TANGU mwaka 1884 fedha
zilizotumika Tanganyika zilikuwa ni sarafu, noti zilianza kutumika mwaka 1905 wakati
wa utawala wa Mjerumani.
Noti hizo zilitolewa
katika thamani ya Rupie 5, 10, 50, 100 na 500. Zanzibar mwaka huohuo wa 1905, noti
za Rupie za Zanzibar zilitolewa katika thamani za Rupie 5, 10, 20, 50, 100 na
500.
Mbali na rupia
iliyodumu kwa muda mrefu katika matumizi ya noti nchini, tangu kupatikana
uhuru, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuwa ikibadilisha noti
zake kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo sheria inayoiruhusu kufanya hivyo
katika kipindi cha miaka mitano mpaka saba.
Kutokana na mamlaka
hayo, BoT, kuanzia mwaka 1966 imefanya mabadiliko kadhaa ya
sura za noti zake pamoja na alama za kiusalama.
Pia kutokana na
kupanda na kushuka kwa thamani ya shilingi, BoT imekuwa ikitoa noti zenye
thamani tofauti tofauti (denomination),
kuanzia ile ya Shs. 10 mpaka sasa ambapo noti yenye thamani ndogo ni Shs. 500
huku kubwa ikiwa ya Shs. 10,000.
Katika historia ya
mabadiliko ya noti, mwanzo kabisa ilikuwa ni mwaka 1966 ambayo yalihusu noti ya
Shs. 20 iliyokuwa na sura ya Rais wa Kwanza wa Tanzania na Shs. 100
'Mmasai' pamoja na nyingine iliyokuwa na simba.
Ilipofika mwaka 1978, Benki Kuu ilitoa
tena noti za Shs. 10 na Shs. 20.
Mabadiliko mengine
katika sura ya noti yalifanyika miaka ya 1985, 1987, 1989, 1990 kwa kuwa na
noti ya Shs. 50 ambayo ilikuwa na sura ya Rais wa Pili Ali Hasani
Mwinyi, pundamilia na picha nyingine zilizokuwa zikiashiria mavuno.
Noti ya Shs. 1,000
yenye sura ya Rais Mwinyi na tembo iliingia mwaka 1993 na mwaka 1995 ilingia
noti ya Shs. 10,000 yenye sura ya Rais Mwinyi na simba.
Mwaka 2000 kuliingizwa
noti ya Shs. 1,000 ikiwa na sura ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere,
tembo na mgodi wa makaa ya mawe, wakati mwaka 2003 ilikuja noti ya Shs. 500 ikiwa na picha ya
nyati, jengo la Nkurumah lililopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na
nyoka.
Mwaka huo huo iliingia
noti ya Shs. 5,000 ikiwa na faru na mgodi na noti ya Shs. 10,000
ikiwa na jengo la benki na tembo.
Kimsingi mpaka sasa
BoT imefanya mabadiliko makubwa ya sura za fedha za Tanzania mara saba,
mabadiliko yaliyohusisha rangi, alama (picha) na alama za usalama wa fedha
hizo.
Mbali na mabadiliko
hayo, Desemba 17, 2010 BoT ilizindua noti mpya ambazo zilianza kutumika rasmi
kwenye mzunguko wa fedha kuanzia wiki ya kwanza ya Januari mwaka 2011.
Wakati wa utambulisho wa noti hizo mwaka
2010, Gavana wa zamani wa BoT, Profesa Beno Ndulu alisema noti hizo mpya zingekuwa
na mabadiliko mbalimbali ikiwemo rangi na alama za utambulisho ambazo zilikuwa na sura za
waasisi wa taifa, Mwalimu Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani
Karume.
“Katika noti za sasa,
kutakuwa na saini Gavana aliyepo pamoja na Waziri wa Fedha aliyepo madarakani,”
alisema
Profesa Ndulu.
Mabadiliko hayo yalizihusha noti zote na
Profesa Ndulu alisema tofauti na za awali, noti za sasa zina alama mpya
tatu, zitakazolinda usalama wake dhidi ya watu wanaoghushi ambao alisema uwezo wao unakuwa
kila siku kutokana na kukua kwa teknolojia.
Alisema alama zilizowekwa
ni pamoja na ile iliyojificha ya picha ya Mwalimu Nyerere inayochukua nafasi ya
twiga katika noti za viwango vyote.
Alama nyingine mpya
kabisa katika teknolojia ya utengenezaji fedha ni ile ambayo inaonekana kama
inatembeatembea wakati noti inapokuwa ikigeuzwa na nyingine ambayo inabadilika
au kugeuka rangi.
