Featured Post

KUFUATILIA NYAYO ZA CHIFU CHIFU MKWAVINYIKA MUNYIGUMBA KILONGE MWAMUYINGA 'MKWAWA' - 2

Hapa nikiwa nimesimama kwenye kaburi na mdogo wake Chifu Mkwawa, Mtwa Msengele Kilekamagana Munyigumba Mwamuyinga 'Msigawabena' ambalo liko pembeni mwa kaburi la Chifu Munyigumba katika Kijiji cha Rungemba.
Upanuzi wa barabara umesababisha kibao hiki king'olewe ambacho kinaelekeza mahali liliko kaburi la Chifu Munyigumba.
Malugala Mwamuyinga (69) akinisimulia historia ya ukoo wa Chifu Mkwawa.

Na Daniel Mbega

Ndugu zangu,
Tunaendelea na simulizi ya ‘Nyayo za Chifu Mkwawa’. Tumeona jinsi Mufwimi alivyotoka Ethiopia (kwa mujibu wa simulizi za ukoo wa Mwamuyinga) na hata alipoingia katika himaya ya Chifu Mwamduda na kujenga naye urafiki kwa sababu ya mawindo yake.
Kwamba baada ya kuwa na uhusiano wa siri na binti wa chifu huyo akawa amempa ujauzito, hivyo akaogopa kwamba Chifu Mwamduda akipata taarifa angeweza kumuua.
Jioni moja akamwita Semduda na kumweleza kwamba yeye anaondoka, lakini akampa maagizo, ikiwa atajifungua mtoto wa kike amwite Mng’anzagala na akiwa wa kiume amwite Muyinga Mufwimi (maana yake ni Mhangaikaji Mwindaji).
Mufwimi alitoroka kwa hofu ya kuuawa na Mwamduda. Akaendelea kuwinda huko na huko hadi Itamba alikouawa na nyati. Hakuna ajuaye lilipo kaburi lake.
Lakini kumbe mtawala huyo alifurahi kusikia bintiye ana mimba ya Mufwimi, maana alijua sasa angekubali kuolewa. Kwa bahati nzuri, binti huyo alijifungua mtoto wa kiume, hivyo akamwita jina la Muyinga Mufwimi kama alivyokuwa ameelekezwa na Mufwimi mwenyewe.
“Kijana huyo alipokua, kwa vile Chifu Mwamduda hakuwa na mtoto wa kiume, akaamua kuukabidhi utawala wake kwa mjukuu ambaye ni Muyinga Mufwimi aliyekuwa hodari wa vita. Kwa hiyo basi, uchifu huu wa Mkwawa ulitoka kikeni, na hapo ndipo uchifu ulipoanzia pamoja na ukoo wote maarufu wa Muyinga,” anafafanua Malugala.
Muyinga Mufwimi akaanza kutawala, akazaa watoto watatu wa kiume – Maliga, Nyenza na Mpondwa. Mtwa Maliga naye akazaa watoto watano wa kiume ambao ni Kitova, Mudegela, Mgayavanyi, Mkini na Kigwamumembe.
Inaelezwa kwamba, katika watoto wake hao, alisema Kitova yeye atakuwa tabibu (mganga wa tiba asilia) na Mudegela atakuwa mtawala, kwa maana hiyo Kitova alikuwa akitibu maradhi mbalimbali, lakini hasa majeruhi wa vita na kizazi chake ndicho kinachoendelea kutibu mifupa katika Kijiji cha Image mpaka sasa.
Mudegela Maliga yeye aliwazaa Lalika, Kalongole, Mbelevele, Wisiko, Kilonge, Kipaule, Mkanumkole, Lusoko na Mwakisonga. Hata hivyo, uchifu wake ulikwenda kwa mwanawe wa tano, ambaye ni Mtwa Kilonge.
Kilonge Mudegela alimuoa Maumba Sekindole aliyemzalia Ngawonalupembe na Munyigumba, lakini pia akamuoa Sekindole mwingine aliyewazaa Gunyigutalamu, mkewe wa tatu aliyeitwa pia Sekindole aliwazaa Magidanga, Mhalwike, Mupoma, Magoyo na Magohaganzali.
“Kilonge alipofariki akazikwa katika eneo ambalo sasa ni Kijiji cha Lupembe lwa Senga (maana yake Pembe ya Ng’ombe), kaburi lake lilikuwa na pembe mbili za tembo, ingawa nasikia pembe zile ziliibwa na tunaambiwa walioiba wote walikufa ukoo mzima. Nasikia serikali ilipeleka pembe nyingine na kuzichimbia ili iwe kumbukumbu,” anasimulia Malugala.
Hata hivyo, uchunguzi wa mwandishi wa makala haya umebaini kwamba, kaburi la Kilonge Mudegela liko katika kijiji cha Uleling’ombe, umbali mfupi tu kutoka kijiji cha Mawambala katika Kata ya Ukumbi wilayani Kilolo. Huko huwa wanafanya matambiko mbalimbali yakiwemo ya kuombea mvua!
Utawala una mambo yake, wakati mwingine unatumia njia halali na haramu ili kuudumisha. Malugala anasema, Munyigumba, ambaye ni mtoto wa pili wa Mtwa Kilonge, alihisi kwamba angeweza kuukosa uchifu kwa kumhofia kaka yake Ngawonalupembe.
“Kwa hiyo akafanya hila na kumuua kaka yake Ngawonalupembe ili yeye atawale, halafu akamchukua Sekinyaga, mke wa marehemu kaka yake kuwa mkewe, lakini wakati anamchukua, kumbe tayari Sekinyaga alikuwa mjamzito.
“Baada ya mtoto kuzaliwa, ambaye alikuwa wa kiume, Mama Sekinyaga akamwita Malangalila Gamoto, pengine kwa maelekezo ya marehemu Ngawonalupembe mumewe. Kwa hiyo Malangalila siyo mtoto wa Munyigumba, bali wa kaka yake ingawa yeye ndiye aliyemlea,” anaeleza Malugala.
Malugala anasimulia kwamba, ugomvi ulitokea baada ya mama huyo kujifungua ambapo alimwambia Munyigumba kwamba huyu siyo mtoto wake. Hapo Munyigumba akakasirika na kuamua kumfukuza Sekinyaga na mwanawe.
Inaelezwa kwamba, alipomfukuzwa, Sekinyaga akaelekea katika maeneo ya Sadani, lakini baadaye Munyigumba akajirudi kwa kuhisi angepata aibu, hivyo ikabidi amrudishe.
“Sasa wafuasi wake aliowatuma wakamchukue huyo mama wakaenda kumuua huko Sadani, hata kaburi lake halijulikani liliko. Wao wakarudi na mtoto Malangalila Gamoto. Kwa hiyo, Malangalila na Mkwawa ni mtu na mdogo wake kasoro baba zao,” anaeleza.
Munyigumba alikuwa na wake watano – Sengimba, Sendale, Sekinyaga (aliyekuwa mke wa kaka yake), Sembame na Sengimba mdogo. Sengimba mkubwa aliwazaa Kilemaganga, Mkwawa, Mpangile, Mulimbila na Wiyolitwe; Sendale alimzaa Mgungihaka; Sengimba mdogo alimzaa Msengele Kilekamagala Msigawabena; Sekinyaga alimzaa Malangalila Gamoto (kwa Ngawonalupembe); na Sembame alimzaa Mpugumoto.
Tutaendelea tena...

Comments