Featured Post

KILIMO CHA UYOGA DAR CHAWAVUTIA WAHISPANIA



 Anna Salado, Mkurugenzi wa taasisi ya Women for Africa Foundation kutoka Hispania, akiwa na uyoga aliouvuna.

“SIJAWAHI kuvuna uyoga katika maisha yangu, achilia mbali kushuhudia namna unavyolimwa,” anasema Anna Salado, Mkurugenzi wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) kutoka Hispania, wakati akikwanyua kikonyo cha uyoga katika shamba la akinamama wa kikundi cha Tunza Women Group, Bunju jijini Dar es Salaam.

Anaongeza: “Kwa hakika ninyi wanawake mmefanya jambo kubwa na muhimu katika jamii, kwa sababu mbali ya kufanikiwa kulisha familia zenu, lakini sasa mtaweza kuongeza kipato kwa kuwauzia wengine zao hili.”

Akiwa ameongozana na maofisa wengine wa taasisi hiyo Alicia ambaye ni mratibu na Noelia ambaye ni mkurugenzi wa miradi, Anna Salado anasema kwamba, wamehamasika sana na kilimo hicho na katika kuunga mkono juhudi za akinamama hao watawasaidia kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kuwawezesha kupanua mradi wao.

Mradi huo wa kilimo cha uyoga ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mama wa Green Voices nchini Tanzania unaofadhiliwa na taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika, ambayo rais wake ni Mama Maria Teresa Fernandez de la Vega Sanz ambaye ni Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania.

Anna na wenzake wamekuwa wakitembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Green Voices nchini Tanzania tangu mradi huo ulipozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Julai 11, 2016 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
 Uyoga ukiwa umeota vizuri ndani ya banda.

Wakati wa ziara yao kwenye mradi wa kilimo cha uyoga, viongozi hao walioambatana na Mratibu wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, walijifunza mambo mbalimbali kuanzia utaarishaji wa shamba, upandaji, uvunaji pamoja na namna ya kufungasha huku pia wakielekezwa mapishi ya uyoga.

“Tunakunywa supu kwenye mahoteli, tunauona tu kwenye picha, lakini leo tumeweza kuuona namna unavyolimwa, tena tumeonja mapishi mengine tofauti,” alisema Anna Salado baada ya kula uyoga ulioungwa kwa nazi.

Mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Bi. Alicia akizungumza na washiriki wa mradi huo, alisema kwamba mradi huo ulikuwa wa majaribio, lakini sasa umewahamasisha na wako tayari kusaidia awamu ya pili ili kuwawezesha wanawake wengi wajikite kwenye kilimo hicho cha uyoga.

“Tumefarijika sana, kwa sababu ni kipindi kifupi tu tangu tulipowapa mafunzo wanawake 15 kule Madrid, lakini leo hii mmeweza kufanya mambo makubwa kama haya, hakika tuko nanyi bega kwa bega,” alisema Alicia.

Mshiriki kiongozi wa mradi wa kilimo cha uyoga, Magdalena Bukuku, alisema kwamba tangu walipoanza kilimo hicho mwezi Machi, tayari wamekwishaona faida yake baada ya kuvuna na kuuza sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.

Magdalena, ambaye yeyé na wanawake wengine 14 walipatiwa mafunzo Hispania mapema mwaka huu, amesema kwamba kutokana na wingi wa akinamama waliojitokeza, amewagawa katika makundi mawili, ambapo kimoja kipo Mtaa wa Kilungule, Bunju na kingine kipo Boko, vyote vikiwa na wanachama 10 kila kimoja.

Hata hivyo, amesema kuwagawa tu hakukuwazuia wanawake wengine kwenda kujifunza, kwani tayari wanajamii katika maeneo hayo wamekuwa wakimiminika kujifunza namna ya kuanzisha mashamba ya uyoga majumbani mwao.

“Mpaka sasa nimekwishawafundisha wanawake wengine zaidi ya 50, wengine wanatoka Zanzibar, Kibaha na Bagamoyo,” alisema.

Mwenyekiti wa kikundi cha Tunza cha Bunju, Sophia Chove, anasema hivi sasa wanafikiria kuongeza shamba jingine la uyoga, ingawa changamoto ya mtaji ndiyo inayowapa shida.

Anasema ili kuweza kupata faida ni muhimu kuongeza shamba hasa ikizingatiwa kwamba mahitaji ya uyoga yameongezeka katika jamii.

“Wateja ni wengi sana kuliko tunachozalisha, hivyo tunaona ni vyema tukaongeza banda jingine, lakini changamoto hapa ni mtaji, tukiwezeshwa tunaweza,” anasema.

Anasema kwamba, tayari wamepata wateja wa maduka makubwa ya bidhaa (super markets) pamoja na jamii inayowazunguka, mahitaji ambayo ni makubwa kuliko uwezo wa kuzalisha.

“Uyoga una faida kubwa, fikiria robo kilo ya uyoga inauzwa Shs. 2,500 wakati kilo moja ni Shs. 10,000,” anaongeza Sophia.
 Bi. Sophia Chove, Mwenyekiti wa kikundi cha Tunza Women cha Bunju jijini Dar es Salaam, akiwaelekeza wageni namna ya kuandaa mahitaji mbalimbali ya kilimo cha uyoga.
 Mratibu wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia, akizungumza na wanawake wakulima wa uyoga wa Bunju na Boko (hawapo pichani).

Mhazini wa kikundi hicho ambaye pia ndiye mwalimu wa ukulima wa uyoga na Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni, Esther Chiombola, anasema kwamba kila wiki wamekuwa wakiwafundisha akinamama kati ya watano hadi 10 kutoka maeneo mbalimbali.

“Hapa pamekuwa kama kituo cha mafunzo, wanawake wengi wamehamasika na tunawafundisha namna ya kuanzisha kilimo hiki ambacho ni rafiki wa mazingira na kina tija kubwa kwa uchumi,” anasema Mama Chiombola.

Anaongeza: “Ni mradi unaotumia gharama kidogo huku mavuno yake yakiwa endelevu, hapa Bunju tayari akinamama wameanza kuvuna.”

Miradi mingine ya Green Voices inatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mwanza, Kigoma na Kilimanjaro ambayo yote inaendana na mkakati wa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, miradi hiyo ya Green Voices nchini inalenga pia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 pamoja na Malengo Endelevu ya Dunia katika kuondoa umaskini, kuongeza ajira, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuhakikisha usalama wa chakula pamoja na kupambana na uharibifu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
 Mambo ya msosi, na kuna rosti la uyoga hapo.
Noellia (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa mwakilishi wa wakulima wa uyoga wa Bunju na Boko jijini Dar es Salaam.


Comments