Featured Post

MWANDISHI AANIKA SIRI NZITO ZA MAUAJI YA ALBINO KWENYE KITABU

AKINAMAMA MOROGORO WAELIMISHWA JINSI YA KUKAUSHA MBOGA NA MATUNDA
 Embe zikiwa zinakaushwa katika kikundi cha Mzinga Green Voives kwenye Kijiji cha Konga, Manispaa ya Morogoro.

KWA Rahma Masenda (36), mkazi wa Kijiji cha Konga, Mzinga mkoani Morogoro, sasa mboga zake za majani hazitaweza kupotea tena kama ilivyokuwa mwanzo, kwani yeye na wenzake wamepata ufumbuzi wa kudumu.
Rahma anasema kwamba, hivi sasa wanaweza kukausha mboga zote – za bustani na za asili – kwa namna ambayo inawawezesha kuhifadhi muda mrefu pamoja na kuongeza mnyororo wa thamani.

Rahma na wenzake wameunda kikundi chao wanachokiita Mzinga Green Voices Women Group ambacho kinatekeleza mradi wa Green Voices unaolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira.
“Tumepata elimu ya kutosha kuhusu namna ya kukausha mboga mboga pamoja na matunda, tunatumia umeme-jua (solar) na kwa hakika tumeweza pia kujifunza jinsi ya kusindika katika ubora unaotakiwa ili tuingie kwenye soko la ushindani,” anasema Rahma, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kikundi hicho chenye wanachama 25.
Rahma anasema kwamba, kabla ya kupatiwa elimu hiyo miezi mitatu iliyopita, mboga zao zilikuwa zimetelekezwa mashambani na kwenye bustani kwa vile hata zinapopelekwa sokoni wanauza kwa bei ndogo.
 Banio linalotumia umeme-jua (solar power) ambalo linatumika kukaushia mboga mboga na matunda. Banio hili ndilo linalotumiwa na akinamama wa Mzinga Green Voices katika Manispaa ya Morogoro.

“Hivi sasa msimu wa kilimo umeishia na wengi wanayatumia mashamba hayo kulima bustani, mboga ni nyingi na zinatofautiana ubora, sasa ukipeleka sokoni unauza kwa bei ndogo, hivyo wengi hujikuta wakishindwa kilimo hicho na mboga nyingi kuharibika,” anaongeza mmoja wa wanachama wa kikundi hicho, Mwakaaje Mrisho.
Bi. Mwakaaje anasema kwamba, kwa miaka yote wamekuwa wakikausha mboga za majani kwa njia za asili lakini siyo za aina zote, hata hivyo baada ya kupatiwa elimu kupitia Mradi wa Green Voices wamegundua kwamba kumbe zipo fursa kubwa za kuongeza kipato kwa ukaushaji wa kisasa ambao unaongeza pia thamani.
“Hata maembe yetu ambayo zamani yaligeuzwa mpira na watoto ambao walikuwa wakiyapiga teke kutokana na kukosa walaji sasa tunaweza kuyakausha na kuyasindika kwa kutumia vifungio maalum, na bei yake ni kubwa kuliko kama tungeyauza vivi hivi,” anasema kwa furaha.
Mboga aina ya mnafu ikiwa imestawi vizuri katika shamba la mmoja wa wanakikundi cha Mzinga Green Voices. Mboga hizi ndizo zinazokaushwa na kikundi hicho.

