Featured Post

UKIONA UTAMADUNI UMEKABWA NI DHAHIRI UCHUMI UTABAKWA



NA ALOYCE NDELEIO
Maendeleo ya binadamu yanaongozwa na kusimamiwa na utamaduni hivyo kumaanisha kujumuisha, kurithisha tabia, sanaa, imani, taasisi na zana nyingine zinazotokana na kazi za binadamu pamoja na fikra za watu au jumuia.
Hali hiyo inamaanisha utamaduni ni zana yenye nguvu katika kuishi kwa binadamu ukiwa ni mtazamo muhimu ambao unabadilika mara kwa mara kutokana na kuwekwa katika fikra tu na kusahau vitendo.

Mara nyingi utamaduni unakuwa unawekwa katika mazingira ya kuzama  na dhana ya kuuokoa ni kuwepo kwa juhudi za kukuza maendeleo ya shughuli zinazouhusu.
Tamaduni za kigeni ambazo zimeingia zikiambatana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kiasi kikubwa zimefuta mitazamo na fikra za familia nyingi na hivyo kushindwa kuhifadhi viambatanisho vyenye thamani katika utamaduni.
Utamaduni uhalisia wake upo katika namna jami inavyojifunza  na kutenda, mafunzo ambayo yanatoka katika familia, marafiki, jumuia na hata taifa.
Aidha ni kupitia njia hizo hujifunza ni aina gani ya vyakula inavyokula, aina ya makazi, kuwasiliana na tabia zipi zinafaa.
Muhimu zaidi ni kwamba ni vyema kufahamu kwamba  jamii inaweza kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia lakini mara nyingine  inashindwa kuwianisha teknolojia na kuhifadhi utamaduni.
Utamaduni unaiwezesha jamii kuunda na kubuni, unaionesha uzuri wa taifa na unaunda heshima kwa watu wake kupitia thamani na imani ambazo zinahitajika.
Ipo dhana ya kujikita katika kukuza utamaduni na utalii kwa kuboresha hifadhi za taifa na kuyaweka pembeni mapenzi  kwa ngoma za asili, muziki, mavazi, vyakula, lugha, sanaa na ubunifu, ujumbe wa lugha unaotokana na  ngoma  za asili, michoro na mengineyo kwamba ni nyenzo nzuri ya kuutangaza utalii.
Vyote hivyo ni sehemu ya utamaduni zinatakiwa juhudi kubwa kuzijumuisha katika mkondo wa  kukuza na kuhifadhi utamaduni.
Hoja inayoweza kuibuka hivi sasa ni kwamba kwanini  iwepo haja ya kuhimizana kuhifadhi na kuthamini utamaduni katika kipindi cha sasa? Jibu lake ni kwamba kuna kasoro ambazo zimeshajitokeza na marekebisho ni muhimu.
Kwa kurejea wakati wa harakati za kutafuta uhuru miongoni mwa nchi za Afrika  kati ya viongozi waliokuwa na maono makubwa na makali ni  Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah ambaye mwaka 1956 alitoa kauli  kwa wapambanaji wenzake  akiwataka  wadai kwanza hitaji lao la msingi.
Alisema, “Utafuteni kwanza Ufalme wa Kisiasa, na mengine yote mtazidishiwa.” Kimsingi ulikuwa ni  msukumo kwamba pindi Afrika ikipata uhuru, hakutakuwepo tatizo lolote ya kupata mafanikio katika mambo mengine yanayohusu uchumi, utamaduni na jamii.
Ukweli ukadhihirika kwa wakoloni kuutoa Ufalme wa kisiasa na zikawepo shamrashamra nyingi.  Lakini kwa upande wa wakoloni licha  kuukabidhi ufalme huo,  mioyoni mwao waliificha furaha kuwa walichokifanya ni kwa mkono mmoja,  wa pili wakaendelea nao kumiliki ufalme wa kiuchumi.
Kilichofurahiwa na Waafrika kiuhalisia  ulikuwa ni ufalme wa bendera au  uhuru wa bendera. Ile kauli ya Nkrumah iliishia katikati kwani mengine ya kuzidishiwa  yalibakia mikononi mwa wakoloni. Kilichofanyika kikawa mgawo wa nusu kwa  nusu.
Baya zaidi ni kuwepo kwa viongozi ambao hawakujali maono yaliyotolewa na wengine kwa wao kutoa fursa za kupakuliwa kwa yale mengine ya kuzidishiwa licha ya uhalali na uhuru wa kuwafanya wayamiliki.
