Featured Post

FAIDA LUKUKI ZA KUFUGA MBUZI WA MAZIWA




Na Daniel Mbega

TUMEONA katika makala iliyotangulia kwamba, mbuzi kama mnyama mwingine wa kufugwa, ana faida mbalimbali. Kwa wachache ambao wanaofuga wanaweza kukwambia kwamba siyo kazi rahisi na huwezi kuwa tajiri!
Hilo siyo kweli ikiwa kama utazingatia mbinu bora za utunzaji wa mifugo yako na kama utaelewa faida zitokanazo za ufugaji huo, ambazo ndizo kichocheo kikubwa kwako kuanzisha ujasiriamali huo.
Mbuzi wanatoa samadi na ikiwa unalima pia, hasa kilimo hifadhi na kinachozingatia uhifadhi wa mazingira, matumizi endelevu ya rasilimali pamoja na kisichotumia kemikali (organic farming), unaweza kuitumia samadi hiyo shambani na ukatoa mazao bora ambayo kwa sasa yana soko kubwa kulinganisha na yale yanayotumia kemikali.
Bustani za mboga mboga, matunda, maua na mazao ya nafaka yanayotumia mbolea asilia ni mazuri kwa afya ya binadamu na mifugo pia.
Lakini bado kuna faida nyingine kwa samadi, ambayo mbali ya kuongeza rutuba kwenye ardhi ya kupanda mimea pia inaweza kutoa kawi ya biogas, nishati ambayo utaitumia hata kijijini kwa ajili ya kupikia na hivyo kuokoa matumizi ya mkaa yanayoendana na ukataji ovyo wa miti.
Bidhaa zingine za wanyama zinazoweza kuuzwa ili kupata pesa zinajumulisha ngozi, pembe na kwato ambavyo hutumika katika viwanda kuzalisha bidhaa zingine.
Nimezungumza katika makala ya Ufugaji Bora Wa Mbuzi Wa Maziwa, kwamba maziwa ya mbuzi ni mazuri kwa afya na yana ladha nzuri kuliko ya ng’ombe, yakiwa na protini nyingi.
Ni mazurikwa lishe, rahisi kunywewa na yana viinilishe vingi kwa sababu yana madini mengi ya kalsiumu, fosforasi na klorine kuliko maziwa ya ng’ombe.
Maziwa ya mbuzi yana uwezo mkubwa wa kuongeza kinga katika mwili (immune) kwa watoto na hata watu wazima. Kuna watu ambao hawawezi kunywa maziwa ya ng’ombe kwa sababu wana mzio (allergy), lakini hakuna anayeweza kushindwa kunywa maziwa ya mbuzi.
Nasisitiza, kwamba, ikiwa unafuga ng’ombe wa maziwa na mbuzi wa maziwa, nakushauri maziwa ya mbuzi uyatumie nyumbani halafu ya ng’ombe ndiyo uyauze.
Nyama ya mbuzi ni tamu sana na inaliwa na watu wengi.
Lakini mbali ya maziwa na nyama, wafugaji wengi wa mbuzi wa maziwa wana faida kubwa ya kutengeneza mtindi, siagi, samli na jibini, mazao ambayo yana soko kubwa. Kimsingi, maziwa ya mbuzi yana mafuta mengi hivyo ni rahisi kupata siagi nyingi zaidi.
Kwa upande mwingine, mbuzi wanahitaji usimamizi mdogo kuliko ng’ombe. Mbuzi wana gharama ndogo sana ya chakula kulinganisha na ng’ombe. Ng’ombe mmoja anaweza kula chakula kinachowatosha mbuzi watatu mpaka sita kwa siku, kutegemeana na aina (breed)na mahitaji ya mbuzi husika. Mbuzi wanaweza kula nyasi, majani na magamba ya miti na kadhalika, vyakula vingine ambavyo ng’ombe hawezi kula.
Faida nyingine kwamba, mbuzi wanazaa mara mbili kwa mwaka wakati ng’ombe anazaa mara moja. Ukipata bahati ya mbuzi wanaozaa mapacha, unaweza kuongeza mifugo ndani ya muda mfupi. Kwa kawaida, mbuzi hubeba mimba kwa muda wa wiki 20 au miezi mitano (siku 150) na hunyonyesha kwa miezi miwili. Kumbuka pia mbuzi pia ni wastaarabu kuliko ng’ombe.
Kuhusu kiasi cha maziwa unayopata kila siku, mbuzi hawako nyuma sana ya ng’ombe. Wakati ambapo ng’ombe aliyetunzwa vizuri anaweza kutoa mpaka lita 15 au 20 kwa siku, mbuzi wa maziwa wa uzao bora na aliyetunzwavizuri anaweza kutoa mpaka lita 7 kwa siku na katika nchi ambayo mbuzi wa kienyeji wanaweza kutoa lita 2 kwa siku, hii ni faida kubwa kuwa na mbuzi wa maziwa.
Kwa maana nyingine, kuwa na mbuzi watatu ni sawa na kuwa na ng’ombe mmoja, jambo ambalo ni la faida pia, kwa sababu ikitokea ugonjwa ng’ombe huyo mmoja anaweza kufa, lakini mbuzi watatu hawawezi kufa wote, unaweza kuwaokoa wengine, hivyo kuendelea kuwa na maziwa.

