Featured Post

BABA GASTON MKALI WA KAKOELE VIVA CHRISTMAS


Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
KILA mwaka katika kipindi kama hiki cha Majirio, yaani kuelekea siku ya kuzaliwa Yesu Kristo (Krismas), kote duniani huwa kuna furaha kubwa mitaani na makanisani, majumba yakiwa yamepambwa kwa miti ya Krismas inayonukia, maua na vikorombwezo anuai kuikaribisha siku hiyo muhimu kwa wanadamu wote.

Zawadi mbalimbali huandaliwa kwa ajili ya kuwapatia ndugu na jamaa, Father Christmas naye akiwaandalia watoto zawadi, huku muziki mwororo ukitawala anga zote kupitia kwenye redio au televisheni.
Ni wakati huu ambapo muziki unaotawala huwa ni wa yule mkongwe wa muziki laini, marehemu Jim Reeves wa Marekani, ambaye vibao vyake 12 kikiwemo cha Jingle Bells pamoja na kundi la Boney M vibao vyao vinatamba duniani kote ikiwa ni pamoja na hapa Tanzania, ambako pia hukolezwa na kibao cha Komandoo Hamza Kalala kisemacho Noel-Krimas.
Lakini mbali na vibao hivyo, kwa ukanda mzima wa Afrika kibao ambacho hutamba zaidi na kuchukua chati ya juu ni kile kinachojulikana kama Kakoele, ama Viva Christmas au Noel Krismas, kwa vyovyote utakavyokiita.
Blogu ya MaendeleoVijijini kwa kuwatakia heri na baraka za kusherehekea sikukuu hiyo ya Krismas pamoja na Mwaka Mpya, kwa nia njema kabisa, leo tumeamua kuwaletea kibao hicho ambacho kimeimbwa kwa lugha ya Kilingala.
Wimbo huo umetungwa na kuimbwa na Baba Gaston Ilunga wa Ilunga, mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (zamani ikiitwa Zaire) ambaye alikuwa maarufu katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.
Kibao hicho kilichomo kwenye albamu yake ijulikanayo kwa majina niliyoyasema hapo juu kilifyatuliwa takriban miaka 40 iliyopita nchini Kenya, lakini bado kinaendelea kutamba na kitaendelea kutamba kwa mashabiki na wafuasi wote wa dini ya Kikristo kutokana na ujumbe uliomo ndani.
Wimbo huo unaosikika kila ikaribiapo sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya uliweza kumjengea jina na sifa kubwa mkongwe huyo ingawa hakuwa mashuhuri kama walivyokuwa akina Joseph Kabasele 'Le Grand Kalle', Dk. Nico, Franco na wengineo kutoka Zaire.
Aliifyatua albamu hiyo kwa ajili ya nyimbo za Krismas tu kama alivyofanya Jimmy Reeves, ambapo ina jumla ya nyimbo tano ukiwemo huo wa Kakoele au Krismas. Nyingine ni Nakumbuka Krismas, Bewela Krismas, Super Krismas na Topele Krismas.
Kakoele anayeimbwa na Baba Gaston ni msichana wa kileo, yaani 'Sister Duu', mkorofi na mchoyo wa mapenzi, lakini ni mzuri ajabu. Baba Gaston kwa kuwa anafahamu Krismas ni siku ya kuzaliwa Masihi aliyekuja kufundisha pendo la kweli kwa wanadamu wote, anamwendea Kakoele siku hiyo hiyo kumkumbusha kwamba Krismas ni siku ya 'Mfalme wa Pendo' (Yesu Kristo).
Kwa hiyo anamtaka ajaribu kujivua uchoyo wake na kuwa mkarimu siku hiyo kisha amwonyeshe angalau pendo linalotakiwa kwa binadamu badala ya lile la 'Chuna Buzi'.
Hali kadhalika, katika ushauri huo kwa Kakoele, anatukumbusha wanadamu wote kuwa tunawajibika wakati huu kushinda udhaifu wetu na kudhihirisha pendo la kweli ambalo limeletwa na Bwana Yesu Kristo.
Ni kibao kilichopambwa na maneno ya kumweleza muhibu wako, lakini kikiwa kimelenga hasa kuwataka wanadamu wote wapendane kama lilivyokuwa kusudi la Bwana Yesu, ambaye wanadamu wote tunaamini kwamba hata wakati anapaa aliwaambia wanafunzi wake kuwa, Wapendane, kama Mungu alivyowapenda wanadamu na kumtuma Yeye ili auokoe ulimwengu na vilivyomo!

