Featured Post

JINSI YA KUANZISHA UFUGAJI BORA WA MBUZI WA MAZIWA



Na Daniel Mbega

WATU wengi hutegemea mifugo kwa riziki lakini hawafugi katika misingi inayotakiwa ili kupata tija zaidi. Ufugaji wa wanyama humpa mkulima nyama na maziwa kwa matumizi ya nyumbani na mapato kutokana na mauzo ya ziada.
Ama mifugo pia ni chanzo cha samadi. Bidhaa zingine za wanyama zinazoweza kuuzwa ili kupata pesa zinajumulisha ngozi, samadi ya kuongeza rutuba kwenye ardhi ya kupanda mimea na pia kutoa kawi ya biogas, pembe, kwato na midomo ya ndege ambavyo hutumika katika viwanda kuzalisha bidhaa zingine.
Zipo aina nyingi za wanyama ambao mkulima anaweza kuwafuga kuanzia ng’ombe, mbuzi, kondoo, ngamia, sungura, nguruwe na vile vile ndege wa nyumbani kama kuku, bata bukini, bata mzinga, bata, hua (njiwa) na mbuni. Siku hizi pia wapo wakulima wanaofunga kwale na kanga.
Chaguo la mnyama wa kufuga hutegemea mambo mengi. Hata hivyo, wakulima wengi hufuga wanyama ambao wana ujuzi wa kuwasimamia na wanawapatia mapato mazuri.
Katika Makala haya tutajifunza namna ya ufugaji bora wa mbozi wa maziwa ambapo tutaanza kuangalia jinsi ya kuanzisha mradi huo na mambo mengine ya awali.
Mbuzi mara nyingi wanafahamika kama “ng’ombe wa maskini” kwa sababu nyingi. Kwa yeyote anayetaka kufuga mbuzi kwa ajili ya maziwa, mbuzi anaweza kuwa rahisi kumhudumia kuliko ng’ombe.
Gharama za uanzishaji wa mradi wa mbuzi wa maziwa mmoja au hata watano ni ndogo ukilinganisha na kuanzisha mradi wa ng’ombe wa maziwa. Chakula na zana za kufanyia kazi pia ni za gharama nafuu. Kufuga ng’ombe wa maziwa kunaweza kuwa changamoto kubwa kwa mtu anayeanza ufugaji, lakini kwa mbuzi ni sawa na kutafuta mnyama mwingine rafiki zaidi ya mbwa.
Mbuzi wamaziwa humpatia mkulima maziwa kwa ajili ya familia na kuuza ili kupata fedha. Samadi ya mbuzi hutumika kurutubisha ardhi na mbuzi wenyewe wanaweza kuuzwa pia. Kipato cha ziada kinachotokana na mazao ya mbuzi kinawawezesha wafugaji kumudu gharama za matumizi zikiwemo kulipa gharama za nyumbani kama chakula na huduma nyingine; kulipia gharama za shule kwa watoto wao ama kuwekeza katika miradi mingine kama kilimo na biashara zingine.
Kwa miaka ya karibuni serikali imekuwa ikihimiza ukulima endelevu ambao unahusisha ufugaji wa kisasa wenye tija kwa kuangalia mifugo ambayo siyo tu itakuwa fahari ya mkulima, bali inaweza kumpatia manufaa kibiashara.
Taasisi mbalimbali zimekuwa zikijitokeza kuwasaidia wakulima kwa mafunzo na kuanzisha miradi ya ufugaji wa mbuzi wa maziwa na ingawa siyo wakulima wengi waliopata mafunzo hayo ama kuanzisha miradi hiyo, lakini kwa wale wachache ambao wameanzisha miradi ya mbuzi wa maziwa, wameona faida zake.
Linapokuja suala la kufuga mbuzi wa maziwa, wengi wanapata hofu na kujiuliza maswali mengi kwamba wanahitaji ardhi yenye ukubwa gani ili kuwafuga, watawalisha nini, na namna gani ya kuwahudumia.
Lakini MaendeleoVijijini ni mtandao ambao uko kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima na wafugaji, pamoja na wananchi wengine wanaotaka kuanzisha miradi ya aina hiyo, na ujasiriamali mwingine na tutakwenda hatua kwa hatua ili kila mmoja aweze kuelewa.
Ufugaji wa mbuzi wa maziwa unaweza kufanywa mahali popote, iwe mjini ama kijijini, kwa sababu mbuzi hawa, tofauti na mbuzi wa kienyeji wanaofugwa zaidi kwa ajili ya nyama, wanaweza kufugwa kwa njia ya ‘Zero Grazing’, kwamba wanaweza kufungiwa kwenye banda maalum na kulishwa.

