- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
BINAFSI nimezaliwa
katika jamii ya wafugaji ambayo ulaji wa nyama, hasa ya mbuzi, ni sehemu ya
maisha. Nakumbuka tangu nikiwa mdogo wakati tunaishi kwenye maboma porini
mwanzoni mwa Vijiji vya Ujamaa, haikuwahi kupita siku tatu kabla baba yangu
hajachinja mbuzi ambaye tulimbanika huku tukimtafuna wakati baba akitusimulia
hadithi.
Ingawa
tulikuwa na kundi kubwa la ng’ombe zaidi ya 1,000, lakini mbuzi walikuwa ni
wengi pia pamoja na kondoo ambao sisi watoto tuliwachunga pamoja na ndama. Ilikuwa
nadra sana kukuta baba yetu akimchinja kondoo, kwa sababu huyo alikuwa kwa
nyakati maalum, hasa pale vijana wanapokwenda jando ambapo walikunywa mafuta
yake.
Lakini kwa
mbuzi, nyama ilikuwa kitu cha kawaida hasa tunapokosa mawindo ya nyamapori.
Wakati mwingine watoto watukutu waliweza kumjeruhi mbuzi mkorofi kwa makusudi
ili kumshawishi mzee amchinje. Unajua mbuzi wa asili ni wakorofi sana na
wanaweza kukimbilia kwenye mashamba ya watu wakati wewe ukihangaika na ndama.
Hata hivyo,
ufugaji wa wakati ule ulikuwa ni wa asili na mazowea. Hakuna aliyefuga mbuzi
kwa ajili ya biashara, labda kama kulikuwa na mahitaji kidogo nyumbani ambapo
mzee angewachukua kadhaa na kuwapeleka mnadani kwa ajili ya fedha za matumizi
kama nguo na kadhalika. Usiulize kuhusu masuala ya hospitali, kwa sababu wengi
tulitumia mitishamba tu.
Lakini kwa
kadiri maendeleo yalivyoongezeka, misitu imepungua ya kumfanya mtu kuwa na
kundi kubwa la ng’ombe huku watu wakitafuta ardhi kwa ajili ya kilimo. Ni changamoto
kubwa sana huku ikichangiwa na mabadiliko ya tabianchi. Ufugaji wa mbuzi nao umepungua
pia huku serikali ikihimiza wananchi kufuga kisasa kwa kuangalia uchumi.
Mbuzi wana
soko kubwa kila mahali. Hapo ulipo au katika miji mikubwa, lakini si watu wengi
wanaofuga mbuzi, tena kibiashara.
Kwa hiyo
basi, ni vizuri tukajifunza namna nzuri ya kufuga mbuzi wa nyama kisasa. Kama
unao tayari, elimu hii itakusaidia kuboresha, lakini kama bado, unaweza
kushawishika kuanzisha mradi wa ufugaji mbuzi hata hapo ulipo.
Mbuzi ni
tofauti na ng'ombe kwa sababu ni wastahimilivu sana dhidi ya ukame. Wanakula
nyasi pia wanakula majani na magome ya miti. Kama nyasi zimekwisha au kukauka
wataendelea kuishi na kuzaliana kwa kula majani ya miti.
Kwa ujumla,
ufugaji wa mbuzi wa nyama ni fursa muhimu kwa wananchi wengi kujipatia
maendeleo hasa ukiongeza thamani kwa kuwafuga kisasa ili kupata soko zuri. Kama
utazingatia kanuni za ufugaji, hakika mbuzi anaweza kukupatia faida kubwa na
kupunguza umaskini.
Ikiwa
umevutiwa, basi tunaweza kuendelea na mjadala wetu.
Jambo la
msingi kabisa ni kwamba lazima uwe na eneo la kufugia, walau shamba lenye
ukubwa wa ekari moja. Ni ndani ya shamba hili ambako mbuzi wanatakiwa wajengewe
banda bora na wapate eneo la malisho.
Mbuzi
wanapenda kulala kwenye banda kavu, lililoinuliwa na kuezekwa vizuri ili
kuwakinga na jua na mvua, lakini pia lililozungushiwa kuta (za udongo, mbao au
mabati) kuwakinga na upepo mkali. Mwanga na hewa ya kutosha ni vitu muhimu
sana. Banda la mbuzi siyo ghali, kwani linaweza kujengwa kwa rasilimali
zinazopatikana mahali ulipo – miti, mabanzi, nyasi.