Kuzaliwa
Baba Gaston alizaliwa Julai 5, 1936 katika mji mdogo wa Likasi, karibu na Lubumbashi katika Jimbo la Shaba kusini-mashariki mwa Zaire na kujipatia elimu yake ya msingi katika shule ya St. Gabriel, Kapolowe katika Jimbo la Shaba na baadaye akafanikiwa kuendelea na masomo ya juu katika shule ya Benedict Catholic Fathers ya mjini Likasi.
Alibadili jina na kujiita Ilunga Chenji Kamanda wa Kamanda Gaston Omer baada ya mtawala wa Zaire wa wakati huo, Mobutu Sese  Seko (Joseph Desire Mobutu) kuwataka Wazaire wote kubadili majina yao kutoka ya Ukristo na kuwa na majina ya Kibantu.
Alijitosa katika ulimwengu wa muziki akiwa na miaka 18 katika Jiji la Kinshasa kwa kuanza kuimba kwaya kanisani kabla ya kuingia kwenye muziki wa Jazz.
Hii ni baada ya kupata mafunzo ya awali ya muziki kutoka kwa mpiga piano maarufu wa Kigiriki, Leonides Rapitis, na akafanikiwa kutunga kibao cha "Barua kwa Mpenzi Gaston" wakati akiwa shule.
Mwaka 1956 akiwa na miaka 20 tu akaanzisha bendi yake ya Baba National Orchestre, ambapo alifanya ziara ndefu katika nchi za Zambia, Zimbabwe na baadhi ya nchi za Ulaya na kuwa miongoni mwa wanamuziki wa kwanza wa Congo kuweka maskani Afrika Mashariki mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Evani Kabila Kabanze, ambaye baadaye alikuja kuwa nyota wa Les Mangelepa, aliimba na bendi ya Orchestra Baba Nationale mjini Lubumbashi. Bendi hiyo ilikuwa na kawaida ya kusafiri kwenda Kinshasa kurekodi.
Mnamo mwaka 1971, kwa sababu ya ubovu wa barabara nchini Congo DR, waliamua kusafiri kwa njia ya Kisangani kupitia Kalemi mpakani mwa Congo na Tanzania. Lakini badala ya kwenda Kinshasa, wakaamua kuingia Afrika Mashariki, baada ya kusikia ubora wa studio zilizokuwepo huko.
Mwaka 1972 gwiji huyo alitua Dar es Salaam ambapo onyesho lake la kwanza lilikuwa katika ukumbi maarufu wakati huo wa White House, Kimara jijini Dar es Salaam, ambako pia ndiko kulikuwa maskani ya bendi ya Orchestra Marquiz du Zaire (OMACO).
Bendi hiyo ilikaa Dar es Salaam kwa miaka minne. Maisha yalikuwa rahisi sana na wakapata mashabiki wengi. Hata hivyo, walikuwa wanakwenda kurekodi Kenya katika Jiji la Nairobi.
Lakini mwaka 1975, Baba Gaston akiwa na mkewe na watoto wake kadhaa aliamua kuchanja mbuga na kwenda Kenya kuweka maskani baada ya kugundua kwamba walikuwa na mashabiki wengi zaidi, kabla ya kwenda Arusha alikozindua kibao chake kingine maarufu cha Talaka Mpakani Yanitoa Jasho na kuongeza raha pale alipozingua na kibao kingine cha Mapendo Kizunguzungu.
Wanamuziki wa Congo walikuwa wakifanya vizuri zaidi nchini Kenya tangu mwishoni mwa miaka ya 1950. Bendi ya OS Africa Band ndiyo iliyofungua njia kwa bendi za Congo kuteka anga la muziki la Kenya katika ukumbi maarufu wakati huo wa Starlight Club jijini Nairobi mwaka 1964. Lakini ilikuwa hadi katikati ya miaka ya 1970, baada ya zama za muziki wa soul wa Marekani kupita, ndipo muziki wa Zaire ulipoanza kutawala kwenye klabu za usiku za Nairobi.
Akiwa mtunzi na kiongozi wa bendi, Baba Gaston alikuwa maarufu katika tasnia ya muziki nchini Kenya kwa miongo mitatu, na hata leo hii anatajwa kwamba ni gwiji wa muziki wa pop wa Kenya.
Nyimbo zake nyingi aliimba Kiswahili na vibao vyake vilipata umaarufu mkubwa nab ado vinaendelea kutamba hhata sasa.
Kibao cha "Kakolele Viva Christmas" (ambacho mwimbaji mkuu ni Kasongo Wakanema ambaye baadaye alijiunga na Super Mazembe) kilimpatia tuzo ya dhahabu, kikiuza nakala 60,000 kupitia kampuni ya Polygram.