Kanuni za ufugaji bora wa mbuzi wa maziwa
Mbuzi wa maziwa wanaweza kufugwa kwa gharama nafuu na kuishi katika mazingira magumu kama ya maradhi na ukame ikilinganishwa na ng’ombe.
Kutokana na umbile lao dogo wanaweza kufugwa katika eneo dogo na pia wanaweza kuhudumiwa na familia yenye nguvukazi na kipato kidogo. Uzao wa muda mfupi unamwezesha mfugaji kupata mbuzi wengi kwa kipindi kifupi.
Wanyama hao hufugwa kwa ajili ya nyama, maziwa, ngozi, na mazao mengine kwa matumizi ya familia na kuongeza kipato.
Hata hivyo, ufugaji bora wa mbuzi wa maziwa lazima uzingatie kanuni zifuatazo:-
1) Wafugwe kwenye banda au zizi bora
2) Wachaguliwe kutokana na sifa za koo/aina na lengo la uzalishaji (nyama, maziwa au vyote kwa pamoja)
3) Wapatiwe lishe sahihi kulingana na umri na mahitaji ya mwili
4) Kuzingatia mbinu za kudhibiti magonjwa kama inavyoshauriwa na wataam wa mifugo
5) Kuweka na kutunza kumbukumbu sahihi za uzalishaji
6) Kuzalisha nyama au maziwa yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko
Ziko faida nyingi za ufugaji wa mbuzi wa maziwa na miongoni mwazo ni:

Lishe bora
Maziwa ya mbuzi ni mazuri kwa afya na yana ladha nzuri mno kuliko ya ng’ombe! Pia maziwa hayo yana protini nyingi kuliko maziwa ya ng’ombe. Ni mazuri kwa lishe, rahisi kunywewa na yana viinilishe vingi kwa sababu yana madini mengi ya kalsiumu, fosforasi na klorine kuliko maziwa ya ng’ombe.
Kwa kuwa makala haya hayajalenga kueleza umuhimu wa madini hayo katika mwili wa binadamu, hatutaweza kujadili bali tutajadili katika makala nyingine, hata hivyo, ieleweke kwamba, maziwa ya mbuzi yana uwezo mkubwa wa kuongeza kinga katika mwili (immune) kwa watoto na hata watu wazima. Wapo watu hawawezi kunywa maziwa ya ng’ombe kwa sababu wana mzio (allergy), lakini hakuna anayeweza kushindwa kunywa maziwa ya mbuzi.
Kama unafuga ng’ombe wa maziwa na mbuzi wa maziwa, nakushauri maziwa ya mbuzi uyatumie nyumbani halafu ya ng’ombe ndiyo uyauze. Lakini kama unao mbuzi wengi ama wanazalisha maziwa ya ziada, bado unaweza kuyauza ambapo bei yake ni zaidi ya mara mbili kwa ile ya maziwa ya ng’ombe.
Nyama ya mbuzi ni tamu sana na inaliwa na watu wengi. Lakini mbali ya maziwa na nyama, wafugaji wengi wa mbuzi wa maziwa wana faida kubwa ya kutengeneza mtindi pamoja na siagi, mazao ambayo yana soko kubwa. Kimsingi, maziwa ya mbuzi yana mafuta mengi hivyo ni rahisi kupata siagi nyingi zaidi.

