Featured Post

UGONJWA WA EBOLA NI JANGA, KAMWE USITUMIWE KAMA MTAJI WA KISIASA


 
NA DANIEL MBEGA
SERIKALI kupitia Wizari wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeshabainisha mikakati mbalimbali kama sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola, endapo utaibuka nchini.

Mikakati hiyo, kama ilivyotangazwa na Waziri Ummy Mwalimu, ni pamoja na kuwapatia mafunzo watendaji mbalimbali wa afya hasa wa maendeo ya mipakani, kuunda timu za dharura, kuwa na timu za ufuatiliaji na tathmini pamoja na kununua vifaatiba na vifaa kinga vitakakvyowasaidia watendaji wa sekta hiyo kuwahudumia wagonjwa ikiwa ugonjwa huo utakuwa umeingia.
Si hivyo tu, lakini wizara hiyo inafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Mambo ya Ndani, hususan Idara ya Uhamiaji, pamoja na wizara nyingine zinazohusika na ulinzi na usalama, ili kuhakikisha kwamba, kila mgeni anayeingia nchini, ambaye atakuwa anatokea katika maeneo yenye ugonjwa huo, hususan nchi ya Congo DR, wanapimwa kila wanapoingia.
Ukimsikiliza kwa makini Waziri Ummy utagundua kwamba siyo tu serikali imeweka mkakati, bali inajitahidi kudhibiti ikiwezekana ugonjwa huo usiingie nchini.
Tunafahamu jinsi ugonjwa huo ulivyowaathiri ndugu zetu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo umesababisha vifo vingi mpaka sasa.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limekwishaeleza kwamba, nchi takriban tisa zinazopakana na Congo DRC, ikiwemo Tanzania, zinatakiwa kuchukua tahadhari ya mapema kufuatia mlipuko wa pili uliotokea huko Kivu Kaskazini.
Hii inatokana na mwingiliano uliopo hasa katika Maziwa Makuu, ambapo kutokana na machafuko yaliyopo huko Kivu baina ya waasi na majeshi ya serikali pamoja na yale ya Umoja wa Mataifa, wananchi wengi wanakimbia makazi yao kutafuta hifadhi ama Uganda, Rwanda, Burundi na hata Tanzania.
Congo DRC inapakana pia na Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Congo, Angola, na Zambia.
Kinga ni bora kuliko tiba, na kwa vile ugonjwa wa Ebola bado haujapata tiba wala kinga, kuweka mikakati ya kuudhibiti ndiyo njia pekee ambayo inaweza ikawanusuru wananchi.
Tayari WHO imetoa takriban Shs. bilioni 5 kwa Serikali ya Tanzania ili kununulia vifaa kinga ambavyo vitatumiwa na watumishi katika maeneo ambayo yametengwa yakiwemo ya mipakani, Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam, na Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mbeya na Temeke ambazo zitahusika kuwahudumia wagonjwa watakaopatikana, ikiwa ugonjwa huo utaibuka.
Tayari Waziri Ummy ameitaka idara ya uhamiaji na watendaji wa vijiji waliopo katika maeneo ya mipakani kuimarisha ulinzi na kutoa taarifa ya wageni ambao siyo raia wa Tanzania wanahohisiwa kuwa na vimelea vya ugonjwa wa Ebola ili kuzuia ugonjwa huo ambao umeripotiwa nchini Congo DRC.