Nyimbo nyingine kali zilikuwa "Ilunga wa Ilunga," "Kai Kai," na "Mayasa." Mara chache sana aliimba kuhusu siasa, lakini bibao chake cha kumsifu Mobutu mwaka 1983 kilimpa tuzo ya dhahabu kutoka kwa rais huyo.
Kuna kipindi Baba Gaston alitamba kwamba aliimba na wanamuziki zaidi ya 700 kupitia bendi hiyo na kwamba bendi yake ilikuwa chuo cha muziki.
Hata hivyo, kama alivyosema Hanz Kinzl, meneja wa studio ya Phonogram, inaonekana bendi ya Baba Gaston ndiyo iliyoongoza kukimbiwa na wanamuziki nchini Kenya, sababu ikiwa kuwapunja posho wanamuziki wake.
Julai 1976 wanamuziki kadhaa wakiwemo Bwami Walumona, Kasongo Wakanema, Evani Kabila Kabanze (mwimbaji na mtunzi), Kalenga Nzaazi Vivi (mwimbaji na mtunzi), Lutulu Kaniki Macky, na Twikale wa Twikale walijiengua kwenye bendi ya Baba Nationale na kuanzisha bendi ya Orchestra Les Mangelepa.
Wanamuziki wengine walitoka kwenye bendi hiyo walianzisha bendi za Bwambe Bwambe, Pepelepe, na Viva Makale.
Majina maarufu ya wanamuziki waliopitia mikononi mwa Baba Gaston ni pamoja na Starzo ya Esta (ambaye ndiye aliyekuwa nguzo ya bendi ya Festival du Zaire), BadiBanga wa Tshilumba Kaikai (mwimbaji na mtunzi, baadaye alikwenda Les Mangelepa na kutunga kibao cha Nyako Konya), Mukala Kayinda Coco, Jimmy Kanyinda, Aloni Vangu, Mukala wa Mulumba Bebe, Zainabu, Pepe Mato, Yassa Bijouley (kwa sasa anaishi Mombasa, Kenya), Lisasi Ebale Mozindo, Zengele Saida, William Tambwe Lokassa, Kasongo Fundi, Kazadi Mbiya Saleh wa Bambu, Medico Bwala, Lukangika Maindusa Moustang, Lumwamga Mayombo Ambassedeur, Mukala wa Mulumba, na Tshimanga Zadios.
Mwimbaji wa kike aliyeimba na Gaston alikuwa Nana Akumu wa Kudu. Anakumbukwa pia kwa kuimba na bendi ya Pepelepe jijini Nairobi kabla ya kujiunga na Franco katika bendi ya TP OK Jazz na kushiriki kibao cha "Mamou" kilichoimbwa pia na Madilu System. Kwa sasa anaendelea kupiga muziki jijini Brussels, akiwa pamoja na mumewe Djo Mali na mpiga gitaa wa zamani wa bendi ya Les Noirs, Dieudos.
Wanamuziki wengine walliopitia kwenye bendi ya Baba Nationale ni Mtanzania John Ngereza (aliyeimbia Les Wanyika hadi alipofariki Februari 2000), Shoushou (Tchou Tchou), Lutulu Kaniki Macky (mwimbaji na mtunzi), Bosho Kayembe Nyonga (aliyeongoza bendi ya Festival Libaku jijini Nairobi hadi alipofariki), Tabu Nkotela Kiombwe (aliyefariki mjini Mombasa, Kenya, wakati akiwa mahabusu kwa kosa la wizi).
Baba Gaston aliachana na muziki mwaka 1989, lakini mwaka 1994 akiwa na familia yake alihamishia maskani yake mjini Arusha akitokea Nairobi, Kenya, ambapo alikuwa akitegemea zaidi biashara zake za duka la kuuza vyakula mbalimbali katika eneo la Majengo katika Barabara ya Sokoine.
Mwanamuziki huyo alifariki dunia Jumamosi Machi 18, 1997 katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo. Alifariki akiwa anakaribia kabisa kufikisha miaka 61 na Machi 25, 1997 akazikwa katika makaburi ya Lang’ata jijini Nairobi, Kenya.
Katika kibao hicho Baba Gaston amemwita Kakoele huku akitoa ushauri wake hivi:
1. Kako yeye ngai nakoloba likamboo
(Kakoele neno nitakalokwambia)
Yo bomba na motema nayo
(lihifadhi moyoni mwako)
Ezalaka makasi kokotana pamba boyee mama
(Ni vigumu kukutana hivi kwa matatizo mama)
Bongo sima nagoo bolingana aa
(Halafu baadaye waishi kwa upendo)
Mama lele bolingo motema pasii x2
(Mama ee pendo linaumiza moyo x2)