Kwa ujumla, kila kabila nchini Tanzania lina utamaduni wa kuhifadhi mboga za majani na namna ya kuhifadhi.
Ukienda Dodoma, wakazi wa huko wanajua namna ya kukausha na kuhifadhi mboga za asili kama mlenda, mgagani pamoja na majani ya kunde kama ilivyo kwa wakazi wa mikoa mingine.
Hata hivyo, kutokana na kukosa utaalamu, wananchi wengi wamekuwa wakishuhudia mboga za majani zikiharibika mashambani huku hata zile zilizohifadhiwa nazo zikiharibika kutokana na kutohifadhiwa kitaalamu.
Bi. Esther Mfui, mratibu wa mradi huo wa Mzinga Green Voices Women Group, anasema kwamba, wanawake na jamii nzima ya Kijiji cha Konga hivi sasa wameongeza kasi ya kilimo cha mboga mboga na matunda baada ya mradi huo kupelekwa kijijini hapo.
Anasema kwamba, hivi sasa wakulima wengi wa Manispaa ya Morogoro wamekuwa wakifunga safari kutoka maeneo mbalimbali kwenda kujifunza namna ya ukaushaji wa mboga na matunda huku wengi, wakiwemo wanaume, wakitaka kujiunga na kikundi hicho.
“Kuna baba mmoja mkulima kutoka Kingolwira amefunga safari kutoka huko kuja huku ili ajifunze na amesema kwamba anakwenda kuwahamasisha wakulima wenzake wajiunge pamoja ili wapatiwe mafunzo hayo, tutawafundisha kwa sababu lengo ni kutaka kuhakikisha wakulima wanaongeza kipato na kuongeza usalama wa chakula, lakini kwa kuhifadhi chakula bora,” anasema.
Anasema kwamba, siku za nyuma ilikuwa vigumu kwa wananchi kupata mboga za majani nyakati za kiangazi, lakini kwa teknolojia hiyo mpya, wana uhakika wa kutumia mboga za majani mwaka mzima ilimradi tu zikaushwe kitaalamu na kuhifadhiwa.
Bi. Esther anasema kwamba, ukaushaji huo unaongeza thamani, kwani wanawake hao wamefundishwa namna ya kuweka katika vifungashio maalum na kuweka alama, ambapo inakuwa rahisi kwao kuuza bidhaa hizo kwa bei ya juu zaidi.
Yeye ni mmoja kati ya akinamama 10 wanaotekeleza mradi wa Green Voices, ambao unafadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ambayo inaongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.
Jumla ya akinamama 10 wanatekeleza miradi mbalimbali ya ujasiriamali nchini Tanzania inayoendana na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.
Mboga ni chakula kinachohitajika katika maisha ya kila siku, lakini wananchi wengi wamekuwa wakitumia mboga za majani kwa wingi katika kipindi cha masika tu na kuzikosa wakati wa kiangazi kutokana na kushindwa namna ya kuzikausha na kuzihifadhi.
Kwa teknolojia wanayotumia akinamama wa Mzinga Green Voices, sasa wananchi wanaweza kukausha kila aina ya mboga kuanzia mchicha, spinachi, Chinese, kabichi, kisamvu, nyanya na kadhalika, hivyo kujihakikishia aiba ya kutosha ya chakula.
Mboga za majani pamoja na matunda ni chanzo kikuu cha vitamini zinazohitajika katika mwili wa binadamu ambazo haziwezi kuhifadhiwa mwilini kama vile protini au wanga.
Hivyo ili kuuwezesha mwili kupata vitamini hizo ni muhimu kula mboga za majani kila siku, kwani mboga mbichi za majani zina vitamini zote zinazotakiwa na mwili kwa ukamilifu na hupatikana kwa msimu.
Ili ziweze kupatikana baada ya msimu wake, inabidi watumiaji wajue na watumie teknolojia za utayarishaji na uhifadhi wa mboga hizo.
Hifadhi ya mboga mbichi ni ngumu na huchukua muda mfupi sana kutokana na uharibifu unaosababishwa na vimelea vinavyosababisha magonjwa na kuoza.
Ili kuwezesha hifadhi ya muda mrefu na upatikanaji wake wakati wote, teknolojia za utayarishaji na ukaushaji wa mboga kama vile mchicha, majani ya mikunde, matembele, kabichi, majani ya muhogo (kisamvu) ni muhimu kuzingatia.
Wataalamu wanaeleza kwamba, usafi ni kanuni ya msingi katika ukaushaji wa mboga ambao mtu anayeshughulika na ukaushaji wa mboga na hifadhi, anapaswa kuwa na mwili safi na nguo zenye uwezo wa kuonyesha uchafu.
Mboga ni lazima zioshwe vizuri kwa maji safi na salama, vifaa na eneo la kufanyia kazi lazima viwe safi na visivyoshika kutu, na lazima mazingira yanayozunguka eneo la kutayarishia na kukaushia yawe safi.
Jambo jingine muhimu kuzingatiwa ni kwamba, ubora wa mboga zilizokaushwa hutegemea ubora wa mboga mbichi, hivyo malighafi zilizo safi na bora hutoa bidhaa bora baada ya kusindika.
Ubora wa mboga zilizokaushwa hutegemea usafi wa mboga mbichi pamoja na utayarishaji bora wa awali lakini pia hutegemea teknolojia iliyotumika kwenye ukaushaji na ufungashaji pamoja na hifadhi.
“Mboga mbichi za majani zilizooshwa vizuri na kukatwa zinapaswa kutayarishwa kabla ya kukaushwa ili kudumisha rangi, harufu na ladha. Utayarishaji wa mboga hizo hufanyika kwa kuziweka kwenye chujio kubwa safi au kitambaa safi cheupe na kuziweka kwenye maji yanayochemka kwa muda usiozidi dakika mbili, kisha hutolewa na kuachwa zipoe. Lengo ni kuzuia kazi ya vimeng’enyo vinavyosababisha mabadiliko yasiyotakiwa kwenye mboga. Utayarishaji huu pia hupunguza upotevu wa vitamini A,” anasema Bi. Esther Mfui.
Bi. Mfui anasema kwamba, matunda ya kukausha hutayarishwa kwa kuoshwa vizuri, kumenywa na kukatwa vipande vidogo vilivyolingana vya ukubwa kati ya milimita tatu hadi sita.
Anasema, mara nyingi hupitishwa kwenye mvuke wa maji moto au kuwekwa kwenye maji yanayochemka kama inavyofanyika kwa mboga, lakini kwa muda usizidi dakika tano.
Mara kwa mara chumvi au sukari au siki au tindikali aina ya sitriki (citric acid) hutumika kwenye utayarishaji wa matunda kabla ya kukausha kutegemea aina ya tunda na matakwa ya walaji.
Dhana ya ukaushaji wa mboga na matunda ni kupunguza maji yaliyoko ndani yake kutoka asilimia 90 hadi asilimia 10.
Bi. Mfui anasema, kukausha mboga au vyakula vingine na hifadhi kuna lengo la kuhakikisha chakula kinapatikana hata baada ya msimu. Teknolojia ya kukausha mboga na vyakula vingine inatumika toka zamani, ingawa kwa sasa ipo teknolojia bora zaidi.
“Kimsingi ukaushaji unasababisha vimelea kama bakteria na fangasi kushindwa kukua na kusababisha uharibifu wa vyakula hivyo, tofauti na kuvichemsha vyakula hivyo ambapo vimelea hivyo hufa.
“Wakati unapokausha unapunguza unyevu kiasi ambacho unaobakia kwenye vyakula hivyo hautoshi kusababisha ukuaji na uongezekaji wa vimelea hivyo. Aidha vyakula vilivyokausha vikipata tena maji vimelea hukua kwa kasi na huongezeka na kusababisha uharibifu wa vyakula hivyo,” anasema.

