- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na
Daniel Mbega
Mbuzi ni
wanyama wavumilivu, wanaweza kufugwa katika mifumo ya huria (freerange),
shadidi (zero grazing) na kwa kutumia njia zote mbili. Lakini mbuzi wanahitaji
sehemu ambayo ni kavu kwa ajili ya kulala na kujikinga na mvua na jua, pamoja
na eneo la kucheza, hususan kama unataka kupata maziwa bora.
Zizi hutumika
katika mfumo huria ambapo mbuzi huchungwa wakati wa mchana na kurejeshwa zizini
wakati wa usiku. Banda maalum hutumika kwa ajili ya kuwafuga katika mfumo
shadidi (zero grazing).
Katika
mazingira niliyokulia – na ndivyo ilivyo hata sasa huko vijijini – hata kama
una kundi la ng’ombe pamoja na mbuzi, lazima uwatengenezee mbuzi zizi la peke
yao, wakati mwingine wanaweza kuchangia pamoja na kondoo na ndama. Mara nyingi
banda hili lazima liwe limeezekwa kuwakinga na mvua na jua.
Katika
mazingira ya joto ambapo kuwakinga na jua na mvua ni jambo muhimu, paa rahisi
ambalo unaweza kuezeka hata kwa makuti, nyasi au mabati ni la muhimu sana.
Lakini lazima liwe na mwanga wa kutosha na kusaidia kuingiza hewa.
Ikiwa unatumia mfumo wa shadidi, ni
muhimu kutengeneza banda hilo katika hali ya ubora na nafasi kulingana na mbuzi
ulionao. Tengeneza mahali pa kulia chakula na kunywea maji ambapo lazima pawe
juu kwa sababu mbuzi hawapendi kula kwenye matope. Tenga eneo la kulishia,
kulala, kukamulia maziwa, eneo la kuchezea na kadhalika. Hata kama unawafuga
ndani, haimaanishi kwamba mbuzi hao hawana haki ya kucheza.
Wafugaji mahiri wa mbuzi
wanapendekeza kwamba eneo linalomtosha mbuzi mmoja linafaa kuwa na ukubwa wa
futi 12 hadi 25 ambalo litawafaa hata katika mazingira ya joto ambapo watatumia
muda mwingi wakiwa nje. Wakati wa baridi watatumia muda mwingi wakiwa ndani, hivyo
unahitaji kuongeza eneo.
Banda na mahitaji yake
Mbuzi
wanapaswa kufugwa katika banda lenye kuwapa uhuru. Hawapaswi kufungwa minyororo
kama mbwa, au kuachiliwa kuzurura mashambani kama kondoo au kuwekwa kwenye
maboma kama ng’ombe. Wanatakiwa kuwa na uhuru kuzunguka ndani ya banda lao na
eneo dogo la kucheza nje.
Huhitaji
kuwa na mtaji mkubwa kujenga banda la mbuzi, lakini kama nilivyosema awali,
linapaswa kuwa na mwanga wa kutosha pamoja na uwezo wa kupitisha hewa safi.
Hata kama unaishi katika eneo lenye baridi kama kule Makete, usiwafuge mbuzi
katika eneo lililozibwa kwa matarajio kuwa unawakinga na baridi, kwa sababu
mvuke unaotengenezwa humo unaweza kuwa na madhara makubwa kuliko baridi yenyewe.
Kama mbuzi
wana eneo zuri la kucheza nje, basi banda lenye ukubwa wa eneo la futi 20 kwa
kila mbuzi linatosha kama maskani.
Eneo la
ndani linaweza kuwa dogo, kama nilivyosema, kwa sababu majira ya joto wanakuwa
wanacheza nje. Huhitaji ghala kufugia mbuzi. Kizimba chenye ukubwa wa futi 8 x
10 kinatosha kabisa kuwahifadhi majike wanne. Kumbuka tu kwamba utalazimika kupanua
banda wakati mbuzi wako watakapozaa na kuongeza kundi lako. Lazima watoto
uwatengenezee mahali pao wasichanganyike na mama zao. Pia utahitaji kuwa na
eneo kwa ajili ya kuhifadhi nyasi na nafaka za kuwalisha, vifaa, na eneo la
maziwa.
Kwa hiyo
ukiangalia hapa utaona kwamba, banda la mbuzi linatakiwa kujengwa katika
misingi kama ile ya kujenga banda la kuku ambalo nalo huhitaji usafi, hewa na
mwanga.