Kadhalika, alisema mbali na
kupunguzwa ukubwa, noti hizo zinatambuliwa kirahisi na walemavu wa macho
kutokana na alama maalum zilizowekwa kwa ajili yao katika kila kiwango.
Alama hizo ni pamoja
na mistari iliyovimba, pamoja na ile ya V ambazo zimewekwa kwa idadi maalum
inayoelezea kila kiwango cha noti husika.
Mabadiliko mengine yalifanywa katika picha za
wanyama simba, nyati pamoja na tembo ambao awali, picha zao zilikuwa
zikionyesha miili yao yote, katika noti za sasa ni picha za vichwa vyao tu zinazoonekana.
Kitu kingine
kinachozitofautisha noti za sasa na zile za zamani ni karatasi zilizotumika
kuzitengenezea.
Noti za sasa zimetengenezwa kwa pamba kwa asilimia 100
tofauti na noti za zamani ambazo karatasi zake zinatokana na mbao.
“Kampuni inayochapisha
noti zetu, ndiyo pia inayochapisha baadhi ya denomination (noti) ya Marekani, kwa hiyo karatasi zinazotumika
kutengeneza Dola ya Marekani ndizo hizo hizo zinazotengeneza fedha
zetu,” alisema Profesa Ndulu.
Kwa mujubu wa Profesa
Ndulu, mchakato wa kubadilisha noti ulianza Aprili mwaka 2009 na mchakato wa
zabuni uliendeshwa na hatimaye makampuni kumi na moja kujitokeza ingawa tisa
ndiyo yaliyoingia katika ushindani.
Kampuni ya Crane AB ya
Sweden ilishinda kutengeneza noti za Shs. 500, Shs. 2,000, Shs. 5,000 na Shs. 10,000 huku kampuni ya Adae La Rue ya
Uingereza ikishinda zabuni ya kutengeneza noti za Shs. 1,000.
Profesa Ndulu alisema gharama ya uchapishaji vipande 1,000
imeshuka ikilinganishwa na wakati ambao Tanzania ilikuwa ikichapa noti zake
katika kampuni ya Giesecke & Devrint ya Ujerumani.
“Kama mwanzo tulikuwa
tukichapisha vipande 1,000 kwa Shs. 10, sasa tunachapisha kwa Shs. 7,” alisema Profesa Ndulu.
Alisema kupungua kwa
gharama hizo kunatokana na ushindani katika kupambanisha wazabuni.
Anasema kwa kawaida
wastani wa noti yoyote kuishi katika mzunguko ni miezi saba na kuwa kutokana na
ubora wa noti za sasa, zitaweza kuishi kwa muda huo ili
kuipunguzia benki gharama ya kuchapisha fedha mara kwa mara kutokana na
uchakavu.
Licha ya madai ya
kushuka kwa uchumi hivyo kupungua kwa thamani ya shilingi, Profesa Ndulu alisema BoT haina mpango
wa kuchapisha noti yenye thamani zaidi ya Shs. 10,000 inayotumika sasa.
“Labda mpaka shilingi
yetu ifikie pabaya sana, lakini kwa sasa tutaendelea kutumia hizi hizi
zilizopo,” alisema Profesa Ndulu.
Mkurugenzi wa mauzo wa
kampuni ya Crane AB, Peter Brown, alisema alama za usalama ambazo zimetumika
katika utengenezaji wa noti hizo ni teknolojia mpya kabisa ambayo haijawahi
kutumiwa na nchi yoyote ya Afrika. Alisema alama hizo ni hatimiliki ya kampuni
hiyo ambayo ilitumia miaka mitatu kuzitengeneza.
“Kutokana na
teknolojia iliyotumika kutengeneza alama za usalama za noti hizo, si rahisi mtu
yeyote kuzigushi,” alisema Brown.
Pia alisema kutokana na kukua
kwa tekinolojia, ni vyema nchi zikawa na utaratibu wa kubadilisha noti zake
kila baada ya muda unaoshauriwa kisheria ili kupambana na wimbi la watu waoghushi.
Alisema kampuni yake inachapisha
noti ya Dola 100 ya Marekani na kuwa teknolojia inayotumika kutengeneza fedha hiyo
yenye soko kubwa duniani ndiyo inayotumika pia kutengeneza noti za Tanzania
ambazo zinatatengenezwa na kampuni hiyo.
Comments
Post a Comment