Featured Post

KUFUATILIA NYAYO ZA CHIFU CHIFU MKWAVINYIKA MUNYIGUMBA KILONGE MWAMUYINGA 'MKWAWA' - 1

Kaburi la Chifu Munyigumba Kilonge Mudegela lililo Rungemba, Mufindi mkoani Iringa.

Daniel Mbega
UKITAJA mashujaa wa Afrika, lazima pia umtaje kiongozi mkuu wa Wahehe, Chifu Mkwavinyika Munyigumba Kilonge Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa. Huyu ana mambo mengi aliyoyafanya, ya kujivunia, ambayo kizazi hiki hakifundishwi tena shuleni na hivyo historia yake inapotea.
Nitajaribu kueleza kwa ufupi ufupi tu kile ambacho nimekipata katika utafiti wangu wa historia mjini Iringa, lakini kwa vile bado ninaendelea na utafiti huo, nakaribisha taarifa zozote kuhusiana na kiongozi huyo shujaa.
Maandiko kadhaa yamekuwepo kuhusiana na historia ya Wahehe na hasa ukoo wa Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga ‘Mkwawa’, lakini yote hayo hayakunizuia kuisaka historia hiyo.
‘Jicho halishibi kuona na sikio halikinai kusikia!’ Hivyo nikaamua kufunga safari hadi Rungemba, yaliko makaburi ya Mtwa Munyigumba na ndugu wengine wa ukoo huo, yapata kilometa 62 kutoka Iringa mjini.
Wapo walioandika kwamba chimbuko la Mtwa Mkwawa ni Ungazija, lakini simulizi ninazokutana nazo hapa ni tofauti, maana zinatoka katika vinywa vya wanaukoo wa Muyinga, ambao nao wameipata ama kurithishwa kutoka kizazi na kizazi kutokana na simulizi za mababu zao.
Wale waliopata kuandika kwamba asili ya akina Mkwawa ni Ungazija wanaeleza kuwa mtawala wa Ngazija aliyeitwa Yusuf Hassan ambaye alikuwa Mwarabu, alizaa watoto wawili wa kiume, Hassan ‘Mbunsungulu’ na Ahmad. Wanasema kwamba Mufwimi alikuwa mmoja wa watoto watatu wa Mbunsungulu aliozaa na mwanamke wa Kikaguru. Ndugu zake wengine walikuwa Ngulusavangi na Ngwila, kwa maelezo yaliyo kwenye baadhi ya maandishi ambayo yanatoweka kutokana na Watanzania kukosa utamaduni wa kutembea, kujifunza na kudadisi.
Rungemba ni kijiji ambacho hakijasikika sana katika historia kama lilivyo jina la Mkwawa, lakini hapa ndipo kwa kiasi kikubwa lilipo chimbuko la Chifu huyo wa kabila la Wahehe na ndipo lilipo kaburi la Mtwa Munyigumba.
Ignas Pangiligosi Muyinga, maarufu kama Malugala Mwamuyinga (62), ambaye ni kitukuu wa Msengele Kilekamagana, anaona fahari kuisimulia historia ya ukoo huo maarufu.
“Shina la ukoo wetu linaanzia kwa mtu aliyeitwa Mufwimi (yaani Mwindaji), ambaye mababu zetu walitusimulia kwamba alitokea Ethiopia,” Malugala anaanza kueleza. “Mufwimi alipita akiwinda kutoka Ethiopia, Kenya kabla ya kuingia Tanganyika na kujikuta yupo Usagara na hatimaye eneo la Nguluhe-Dabaga akipitia Ikombagulu, himaya ya Chifu Mwamduda. Wengi walimfananisha na mtu wa kabila la Wakamba kutoka Kenya kutokana na umbile lake kubwa.”
Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa Iringa lilikuwa na makabila mbalimbali. Walikuwepo ‘Wahafiwa’ katika Bonde la Milima Welu, Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalang’ombe, Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.
‘Vanyategeta’ wao waliishi Udzungwa, Kitelewasi na Lundamatwe, ambao walikuwa wahunzi hodari. ‘Vanyakilwa’ walilowea Mufindi wakitokea Kilwa; ‘Vasavila’ waliishi milima ya Welu huko Makungu (Kihanga ya sasa), Magubike na Malangali; na ‘Vadongwe’ waliishi kando ya milima ya Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Mufwimi alikuwa mwindaji mkubwa wa nyati ambapo aliichoma nyama yake kwa kuipaka chumvi ambayo ilikuwa haifahamiki kwa wakazi wa himaya hiyo, alimpelekea zawadi ya nyama-choma Chifu Mwamduda aliyeipenda mno kwa ladha yake.
Alipendwa na kukaribishwa na Mwamduda kuishi kwake, lakini akaanzisha mapenzi ya siri na Semduda, binti wa Chifu huyo, ambaye alikuwa amewakataa wachumba wengi. Binti huyo akapata ujauzito. Mufwimi akaogopa kwa kuona amefanya kosa kubwa.
Tutaendelea nayo….

Comments