Ukiamua kufuga
mbuzi kwa lengo la kibiashara unaweza kupata faida kubwa kwa sababu kwa kawaida
mbuzi anazaa mara mbili kwa mwaka. Anabeba mimba kwa miezi mitano (yaani siku
145 hadi 155) na wananyonyesha kwa miezi miwili.
Wapo mbuzi
ambao wanazaa mapacha, na kwa hiyo unaweza kuongeza kundi lako katika muda
mfupi.
Kwa kawaida,
mbuzi anakuwa tayari kuzaa anapofikisha miezi 7 hadi 8. Hata kama mbuzi wako
siyo wa kuzaa mapacha, lakini kama wanazaa mara mbili kwa mwaka, ukianza na
mbuzi 20, una uhakika kwamba kwa mwaka mmoja utakuwa umeongeza mbuzi 40, ambao
kwa mwaka unaofuata – ikiwa majike watakuwa 20 kati ya watoto hao, basi
utaongeza mbuzi 120 na katika mwaka wa tatu utakuwa umeongeza mbuzi wengine
240, hivyo jumla unaweza kuwa na kundi la mbuzi 320 ndani ya miaka mitatu.
Kama unataka
kuzalisha zaidi, basi unaweza kuamua kuwauza madume na kubakiwa na majike
ambayo yataendelea kuzaa na kuongeza kundi lako.
Faida za
mbuzi ni nyingi sana, lakini mbali ya kuwauza wakiwa hai, ukiwachinja utapa
nyama, ngozi, kwato na pembe ambazo ni rasilimali nyingine zinazoweza kuuzwa
kwenye viwanda ili kuzalisha bidhaa nyingine za ngozi na nta.
Katika
nchi nyingi, nyama ya mbuzi inapendwa sana kwa sababu ni tamu na haina lehemu
(cholesterol) wala mafuta mengi kulinganisha na nyama nyingine.
Aina ya mbuzi wa nyama
Inawezekana
umesikia aina mbalimbali ya mbuzi, lakini hujajua ni wepi wanaofaa kufugwa kwa
ajili ya nyama. Ukumbuke kwamba, wapo mbuzi wanaofugwa kwa ajili ya nyama,
maziwa, na nyuzi.
Sasa hapa
tunazungumzia mbuzi wa nyama tu na kidogo mbuzi wanaofugwa kwa ajili ya nyuzi,
makala nyingine zinaelezea kwa kina mbuzi wa maziwa na aina zake.
Boer
(Mbuzi Kaburu)
Mbuzi
wanaofaa zaidi kwa nyama hasa unapofuga kibiashara ni jamii ya Boer (maarufu
kama Mbuzi Kaburu), ambao ni chotara wanaokua kwa haraka, wana umbo kubwa,
nyama yao ni ya kiwango cha juu.
Mbuzi
hawa wana rangi nyeupe, kichwa chenye rangi ya udongo au nyekundu, masikio
makubwa na pembe ambazo zimepinda kwa nyuma na chini.
Mbuzi
jike mkubwa wa jamii ya Boer ana uzito wa kilogramu kuanzia 68 hadi 102, wakati
beberu mkubwa ana uzito wa kilogramu 80 hadi 150.
Unaweza
kuona ni kwa jinsi gani mbuzi hao wanavyokuwa wakubwa na uzito mkubwa sana.
Kiko
Kiko ni
jamii ya mbuzi inayokuja kasi baada ya Boer hata katika utoaji wa nyama. Wana uwezo
wa kula nyasi na kuzibadili kuwa nyama, hivyo wananenepa haraka. Mbuzi hawa
wanaweza kuwa na rangi tofauti, ingawa wengi wao ni weupe. Pembe za beberu ni
ndefu zilizojiviringa wakati pembe za jike ni fupi. Jike ana uzito wa kilogramu
45 na beberu ana uzito wa kilogramu 80.
Pygmy
(Mbuzi Mbilikimo)
Mbuzi
jamii ya Pygmy ni wadogo kwa umbo lakini wenye miili imara na minene iliyojaa
minofu; miili yao ni mipana. Mbuzi hawa wana manyoya marefu. Mbuzi jike mkubwa
ana uzito wa kati ya kilogramu 16 hadi 23, na beberu mkubwa ana kilogramu kati
ya 20 hadi 32.
Pamoja na
udogo wake, lakini mbuzi aina ya Pygmy wanatoa kiwango sawa cha maziwa kama
mbuzi jamii ya Nigerian Dwarf ingawa Pygmy huwa hawakamuliwi mara kwa mara
kutokana na udogo wa matiti yao.
