- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mkurugenzi wa Namaingo, Biubwa Ibrahim, akielezea uzoefu wake katika kuendesha miradi ya ujasiriamali.
Rais wa VICOBA Endelevu, Mhe. Devita Likokola, akingea na akinamama wa Green Voices jinsi Vicoba vinavyoweza kuwa chanzo cha mtaji kwa miradi ya Green Voices.
MKURUGENZI
Mtendaji wa kampuni ya Namaingo Business Agency, Biubwa Ibrahim, amewataka
akinamama wanatekeleza mradi wa Green Voices Tanzania kuwa wabunifu na kutokata
tamaa katika shughuli wanazozifanya.
Akizungumza
wakati wa kufunga semina ya siku sita ya mafunzo yaliyowashirikisha akinamama
15, Biubwa alisema kwamba, ubunifu, jitihada na kutokata tamaa ndiyo silaha
kubwa katika mafanikio, huku akiwahimiza watafute fedha bila kuchoka.
“Lazima
muwe wabunifu, halafu ni dhambi kubwa kukata tamaa bali mnatakiwa kuongeza
jitihada katika mradi yenu,” aliwahimiza.
Aidha,
alisema kwamba, mafanikio yoyote hayawezi kuja kwa siku moja, hivyo wanapaswa
kuwa wavumilivu daima ili waweze kufanikiwa.
Akinamama
hao wa Green Voices wanatekeleza miradi mbalimbali ya kilimo inayoendana na
mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, ambayo
inadhaminiwa na taasisi ya Women for Africa Foundation ya Hispania inayoongozwa
na makamu wa rais mstaafu wa nchi hiyo, Bi. Maria Tereza Fernandes de la Vega.
Biubwa
alisema, wajasiriamali wengi wanaposhindwa kuona faida ya shughuli
wanazozifanya huvunjika moyo mapema, lakini hilo lisiwe kikwazo kwao kwani
wanapaswa kukaa chini na kutafakari njia mpya ya kuendesha biashara ama miradi
yao.
“Inabidi
kujiuliza wewe mwenyewe kama hapo ulipo ndipo mahali sahihi, vinginevyo usife
moyo unapoona mambo hayaendi, bali angalia wapi ulipokosea na ujipange upya
halafu utaona matokeo yake,” alisema.
Akaongeza:
“Mimi nilianza na mtaji wa shilingi elfu nne tu, nimepitia changamoto nyingi
ikiwemo kudhulumiwa fedha, lakini katu sikukata tamaa nimeendelea kupambana na
mpaka sasa kupitia kampuni yangu nimeweza kusajili wakulima 400,000 nchi
nzima.”
Dkt. Neema Mori akifundisha njia za kupata mitaji kwa biashara kwa akinamama wa Green Voices.
Mradi wa
Green Voices unatekelezwa nchini Tanzania pekee, ambapo akinamama 10 kati ya 15
wanaendesha miradi mbalimbali ya kilimo, ufugaji wa nyuki, ukaushaji wa mboga
na matunda pamoja na utengenezaji wa majiko rafiki katika jitihada za kupambana
na mabadiliko ya tabianchi.
Akinamama walioanzisha miradi hiyo – miradi na mikoa
watokayo vikiwa kwenye mabano –ni Regina Kamuli (Mkuranga, Pwani – Majiko
Banifu), Abiah Magembe (Kisarawe, Pwani – Usindikaji
wa Muhogo na Mtama), Magdalena Bukuku (Kinondoni, Dar es Salaam – Kilimo
cha Uyoga), Mariam Bigambo (Dakawa, Morogoro – Ufugaji
wa Nyuki), na Esther Muffui (Morogoro – Ukaushaji
wa Mboga na Matunda).
Wengine ni Farida Makame (Kilimanjaro – Majiko
ya Umeme-Jua), Leocadia Vedastus (Ukerewe, Mwanza – Kilimo
na Usindikaji wa Viazi Lishe), Monica Kagya (Kisarawe, Pwani – Ufugaji
wa Nyuki), Dkt. Sophia Mlote (Kinyerezi, Dar es Salaam – Kilimo
Hai cha Nyanya na Mbogamboga), na Evelyn Kahembe (Uvinza, Kigoma – Kilimo
cha Matunda).
Mradi huu wa Green Voices ambao mwaka huu uko
katika awamu ya pili, ulizinduliwa Julai mwaka 2016 na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan.
