Featured Post

UJENZI NA SIFA ZA BANDA BORA LA MBUZI




Na Daniel Mbega
Mbuzi ni wanyama wavumilivu, wanaweza kufugwa katika mifumo ya huria (freerange), shadidi (zero grazing) na kwa kutumia njia zote mbili. Lakini mbuzi wanahitaji sehemu ambayo ni kavu kwa ajili ya kulala na kujikinga na mvua na jua, pamoja na eneo la kucheza, hususan kama unataka kupata maziwa bora.
Zizi hutumika katika mfumo huria ambapo mbuzi huchungwa wakati wa mchana na kurejeshwa zizini wakati wa usiku. Banda maalum hutumika kwa ajili ya kuwafuga katika mfumo shadidi (zero grazing).
Katika mazingira niliyokulia – na ndivyo ilivyo hata sasa huko vijijini – hata kama una kundi la ng’ombe pamoja na mbuzi, lazima uwatengenezee mbuzi zizi la peke yao, wakati mwingine wanaweza kuchangia pamoja na kondoo na ndama. Mara nyingi banda hili lazima liwe limeezekwa kuwakinga na mvua na jua.

Katika mazingira ya joto ambapo kuwakinga na jua na mvua ni jambo muhimu, paa rahisi ambalo unaweza kuezeka hata kwa makuti, nyasi au mabati ni la muhimu sana. Lakini lazima liwe na mwanga wa kutosha na kusaidia kuingiza hewa.
Ikiwa unatumia mfumo wa shadidi, ni muhimu kutengeneza banda hilo katika hali ya ubora na nafasi kulingana na mbuzi ulionao. Tengeneza mahali pa kulia chakula na kunywea maji ambapo lazima pawe juu kwa sababu mbuzi hawapendi kula kwenye matope. Tenga eneo la kulishia, kulala, kukamulia maziwa, eneo la kuchezea na kadhalika. Hata kama unawafuga ndani, haimaanishi kwamba mbuzi hao hawana haki ya kucheza.
Wafugaji mahiri wa mbuzi wanapendekeza kwamba eneo linalomtosha mbuzi mmoja linafaa kuwa na ukubwa wa futi 12 hadi 25 ambalo litawafaa hata katika mazingira ya joto ambapo watatumia muda mwingi wakiwa nje. Wakati wa baridi watatumia muda mwingi wakiwa ndani, hivyo unahitaji kuongeza eneo.

Banda na mahitaji yake

Mbuzi wanapaswa kufugwa katika banda lenye kuwapa uhuru. Hawapaswi kufungwa minyororo kama mbwa, au kuachiliwa kuzurura mashambani kama kondoo au kuwekwa kwenye maboma kama ng’ombe. Wanatakiwa kuwa na uhuru kuzunguka ndani ya banda lao na eneo dogo la kucheza nje.
Huhitaji kuwa na mtaji mkubwa kujenga banda la mbuzi, lakini kama nilivyosema awali, linapaswa kuwa na mwanga wa kutosha pamoja na uwezo wa kupitisha hewa safi. Hata kama unaishi katika eneo lenye baridi kama kule Makete, usiwafuge mbuzi katika eneo lililozibwa kwa matarajio kuwa unawakinga na baridi, kwa sababu mvuke unaotengenezwa humo unaweza kuwa na madhara makubwa kuliko baridi yenyewe.
Kama mbuzi wana eneo zuri la kucheza nje, basi banda lenye ukubwa wa eneo la futi 20 kwa kila mbuzi linatosha kama maskani.
Eneo la ndani linaweza kuwa dogo, kama nilivyosema, kwa sababu majira ya joto wanakuwa wanacheza nje. Huhitaji ghala kufugia mbuzi. Kizimba chenye ukubwa wa futi 8 x 10 kinatosha kabisa kuwahifadhi majike wanne. Kumbuka tu kwamba utalazimika kupanua banda wakati mbuzi wako watakapozaa na kuongeza kundi lako. Lazima watoto uwatengenezee mahali pao wasichanganyike na mama zao. Pia utahitaji kuwa na eneo kwa ajili ya kuhifadhi nyasi na nafaka za kuwalisha, vifaa, na eneo la maziwa.
Kwa hiyo ukiangalia hapa utaona kwamba, banda la mbuzi linatakiwa kujengwa katika misingi kama ile ya kujenga banda la kuku ambalo nalo huhitaji usafi, hewa na mwanga.
Wafugaji wengi wanapendelea sakafu ya vumbi, kwa sababu zina joto na kavu kuliko sakafu ya sementi na haziwezi kuoza miguu kama kwenye sakafu ya mbao.
Wafugaji wengi wanaoanza, hususan wasio na uzoefu na mifugo, hujikuta wakinunua wanyama na kwenda nao nyumbani na ndipo wanaanza kupanga mahali pa kuwaweka. Hili ni kosa na inaonekana unakuwa umeanza na mguu mbaya.
Unapojenga banda lako la mbuzi, hakikisha unatenga eneo maalum kwa ajili ya kujifungulia. Hii itawasaidia majike wazae bila kusumbuliwa na wengine.
Ikiwa utawatenganisha watoto na mama yao, utahitaji kuwa na banda maalum kwa ajili yao.
Hakikisha kwamba unaweka uzio kuzunguka banda lako la mbuzi. Hii itazuia watu kuingia ovyo kwa sababu kuingia bila utaratibu husababisha pia magonjwa kwa mbuzi. Uzio pia utasaidia kuwakinga na wezi, wanyama hatari na kadhalika.




