- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Maofisa wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) Anna Salado na Alicia (kushoto) wakipata maelezo ya fugaji nyuki katika msitu wa hifadhi wa Pugu.
WANAWAKE
wanaofuga nyuki wataokoa hekta 7,270 za misitu ya hifadhi ya Pugu na
Kazimzumbwi, imefahamika.
Misitu hiyo,
ambayo ni miongoni mwa Misitu ya Hifadhi 486 iliyopo nchini, imekuwa hatarini
kutoweka kutokana na shughuli za kijamii hususan uvamizi wa mipaka na ukataji
wa miti kwa ajili ya uchomaji mkaa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukifanywa na
wananchi mbalimbali.
Meneja wa
Misitu hiyo kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mathew Mwanuo, anasema
kwamba, misitu hiyo iliyopo katika wilaya za Ilala mkoani Dar es Salaam na
Kisarawe mkoani Pwani, imekuwa hatarini kutoweka licha ya jitihada za serikali
za kukabiliana na wavamizi hao.
“Lakini sasa
miradi hii ya ufugaji nyuki inayowahusisha wanawake wa Pugu na Kisarawe itakuwa
mkombozi kwa sababu wananchi wenyewe wanahusishwa moja kwa moja na suala la
ulinzi,” anasema Mwanuo wakati akiwaelekeza wageni kutoka taasisi ya Mfuko wa
Wanawake wa Afrika (WAF) kutoka nchini Hispania waliotembelea miradi hiyo hivi
karibuni.
Mwanuo anasema
kwamba, ndani ya misitu hiyo ya hifadhi kuna jumla ya vikundi vinne vya
akinamama vinavyojihusisha na ufugaji wa nyuki wa kisasa, ambapo viwili
vinafadhiliwa na mradi wa Green Voices Tanzania na viwili vinafadhiliwa na TFS.
Anna Salado akiwa msituni kuangalia ufugaji wa nyuki kwenye hifadhi ya Pugu.
“Kazi ni
kubwa katika kuilinda misitu hii, tunao askari wetu wanaozunguka humu, lakini
hawatoshi kuweza kuzunguka maeneo yote na ndiyo maana huko nyuma watu walikuwa
wakivamia kukata miti na kuchoma mkaa.
“Zamani
ulikuwa ukipita pembeni unaona misitu inapendeza, lakini ukiingia ndani
kulikuwa na watu wanachoma mkaa huku mambo mengine yakiendelea kama uuzwaji wa
vinywaji na kadhalika… yaani hali ilikuwa mbaya sana,” anasema.
Mshiriki kiongozi
wa miradi hiyo ya ufugaji wa nyuki chini ya Green Voices, Monica Kagya, anasema
kwamba, anaishukuru taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika (WAF) kwa kumwezesha
yeye na wenzake 14 kupata mafunzo nchini Hispania mapema mwaka huu ili kuwapa
uwezo wanawake kushiriki shughuli za utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi.
Mshiriki kiongozi wa mradi wa ufugaji nyuki Pugu na Kazimzumbwi, Monica Kagya, akitoa maelezo kwa wageni (hawapo pichani).
“Nilichagua
mradi huu wa ufugaji wa nyuki kwa sababu naamini misitu hii ya Pugu na
Kazimzumbwi inaweza kuokolewa kutoka katika hatari ya kutoweka, lakini ndiyo
mapafu halisi ya Dar es Salaam kwa kuwa inasaidia kutoa hewa ya oksijeni kwenye
jiji hilo ambalo idadi ya watu inaongezeka kila siku pamoja na shughuli za
uchumi, vikiwemo viwanda,” anasema Kagya.
Bi. Kagya,
ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa TFS, anasema kwamba, ili kutunza mazingira ni
muhimu kuwashirikisha wanawake ambao ndio wahanga wakubwa wa mabadiliko ya
tabianchi kutokana na kushughulikia majukumu yote ya nyumbani ikiwemo utafutaji
wa nishati za kupikia, hususan kuni na mkaa.
Anasema kwamba,
vikundi vyote viwili vinavyotekeleza mradi wa Green Voices vipo katika msitu wa
hifadhi wa Pugu ambapo kimoja kina mizinga 12 na kingine kina mizinga 52.
“Vikundi
vingine viwili vinavyofadhiliwa na TFS vipo katika msitu wa hifadhi wa
Kazimzumbwi,” anasema.
Mkurugenzi wa
Mfuko wa Wanawake Afrika, Anna Salado, ambaye aliwaongoza wenzake kukagua
mizinga pamoja na kushuhudia zoezi la urinaji wa asali katika msitu wa
Kazimzumbwi, alieleza kufurahishwa kwake na jitihada za kutunza mazingira
pamoja na mafanikio ya mradi huo.
“Hakika
jitihada hizi ni kubwa, tumefurahi sana kuona akinamama wanakuwa mstari wa
mbele kupambana na uharibifu wa mazingira lakini wakati huo huo wanafanya
miradi inayoweza kuwakwamua kiuchumi,” alisema Bi. Salado.
Meneja wa Misitu ya Hifadhi ya Pugu na Kazimzumbwi, Mathew Mwanuo, akitoa maelezo na changamoto zinazowakabili.Maofisa wa Mfuko wa Wanawake Afrika unaofadhili mradi wa Green Voices nchini Tanzania wakiwa wanakaribishwa na wanawake wafuga nyuki katika misitu ya Pugu na Kazimzumbwi kabla ya kuingia msituni kuangalia shughuli za ufugaji huo wa nyuki.
Alicia (wa pili kulia), mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka Hispania, akiangalia sega la nyuki katika msitu wa Kazimzumbwi.
Alphonce Matata akiwasha moto kabla ya kuanza shughuli ya urinaji asali.
Bi. Salado
ameahidi kwamba, katika awamu ya pili ya mradi wa Green Voices, watajitahidi
kuwawezesha washiriki katika suala zima la kuongeza uelewa wa madhara ya
uharibifu wa mazingira pamoja na kuangalia uwezekano wa kutatua changamoto
zinazowakabili, zikiwemo za vitendea kazi kama mavazi pamoja na mizinga ya
kutosha.
Mradi wa
Green Voices unatekelezwa nchini Tanzania pekee chini ya ufadhili wa WAF na
ulizinduliwa jijini Dar es Salaam Julai 11, 2016 na Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa sambamba na rais wa
taasisi ya WAF ambaye pia ni makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Maria Teresa
Fernandez e la Vega, ambaye tayari amekwisharejea jijini Madrid.
Mratibu wa
mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, amepongeza
jitihada za akinamama hao na kuwataka wawe walimu wa jamii nzima ili kuokoa
misitu hiyo.
Bi.
Secelela, ambaye ni mwanahabari kitaaluma, amesema kwamba, walau hali sasa
inaonyesha kubadilika kuliko ilivyokuwa siku za nyuma ambapo misitu hiyo
ilikuwa inakaribia kutoweka.
“Nilikuja
huku miaka mitano iliyopita wakati nikiandika habari za mazingira, hali ilikuwa
mbaya sana, maana katikati yam situ nasikia kuna watu waliweka mpaka baa,
lakini sasa kwa kuanzisha miradi hii ambayo inawataka wanamradi kuzungukia kila
wakati kwenye mizinga yao kutawakimbiza wavamizi wote,” alisema.
Ameongeza kwamba,
uwepo wa misitu hiyo ni muhimu kwa sababu ndiyo ‘mapafu ya Dar es Salaam’
katika kukabiliana na hewa chafu inayozalishwa jijini humo.
Comments
Post a Comment