Featured Post

TATTOO, UTOGAJI, MAPAMBO YA MPITO, MADHARA YA KUDUMU



NA MWANDISHI WETU
Katika Mkutano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoendelea jijini Dodoma Naibu Waziri, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile katika moja ya majibu ya maswali alibainisha kuwa kwa mwaka takribani wagonjwa 700 hupokelewa katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili wakiwa na matatizo ya ngozi yatokanayo na kijichubua.

Hali hiyo ilidhihirisha wazi kuwa wale wanaokuwa wamejichubua wanakuwa wamepata mapambo ya mpito lakini hatimaye wakajikuta wakuikumbana na madhara ya kudumu na linaweza kuunganishwa na mambo mengine yaliyo na madhara kwa ngozi au miili kwa ujumla.
Mwandishi wa makala haya kwenye makala yake moja ilikuwa na kichwa cha habari “Utogaji, michoro ya tattoo hupoteza haiba ya vijana” na hata hivyo yapo mengine ambayo yanahusiana na madhara kwa ngozi au miiili kama ilivyobainishwa kwa wale wanaojichubua.
“Kijana mmoja wa kike alikuja katika zahanati yangu akitaka niufute mchoro wa tattoo  aliyokuwa  amejichora mwilini, kisa ni kwamba mchumba wake alimwambia kuwa hataki kuiona la sivyo kuendelea kubaki nayo  ulikuwa ni mwisho wa uhusiano wao,” anasema daktari mmoja wa jijini Dar es Salaam ambaye amebobea katika magonjwa ya ngozi.
Daktari huyo anasema kuwa miongoni mwa nchi zilizoendelea  uchoraji wa tattoo hufanywa na wataalamu waliobobea na katika mazingira ya tiba na yaliyothibitishwa kwa kuwa na leseni.
Kufuta tattoo alisema kuwa nchi zilizoendelea watu wengi hujichora na kuzifuta tattoo kirahisi kwa kutumia mashine  zinazofahamika kama (laser- light amplified stimulation emission radiation), ambayo huvuta sehemuhusika na kufuta kama kifuto kwa maandishi yaliyoandikwa na penseli.
Hata hivyo akasema kuwakatika mazingira ambayo hakuna kifaa hicho inalazimu kukwangua ngozi na hivyo mhusika hubakia na kovu.
Kwa kuzingatia hali hiyo basi fikiria kwamba una binti yako ambaye sio tu anapenda michoro ya tattoo bali pia anaonekana kufikiria na kutaka kujua kwani alishawahi kusikia kuwa michoro hiyo na utogaji mwili ni vitu ambavyo vinaweza kumsababishia mtu madhara.
Mtihani unaokumbana nao ni kwamba unawezaje kumtaarifu binti huyo kuhusu madhara ambayo yanatokana na kuwatoga sanjari na kujichiora tattoo mwilini?
Lazima mtu atakuwa kwenye wakati mgumu kwa sababu michoro ya tattoo na utogaji mwili yamekuwa ni mambo maarufu miongoni mwa vijana wa jinsia zote siku hizi na kwa kiwango kikubwa yamekuwa ni mambo yanayoonekana kuwa ni mtindo au mitindo wa kisasa.
Aidha wengine wamekuwa wakiyachukulia kuwa ni namna ya kujionesha au kuonekana mbele ya rika lao kwamba wana hadhi ya aina fulani. Hata hivyo pamoja na kuwa hali hiyo inaweza kuwajengea umaarufu au la bado zimekuwepo athari nyingi ambazo zinasikitisha.
Katika kuikabili hali hiyo iwapo binti huyo atafumbuliwa na kupata mwangaza wa jinsi mambo yalivyo anaweza kuachana na fikra za aina hiyo na kuyaona ni mambo yasiyo na maana.

