- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mgeni rasmi katika
uzinduzi wa jiko la umeme-jua, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa
Manispaa ya Moshi, akisikiliza maelezo ya namna jiko hilo linavyofanya kazi
kutoka kwa Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia wa Kituo cha Zana za Kilimo na
Teknolojia Vijijini – CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi. Kushoto kwa Noela
ni mshiriki kiongozi wa mradi wa Green Voices Moshi, Farida Makame. Wengine
pichani ni washiriki wa kikundi hicho. Uzinduzi wa jiko hilo lililotengenezwa
na CAMARTEC kwa ufadhili wa Green Voices ulifanyika hivi karibuni mjini Moshi.
Jiko la umeme-jua ambalo limetengenezwa na CAMARTEC
kwa ufadhili wa mradi wa Green Voices Tanzania kwa ajili ya kikundi cha
akinamama wa TAWOCA Moshi. Jiko hilo linafaa kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira.
Wanakikundi wa TAWOCA Green Voices Moshi wakihakikisha
jinsi joto la jua linavyosaidia kupika kwa kutumia jiko la umeme-jua. Kushoto
ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa jiko hilo, Robert George, ambaye ni Ofisa
Ushirika wa Manispaa ya Moshi.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa jiko la umeme-jua, Ofisa
Ushirika wa Manispaa ya Moshi, Robert George, pamoja na akinamama wakisikiliza
maelezo ya namna jiko hilo linavyofanya kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa
Uhawilishaji Teknolojia wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini –
CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi.
Mhandisi Noela
Byabachwezi, mwenye kofia kulia, akionyesha kwa vitendo jinsi jiko la umeme-jua
linavyofanya kazi.
Ofisa Ushirika wa
Manispaa ya Moshi, Robert George – kulia – akisikiliza maelezo mbalimbali ya
akinamama wa TAWOCA Green Voices Moshi kabla ya kuzindua jiko la umeme-jua.
Picha ya pamoja.
VIUNGA vya
ukumbi wa Aroma mjini Moshi vimesheheni akinamama wengi katika siku hii ya
Jumamosi, kama ilivyo kawaida kwa siku kama hiyo, ambapo wote wanaonekana kuwa
na nyuso za furaha kutokana na mijadala inayoendelea.
Lakini
tofauti na Jumamosi nyingine ambapo akinamama wa kikundi cha Wamama wa Kahawa ambao
ni wanachama wa Tanzania Women Coffee Association - TAWOCA mjini humo kujadili
masuala mbalimbali ya ujasiriamali, siku hii inaonekana kuwa ya tofauti kwa
sababu licha ya idadi ya akinamama kuongezeka, lakini kuna tukio kubwa na
muhimu ambalo limewakutanisha.
"Leo
tunazindua rasmi jiko la umeme-jua, yaani parabolic solar cooker, ambalo
kupitia udhamini wa mradi wa akinamama wa Green Voices, hatimaye limeweza
kupatikana baada ya jithada za miezi kadhaa," ndivyo anavyoanza kuelezea
Farida Makame, mshiriki kiongozi wa mradi wa Green Voices wa kikundi hicho,
huku akionyesha kifaa kinachofanana na dish kama la satellite ambacho katikati
yake kumewekwa sufuria inayong’aa kama taa kubwa ya umeme.
Anasema
kwamba, jiko hilo linaweza kupika kila aina ya chakula kwa kutumia mionzi ya
jua ya moja kwa moja bila kuathiri mazingira.
"Kwa
kutumia jiko hili maana yake huhitaji kutafuta mkaa wala kuni, hivyo kuokoa
misitu ambayo inateketea kila siku kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya
kutafuta nishati ya kupikia," anaongeza.
Farida,
ambaye pamoja na akinamama wengine 14 – wakiwemo wanahabari watano wanawake –
walipatiwa mafunzo ya takriban miezi miwili jijini Madrid, Hispania mapema
mwaka huu wa 2016, anasema kwamba lengo la kubuni na kutengeneza jiko hilo la
umeme-jua ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupambana na
uharibifu wa mazingira.
Anaeleza
kwamba, haikuwa kazi rahisi kwake kukamilisha ubunifu wake, wazo ambalo
aliliwasilisha akiwa mafunzoni, na kwamba ndiyo maana mradi wake umechelewa
kutokana na kuhitaji teknolojia zaidi.
