DC UKEREWE ASHAURI WANANCHI KULIMA VIAZI LISHE KWA WINGI Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandez akisalimiana na viongozi wa serikali wilayani Ukerewe mara baada ya kuwasili katika bandari ya Nansio tayari kwa kuzindua mradi wa wanawake.


 Mama Maria Tereza akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya mkuu wa wilaya Ukerewe.
 Mama Maria Tereza akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wilaya. Kushoto kwake ni Balozi Getrude Mongella.
Wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara mjini Nansio.

MKUU wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Estomih Chang’a, ameshauri wananchi wa wilaya hiyo kulima kwa wingi viazi lishe (viazi vitamu vya njano) ili kuongeza uhakika wa chakula.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kilimo cha viazi lishe wa kikundi cha wanawake wa Green Voices Bukongo Jumanne Julai 12, 2016, DC Chang’a alisema kwamba kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira, ni vizuri wananchi kugeukia kilimo cha viazi lishe ambavyo vinastahimili ukame, lakini pia vina tija kubwa kwa kuongeza pato la familia.
“Ninashauri wananchi wote wa Ukerewe kulima viazi lishe kwa sababu mbali ya kuongeza akiba ya chakula, lakini vinaongeza pato la familia na taifa hasa vikichakatwa ili kutoa bidhaa mbalimbali,” alisema.
Kikundi cha wanawake 25 cha Green Voices Bukongo katika mji wa Nansio, kinachoongozwa na Leokadia Vedastus kinatekeleza mradi wa kilimo cha viazi lishe pamoja na uchakataji wa bidhaa mbalimbali za zao hilo ikiwa ni jitihada za kuwawezesha wanawake kushiriki miradi inayolenga kutunza mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandez de la Vega, alivutiwa na mradi huo na kusema ni vizuri jamii ikahamasishwa kulima zao hilo ili kujikomboa kiuchumi pamoja na kujihakikishia usalama wa chakula.
Mama Tereza, ambaye ni Rais wa taasisi ya Women for Africa Foundation inayofadhili miradi ya Green Voices Tanzania, aliwataka wanawake wa kikundi hicho waongeze juhudi pamoja na kuwa waalimu wa wenzao kuhakikisha kilimo hicho kinasonga mbele.
“Dunia inapambana na mabadiliko ya tabianchi, sasa mradi huu unapaswa kuwakomboa akinamama kwa sababu unawahakikishia upatikanaji wa chakula kwa familia na wanaweza kuongeza mnyororo wa thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali,” alisema.
Naye balozi wa Mfuko huo wa Wanawake Afrika, Getrude Mongella, akizungumza katika uzinduzi huo kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Bukongo mjini Nansio, aliwaomba watendaji wa serikali kusimamia kidete mradi huo ili kuondoa njaa katika visiwa vyote vya wilaya ya Ukerewe.
Alisema kwamba, kuanzishwa kwa mradi huo wilayani humo siyo tu kutawakwamua wanawake na wananchi wote, lakini pia kunaifanya Ukerewe kuwa kiini cha usambazaji wa zao hilo katika maeneo mengine ya Mkoa wa Mwanza.
“Ninawaomba watendaji wa serikali ya wilaya hamasisheni zao hili lilimwe katika visiwa vyote na kama ilivyokuwa zamani ambao mbegu zote za pamba zilitoka Ukerewe, basi tengenezeni na zalisheni mbegu za kutosha msambaze katika wilaya nyingine za Mkoa wa Mwanza.
“Naamini mkoa wote ukilima zao hili njaa haitakuwepo na wanawake wanaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo wakiziuza zitawakwamua kiuchumi,” alisema.
Awali, kabla ya uzinduzi huo, Mama Maria Tereza na ujumbe mkubwa kutoka Dar es Salaam walitembelea mradi husika na kujionea kilimo hicho pamoja na uoteshaji wa mbegu, ambapo mshiriki kiongozi wa mradi huo, Leokadia Vedastus, alisema kwamba ekari moja iliyostawi vizuri inaweza kutoka jumla ya tani 7 (kilogramu 7,000) za viazi.
Mbali ya kiasi hicho, Leokadia alisema kwamba, viazi hivyo licha ya kuliwa kwa mapishi ya kawaida, lakini bado vinaweza kuchakatwa na kutoa bidhaa zaidi ya hamsini zikiwemo pilau la viazi, maandazi, kaukau (chips), chapatti, tambi na sambusa.
Leokadia ni mmoja wa wanawake 15 ambao walipatiwa mafunzo nchini Hispania mapema mwaka huu kuhusu uanzishaji wa miradi inayoendana na utunzaji wa mazingira na baada ya kurejea alifanikiwa kuwaunganisha wanawake 25 kutekeleza mradi huo.
Hata hivyo, alisema kwamba mpaka sasa wanawake wengi wamekuwa wakijitokeza kutaka kujifunza, ambapo alibainisha kwamba wameamua kuendesha mafunzo kila Jumamosi ili kuwapa fursa wanawake wengi kushiriki katika kilimo hicho.
Kwa upande mwingine, Leokadia amehamasisha mradi huo hadi kwa wanafunzi wa sekondari ambao wamepatiwa elimu ya uelewa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na namna ya kupambana na uharibifu wa mazingira na mpaka sasa jumla ya wanafunzi 50 ambao ni mabalozi wa vita dhidi ya uharibifu wa mazingira wamekwishapatikana.
Mradi wa Green Voices unatekelezwa nchini Tanzania katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na Kilimanjaro ambapo wanawake 10 wanatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kilimo cha viazi vitamu, kilimo hca matunda, kilimo cha uyoga, mboga mboga, ufugaji wa nyuki, usindikaji wa mazao ya muhogo, ukaushaji wa mboga mboga na kadhalika.
Nchini Tanzania, mradi huo unaratibiwa na Secelela Balisidya.