambanja, Wambesa, Wambo, Wambole, Wambuti, Wamedje, Wamituku, Wamondunga, Wamongo, Wamotembo na Wamuserongo.
Kwa kumalizia baadhi ya makabila hayo, maana tukitaka kuyataja yote tutaishia kutaja makabila tu kutokana na idadi yake, ni Wamvuba, Wanalu, Wanande, Wandaaka, Wandaka, Wandengese, Wandolo na Wangala. Pia kuna Wangombe, Wakundo, Wankutu, Wantomba, Wanyali, Wanyanga, Wanyindu, Waotetela, Wapere, Wapopoi, Washi na Wasonge.
Mengine ni Wasongola, Wasundi, Watabwa, Watembo, Watopoke, Watumbwe, Watutsi, Wagoma-Babuye, Wawongo, Wawoyo, Wayaka, Wayombe, Wazande, Wazimba na Wazombo.
Nadhani mnaona jinsi huko walikotokea ndugu zetu hawa, kulivyojazana makabila mengi. Wabembe ambao utamaduni wao umegubikwa na mambo ya maeneo yao ya asili, pamoja na majirani zao waliowiana nao, mfumo wao wa kijamii umeelemea uzao wa ndoa.
Hata kama watu wa familia moja watatawanyikia maeneo ya mbali, lakini utambulisho wao waliouhifadhi huwawezesha kutambuana hata kwa vizazi vitatu kabla au baada.
Vijiji vya makazi yao vinasimamiwa kwa uongozi wa machifu, ambapo chifu husika ‘ngaluba’ ana jukumu la kuwasiliana na mizimu kwa kuwa wanaamini katika mizimu.
Uwindaji ndiyo shughuli yao kuu, kwa kawaida kabla ya kwenda mawindoni, kiongozi wao huwasiliana na mizimu. Hutumia vinyago vilivyochongwa mahsusi, akipiga magoti mbele yake kama mwindaji anayejitayarisha kumuangamiza mnyama mawindoni.
Licha ya kuamini mizimu, Wabembe pia wanaamini kuwa kuna Mungu muumba ‘Nzambi’ ambaye kutokana na ukuu wake na uwezo alionao, hawakuweka kitu chochote kukifananisha naye. Mjadi mwenzangu, tumeshawahi kuona huko nyuma, kuna makabila ambayo yana alama yanayozichukulia kama taswira ya Mungu.
Alama hizo ni kama jua nakadhalika, lakini hawa Wabembe hawakujiwekea alama yoyote ya kitaswira kutokana na imani yao juu ya ukuu wa Mungu. Kwao, Nzambi, yaani Mungu, ndiye anayedhibiti maisha na kifo, japo wanaamini pia kuwa kifo kinaweza kutokana na ulozi wa mchawi ‘ndoki’ ambaye anaweza kutumia ushirikina wake kuroga.
Wao huamini kuwa, mizimu ya mababu zao inahusiana kwa karibu na watu walio hai, huwatolea mizimu hao sadaka.
Hufanya ibada zinazoongozwa na kuhani, ambaye hutimiza ibada hizo mbele ya vinyago vinavyoitwa ‘kitebi’ au ‘bimbi’ vilivyochongwa na waganga.
Vinyago hivyo ambavyo huwakilisha taswira za mizimu, huvishwa kama waganga au wawindaji.
Kusujudu mbele ya vinyago vya mizimu ya mababu ni jambo walilolianza siku nyingi kwenye kabila lao.
Japokuwa hapo zamani mambo hayo yalianzishwa na waganga, waliotumia ‘nkisi’ yaani vinyago vyao vya kupigia ramli.
Tumeshapiga hodi kwa Wabembe na tumeshaanza kuona mambo yao.
Tukutane kesho.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Novemba 29, 2008.

Comments