Sifa za zizi bora la mbuzi ni kama zifuatazo:
• Ambalo imara linaloweza kumkinga mbuzi dhidi ya wanyama hatari na wezi
Lililojengwa mahali pa mwinuko pasiporuhusu maji kutuama
Ukubwa wa zizi lazima uzingatie idadi na umri wa mifugo. Ni vyema mbuzi watengwe kulingana na umri wao; na
Liruhusu usafi kufanyika kwa urahisi.
Pale ambapo mbuzi wanafugwa kwa mfumo wa shadidi hufugwa katika banda wakati wote.

Banda bora la mbuzi linatakiwa kuwa na sifa hizi:
Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari
Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi
Lijengwe sehemu isiyoruhusu maji kutuama na liwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu. Pia ujenzi uzingatie mwelekeo wa upepo ili hewa kutoka bandani isiende kwenye makazi
Liwe na sakafu ya kichanja chenye urefu wa mita 1 kutoka ardhini
Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji na mahali pa kuweka jiwe la chumvichumvi; na
Liwe na vyumba tofauti kwa ajili ya majike na vitoto, mbuzi wanaokua, wanaonenepeshwa na wanaougua.

Eneo la mbuzi linalotakiwa

Kundi la Mbuzi                Eneo kwa Mnyama Mmoja (Mita2)
Vitoto                                                 0.3
Wasio na mimba                             1.5
Wenye mimba                                 1.9
Dume                                                 2.8

Paa lijengwe kwa kutumia vifaa kama miti, mbao, na kuezekwa kwa nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati au hata vigae kwa kutegemea uwezo wa mfugaji,
Kuta zijengwe kwa kutumia mabanzi, mbao, nguzo, wavu wa waya, fito na matofali. Kuta ziwe imara zinazoruhusu hewa na mwanga wa kutosha.


Mlango uwe na ukubwa wa sentimita 60 x 150
Sakafu inaweza kuwa ya udongo au zege. Sakafu ya kichanja inaweza kujengwa kwa kutumia miti, fito, mianzi, mbao au mabanzi na iweze kuruhusu kinyesi na mkojo kupita. Chumba cha majike na vitoto kiwe na nafasi ya sentimita 1.25 kati ya papi na papi, fito na fito au mti hadi mti.
Chumba cha mbuzi wakubwa iwe sentimita 1.9 kati ya mbao na mbao.

KUMBUKA: Hupaswi kutumia gharama kubwa sana kujenga banda la mifugo. Unaweza kutumia rasilimali zilizopo hapo ulipo kujenga banda zuri. Kama hali inaruhusu kujenga banda aghali sawa, lakini vinginevyo ninakushauri jenga banda zuri, lenye vipimo sahihi, kwa kutumia rasilimali zilizopo, na utaokoa fedha ambazo unaweza kuzitumia hata kuongeza mifugo mingine.

Kwa maoni na ushauri, usisite kunipigia ama kuwasiliana name kwa whatsapp kupitia namba 0656-331974. Au barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.


Comments