Featured Post

MAONYESHO YA SAYANSI YAIBUA DIVISION ONE KATIKA MASOMO YA SAYANSI MTWARA GIRLS

Diana Sosoka na Nadhra Mresa kutoka Shule ya Sekondari Mtwara Girls ambao mwaka 2016 waliibuka washindi wa jumla wa mashindano ya Wanasayansi Chipukizi (YST). Hapa ni baada ya kukabidhiwa hati zao za ufadhili wa masomo kutoka taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation.
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
MATOKEO ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara kwa mwaka 2017 yamewashtua wengi baada ya kushuhudia ufaulu wa daraja la kwanza (Division One) kwa masomo ya sayansi, jambo ambalo lilikuwa adimu.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini umebaini kwamba, kwa miaka takriban 10 mchepuo wa masomo ya sayansi, Kemia, Baolojia na Jiografia (CBG), haujawahi kutoa hata mwanafunzi mmoja aliyepata daraja la kwanza katika matokeo ya kidato cha sita.
MaendeleoVijijini imegundua kwamba, miaka yote ufaulu mkubwa wa masomo ya sayansi shuleni hapo umekuwa daraja la pili (division two) ambao nao haukuwa wa kuridhisha ikilinganishwa na masomo ya sanaa na uchumi, huku wanaochukua mchepuo wa sayansi ‘wakiongoza’ kwa kupata daraja la nne pamoja na kupata sufuri.
Kati ya wanafunzi nane waliopata Daraja la Kwanza mwaka 2017 shuleni hapo, wawili walikuwa wanachukua mchepuo wa sayansi na kati ya wanafunzi 57 waliopata daraja la pili, 17 wanatoka mchepuo wa sayansi pia.
Lakini Mwalimu Rashid Namila anayefundisha sayansi shuleni hapo anaijua siri ya mafanikio hayo.
“Siri kubwa ni kwamba, hivi sasa kuna hamasa kubwa ya wanafunzi kusoma sayansi tangu nilipoanza kuwaongoza wanafunzi kushiriki mashindano ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania yanayoandaliwa na Shirika la Young Scientists (YST) miaka minne iliyopita,” anasema.
Mwalimu Namila ameiambia MaendeleoVijijini wakati wa maonyesho ya siku mbili ya wanasayansi chipukizi jijini Dar es Salaam yaliyofikia kilele jana Agosti 9, 2017 kwamba, ushiriki wa shule yake kwenye maonyesho hayo umefanya kuwepo na ushindani mkubwa shule kwake katika masomo ya sayansi ambapo mbali ya ubunifu, wanafunzi hao wanachuana vilivyo darasani.
“Kuna hamasa kubwa, wanafunzi wanafanya vizuri darasani, wameongeza ubunifu na inanipa kazi kubwa kila mwaka kuchagua nani anayeweza kufaa kushiriki kitaifa,” anasema Mwalimu Namila.
Ushindi wa Diana Sosoka na Nadhra Mresa kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara, ambao walikuwa washindi wa jumla mwaka 2016 umeongeza hamasa kubwa miongoni mwa wanafunzi wa Mtwara Girls, kwa mujibu wa Mwalimu Namila.
Diana na Nadhra ambao walipata ushindi kwa kubuni mashine ya kienyeji ya kutotoresha mayai, pia walipata udhamini wa masomo ya chuo kikuu kutoka taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation.
Wote kwa pamoja walikuwa wanachukua mchepuo wa Kemia, Balojia na Jiographia (CBG) na kwa bahati nzuri, wote wawili wamepata Division Two ya alama 12 na sasa wanajiandaa kwenda vyuo vikuu.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, wazo la utafiti wao la ‘Umaskini Siyo Suala la Msingi kwa Wanawake Mkoani Mtwara’ (Poverty Is No Longer An Issue For Women In Mtwara Region) ndilo lililowapa ushindi ambapo walizawadiwa nishani, tuzo kubwa na hundi ya Shs. 1.8 milioni.
Ushindi huo pia uliwapa fursa ya kwenda Dublin, Ireland kushiriki maonyesho ya sayansi, wakiongozana na mwalimu wao, ambako walijifunza mambo mengi yanayozidi kuwapa chachu ya kupenda sayansi.
“Kweli ni maajabu kwa mara ya kwanza kuna Division One kwenye CBG pale shuleni kwetu, ni mafanikio ambayo yametokana na hamasa ya kuwepo kwa mashindano haya ya sayansi na sisi tunashukuru kuwa sehemu ya mafanikio,” anasema Diana.
Kwa upande wake, Nadhra anasema anashukuru Mungu na waandaaji wa maonyesho ya YST pamoja na wadhamini Karimjee Jivanjee Foundation, kwani sasa hawezi kwenda kupanga foleni ya kuomba mkopo katika Bodi ya Mikopo ya Vyuo Vikuu kutokana na ufadhili alioupata.
Lakini Mwalimu Namila bado anaendelea kujivunia mwaka huu kwani wanafunzi wake Masha Mbwana na Heavenlight Mshomi hawakurudi mikono mitupu baada ya utafiti wao wa ‘Uhaba wa Walimu wa Sayansi ni Tatizo Sugu Mtwara?’ (Is Science Teacher Shortage a Problem in Mtwara?) kushika nafasi ya tatu katika eneo la Sayansi ya Kijamii na Kitabia.
“Hii inanipa hamasa ya kuongeza juhudi katika ufundishaji, naamini mwakani division one zitafika 10 na nataka nisione hata sufuri moja kwa wanafunzi wangu wanaochukua sayansi,” amsema Namila.

