Featured Post

MKATABA WA KILAGHAI WA KARL PETERS NA CHIFU MANGUNGO WA USAGARA MWAKA 1884 HUU HAPA!



 Dk. Karl Peters (kati) akiwa na wenzake Dk. Karl Juhlke na Joachim Graf.

Na Daniel Mbega
MIKATABA ya ulaghai! Ndivyo inavyoitwa. Naam, ni ile mikataba iliyofanywa kwa hila na Mjerumani Dk. Karl Peters dhidi ya watawala wa Kiafrika ambayo ndiyo ilikuwa mwanzo wa kuitishwa kwa Mkutano wa Kuligawa Bara la Afrika mwaka 1884-1885 kule Berlin na kuanza kwa ukoloni barani humu.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, mkutano huo ambao pia unafahamika kama Congo Conference ulifanyika siku ya Jumamosi, Novemba 15, 1884 katika makazi rasmi ya Chancellor Otto von Bismarck huko Wilhelmstrasse.

Mataifa 14 yaliyohusika na mkutano huo muhimu yalikuwa Muungano wa Austria-Hungary, Ubelgiji, Denmark, Ufaransa, Dola ya Ujerumani yenyewe, Italia, Uholanzi, Dola ya Ottoman (Uturuki ya sasa), Ureno, Russia, Hispania, Muungano wa Sweden-Norway, Uingereza na Marekani.
Bismarck alikubali kuwa mwenyekiti. Mwakilishi wa Uingereza alikuwa Sir Edward Malet (Balozi wa Uingereza katika Dola ya Ujerumani). Henry Morton Stanley alihudhuria kama mwakilishi wa Marekani.
Akitumia ‘ujinga’ wa watawala wetu wa jadi ambao hawakujua kusoma wala kuandika, achilia mbali kuijua lugha ya Kijerumani, Karl Peters alitumia hila na kuwasainisha mikataba ya kilaghai ambapo bila wenyewe kuelewa, walijikuta wakimkabidhi, kwa niaba ya Ujerumani, himaya zao zote na wao wakawa watawaliwa.
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, mkataba wa ulaghai ambao umekuwa ukipigiwa mfano zaidi nchini Tanzania ni ule wa Karl Peters na Chifu Mangungo wa Usagara huko Msowero, Wilaya ya Kilosa katika Mkoa wa Morogoro.
Vizawadi vidogo vidogo na hila nyingi, huku akitumia watumishi wake Waafrika ‘kutafsiri’ Kijerumani – ambacho pia hawakukijua – viliweza kumfanya Karl Peters amrubuni Chifu Mangungo aisalimishe himaya yake yote kwa Wajerumani bila kutambua.
Karl Peters, akiwa na miaka 28 tu wakati huo, na rafiki zake Dk. Karl Juhlke, Pfeil na August Otto waliondoka Ujerumani mwezi Septemba 1884. Walisafiri wakijifanya mafundi makenika huku wakitumia majina ya bandia hadi walipoingia Zanzibar ambako waliwasili Novemba 4, 1884. Baadaye wakavuka kuingia bara. Waliondoka Sadani mnamo Novemba 10 wakiwa na wapagazi 36.
Wakasafiri hadi Uzigua (ambako walimsainisha mkataba wa kwanza kabisa wa kilaghai Chifu Mbwela wa Wazigua) wakipitia Mto Wami hadi kuingia Uluguru, ambako kote walifanya mikataba ya ulaghai (bogus treaties) katika kila walikopitia. Chifu Mangungo wa Msowero katika Usagara mara nyingi ndiye anayetajwa kwenye mikataba hiyo ya kilaghai.
Mkataba wa ulaghai baina ya Karl Peters na Mangungo, ambao MaendeleoVijijini imeuona, unasomeka hivi kwa Kiingereza:
Mangungo, Sultan of Msovero in Mwenyisagara, and Dr. Karl Peters. Mangungo simultaneously for all his people and Dr. Peters for alt his present and future associates hereby concluded a treaty of Eternal Friendship.

Mangungo offers all his territory with all its civil appurtenances to Dr. Karl Peters, as the representative of the Society for German Colonization, for the exclusive and universal utilization for German colonization.

Dr. Karl Peters, in the name of the Society for German Colonization declares his willingness to take over the territory of the Sultan Mangungo with all rights for German Colonization subject to any existing suzerainty of Mwenyi Sagara.

In pursuance thereof, Sultan Mangungo hereby cedes all the territory of Msovero, belonging to him by inheritance or otherwise for all time, to Dr. Karl Peters, making over to him at the same time all his rights.

Dr. Karl Peters in the name of the Society for German Colonization undertakes to give special...attention to Msovero when colonizing Usagara.