Masoko
Kuuza maziwa ni suala la msingi. Kama unao mbuzi wengi ama wanazalisha maziwa ya ziada, unaweza kuyauza ambapo bei yake ni zaidi ya mara mbili kwa ile ya maziwa ya ng’ombe.
Tatizo wengi wanalalamika kwamba watapata wapi soko la maziwa ya mbuzi. Ukiwa mfugaji wa mbuzi wa maziwa huna haja ya kuhofia kuhusu uchakataji wa maziwa yako ili utoe siagi, jibini na samli, kwa sababu soko la uhakika la maziwa lipo, tena kubwa hata hapa Tanzania.
Nchini Kenya, kwa mfano, wakati lita moja ya maziwa ya ng’ombe inauzwa kwa KShs. 40 (takriban Shs. 800 ya Tanzania), maziwa ya mbuzi yanauzwa kati ya KShs. 80 na 100 (TShs. 1,600 na 2,000) kwa lita.
Inawezekana hujalisikia soko la maziwa kwa sababu wewe siyo mfugaji wa mbuzi wa maziwa, ama huyahitaji maziwa hayo.
Lakini ukweli ni kwamba, kama ilivyo kwa biashara nyingine, unapokuwa mfugaji wa mbuzi wa maziwa lazima utaanza kutafuta soko na hapa nikwambie, kabla hujaanza kwenda kuuliza kwenye hoteli na migahawa, wateja wako wa kwanza wanaweza kuwa jirani zako.
Hawa, mbali ya kuwa wateja, lakini pia wanaweza kutumika kama ndio ‘maofisa masoko’ wako kwa sababu watakwenda kueneza taarifa kwamba kwa Mbega kuna maziwa ya mbuzi. Wateja wengine ni watengenezaji wa jibini na siagi.
Hata hivyo, kwa kuwa ufugaji huu wa mbuzi wa maziwa unahamasishwa pia na serikali ili kumuondolea mwananchi umaskini katika kutekeleza Mpango wa Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi Tanzania (Mkukuta II) na Mpango wa Maendeleo Endelevu ya Dunia, ni wazi kwamba unapokuwa mfugaji kuna mahali ambako utapata soko.
Katika kipindi hiki cha Awamu ya Tano, hata Rais John Magufuli amekwishasisitiza kwamba anataka kuona ‘Tanzania ya viwanda’ kwa kuhimiza viwanda vidogo vidogo vya kusindika bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo na mifugo. Kwa hiyo, umoja wa wafugaji ukijizatiti unaweza ama wenyewe kukusanya fedha kwa ajili ya kuanzisha kiwanda kidogo cha kusindika maziwa ya mbuzi au kuwawezesha wakulima elimu ya namna ya kutengeneza wenyewe samli, siagi na jibini.
Uwekezaji wa viwanda vikubwa mara nyingi hutegemea na upatikanaji wa malighafi, lakini kama Watanzania wengi watahamasishwa kufuga mbuzi wa maziwa na maziwa yakapatikana kwa wingi, haihitaji kupiga baragumu kuwahimiza wawekezaji wajenge viwanda, bali wenyewe tu watajenga kwa sababu malighafi zipo za kutosha.
Katika baadhi ya mataifa, wafugaji wa mbuzi wa maziwa hugandisha maziwa yao na kuuza kama mtindi, lakini wengine wamepatiwa utaalam na wanatengeneza wenyewe samli, siagi na jibini katika kuongeza ubora na mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo.
Kutengeneza jibini ya maziwa ya mbuzi ni rahisi. Inahitaji vifaa vichache au viungo ambavyo havipo nyumbani. Utahitaji birika kubwa, vijiko, kisu kikubwa, nguo maalum ya kuchujia jibini, kipimajoto maalum kwa ajili ya jibini (au chochote ambacho kitakuonyesha kwamba maziwa yana joto kati ya nyuzi 86º na 100ºF) na viungo vingine hasa rennet. Rennet, ambayo inapatikana katika vidonge au majimaji, inasaidia kuigandisha na huwa ina maelekezo ya namna ya kutengeneza jibini.
