- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Tanzania ni moja ya nchi barani Afrika ambazo uchumi unakuwa
kwa kasi. Toka mwaka 2017 kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni 7%. Moja ya
chachu ya kasi hiyo ni biashara ndogondogo ambazo kwa kiasi kikubwa
zinamilikiwa na wanawake.
Takwimu za usawa wa kijinsia katika ajira zinaonyesha kwamba
kufikia mwaka wa 2014 Watanzania milioni 2.1 walikuwa wameajiriwa katika sekta
rasmi , ikiwa ni pamoja na serekalini na sekta binafsi, kwa mujibu wa kituo cha
taifa cha takwimu nchini humo.
Hatahivyo takwimu rasmi za serikali zinaonyesha pia kwamba
zaidi ya 60% ya wanawake walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 24 yaani milioni
13.9 wanajishughulisha na shughuli zisizo rasmi yaani biashara ndogondogo na
kilimo.
Hii maana yake ni kwamba ni asilimia 0.75 tu ya wanawake
walioko katika umri wa kufanya kazi ndio wapo katika sekta rasmi. Kwa maneno
mengine, idadi kubwa ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi nchini
Tanzania ni wajasiriamali.
Licha ya kuwa na idadi kubwa ya wanawake wenye ujasiri wa
kubuni na kuendesha biashara, kasi ya ukuaji wa mitaji yao bado ni finyu.
Chanzo kikuu cha mitaji karibuni duniani kote ni mikopo
rasmi ya kibiashara. Hata hivyo, tafiti zinaonesha kuwa wanawake wengi
wajasiriamali kutoka nchi zinazoinukia ikiwemo Tanzania hawana mikopo kutoka
benki na taasisi rasmi za kifedha.
Kwa miaka mingi, dhana iliyoaminika ni kuwa wanawake wengi
hawapati mikopo sababu pesa hazitoshi, lakini takwimu zinapingana na dhana
hiyo.
Utafiti uliochapishwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka
2014 unaonesha kuwa zaidi ya 80% ya maombi ya mikopo ilitengwa kwa ajili ya
wajasiriamali wanawake na 90% iliiva kwa ajili ya kutolewa. Hatahivyo, ni 18%
ya wanawake wajasiriamali ambao waliomba mikopo benki na 28% waliomba mikopo
katika taasisi nyenginezo za kifedha.
Takwimu hizo zinaashiria kuwa tatizo si uwepo wa fedha za
mikopo bali utayari wa wanawake wajasiriamali kukopa.
Moja ya wataalamu waliondaa utafiti huo Vanessa Naegels hivi
karibuni ameandika katika jarida la The Conversation kuwa, utayari wa wanawake
kuomba mikopo unaathiriwa na mambo makuu mawili, dhana hasi juu ya mikopo rasmi
ya kifedha na kukatishwa tamaa.
Kutokuwa na imani
(dhana hasi)
Kwamujibu wa utafiti huo, wanawake wengi wamebainisha kuwa
hawaamini kuwa wanabaguliwa na maafisa mikopo kwenye taasisi za kifedha.
Kilio cha waliowengi ni masharti yanayoambatana na mikopo
hiyo ambayo yanakuwa kikwazo kwao. Sharti la kwanza lililolalamikiwa ni viwango
vikubwa vya riba vinavyotozwa na mabenki kufikia 20% mpaka 30% kwa mwaka.
Wanawake hao pia wametaja kama dhamana ya mali kuwa ni
kikwazo, wengi wao hawana mali kama nyumba au ardhi za kuweka rehani ili wapate
mikopo.
Kwa wale ambao wenye mali hizo ni waume wamesema wenza wao
hawawezi kuwapa ruhusa ya kuziweka rehani.
Kuna ambao wanamali zinazofaa kuwekwa rehani, lakini
wamesema hawawezi kuzikopea wakiogopa kuzipoteza pale watakaposhindwa kulipa
madeni yao.
Baadhi ya wajasiriamali wamelalamikia mchakato ni mrefu na
wenye gharama. Kuna ambao wamelalamikia tabia za baadhi ya maafisa mikopo
wakisema kuna ambao huwatongoza na kutaka wawape rushwa ya ngono ili
wawasaidie.
Kutokuwa na ufahamu mzuri wa masuala ya kifedha na mikopo
pia umetajwa kuwa ni kikwazo, wajasiriamali wengi wanawake wamesema hawakuwa
wakijuwa kuwa wanapochelewa kulipa mikopo yao gharama za malipo huongezeka ama
benki wana uwezo wa kuuza mali zao pale watakaposhindwa kulipa madeni kwa
wakati.
Maumivu ya mikopo
Utafiti umeonesha kuwa kuna machungu ya aina mbili, ya moja
kwa moja na ya kusikia kwa wengine. Hali zote mbili hizo zinachangia wanawake
wajasiriamali kutoomba mikopo.
Baadhi ya wanawake waliohojiwa kwenye utafiti huo wamesema
walishaomba mikopo huko nyuma na kukataliwa, wengine walipitia mashaka tele
kwenye kulipa madeni yao na wengine kuombwa rushwa. Baadhi yao wamepata
matatizo hayo kwenye mikopo isiyorasmi hali iliyopelekea kuwa na dhana hasi
mpaka kwenye utayari wao kwenye kuomba mikopo rasmi.
Kwa kiasi kikubwa kuna ambao wamesikia habari za ugumu wa
kupata na kurejesha mikopo kutoka kwa watu wengine ima wajasiriamali wenzao au
habari zilizozagaa kwenye jamii.
Simulizi hizo huwafanya baadhi kutojaribu kabisa kuomba
mikopo. Kuna ambao wanaamini wakiwa na mikopo watakosa uhuru wa kutumia pesa
zao kwa namna wanavyoona inafaa.
Nini kifanyike
Ni dhahiri kulingana na utafiti wa ILO kuwa si kweli kuwa
wanawake wajasiriamali waliowengi hawapati mikopo sababu ya ufinyu wa pesa.
Tatizo si pesa, bali dhana hasi zilizoota mizizi mirefu juu
ya mikopo ya kibiashara. Ili kujenga utayari wa wajsairiamali wanawake kukopa
dhana hizo potofu inabidi ziondoshwe, lakini haitakuwa kazi nyepesi.
Kwa mujibu wa watafiti, njia bora zaidi na yenye tija ni
kutoa elimu mahususi ya masuala ya kifedha kwa wanawake wajasiriamali. Ni
kupitia elimu pekee wajasiriamali wanawake wanaweza kutunza hesabu zao na
kulinda mitaji yao na kuikuza kwa kupitia mikopo rasmi.
BBC
Comments
Post a Comment