This treaty has been communicated to the Sultan Mangungo by the interpreter Ramzan in a clear manner and has been signed by both sides, with the observation of the formalities valid in Usagara the Sultan on direct enquiry having declared that he was not in anyway dependent upon the Sultan of Zanzibar, and that he did not even know the existence of the latter.

Sgd. Dr. KARL PETERS
Sgd. MANGUNGO

This contract has been executed legally and made valid for all time before a great number of witnesses, we testify herewith:
Kwagakinga (mark);
Sultan Mangungo’s son of Golola (mark);
Sultan Mangungo’s second son of Draman (mark);
Graf Pfeil August Otto;
Mark of the intepreter Ramazan etc.
Dr. Karl Juhlke.
Msovero Usagara November 29, 1884.

Hii ni tafsiri isiyo rasmi ya MaendeleoVijijini:
Mangungo, Sultan wa Msovero katika Mwenyisagara, na Dk. Karl Peters. Mangungo sambamba na watu wake wote na Dk. Peters kwa niaba yake na washirika wake wengine wajao kwa pamoja wanaweka mkataba wa Urafiki wa Kudumu.

Mangungo amekubali kutoa himaya yake yote pamoja na watu wake na hadhi yake kwa Dk. Karl Peters, kama mwakilishi wa Umoja wa Ukoloni wa Kijerumani (Society for German Colonization), kwa ajili ya matumizi ya moja kwa moja koloni la Kijerumani.

Dk. Karl Peters, kwa niaba ya jina la Umoja wa Ukoloni wa Ujermani anatangaza dhamira yake ya kuitwaa himaya yote ya Sultan Mangungo na haki zote kwa ajili ya Koloni la Ujerumani inayohusisha kila kona na amali za Mwenyi Sagara.

Katika kutekeleza hilo, Sultan Mangungo anakabidhi himaya yote ya Msovero, inayomilikiwa nay eye mwenyewe kwa urithi au kwa namna yoyote ile kwa nyakati zote, kwa Dk. Karl Peters, na wakati huo huo kumkabidhi haki zake zote.

Dk. Karl Peters kwa niaba ya Umoja wa Ukoloni wa Kijerumani anakusudia kuweka mkazo maalum kwa eneo la Msovero wakati wa kuitawala Usagara.

Mkataba huu umewasilishwa kwa Sultan Mangungo na mkalimani Ramzan katika dhana ya wazi kabisa na umesainiwa na pande zote, kwa kuzingatia taratibu zilizopo katika Usagara, Sultan baada ya kuhojiwa moja kwa moja alikiri kwamba hakuwa na ushirika ama kutegemea kwa namna yoyote Sultan wa Zanzibar, na kwamba hakuwa hata akimfahamu.

Imesainiwa. Dk. KARL PETERS
Imesainiwa. MANGUNGO

Mkataba huu umefanyika kihalali kabisa na umehuishwa kwa nyakati zote mbele za mashahidi wengi, ambao tunakiri hapa:
Kwagakinga (dole gumba);
Golola mtoto wa Sultan Mangungo (dole gumba);
Draman mtoto wa pili wa Sultan Mangungo (dole gumba);
Graf Pfeil August Otto.
Dole gumba la mkalimani Ramazan etc.
Dk. Karl Juhlke.
Msovero Usagara Novemba 29, 1884.

Hii ndiyo ilikuwa aina ya mikataba ambayo Karl Peters aliisaini na watawala wa jadi. Ni ukweli ulio wazi kwamba Chifu Mangungo, na kwa kiongozi yeyote wa Kiafrika kwa maana hiyo, angeweza kuingia mkenge na kuiachia ardhi yake na mamlaka yake kwa mgeni laghai kama Karl Peters.
Ni dhahiri kwamba Mangungo hakujua kusoma wala kuandika Kijerumani. Inaonekana pia kupitia kwenye maelezo ya mkataba kwamba mkalimani mwenyewe hakujua kusoma wala kuandika kabisa. Kwa gharama yoyote ile, ikumbukwe kwamba Ramazan alikuwa ameajiriwa na Karl Peters na alitakiwa kufuata maelekezo yake.
Karl Peters aliwasili Ujerumani Februari 7, 1885 akiwa na lundo la mikataba. Peters alitumia mikataba hiyo kupata kibali maalum - Schutzbrief – ili kutambuliwa kwa madai yake Februari 27, 1885.
Kwa maneno mengine, Otto von Bismarck, Chancellor mkuu wa Ujerumani wakati huo, alikuwa amebadili sera yake ya awali dhidi ya Ujerumani katika kutafuta makoloni.

Imeandaliwa na MaendeleoVijijini

Comments