Featured Post

BADIBANGA WA TSHILUMBA ‘KAI KAI’ NDIYE MTUNZI WA KIBAO CHA NYAKO KONYA


Na Daniel Mbega
Badibanga wa Tshilumba ‘Kai Kai’ (alizaliwa mwaka 1946, Mbuji Mayi, Mashariki wa Congo) alikuwa mwanamuziki wa Congo aliyepitia katika bendi nyingi akiwa mtunzi, mwimbaji na mpiga tumba, tarumbeta na trombone.

Maisha yake ya awali
Mwaka 1966 alijiunga na Jeshi la Congo (ANC) ambako alijiunga na bendi ya jeshi hilo akiwa anapiga tarumbeta na trombone.
Mnamo mwaka 1968 alijitoa kwenye jeshi na kujiunga na Orchestra Lupa Jazz iliyokuwa na maskani yake mjini Lubumbashi, wakati huo ukijulikana kama Elisabethville ambako alitunga nyimbo kama Tatu Kalonji na Tikela Ngay ye.

Katika mwaka 1970 aliyekuwa anapiga muziki wa Congo nchini Zambia alimwita Kai Kai aende Zambia na kujiunga na Orchestra Micky Jazz iliyokuwa ikitumbuiza kwenye ukumbi wa La Gondola jijini Lusaka.
Mwaka 1972 bendi ya Micky Jazz ilikwenda kwa ziara jijini Dar es Salaam, ambako Ndala Kasheba alimuona Kai Kai na kumtaka ajiunge na bendi yao ya Fauvette Jazz. Ndala Kasheba na Micky Kalonda walikuwa anafahamiana tangu wakiwa mjini Likasi, mji ambao wakati huo uliitwa Jadotville. 
Baadaye akajiunga na bendi ya Baba Nationale iliyokuwa chini ya Baba Gaston ambayo ilikuwa inakusudia kufanya ziara nje ya Congo. 
Kai Kai alikuwa mmoja wa wanamuziki waliokuwa katika kundi la Baba Gaston Ilunga wa Ilunga lililoondoka Congo na kwenda Afrika Mashariki kutafuta maisha, na walipokewa vyema Dar es Salaam na bendi hiyo kurekodi nyimbo kadhaa katika studio ya TFC.
Hatimaye kundi hili lilihamia Nairobi na kuwa likifanya maonyesho Park Restaurant iliyoko Uhuru Park, na hapo ndipo walipokuja na kibao Kakoele Viva Christmas ambamo Kanema wa Kanema anasikika akilalamika kwenye wimbo huo maarufu.
Wakati Baba Gaston anamchukua kwa Ndala Kasheba alimuahidi kwamba angempatia Dola 100 ndipo wakaondoka kwenda Dar es Salaam. 
Lakini mpaka walipofika Nairobi, Baba Gaston hakuwa amemlipa hiyo fedha, hivyo Kai Kai na Nana Akumu wa Kudu (mwanamuziki aliyeitikia katika wimbo wa Mamou wa T.P. O.K. Jazz), Kalenga Nzaazi ‘Vivi’, Coco Mukala na wengineo wakamkimbia Baba Gaston na kuunda kundi la Mangelepa lililojaa wanamuziki Wacongo watupu.
Mwaka 1976 baada ya kuondoka katika bendi ya Baba National akiwa na Soliste Bwami Walumona Capitaine, Kasongongo wa Kanema, Evani Kabila Kabanze (mpwa wa Rais wa zamani wa Congo hayati Laurent Kabila), Kalenga ‘Vivi’ Nzaazi, Lutulu, Kaniki Macky, Twikale wa Twikale wakaanzisha bendi ya Les Mangelepa ambapo Kai Kai aliibuka na nyimbo za Walter, na Bibi.
Umaarufu wa Les Mangelepa ulifanya vikundi vingi vya wanamuziki wa Congo kuhamia Nairobi, hivyo kukaweko na makundi kama Les Kinois, Super Mazembe, na Viva Makale, Shika Shika na mengine mengi na kufanya biashara kuwa ya mashindano magumu ya kimuziki, ukichukulia pia kulikuwa na bendi kama Simba wa Nyika, Les Wanyika, na bendi za Wakenya kama Maroon Commandoes, Kilimambogo Boys na kadhalika.
Kati ya mwaka 1985 na 1986, bendi hiyo ilifanya ziara katika nchi za Djibouti, Malawi, Zambia na wakiwa huko wakapata matatizo na bendi ikasambaratika. Kai kai alibakia nchini Zambia kwa muda kabla ya kuhamia Afrika Kusini, wakati wanamuziki wengine wakarejea Nairobi baadhi yao wakajiunga na bendi ya Cheers Boys iliyoutwa na Wacongo ikiwa katika mji wa Kitwe.
Kai Kai ndiye aliyetunga wimbo maarufu wa Nyako Konya wa Orchestra Les Mangelepa, bendi iliyotingisha anga la muziki la Afrika Mashariki na Kati enzi hizo ikitamba pia na vibao maarufu kama Embakassy, Walter, Maindusa.

Mauti
Badibanga Wa Tshilumba Kai Kai alifariki Jumatatu, Februari 2, 2015 nchini Afrika Kusini na akazikwa Johannesburg Februari 7, 2015 na kuzikwa.


Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Ukinakili tafadhali taja chanzo hiki.

Comments