Featured Post

NAIBU WAZIRI MABULA AAGIZA KUPIMWA UPYA MIPAKA YA VIJIJI VYA KONO NA KETEMBERE SERENGETI MARA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe.  Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kono na Ketembere wilayani Serengeti mkoa wa Mara jana alipokuenda kutatua mgogoro wa mpaka baina ya vijiji hivyo.

Na Munir Shemweta,  WANMM Serengeti
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.  Angeline Mabula ameagiza zoezi la kupima upya mipaka  ya vijiji vya Kono na Ketembere vilivyopo kata ya Nata na Rigicha wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara kuanza mara moja na kufikia Desemba 2018 ramani ya mipaka ya vijiji hivyo iwe imetoka.
Agizo la mhe.  Mabula linafuatia mgogoro wa muda mrefu uliokuwepo baina ya mipaka ya vijiji hivyo jambo linalosababisha shughuli za maendeleo ikiwemo mpango wa matumizi bora ya ardhi kushindwa kufanyika.
Akiwa katika ziara yake ya kutatua mgogoro huo,  Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema mgogoro wa mpaka baina ya vijiji hivyo ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na wataalamu kutoka Wizara ya ardhi kushindwa kufuata taratibu za kupima mipaka kwa kuwashirikisha wananchi wa pande zote mbili.
"Makosa yaliyofanywa na ofisi hayawezi kuleta ugomvi katika vijiji hivyo na ramani ya eneo hili itarekebishwa kulingana na dira na wizara itaangalia namna ya kushughulika na waliokwepesha mipaka ili kujua walikuwa na maana gani" alisema Mabula.
Kwa mujibu wa mhe.  Mabula lengo la kupima mipaka ni kuwezesha kuwepo mpango wa matumizi bora ya ardhi ambapo kupitia mpango huo wananchi wataweza kupatiwa hati miliki ikiwemo hati za kimila kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi na kusisitiza kuwa ardhi ndiyo mtaji pekee kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Awali Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwapa nafasi  wananchi wa vijiji vya pande zote mbili kueleza jinsi wanavyoifahamu mipaka ya vijiji vya Kono na Ketembere ambapo wengi waliutambua mto Masara kama mpaka wa vijiji hivyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kono Michael Oyatason alisema, vijiji hivyo awali havikuwa na mgogoro wowote ila tatizo lilianza mara baada ya uwekaji alama za mipaka ambao haukushirikisha pande zote mbili kinyume kabisa na utaratibu wa kuainisha mipaka.
Mpima Ardhi Kanda ya Simiyu Godwin Saiguran alimuahidi  Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa zoezi la uanishaji mipaka ya vijiji vya Kono na Ketembere  kwa kushirikisha wananchi wa pande zote mbili litakamilika ndani ya siku nne na kufikia tarehe 25 Oktoba 2018 zoezi litakuwa limekamilika.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe.  Angeline Mabula ametatua mgogoro mkubwa baina ya vijiji vya Kazi na Rwamchanga vilivyopo katika kata ya Manchira wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara.
Mgogoro katika eneo hilo unachangiwa na msuguani wa wananchi wanaotaka kuwa na vijiji viwili kama ilivyoainishwa katika mipaka ya kiutawala ama kuwa na kijiji kimoja ambapo awali kabla ya kuzungumza na wananchi wa vijiji hivyo mhe Mabula alizungumza na wajumbe wa serikali ya vijiji ambapo alipowahoji viongozi wanaotaka kuwepo kijiji kimoja ama viwili ni wajumbe wawili kati ya nane waliokuwa wakihitaji kijiji kimoja.
Ilielezwa katika kikao baina ya mhe.  Mabula na wananchi wa vijiji vya Kazi na Rwamchanga kuwa,  mgogoro katika kijiji hicho unachangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya viongozi waliokuwa wakiwashawishi wananchi kutokubaliana na mipaka ya kiutawala iliyokuwepo  kwa sababau walizokuwa wakizijua wenyewe.
Kwa mujibu wa Mpimaji wa Ardhi Kanda ya Simiyu Godwin Saiguran, tatizo kubwa katika eneo hilo ni uhakiki wa mipaka ambayo awali  ilikuwa haikuwekwa sawa na tayari sasa timu ya kubainisha mipaka hiyo iko tayari kuanza kazi na kwa sasa timu  hiyo iko Wilaya ya Rorya mkoĆ  wa Mara na inatarajia kuwasili eneo la vijiji hivyo muda wowote.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe Angeline Mabula akiangalia alama za mpaka kati ya kijiji cha Kono na Ketembere katika wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara.  Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula akifafanua jambo mbele ya wananchi wa vijiji vya Kono na Ketembere wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara alipokuenda kutatua mgogoro wa mpaka wa vijiji hivyo jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba  na Maendeleo ya Makazi akizungumza na wananchi wa kijiji cha Rwamchanga na Kazi  wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara alipokuenda kutatua mgogoro wa vijiji hivyo.
Baadhi ya wananchi wa vijiji vya Rwamchanga na Kazi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  hayupo pichani wakati alipoenda kutatua mgogoro wa vijiji hivyo.
Naibu  Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kono na Ketembere katika wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiangalia chanzo cha Maji kinachojulikana kwa jina la Zanzibar ambacho kinatumiwa na wananchi wa vijiji vya Kono na Ketembere wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara alipokuenda kutatua mgogoro wa mpaka kati ya vijiji hivyo.
(Picha zote na Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi)

Comments