Ili kufanikiwa katika mengine  mfumo wa uhusiano unaotaka mataifa kuwa na mlango usio na kitasa wala komeo ambao ni utandawazi ukaibuliwa na nchi zilizokuwa zikitawala. Ni kiasi cha kufikiria kwamba mifugo iliyopo katika banda ambalo mlango uko wazi haiwezi kuishi humo bila kamba shingoni. Kama kula majani ni kwa kipimo au masharti.
Ufalme wa kisiasa uliokuwa umepatikana mikakati iliyokuwa ndani yake ilikuwa ni kufufua uhalisia na uhai wa kuipenda nchi, mila na tamaduni, lengo likiwa ni kujiimarisha katika uvaaji, lugha, kauli, na hata kujijengea maadili ya taifa. Ili kupata hilo Wizara ya Utamaduni  ikaundwa.
Kuwa chini ya utawala wa kikoloni na kuishi katika tamaduni za kulazimishwa  kulizifanya nchi nyingi kuufanya utamaduni  kuwa lengo la msingi. Huko ndiko kulikokuwa mwanzo wa   tamasha la Wasanii la bara zima la kila mwaka – FESTAC, mahsusi  kutangaza, kuimarisha na kubadilishana tamaduni.
Kadhalika liliiwezesha Afrika kushiriki matamasha ya kimataifa ya utamaduni (EXPO), kwa ajili ya kutangaza utamaduni wa  Mwafrika duniani.
Rejea katika hili ni maonesho ya EXPO 70, yaliyofanyika Japan mwaka 1970. Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoshiriki ikiwakilishwa na Hayati Mzee Moris Nyunyusa, gwiji wa  kupiga ngoma 10 kwa wakati mmoja; (Kazi yake imekuwa kiashiria cha kuanza kwa  Taarifa ya Habari, Redio Tanzania);  Bendi ya Polisi, chini ya uongozi wa hayati, Mzee Mayagilo; (Huyu naye wimbo wake umekuwa kiashiria cha kuanza kipindi cha Usalama Barabarani Redio Tanzania pia).
Kwa upande wa bendi za muziki Hayati  Mbaraka Mwinshehe na Bendi yake ya Morogoro Jazz, alioonesha utangazaji wa nchi kwa kiwango kikubwa. Wimbo wake EXPO 70 unadhihirisha hilo ambapo anawataja wazee hao  na kile walichokifanya huko. Kadhalika  akaweka kikolombwezo cha lugha ya Kijapan ‘Sayounara Japan’ kikimaanisha ‘Kwa heri Japan’.  Pia walikuwepo Wanasanaa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Lakini katika kuukumbatia utandawazi pamoja na kuwepo kwa Wizara ya Utamaduni  haziwezi  kuwepo tambo kuwa utamaduni unapewa kipaumbele kile kilichokuwa kinabainishwa kama mengine yatakayofuata baada ya uhuru wa kisiasa.
Katika eneo la Afrika Magharibi uvaaji wa watu kama Rais Mstaafu wa Ghana Jerry Rawlings na Rais Mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo unaweza kubainishwa kuwa ni wa kiutamaduni.  Leo hii ni nani yupo katika ngazi za juu atakayeonekana bila  tai pamoja na suti?   Mjadala wa kuwa na vazi la taifa uliishia wapi?
Mwanaharakati wa uhuru katika Afrika, Frantz Fanon, Katika kitabu chake Ukoloni Unaokufa, alisema, “Jinsi watu wanavyovaa wao wenyewe, pamoja na tamaduni  za kuvaa  na uzuri wa desturi unaotumika unajumuisha muonekano wa kipekee wa jamii.
“Yaani inaweza kusemwa aina moja ambayo  inakubalika … ni kupitia nguo zao ambazo jamii imefahamika kuwa nazo mwanzoni, iwe ni kupitia kumbukumbu za  maandishi  au picha  au sinema.
“Hivyo yapo maendeleo bila tai, msuli au bila kuwepo kofia. Ukweli wa kitu  kinachomilikiwa katika kundi la jamii kwa  kawaida unafahamika kutokana na tamaduni za mavazi.”
Katika mazingira yoyote yale ni kwmaba utamaduni umekuwa unakabwa ili kuweka mianya mizuri ya kuubaka uchumi na hilo ndilo limekuwa likifanya pindi nchi zilizoendelea zinapovizia rasilimali ndani ya nchi zinazoendelea.

Comments