Featured Post

MWANDISHI AANIKA SIRI NZITO ZA MAUAJI YA ALBINO KWENYE KITABU

 Jalada la kitabu cha ‘MIFUPA YA ALBINO’.
Mwandishi Daniel Mbega, akiwa ameshikilia Karunguyeye waliokaushwa nyumbani kwa mganga wa jadi.

MWANDISHI wa habari mwandamizi nchini, Daniel Mbega, amekamilisha kuandika kitabu kinachofichua siri zilizo nyuma ya pazia kuhusiana na mauaji ya vikongwe na albino nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Mwandishi huyo, ambaye alifanya utafiti kwa kipindi cha miezi nane mfululizo katika mikoa 10 ya Kanda ya Maziwa Makuu, amesema kitabu hiyo alichokipa jina la ‘MIFUPA YA ALBINO’ kinatarajiwa kuwaingia kiwandani wakati wowote.
Bw. Mbega amesema kwamba, katika utafiti wake huo alifanikiwa kukutana na waganga wa jadi, wachawi na matapeli katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Simiyu, Mwanza, Kagera, Mara, Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa, ambako alikaa kwa miezi miwili akifanya uchunguzi.
“Nimekamilisha, nimeona nijikamue ninavyoweza ili kitabu hiki kitoke. Nimetumia zaidi ya miezi minane nikiwa porini, nikirusurika kukatwa mapanga, ajali na hatari mbalimbali kwa ajili ya kupata ukweli unaosababisha mauaji dhidi ya ndugu zetu wenye ualbino.
“Nimetamani sana kitabu hiki kitoke pamoja na kushindwa kupata udhamini popote. Najua ujumbe uliomo ni muhimu sana kuliko fedha, nahitaji jamii isome na ielewe yale yanayoendelea.
"Nilikutana na wakata mapanga, wanasiasa, waganga, wachawi na watu wa kila aina. Nililazimika kukamata matunguri kwa waganga na wachawi, nikakutana na pembe zilizojaa damu za watu na makorokoro mengine ambayo hayafai hata kusimulia,” aliongeza.
Aidha, amesema kwamba, katika uchunguzi wake huo alishiriki pia kikamilifu katika misako mbalimbali ya wahalifu walioshiriki kwenye matukio hayo na kushuhudia namna vyombo vya ulinzi na usalama vinavyotenda kazi.
Kunusurika kifo kwa ajali ama kuzingirwa na baadhi ya wananchi ni moja ya hatari alizokumbana nazo wakati wa uchunguzi wake, huku akisafiri umbali wa zaidi ya kilometa 40,000 katika kipindi hicho.
“Wakati mwingine nilikosa usingizi hata kwa siku tano mfululizo, nililazimika kusafiri mchana na usiku katika mazingira mengi hatarishi nikikusanya habari,” alisema.
Akaongeza: “Haikuwa kazi rahisi kuweza kufanya mahojiano na waganga wa jadi, achilia mbali wachawi ambao baadhi yao waliamua kujiweka wazi na kueleza mambo yanayotendeka katika ulimwengu wa giza na jinsi yanavyohusiana na mauaji ya wenye ualbino.”
Alisema katika uchunguzi huo alikumbana na mambo mengi ya ajabu ikiwa ni pamoja na kushika matunguli, pembe zinazofoka damu, damu na maiti, mifupa inayodhaniwa kuwa ya binadamu na mambo mengine kadha wa kadha.
Aidha, alisema kwamba, alizungumza pia na wanamichezo, baadhi ya viongozi wa dini ambao nao wanatumia nguvu za giza ambapo waganga walieleza jinsi nao wanavyoshiriki katika matukio hayo ya mauaji ya wenye ualbino.
“Ni mtandao mpana sana, siyo Tanzania tu, bali hata katika nchi jirani za Kenya, Malawi, Burundi, Msumbiji, Afrika Kusini na Swaziland… naamini kkitabu hiki kitaiamsha jamii na kubadilisha mitazamo ya watu mara watakapojifunza yale niliyoyakusanya kutoka kwa vinywa vya wahusika wenyewe,” amesema na kusisitiza kwamba amepanga kitabu hicho kiwwe mtaani mwishoni mwa mwezi Septemba ikiwa atapata msaada wa kufanikisha uchapaji. 
Mganga wa jadi akimpigia ramli mwandishi wa kitabu hiki (hayuko pichani) baada ya kutoa Shs. 2,000 akitaka amwangalizie kwanini 'mkewe' (askari mmoja wa kike aliyekwenda naye wakiwa kikazi) alikuwa hazai. Mganga alisema mwanamke huyo alikuwa 'amelogwa' na mwanamke aliyetaka kuolewa na mwandishi halafu yeye akamkataa, ambapo kiuhalisia hakuwepo mwanamke wa aina hiyo na hata huyo aliyekwenda naye walikutana kikazi na hawakuwa wakifahamiana kabisa. 
Mtoto Baraka Cosmas akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya baada ya kukatwa kitanga cha mkono Machi 7, 2015.
Mwandishi Daniel Mbega (mwenye fulana nyekundu na kofia ya sweta) akiwa sambamba na wanausalama katika nyumba ambamo Baraka Cosmas alikatwa kitanga cha mkono Machi 7, 2015.
Mtuhumiwa Sajenti Kalinga Malonji akiwa chini ya ulinzi baada ya kukishusha kiganja cha Baraka Cosmas kwenye mti nyumbani kwake kijijini Hanseketwa, Mbozi siku ya Jumapili, Aprili 26, 2015. Sajenti tayari amehukumiwa miaka nane jela na wenzake wamehukumiwa vifungo vya hadi miaka 20 jela.
Mwandishi Daniel Mbega, akiwa kwa mganga huko Kachwamba, wilayani Chato wakati akifanya uchunguzi wa mauaji ya albino.

Comments