Kiuchumi
Mbuzi wana gharama ndogo sana ya chakula kulinganisha na ng’ombe. Ng’ombe mmoja anaweza kula chakula kinachowatosha mbuzi watatu mpaka sita kwa siku, kutegemeana na aina (breed) na mahitaji ya mbuzi husika. Mbuzi wanaweza kula nyasi, magamba ya miti na kadhalika, vyakula vingine ambavyo ng’ombe hawezi kula. Mbuzi wanazaa mara mbili kwa mwaka wakati ng’ombe anazaa mara moja. Ukipata bahati ya mbuzi wanaozaa mapacha, unaweza kuongeza mifugo ndani ya muda mfupi. Kwa kawaida, mbuzi hubeba mimba kwa muda wa wiki 20 au miezi mitano (siku 150) na hunyonyesha kwa miezi miwili. Kumbuka pia mbuzi pia ni wastaarabu kuliko ng’ombe.
Ukiwa mfugaji wa maziwa huna haja ya kuhofia kuhusu uchakataji wa maziwa yako ili utoe siagi, jibini na samli, kwa sababu soko la uhakika la maziwa lipo, tena kubwa hapa Tanzania.
Nchini Kenya, kwa mfano, wakati lita moja ya maziwa ya ng’ombe inauzwa kwa KShs. 40 (takriban Shs. 800 ya Tanzania), maziwa ya mbuzi yanauzwa katika KShs. 80 na 100 (TShs. 1,600 na 2,000) kwa lita.
Kuhusu kiasi cha maziwa unayopata kila siku, mbuzi hawako nyuma sana ya ng’ombe. Wakati ambapo ng’ombe aliyetunzwa vizuri anaweza kutoa mpaka lita 15 au 20 kwa siku, mbuzi wa maziwa wa uzao bora anaweza kutoa mpaka lita 7 kwa siku na katika nchi ambayo mbuzi wa kienyeji wanaweza kutoa lita 2 kwa siku, hii ni faida kubwa kuwa na mbuzi wa maziwa.
Kwa maana nyingine, kuwa na mbuzi watatu ni sawa na kuwa na ng’ombe mmoja, jambo ambalo ni la faida pia, kwa sababu ikitokea ugonjwa ng’ombe huyo mmoja anaweza kufa, lakini mbuzi watatu hawawezi kufa wote, unaweza kuwaokoa wengine, hivyo kuendelea kuwa na maziwa.
Kwa upande mwingine, mbuzi wanahitaji usimamizi mdogo kuliko ng’ombe.

Mambo muhimu ya kuzingatia kuhusu ufugaji wa mbuzi wa maziwa
Kama nilivyokwishaeleza hapo juu, maziwa ya mbuzi ni mazuri na yana madini muhimu kwenye mwili hivyo basi kila mmoja anapaswa kujifunza kuyatumia.
Maziwa ni chakula muhimu chenye madini muhimu mwilini na pia ndiyo njia mojawapo ambayo watu huambukizwa magonjwa haswa kwa kupuuza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa.
Lakini lazima ifahamike kwamba, ufugaji wa mbuzi wa maziwa ni uwekezaji mzuri hasa kwa wakulima wenye mashamba madogo na hata yule mkazi wa mjini ambaye anaweza kulitumia eneo lake la uwani kufuga.
Ifahamike pia kwamba, ukulima ni sawa na biashara na biashara nzuri lazima iwe na mpangilio mzuri hasa kwa matumizi ya pesa zinazoapatikana. Kabla ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa mbuzi wa maziwa, lazima uwe na mpango mzuri hata kama unaanza na mbuzi wawili, kwani kwa kufanya hivyo utaweza kujua gharama zake na hiyo itakusaidia pia hata kuongeza mbuzi wengine na kupanua mradi.
Mpango wako wa mradi ndio pia utatoa taswira ya matumizi ya fedha kwa sababu kama hutakuwa na matumizi mazuri ya pesa hizo huenda iwe vigumu kununua vitu muhimu ili kuendeleza biashara hiyo.
Kwa maana hivyo, hata baada ya kuanzisha mradi huo, ni vyema ukumbuke kuweka rekodi ili kujua ikiwa unapata faida au hasara na ili kuweza kubaini matatizo yanayoikumba biashara yako.
Ufugaji wa mbuzi wa maziwa ni mradi unaoweza kuanzishwa katika vikundi, lakini pia unaweza kuanzishwa na mtu mmmoja mmoja.
Wakulima hao ni lazima waunde vikundi au vyama ambavyo watafaidika navyo na pia vitasaidia kupigania kupata bei nzuri ya bidhaa zao pamoja uimarishaji wa sera za serikali ili kuwawezesha kufanya biashara yao chini ya usaidizi mzuri kutoka kwa serikali.
Tanzania ni mojawapo ya nchi zilizo na maofisa kilimo na mifugo (maofisa ugani) waliohitimu vizuri lakini wananchi wengi huwa hawawatumii maofisa hawa ipasavo ambao kazi yao kuu ni kukuhudumia. Ukitaka kufuga vizuri utafanikiwa ikiwa utatafuta msaada na ushauri kutoka kwa maofisa hao wa serikali walio kwenye eneo lako.