Mtaji wa kisiasa
Huu ni Mto Ebola kaskazini wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Lakini hofu kubwa iliyopo ni kwamba, upo uwezekano wa ugonjwa huo, ambao ni janga kama yalivyo majanga mengine, ukachukuliwa na wanasiasa kama mtaji wao.
Uzoefu uliopo unathibitisha hili kwa sababu mara kadhaa wanasiasa wetu walio wengi wa wa Afrika hushindwa kutanguliza mbele uzalendo na kuangalia zaidi maslahi yao ikiwa ni pamoja na kujipatia wafuasi katika jamii kwa kupotosha ukweli hata katika mambo ya msingi kabisa.
Tumewahi kushuhudia kuhusu majanga mengine ya asili ambayo yamepata kutokea kama mafuriko, tetemeko la ardhi, ukame na njaa, ambao wanasiasa wengi walishindwa kutumia busara na kupotosha kwa makusudi kwamba, yote hayo yametokea kwa sababu ya "uzembe wa serikali."
Mbali ya kuituhumu serikali kwa wanachokiita "uzembe", wanasiasa hao pia huthubutu kuharibu uhusiano wa kimataifa kwa kusingizia kwamba, magonjwa kama Ebola yamelewa na "Wazungu" ambao wanataka kuwaangamiza Waafrika.
Taarifa za aina hii zinazotolewa na wanasiasa kama mitaji yao zinachangia kuleta hofu kwa wananchi ambao mara nyingi huwaamini wanasiasa hao kiasi kwamba hata mamlaka husika zinapotoa taarifa sahihi inakuwa vigumu kwa wananchi hao kuziamini kwa sababu tayari wamekwishapotoshwa.
Haya yametokea hata katika mataifa ya Afrika Magharibi kama Sierra Leone, Guinea na Liberia, ambapo serikali za nchi hizo pamoja na mashirika ya kiutu ya kimataifa likiwemo Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) zilitumia nguvu na gharama kubwa kuubadilisha uongo huo ili kusema ukweli.
Lingekuwa jambo jema zaidi ikiwa wanasiasa wetu wakaacha siasa na kuongozwa na uzalendo kwa taifa letu ili kutumia majukwaa yao, hata kwenye mitandao ya kijamii, kueleza madhara ya ugonjwa huo na namna ya kujikinga ili wananchi wapate uelewa.

Athari kiuchumi, kiusalama
Iwe ni wanasiasa, ama mwananchi yetu, kama atasambaza taarifa ambazo si sahihi, madhara yake ni makubwa sana kiuchumi na kiusalama pia.
Mwananchi akipewa taarifa za upotoshaji ni wazi taifa litakumbwa na hofu kubwa, amani itatoweka na hakutakuwa na utulivu kiusalama.
Hali hiyo italeta ugumu hata wa kuwahudumia watu katika nyanja tofauti, jambo ambalo litayumbisha uchumi kwa kuwa hawataweza kuzalisha mali.
Kiusalama ni hatari kwa kuwa wananchi wanapokuwa wamekumbwa na hofu, hata vyombo vya usalama vitashindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu na itahitaji nguvu kubwa na gharama kubwa pia kuweza kurejesha amani.
Lakini kwa upande mwingine, uchumi utayumba kwa sababu hata wawekezaji tulionao wanaweza kukusanya mabegi yao na kuondoka, na wale wanaotaka kuja nchini, wakiwemo watalii, kamwe hawataingia.
Haya yameshuhudiwa katika mataifa ya Afrika Magharibi na ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na wanasiasa.

Ni ugonjwa hatari
Ugonjwa wa Ebola unasababishwa na virusi vya Ebola (EVD) na mara ya kwanza kugundulika barani Afrika ilikuwa mwaka 1976 wakati kulipokuwa na matukio mawili yaliyotokea kwa wakati mmoja, moja katika eneo la Nzara huko Sudan Kusini, na jingine katika katika eneo la Yambuku, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, karibu na Mto Ebola na ndiyo maana ugonjwa huo ukapewa jina la Ebola.
Mwaka huo 1976, kulikuwa na wagonjwa 318 huko Congo DRC na kati yao 218 walifariki dunia ambayo ni sawa na asilimia 88, kwa mujibu wa takwimu za WHO.
Huko Sudan (Kusini) kulikuwa na wagonjwa 284, na vifo 151 viliripotiwa ambayo ni sawa na asilimia 53.
Tangu mwaka huo 1976, kumekuwepo na matukio takriban 28 ya ugonjwa wa Ebola katika nchi za Afrika, zikiwemo Congo DRC, Sudan (Kusini), Gabon, Cote d'Ivoire,  Afrika Kusini, Uganda, Congo, Guinea, Sierra Leone,  Mali, Nigeria na Liberia; Marekani, na Hispania.
Congo DRC ndiyo nchi yenye matukio mengi zaidi (9) ikifuatiwa na Uganda matano na Gabon matatu.
Katika mlipuko wa karibuni huko Kivu Kaskazini, inaelezwa kwamba, kulikuwa na wagonjwa 116 ambapo vifo vilivyoripotiwa ni 77.
Tukiungana kwa pamoja, tukatanguliza uzalendo, tunaweza kusaidia taifa letu lisipatwe na majanga kama yalivyotokea kwa wenzetu, na hasa tunapaswa kupata taarifa sahihi kutoka vyanzo sahihi badala ya kutumia siasa.

Comments