Matokeo ya kutisha
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, mwaka 2017 Mtwara Girls imeshika nafasi ya 7 na ya mwisho kimkoa na nafasi ya 295 kitaifa kati ya shule 449 zenye watahiniwa zaidi ya 30 ambapo ilikuwa na Division One (8), Division Two (57), Division Three (85), Division Four (6) na hakuna aliyepata sufuri.
Kati ya wanafunzi 76 waliokuwa wanachukua sayansi, wawili walipata daraja la kwanza na 17 wakapata daraja la pili, ingawa waliopata daraja la nne wote ni wa sayansi.
Mchepuo wa Historia, Kiswahili na Kiingereza - HKL (a.k.a Hakuna Kusoma Lala) ndio ulioongoza ukiwa na Div. One 4 na Div. Two 13, wakati EGM kulikuwa na daraja la pili 6, HE ilikuwa na daraja la kwanza moja na daraja la pili 8, HGK ilikuwa na daraja la pili 5, na HGL ilikuwa na Div. One moja na Div. Two 7.
Mwaka 2016 kulikuwa na Division One mbili tu hapo Mtwara Girls na zote zilitoka katika mchepuo wa HKL ambako pia kulikuwa na Div-II 18.
Mchepuo wa sayansi (CBG) kulikuwa na Div-II 14 na sufuri pekee ya shule nzima ilitoka huko.
Orodha ya wanafunzi wengine waliopata daraja la pili ilikuwa: EGM (wawili), HGE (8), HGK (17), na HGL (10).
Aidha, mwaka 2015 mchepuo wa sayansi (CBG) haukuambua Distinction, bali ulipata Merit 9 kati ya 35.
Distinction za shule nzima zilikuwa 9 tu na zilitoka HE (2), HGL (4) na HKL (3), wakati Merit nyingine zilitoka EGM (2), HE (14), HGL (7), na HKL (3).
MaendeleoVijijini imebaini pia kwamba, mwaka 2014 Mtwara Girls ilikuwa na Div-I nne tu na zilitoka EGM (2) na HKL (2), wakati Div-II zilikuwa 27 ambapo CBG iliambulia tano.
Nyingine zilitoka EGM (4), HE (4), HGK (1), HGL (9) na HKL (4).
Ufaulu mkubwa wa wanafunzi waliokuwa wanachukua mchepuo wa CBG mwaka 2013 ulikuwa Div-III ambapo walikuwa 14 kati ya 64 wa shule nzima na saba wote waliopata Div-IV kwa shule nzima walitoka CBG pamoja na mmoja aliyepata sufuri.
Mwaka huo hakukuwa na Div-I hata moja, lakini Div-II zilikuwa tano tu ambazo zilitoka HGK (3), HGL (1) na HKL (1).
Mwaka 2012 ni mwanafunzi mmoja tu kati ya wahitimu 31 wa CBG aliyepata Div-II, lakini 21 walipata Div-III na wane walipata sufuri kati ya sufuri 6 za shule nzima.
Div-I zilikuwa nne tu na zilitoka HGK (2) na HGL (2) ambako pia kulikuwa na wawili waliopata sufuri.
Wengine waliopata Div-II walitoka HGK (7), HGL (8) na HKL (5).


Comments