Maswali ya msingi yanayoulizwa na watu wengi:
Kwa wastani, mbuzi anaweza kutoa lita 800 kwa mwaka. Hata hivyo, kiasi hiki hutofautiana kutegemeana na aina ya mbuzi, lakini hii inamaanisha kwamba, anaweza kutoa lita kuanzia lita 2 hadi 7 kwa siku. Hii inategemea aina ya mbuzi, namna ya utunzaji na chakula unachomlisha. Kwa matumizi ya nyumbani tu, kiasi hicho ni kikubwa kwa siku.
Kumbuka kwamba, mbuzi anakamuliwa kwa kipindi cha miezi 10 kwa mwaka na wanaachwa kwa miezi miwili ili kuwapa nafasi ya kuzaa tena. Mbuzi hutoa maziwa mengi baada ya kuzaa (kitaalam wanasema ‘kidding’). Ukiwa na mbuzi mmoja au wawili, huwezi kukosa maziwa kwa mwaka mzima.

Ladha ya maziwa ya mbuzi ikoje? Ni matamu kuliko ya ng’ombe?
Kama nilivyoeleza hapo awali, maziwa ya mbuzi yana ladha nzuri ingawa katika mazingira mengi, ni wachache ambao wanaweza kutofautisha. Maziwa ya mbuzi ni meupe sana.
Mbuzi pia wanatofautiana kutokana na aina, ambapo mbuzi aina ya Nubian maziwa yao yana mafuta mengi kuliko mbuzi aina ya Saanen kama ilivyo kwa ng’ombe aina ya Jerseys na Holsteins. Lakini kuna mambo mengine yanayochangia maziwa kuwa na mafuta mengi au kutokuwa na mafuta, kama uachishaji wa unyonyeshaji na ulishaji.

Inagharimu kiasi gani kufuga mbuzi wa maziwa?
Hii inatofautiana kila mwaka na kila mahali, kutegemeana na mazingira ya upatikanaji wa chakula, na aina ya chakula unachomlisha mbuzi huyo. Katika mazingira ya kijijini ambako unaweza kumfungulia mbuzi akajichungia mwenyewe, gharama ni ndogo sana, pengine ni dawa za chanjo. Mbuzi anahitaji chakula kuanzia nusu tani hadi tani mbili kwa mwaka, kutegemeana na aina ya mbuzi, kiwango cha ubora wa chakula chenyewe, na mazingira mengine kwa ujumla.
Mbuzi pia anahitaji chakula cha nyongeza kama mahindi au mchanganyiko wa mahindi na ngano, pumba za nafaka na nafaka nyinginezo. Kwa kawaida, inategemea na nini kinacholimwa kwenye eneo husika au kinachopatikana. Mbuzi jike anahitaji chakula cha ziada ili kutoa maziwa mengi.
Upatikanaji wa vyakula hivyo ndio utakaoonyesha ni gharama kiasi gani unazotumia kumlisha mbuzi huyo. Suala la gharama za tiba nalo ni muhimu.
Gharama nyingine za kuangalia ni zile za kuanzia kama banda la mbuzi, uzio, vifaa vya kulishia na kunyweshea, uhifadhi wa nyasi, na vifaa vya kukamulia.
Angalia, usitumie gharama kubwa, bali unaweza kuanza na vile vinavyopatikana katika mazingira uliyopo. Usiwaze kujenga banda la gharama wakati unaweza kutumia miti ya kawaida tu. Usinunue chakula kama nyasi zinapatikana kwa wingi.

Sina nafasi ya kutosha, je, bado naweza kufuga mbuzi kadhaa?
Mbuzi ni wanyama wanaofaa kufugwa katika eneo dogo nyumbani. Mbuzi wanahitaji eneo lenye ukubwa wa futi 12 x 20 kwa kila mmoja kama unatumia mfumo wa Zero Grazing, na katika mazingira ambayo mbuzi wanakwenda kuchunga wenyewe, wanahitaji eneo dogo. Banda linapaswa kuwa kavu kwa sababu mbuzi siyo kama ng’ombe, hawawezi kulala kwenye tope.