"Tumeanzisha
huu mradi baada ya kukaa na akinamama wa TAWOCA na kuwauliza changamoto
mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao, moja ya changamoto ni upatikanaji
wa kuni na mkaa, gesi na umeme.
"Kwahiyo
tukaangalia kama kuna njia mbadala ambayo akinamama wanaweza kuitumia na ikawa
nafuu na pia kiafya, kwa sababu njia ya kutumia umeme-jua ina manufaa sana
kiafya, kwa hiyo tukaungana na wenzetu wa Kituo cha Zana za Kilimo na
Teknolojia Vijijini, CAMARTEC, kwa sababu ndio watafiti wa mashine na zana za
kilimo, ili kutengeneza jiko hili linalotumia nishati ya jua," anasema.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia wa CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi
anasema imekuwa ni fursa kubwa kwao kufanya kazi na mradi wa Green Voices,
kwani wameweza kutengeneza kwa mara ya kwanza jiko hilo ambalo limewapa hamasa
wahandisi wa kituo hicho kuliboresha zaidi kwani linaonekana kuwa na manufaa
makubwa.
Anakiri
kwamba, ingawa wanabuni teknolojia mbalimbali ikiwemo kutengeneza majiko na
makaushio yanayotumia umeme-jua, lakini hiyo ndiyo mara ya kwanza kwa kituo
hicho kutengeneza jiko linalotumia nguvu ya jua moja kwa moja.
"Hivi
sasa tunafanya utafiti kama tunaweza kulitengeneza dogo lakini lenye nguvu au
kutengeneza jiko linaloweza kukunjwa na kuhifadhiwa kirahisi kwa sababu hili ni
kubwa na inakuwa shida ikiwa mtu hana nafasi kubwa ya kuhifadhia," anasema
Mhandisi Noela.
Akizungumzia
kuhusu ufanisi wake, Noela anasema kwamba, jiko hilo ni rafiki mkubwa wa
mazingira na lina uwezo mkubwa wa kupika na hata kuoka vyakula vya aina zote ikiwa tu kutakuwepo na
jua la kutosha.
Kwa maeneo
kame na yenye jua kali kama mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na hata
Dar es Salaam, jiko hilo linafaa sana kutumiwa bila shida, anaongeza mhandisi
huyo.
Aidha,
anafafanua kwamba, jiko hilo linaweza kupika chakula kwa ajili ya watu wengi na
kwamba ni jukumu la jamii kugeukia matumizi ya jiko hilo lisilotumia mafuta
wala nishati nyingine kwa sababu siyo tu linapunguza gharama, lakini pia
linaokoa misitu kwa vile miti haitakatwa ikiwa watakuwa wanalitumia.
"Jambo
jingine la muhimu ni kwamba, upikaji kwa kutumia jiko la umeme-jua mara nyingi
hufanyika nje na katika mazingira ambayo yanahitaji matumizi madogo ya mafuta
na kuni, au hatari ya ajali za moto na inaokoa afya za wanajamii, hususan
akinamama pamoja na kuyalinda mazingira yetu," anaongeza Mhandisi Noela.
"Kama
unavyoliona, jiko hili limetengenezwa kwa vifaa maalum vikiwemo vioo, ambavyo
vinang’aa na kuakisi mwanga wa jua, vimepangwa kitaalam na mwanga huu
unapoakisiwa unakwenda moja kwa moja kwenye sufuria ambayo kutokana na joto
lake, chakula chochote kinachopikwa kinaiva bila wasiwasi wowote. Kama jua
litakuwepo la kutosha, joto linalozalishwa na jiko hili linaweza kufikia hadi
nyuzijoto 400 °C."
Kwa mujibu
wa mhandisi huyo, vyakula vinavyopikwa kwa kutumia jiko la aina hiyo ni vyema
vikawa katika maumbile madogo ili kusaidia kuiva haraka na kwamba muda wa
chakula kuiva unategemea na vifaa unavyotumia, kiwango cha jua, na kiasi cha
chakula kinachopikwa.
Faida
kubwa za utumiaji wa jiko la umeme-jua zinatajwa kwamba, mbali ya kuokoa
mazingira, ni uwezo wa kupika vyakula vigumu, kukaanga nyama, kupika supu,
kuoka mikate na kuchemsha maji kwa muda mfupi.
Hata
hivyo, jiko hilo linahitaji zaidi uwepo wa jua, kwani ndiyo chanzo cha joto
linalofaa kupikia.