Katika awamu ya pili kinamama hawa
wameendelea kuboresha kilimo cha mazao yao kinachozingatia uhifadhi wa
mazingira na mabadiliko ya tabia nchi katika mikoa sita nchini.
Akinamama wa Green Voices wakati wa mafunzo ya siku sita kujifunza mbinu za kuboresha kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi na kuboresha mazao yanayotokana na kilimo wanachokifanya.
“Pamoja na kilimo, Mradi wa Green Voices
umaeandaa mafunz mbalimbali ya kuongeza ujuzi katika kilimo (climate smart
agricultura) pamoja na mafunzo ya jinsi ya kuandaa mazao au bidhaa
wanazozalisha kupitia kilimo,” alisema Mratibu wa Green Voices nchini Tanzania
Secelela Balisidya.
Katika kutekekelza hilo, Green Voices kupitia
mfadhili wake, Women for Africa Foundation, walishiriki katika mafunzo
mbalimbali ya Mbinu bora za kuweka nembo na kufungasha bidhaa za vyakula,
Viwango vya Ubora, na Kanuni za uchakataji wa vyakula.
Mafunzo hayo ambayo yalifanyika Julai 16 -22,
2017 yalizinduliwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani
Jaffo, ambaye aliahidi kuwapa ushirikiano akina mama hao.
Utengenezaji bidhaa na ufungashaji
Kwa siku
sita baada ya kuzinduliwa kwa mafunzo, akinamama hao walijifunza kuhusu Mchango
wa kilimo katika mabadiliko ya tabianchi, Jinsi ya kuweka mazingira bora ya
umwagiliaji, Mikakati ya biashara katika ujasiriamali wa kilimo, Utafutaji wa
rasilimali na mkakati wa kuongeza mtaji, Ukuzaji wa mtaji kupitia Vicoba, na Mbinu
za uongozi.
Akinamama
hao walipata fursa ya kutembelea Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la
Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) ambapo ilikutana na wajasiriamali walio
katika hatua za juu za kufungasha na kuuza bidhaa zao, ambapo walipata nafasi ya
kubadilishana nao mawazo ili kuongeza ujuzi wao.
Katika
mafunzo hayo, Linus Gedi ambaye ni mtaalam wa ubora wa chakula na viwango kabla
ya kuvipeleka sokoni, aliwaeleza washiriki kwamba ni muhimu kufungasha na
kuweka nembo kwani inasaidia kuhifadhi bidhaa na inarahisisha mteja kutambua hiyo ni bidhaa ya aina gani,
imetengenezwa wapi na ina mchanganyiko gani.
Akinamama wanaotekeleza mradi wa Green Voices walipotembelea Ofisi za SIDO jijini Dar es Salaam.
“Ni
muhimu sana kuhakikisha chakula hakisababishi maradhi, lakini pia kinafikia
malengo ya walaji, hii huepusha sumu kwenye chakula, mchanganyiko usiofaa,
upotevu wa chakula, kupoteza bidhaa na kuepukana na masuala ya kisheria,”
alisema Linus.
Alisema
uzalishaji wa chakula unatakiwa kuzingatia mbinu bora za uzalishaji na pamoja
na usafi.
Aidha,
aliwataka kuzingatia ubora, usafi na viwango vya chakula wanachozalisha ili
kifikia malengo ya walaji.
Kwa upande
wake, Richard Jackson akielezea umhimu wa kunadi bidhaa, alisema ni lazima kuwa
na mikakati imara ya masoko ili kuhakikisha mjasiriamali anapata faida.
Alisema ni
vizuri kujua wateja maalum na wateja wa ujumla na nini hasa wanahitaji ikiwa ni
pamoja na namna ya kuwafikia.
“Ni lazima
kujua kati ya wanaohitaji bidhaa zako, ni nani ambao siyo wateja wako walengwa
na kwa nini wateja wanunue bidhaa zako na siyo kwa washindani wako? Lazima ujue tabia zao na ukubwa wa soko lako,” alisema Jackson.
Aidha, alisema ni muhimu kuwajua wateja wako ili kuelewa
mahitaji yao na kwa nini wananunua bidhaa wanazonunua pamoja na kutambua mambo
yanayowaudhi ili usiwakwaze.
Kwa upande wa uchangishaji fedha na kutafuta
mitaji kwa biashara na kilimo, Rais wa VICOBA Endelevu Tanzania, Devota
Likokola, alieleza jinsi mfumo wa VICOBA Endelevu unavyoweza kuwasaidia
kinamama wa Green Voices kupata mitaji ya kuendeleza miradi yao.
Comments
Post a Comment