Wafugaji
wengi wanapendelea sakafu ya vumbi, kwa sababu zina joto na kavu kuliko sakafu
ya sementi na haziwezi kuoza miguu kama kwenye sakafu ya mbao.
Wafugaji
wengi wanaoanza, hususan wasio na uzoefu na mifugo, hujikuta wakinunua wanyama
na kwenda nao nyumbani na ndipo wanaanza kupanga mahali pa kuwaweka. Hili ni
kosa na inaonekana unakuwa umeanza na mguu mbaya.
Unapojenga
banda lako la mbuzi, hakikisha unatenga eneo maalum kwa ajili ya kujifungulia.
Hii itawasaidia majike wazae bila kusumbuliwa na wengine.
Ikiwa
utawatenganisha watoto na mama yao, utahitaji kuwa na banda maalum kwa ajili
yao.
Hakikisha
kwamba unaweka uzio kuzunguka banda lako la mbuzi. Hii itazuia watu kuingia
ovyo kwa sababu kuingia bila utaratibu husababisha pia magonjwa kwa mbuzi. Uzio
pia utasaidia kuwakinga na wezi, wanyama hatari na kadhalika.
Sifa za zizi bora la mbuzi ni kama zifuatazo:
• Ambalo
imara linaloweza kumkinga mbuzi dhidi ya wanyama hatari na wezi
• Lililojengwa
mahali pa mwinuko pasiporuhusu maji kutuama
• Ukubwa
wa zizi lazima uzingatie idadi na umri wa mifugo. Ni vyema mbuzi watengwe
kulingana na umri wao; na
• Liruhusu
usafi kufanyika kwa urahisi.
Pale ambapo
mbuzi wanafugwa kwa mfumo wa shadidi hufugwa katika banda wakati wote.
Banda bora la mbuzi linatakiwa kuwa na sifa hizi:
• Imara,
lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa
mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari
• Lenye
mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi
• Lijengwe
sehemu isiyoruhusu maji kutuama na liwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu.
Pia ujenzi uzingatie mwelekeo wa upepo ili hewa kutoka bandani isiende kwenye
makazi
• Liwe
na sakafu ya kichanja chenye urefu wa mita 1 kutoka ardhini
• Liwe
na sehemu ya kuwekea chakula, maji na mahali pa kuweka jiwe la chumvichumvi; na
• Liwe
na vyumba tofauti kwa ajili ya majike na vitoto, mbuzi wanaokua,
wanaonenepeshwa na wanaougua.
Eneo
la mbuzi linalotakiwa
Kundi
la Mbuzi Eneo kwa Mnyama
Mmoja (Mita2)
Vitoto 0.3
Wasio na mimba 1.5
Wenye mimba 1.9
Dume 2.8
• Paa
lijengwe kwa kutumia vifaa kama miti, mbao, na kuezekwa kwa nyasi, makuti,
majani ya migomba, mabati au hata vigae kwa kutegemea uwezo wa mfugaji,
• Kuta
zijengwe kwa kutumia mabanzi, mbao, nguzo, wavu wa waya, fito na matofali. Kuta
ziwe imara zinazoruhusu hewa na mwanga wa kutosha.
Mlango uwe na
ukubwa wa sentimita 60 x 150
• Sakafu
inaweza kuwa ya udongo au zege. Sakafu ya kichanja inaweza kujengwa kwa kutumia
miti, fito, mianzi, mbao au mabanzi na iweze kuruhusu kinyesi na mkojo kupita.
Chumba cha majike na vitoto kiwe na nafasi ya sentimita 1.25 kati ya papi na
papi, fito na fito au mti hadi mti.
Chumba cha
mbuzi wakubwa iwe sentimita 1.9 kati ya mbao na mbao.
KUMBUKA: Hupaswi kutumia gharama kubwa sana kujenga banda la mifugo. Unaweza kutumia rasilimali zilizopo hapo ulipo kujenga banda zuri. Kama hali inaruhusu kujenga banda aghali sawa, lakini vinginevyo ninakushauri jenga banda zuri, lenye vipimo sahihi, kwa kutumia rasilimali zilizopo, na utaokoa fedha ambazo unaweza kuzitumia hata kuongeza mifugo mingine.
Comments
Post a Comment