Mmoja wa
wanakikundi hicho, Esther Moshi, amesema kupatikana kwa jiko hilo kutawakomboa
wanawake wengi ambao mara nyingi ndio wanaokabiliwa na changamoto ya utafutaji
wa nishati za kupikia kama kuni na mkaa.
"Tunashukuru
mradi wa Green Voices kwa sababu unalenga kumkomboa mwanamke kutokana na adha
ya upatikanaji wa nishati ya kupikia, kama majiko haya yatatengenezwa kwa wingi
na kila familia kulipata, hakika yatakuwa mkombozi na yatasaidia kuokoa
mazingira, " anasema.
Fatima
Aziz Faraji ni mwenyekiti wa Chama cha TAWOCA, amesema ni muhimu kwa wanawake
kuzidisha umoja wa vikundi ili waweze kusonga mbele na akaupongeza mradi huo
kwamba utakuwa mkombozi si kwa wanawake pekee, bali jamii nzima.
Mgeni
rasmi katika uzinduzi wa jiko hilo, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa
Manispaa ya Moshi, ameupongeza mradi wa Green Voices pamoja na akinamama hao na
akahimiza kuwa, ni vyema kutumia teknolojia ambazo ni rafiki wa mazingira.
Amesema
akinamama ndio waathirika wakubwa wa matumizi ya nishati za kupikia, na kwamba
ndio wanaoongoza kupata madhara kiafya, hasa wanapotumia mkaa na kuni.
"Jitihada
hizi za wenzetu wa Green Voices zinapaswa kuongezwa, kwa sababu zinalengo siyo
tu kumkomboa mwanamke, bali kulinda mazingira yetu ambayo yanazidi kuteketea
kila uchao kutokana na ukataji wa misitu kwa madhumuni ya kutafuta kuni na
mkaa.
"Akinamama
wanaathirika sana, wengine utakuta macho mekundu kutokana na moshi wa kuni, na
wanapokuwa wazee ndio wanaoshambuliwa na watu wengine wasio na utu kwamba eti
ni wachawi kwa sababu macho yao ni mekundu, lazima kutumia teknolojia mbadala
kuwanusuru mama zetu, " alisema.
Hata
hivyo, aliwataka akinamama hao kushikamana pamoja katika shughuli zao ili
waweze kujiletea maendeleo, kwani umoja ni nguvu.
Kwa upande
wake, Mratibu wa Mradi wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela Balisidya,
amesema, mradi wa jiko la umeme-jua ni sehemu ya miradi 10 inayotekelezwa chini
ya Green Voices ambapo Tanzania ndiyo pekee iliyopendekezwa kutekeleza mradi
huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika, , ambayo inaongozwa na
makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandez de la Vega Sanz.
Hata hivyo, taasisi
hiyo inafadhili miradi 15 ya wanawake katika nchi 12 barani Afrika ambayo
imeonyesha mafanikio, huku mradi wa Green Voices ukitajwa kuwa na mafanikio
makubwa katika kipindi kifupi.
Kwa mujibu wa Bi. Secelela, Mradi wa Green Voices
unatekelezwa katika mikoa sita ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma,
Morogoro na Kilimanjaro.
“Miradi hiyo ni kilimo cha miti
ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi lishe visiwani Ukerewe mkoani Mwanza,
Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na Pwani, ukaushaji wa mbogamboga kwa kutumia
nishati ya jua mkoani Morogoro, usindikaji wa vyakula mbalimbali kutokana na
muhogo mkoani Pwani, kilimo hai cha mbogamboga, na kilimo cha uyoga mkoani Dar
es Salaam, mradi wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi huu wa utafiti wa jiko
linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanjaro,” anafafanua Secelela.
Anasema, lengo kubwa la mradi
wa Green Voices ni kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao wa kupambana na
mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya kitanzania iweze kujifunza zaidi na
kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Serikali kupitia taasisi na idara zake zilizo chini ya
Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii imekuwa
ikiendesha program mbalimbali za mafunzo ya ufundi ikiwemo utengenezaji wa
majiko banifu na sanifu kama inayoendelea katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii
Malampaka wilayani Maswa.
Hata hivyo, bajeti ndogo imekuwa changamoto kubwa
kukwamisha kuwafikia wananchi wengi na kuwapatia elimu ya aina hiyo.
Comments
Post a Comment