2. Lokola ngai nayebanisee, Kako ee mama
(Kwa kuwa mimi nafahamika sana, Kako ee mama)
Na basemeki na ngai
(Na mashemeji zangu)
Ebingi tolingana
(Tunapaswa tupendane)
Ezalaka makasi tokutana pamba boyee
(Ni vigumu tukutane (maishani) hivi kwa matatizo)
Bongo sima nayoo tolingana aa
(Halafu baadaye tuishi kwa upendo)
Mama lele bolingo motema pasii x2
(Mama ee pendo linaumiza moyo x2)

Kiitikio:
Kakoele mama Kakoele x2
(Kakoele mama Kakoele x2)
Kakoele mama Kakoele, Papy akolela
(Kakoele mama Kakoele, Papy analia)
Mama yoka kooo
(Mama hebu sikia)
Kakoele mama elingi yaye
(Kakoele mama anataka pendo lako)
Papy akolela, yoka mama
(Papy analia, sikia mama)
Kakoele mama Kakoele
Viva Krismas x2
(Kakoele mama Kakoele,
Idumu Krismas x2)
Noeli mama Yesu abotami - tolingana
(Ni Krismas mama, Yesu amezaliwa - nasi tupendane)
Viva Krismas x2 Yesu abotami
(Idumu Krismas x2 Yesu amezaliwa)
Kakoele mama Kakoele x3
Yoka ko! Yoka ko!
(Kakoele mama Kakoele x3
Sikiliza! Hebu sikia!).

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com Simu: +255 656 331974.

Comments