Mbuzi wanaweza kuwa wanyama rafiki?
Ndiyo. Ni wanyama welevu na wenye kujenga urafiki. Kama kuna mbuzi mkorofi, basi ujue hakutunzwa vizuri ama alikuwa akinyanyaswa. Lakini kumbuka kwamba mbuzi ni mifugo, siyo kama mbwa. Hupaswi kuwafunga Kamba muda wote, bali wanapokwenda kuchunga hasa kama katika mazingira uliyopo wanaweza kuharibu mali zilizopo kwa kuwa wanapenda kucheza na huvutiwa na vitu vingine. Jihadhari, usiegeshe gari lako jirani na banda la mbuzi, kwa sababu wanaweza kuliharibu kwani wanaweza kupanda juu n ahata kuvunja vioo.

Vipi kuhusu maradhi?
Mbuzi mara nyingi ni wastahimilivu wa mazingira na magonjwa na wana matatizo machache ikiwa watatunzwa vizuri. Kwa kawaida wana wadudu tumboni, hasa minyoo (na hawawezi kuishi bila kuwa nao), lakini mtaalam wa mifugo anaweza kusaidia kuwatibu minyoo hiyo kwa kuanzisha program ya kuondoa minyoo.
Ugonjwa wa Mastitis (kuvimba kwa kiwele) mara nyingi huwakumba mbuzi wengi, lakini huo unaweza kudhibitiwa katika suala la ukamuaji.
Kwa ujumla, kama unataka kufuga kibiashara au una mbuzi wengi ndipo utamhitaji ofisa ugani wa mifugo, lakini kama unao wachache, ni rahisi kuwamiliki na kukabiliana na changamoto ndogo ndogo.

Vipi kuhusu majukumu?
Mbuzi wanatakiwa kulishwa na kunyweshwa maji kila siku. Kama wanakamuliwa, unapaswa kuwakamua kila baada ya saa 12 – lakini hiyo haimaanishi kila mshale unapogonga, na inaweza kuwa saa 1 asubuhi na saa 1 usiku au mchana na usiku mnene.
Unatakiwa kusafisha vizimba vyao na kuweka matandazo mahali wanapolala.
Mbuzi wanatakiwa kupunguzwa pembe zao mapema kwa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwemo kuogopa wasije wakaumizana wanapocheza ama kupigana. Pia wanatakiwa kupunguzwa kwato kila mara, kwa sababu kwao za mbuzi wanaofugwa bandani tu hukua haraka kuliko za mbuzi wazururaji. Punguza kwato mara moja kwa mwezi.

Nimeambiwa nyama ya mbuzi ni tamu sana, je ni kweli?
Nyama ya mbuzi (chevon au cabrito kwa Kiingereza) inafanana kidogo na nyama ya kondoo. Watu wengi wanaipenda kwa sababu ni tamu, lakini kwa sababu mbuzi jike anatakiwa azae ilia toe maziwa, wengi wanategemea kwamba atazaa dume ambaye baada ya muda ataliwa.

Ninapaswa kuwa na beberu ninapoanza ufugaji?
Hapana, hususan kama ni mfugaji mdogo wa mbuzi. Inaweza kuongeza gharama za uchumi bure. Ukishajifunza kuhusu aina za mbuzi, nasaba haiwezi kuwa na umuhimu sana, kwa sababu unaweza kuamua kutumia mabeberu kadhaa tofauti. Unaweza kukodisha bebeeru au unaweza kutumia mabwana mifugo kupandikiza mbuzi wako.

Kuna jambo la ziada ninalopaswa kujua?
Ndiyo! Uamuzi wa kununua mbuzi haupaswi kufanywa kwa ghafla bila uhakika. Mbuzi atachukua muda wako na kiasi cha fedha. Atarejesha faida ikiwa utamtunza vyema. Kuna mambo mengi ya kujifunza. Hata wataalam na wazoefu wa kufuga nao hujifunza kila siku. Mbali ya hayo, huhitaji kuwa mtaalam ndipo uanze ufugaji wa mbuzi wa maziwa. Kwa ujumla, hakuna njia ya uhakika ya kupata elimu na uzoefu bila mwenyewe kuanza ufugaji. Ni wajibu wako wewe kuingia kwenye ujasiriamali huo.

Makala itakayofuata tutaangalia kwa kina faida za mbuzi wa maziwa. Kama una swali au maoni, nipigie ama nitumie ujumbe wa whatsapp kwa namba 0656 331974, au barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com

Comments