Maziwa ya mbuzi yanaweza kugandishwa na kuwa mtindi, tena mtamu sana.
Ngozi za mbuzi zinaweza kutengenezwa bidhaa za ngozi kama mikoba na kadhalika. Manyoya ya mbuzi ni mazuri kwa kazi mbalimbali zikiwemo nyuzi na weaving. Kwa ujumla, kuanzia mwanzo hadi mwisho, mbuzi ndiye mnyama mwenye faida kubwa ambaye anafugwa. Haishangazi kuona hivi sasa watu wengi wametambua umuhimu wake na wameanza kuwafuga.
Soko ni muhimu, lakini wakati mwingine lisiwe kikwazo kwako kwa kubuni mradi ambao unadhani kwamba unaweza kuleta manufaa.
Vinginevyo tusingeweza leo hii kuwa na simu, magari, ndege na mitambo kwa sababu hata wabunifu wa mambo hayo wakati wanaanza utafiti wao hawakujiuliza kama kulikuwa na soko bali walitengeneza na baadaye masoko yakapatikana, tena kwa wingi.
Jambo la msingi zaidi ili upate faida katika mradi wako wa mbuzi wa maziwa ni kuhakikisha unakuwa na mpango wa mradi (project plan) hata kama ni mdogo, halafu baadaye uwe na mpango wa biashara (business plan) pamoja na mpango wa masoko (market plan). Hii itakusaidia sana kuona unawekeza namna gani na utapata faida kiasi gani, baada ya muda gani na wapi utauza bidhaa zako.
Muhimu tu ni kuweka rekodi zako vizuri kuanzia unapoandaa banda la mifugo, kununua mbuzi, chakula, tiba na mambo yote ikiwa ni pamoja na gharama nyingine za wahudumiaji (labour force).
Niwaambie tu ndugu zangu, hakuna kazi rahisi duniani na wala hakuna kazi ngumu. Urahisi wa kazi unakuja kutokana na kujitoa kwako na kuzingatia maadili ya kazi hiyo, vivyo hivyo, ugumu wa kazi unakuja ikiwa hujazingatia misingi ya kazi husika.
Ukulima na ufugaji ni kazi rahisi ukiwa na nia ya dhati, mpango na malengo. Kwa sasa inaonekana kuwa ngumu kwa sababu siku zote tumekuwa tukilima ama kufuga kwa mazowea tu, hatuzingatii misingi ya kilimo bora ama ufugaji wa kisasa ndiyo maana wengi wetu tunaendelea kuogelea katika umaskini.
Ukikutana na mkulima ama mfugaji wa miaka yote ambaye hajaona faida ya kile anachokifanya ukampa wazo hilo kwamba na wewe unataka kuingia kwenye kilimo na ufugaji, anaweza kukukatisha tamaa pengine hata kwa kumtazama tu. Lakini nakuhakikishia ndugu yangu, leo hii unaweza kujiingiza kwenye ufugaji au kilimo na ukawa mfano wa kuigwa kutokana na matunda utakayoyapata. Hata wale wazoefu wanaweza kuja kwako kujifunza. Usikate tamaa.
Wakati mwingine ukipata nafasi nenda kawatembelee wafugaji amba wakulima waliofanikiwa uone wametumia njia ama teknolojia gani. Hiyo itakusaidia sana.
Zaidi jenga tabia ya kujisomea mambo mbalimbali, tembelea hapa MaendeleoVijijini kila mara ili ujifunze mambo mbalimbali pamoja na kusoma ama kusikiliza shuhuda za watu waliofanikiwa katika miradi mbalimbali.
Usijiulize mara mbili wala usianze kuwaza mambo ambayo yatakuwa vikwazo kwako kabla hujaanza. Anza kufuga mbuzi wa maziwa, halafu faida yake utaiona.

Kwa maoni na ushauri, usisite kunipigia ama kuwasiliana name kwa whatsapp kupitia namba 0656-331974. Au barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.



Comments