Michoro ya tattoo
Kwa vijana ambao wanapenda kujichora tattoo kwenye sehemu mbalimbali za miili yao huwa hawana muda wa kuangalia ni sehemu gani ambayo wanaweza kupata 'huduma' hiyo na ambayo inakaguliwa mara kwa mara na iwapo ina leseni ya kuendesha 'huduma' hiyo.
Katika hali hiyo kama kuchora tattoo itakuwa ni shughuli inayoendeshwa kwa utaalamu na wahusika kuwa na leseni wakiwa wanafuata tahadhari zinazotolewa ni wazi kuwa tishio la kiwango cha madhara litakuwa ni kidogo.
Katika msingi huo ni kwamba kijana ambaye atataka kuchora tattoo mwilini mwake atagundua kuwa michoro hiyo ni ghali na husababisha maumivu kwani kuziondoa alama sio kwamba ni jambo ambalo haliwezekani bali ni la gharama, husababisha maumivu na huchukua muda.
Katika hali yoyote ile hali ya ngozi haitakuwa ni ile iliyokuwepo awali. Tahadhari zinatakiwa kuchukuliwa dhidi ya matangazo ya biashara yanayodai kuwa kupaka aina fulani ya krimu ni njia ya ya uhakika ya kuondoa michoro hiyo kwani njia hiyo haijathibitishwa na wataalamu kwamba ni sahihi.
Katika mazingira hayo ni kwamba kile ambacho kinaonekana kwenye mazingira au maisha ya ujana kuwa ni kizuri kinaweza kugeuka kuwa kadhia kwenye miaka ya utu uzima na kusababisha kuwa na shinikizo la mawazo la kujilaumu. Hapa ndipo itakapoingia ile methali 'Maji yakishamwagika hayazoleki.'
Hali kadhalika katika kujichora huko ni kwamba baadhi ya magonjwa yanaweza kusambazwa kwa kutumia sindano ambazo sio safi. Maambukizi ya magonjwa ya ngozi kupitia tattoo yanaweza kuwa mabaya na hata kuharibu umbo na sura ya mtu.

Kutoga mwili
Utogaji wa mwili sio jambo lililo salama. Wataalamu au madaktari wa ngozi wanapinga aina yoyote ya utogaji wa mwili isipokuwa kwa masikio na wataalamu au madaktari wa meno wanapinga utogaji kwenye mdomo kwa kiwango cha kuita kitendo hicho kuwa madhara ya wazi kwa afya ya umma.
Madhara ya kiafya yanayohusiana na utogaji wa mwili ni pamoja na kuvuja damu nyingi kupita kiasi, kovu, pepo punda, majipu, uvimbe na maambukizi hatari kama vile ugonjwa wa kutoa harufu mbaya mdomoni ambako kutasababishwa na hereni zilizovikwa kwenye sehemu ya iliyotogwa kwenye ulimi.
Maambukizi ya homa ya manjano aina B na C ambayo ni tishio na haina tiba sahihi yanaweza kutokea kutokana na kutoga. Pamoja na hali hiyo ni kwamba muda wowote shimo la kudumu linakuwa limetokea kwenye midomo, pua na kwenye kope na ambalo sio rahisi kufanyiwa ukarabati.
Utogaji wa masikio na hususani kwa sehemu ya juu ya sikio mara nyingi husababisha maambukizi yanayochukua muda mrefu na mara nyingine kuishia kuharibu umbo la sikio ambalo linakuwa ni la kudumu.
Mara nyingine vyuma au hereni zinaweza kujishika kwenye nguo na katika kuzivuta zinaweza kusababisha kuchanika sehemu kubwa ya ngozi, sikio, mdomo, ulimi na sehemu nyinginezo.
Katika mazingira ya aina hiyo ya kumwelewesha mtoto athari za kutoga mwili, ni wazi kuwa kama mzazi inafaa kujiweka katika mazingira ya kusikitika na kwamba unaonesha umuhimu wa usalama kuliko kuwa kwenye mazingira ya kujaribu kuelezea nini cha kufanya.
Vijana mara nyingi hugeuka dhidi ya matamanio ya wazazi wao. Kutokana na hali hiyo ni muhimu kumhoji ni kwanini anataka kujichora tattoo au kutoga na majibu yake ndio yatakayowezesha kupatikana kwa suluhisho mbadala.
Hali kadhalika mzazi anaweza kuzungumza na mtaalamu au daktari wa ngozi na mara nyingine anaweza kufanya tafiti za picha za tattoo ambazo zinaonesha ni jinsi gani ambavyo haipendezi baada ya mtu kufikia umri mkubwa wa uzeeni, au kuongezeka mwili/uzito, au kuamua kuondoa michoro hiyo.
Taswira isiyovutia ambayo ni madhara ya miaka mingi yanaweza kuwepo kwa kujichora tattoo yanaweza kubadilisha mtazamo wa kijana kwa haraka.
Hata hivyo vijana wamekuwa wanatakiwa kupewa msukumo wa kufikiria kujichora tattoo na kutoga mwili. Bila kujali ni aina gani ya utendaji unafanywa na rika ni muhimu vijana kutambua kwamba kile ambacho kinaonekana kuwa kipo kwenye nyanja ya mtindo wa kisasa leo hii hakitaweza kuwa ni kile ambacho wangekitaka baadaye kwenye maisha yao.
Kutokana na hali hiyo msukumo unatakiwa na ambao utakuwa unawawezesha kufanya maamuzi ya kiutu uzima pamoja na kusaidiwa na hata kufundishwa namna ya kukabiliana na mashinikizo yanayotisha au kuogofya kutoka kwa makundi ya rika moja.


Comments