Spanish
Kabla
mbuzi jamii ya Boer na Kiko hawajawa maarufu, hususan Marekani, mbuzi wengi
waliofugwa kwa ajili ya nyama walikuwa wakiachwa kujitafutia wenyewe chakula kwenye
mabonde na vichakani Kusini na Kusini Magharibi mwa Marekani ili kusafisha
mashamba yasiwe na vichaka na nyasi – kama ilivyo kwa mbuzi wetu wa asili hapa
Tanzania.
Mbuzi hao
huko Marekani waliitwa Spanish kwa sababu walipelekwa kwa mara ya kwanza na
wapelelezi wa Kihispania na wakaachwa huko ili wawafae kwa kitoweo wakati
mwingine watakaporejea tena.
Kwa vile
mbuzi hao wanatofautiana kwa maumbo na rangi, kwa hiyo jina la Spanish
halimaanishi aina moja ya mbuzi. Mbuzi jike mkubwa ana uzito wa kilogramu kati
ya 30 hadi 60 wakati beberu ana uzito wa kati ya kilogramu 36 na 91.
San
Clemente
Katika
miaka ya 1500, mbuzi wa Kihispania waliachwa kwenye Kisiwa cha San Clemente,
kutoka Pwani ya California jirani na San Diego. Mbuzi hao walizaliana na
wameendelea kuzaliana huko hivyo kupewa jina la San Clemente. Wakati fulani
mbuzi walikuwa wengi mno kisiwani humo kiasi kwamba walikaribia kuharibu
mazingira ya kisiwa, hivyo ikabidi wapunguzwe.
Mbuzi wa
jamii hii ni wadogo na wana nyama nzuri kuliko jamii nyingine ya mbuzi kutoka
Hispania, na pembe zao zinakuwa ndefu kwa kwenda juu.
Mbuzi
hawa wana rangi tofauti na mabaka ya rangi ya udongo au nyeusi. Mbuzi jike
mkubwa ana uzito wa kati ya kilogramu 15 na 32 wakati bebeeru lina uzito kati
ya kilogramu 18 na 36.
Myotonic
Hawa ni
jamii ya mbuzi ambao hawapatikani sana ingawa wanafugwa kwa ajili ya nyama. Ni
mbuzi ambao mara nyingi wanaitwa ‘mbuzi wa kuzimia’ kwa sababu wanakuwa na
ulemavu fulani ambao kitaalam unaitwa myotonia. Mbuzi mwenye ulemavu wa aina
hiyo ambao hutokana na ulemavu wa jeni mara nyingi hukumbwa na hofu wanaposikia
kelele, misuli hukakamaa na miguu hufa kazi. Kama mbuzi huyo atapata na mshtuko
huo kwa ghafla, anaweza kudondoka na hawezi kuinuka mpaka misuli ya miguu
ilegee.
Kwa
mfugaji mwenye mbuzi hao, ambaye kila mara atakuwa akiwaminya misuli kwenye
miguu, huwafanya mbozi hao kuwa na minofu mingi kwenye mapaja, hivyo kuwa
wanyama bora kwa nyama.
Kutokana
na ulemavu huo, ambao hauna madhara kwa kula nyama yake, huwafanya mbuzi hao
wasiwe wasumbufu na kuwa watulivu daima.
Hata hivyo, nchini Tanzania kuna mbuzi wengine chotara walioboreshwa ambao waliwahi kugawiwa kwa wafugaji katika mradi maalum. Wasiliana na ofisa mifugo aliye jirani ili akuelekeze vyema ni aina gani ya mbuzi wanaofaa kufugwa katika eneo lako na hasa hao walioboreshwa na namna ya kuwapata. Mbuzi walioboreshwa mara nyingi huzaa pacha.
Hata hivyo, nchini Tanzania kuna mbuzi wengine chotara walioboreshwa ambao waliwahi kugawiwa kwa wafugaji katika mradi maalum. Wasiliana na ofisa mifugo aliye jirani ili akuelekeze vyema ni aina gani ya mbuzi wanaofaa kufugwa katika eneo lako na hasa hao walioboreshwa na namna ya kuwapata. Mbuzi walioboreshwa mara nyingi huzaa pacha.
Kwa mawasiliano nipigie au nitumie ujumbe wa
whatsapp kupitia namba 0656-331974, au niandikie barua pepe: maendeleovijijini@gmail.com. Twitter:
@MaendeleoVijiji; Facebook: Maendeleo Vijijini; Instagram #maendeleovijijini. Daima
usikose kutembelea www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Comments
Post a Comment