Mwanahabari Tukuswiga Mwaisumbe (kulia) akipiga vigelegele baada ya kumaliza kupanda mti wa ukumbusho wa kikundi cha Mzinga Green Voices.

Uwepo wa teknolojia hiyo utaongeza kasi ya uzalishaji wa mboga mboga, mazao ambayo yanazalishwa kwa wingi nchini China ambapo kwa mwaka 2015 pekee nchi hiyo ilizalisha takriban tani milioni 580, ambapo inauza nchi za nje.
“Ukaushaji na usindikaji wa mboga ni biashara nzuri kwa akinamama na jamii kwa ujumla, unaweza kuongeza pato la taifa kwa sababu ikiwa akinamama hawa watapatiwa nyenzo za kutosha kwa kuongezewa mtaji na kupanua kiwanda, wanaweza wakauza mboga kavu hata nje ya nchi,” anasema Mohammed Omar Mwalimu maarufu kama Chamuzhimu, ambaye ni Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Manispaa ya Morogoro.
Chamuzhimu anawashauri akinamama hao kupanua mashamba yao, lakini pia waanzishe na miradi ya ufugaji wa kuku na samaki, kwani mabaki ya mboga mboga ni chakula bora kwa kuku na samaki.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, ambaye muda mfupi baada ya mwandishi wa Makala haya kufanya naye mahojiano akateuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, anasema kwamba ili kupambana na mfumo dume pamoja na kuongeza kipato kupitia ujasiriamali, ni lazima wajifunze.
Anasema Halmashauri ya Manispaa imewajengea jengo maalum akinamama, ambapo watafundishwa ujasiriamali pamoja na kuendesha shughuli zao.
“Nawapongeza akinamama wa Mazinga ambao kwa kweli wanaleta mapinduzi katika suala zima la ukaushaji na uhifadhi wa mboga, lakini naona changamoto kubwa ni usindikaji (packaging), soko lipo kubwa,” anasema.
Katika mahojiano hayo, Bi. Mahongo alisema kwamba serikali imejizatiti katika kuwawezesha wanawake katika shughuli za maendeleo na akawataka wajitokeze kila wakati kushiriki maonyesho mbalimbali ya bidhaa za kilimo.
Ukaushaji wa mboga mboga unakwenda sambamba na ukaushaji pia wa ndizi, ambazo zinaongezeka ubora katika mnyororo wa thamani. Hili ni shamba mojawapo la mwanakijiji wa Konga, Mzinga katika Manispaa ya Morogoro.