- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
TANZANIA YAJIVUNIA UONGOZI WA MAPAMBANO DHIDI YA UTAKASISHAJI FEDHA HARAMU NA UFADHILI WA UGAIDI MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mwenyekiti wa Umoja wa Udhibiti wa Fedha Haramu wa Nchi za
Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG), aliyemaliza muda wake, Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kulia), akiwa meza kuu
na Mwenyekiti mpya wa umoja huo, Waziri wa Fedha, Biashara, Uwekezaji na
Mipango ya Kiuchumi wa Seychelles, Balozi Maurice Lousteau – Lalanne, wakati wa mkutano wa 18 wa Umoja huo
uliofanyika, Mahe-Seychelles.
NA BENNY MWAIPAJA, WFM, MAHE,
SEYCHELLES
TANZANIA
imekabidhi uongozi wa mwaka mmoja wa Umoja wa Udhibiti wa Fedha Haramu wa Nchi
za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG) kwa nchi ya Seychelles, huku
ikijivunia mafanikio makubwa ya kuhakikisha kuwa nchi wanachama wa umoja huo
zinakuwa na sera, sheria, taasisi na mifumo imara inayowezesha mapambano dhidi
ya vitendo vya utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekabidhi uongozi huo kwa niaba ya
Serikali ya Tanzania kwa Waziri wa Fedha, Biashara, Uwekezaji na Mipango ya
Kiuchumi wa Seychelles Balozi Maurice Lousteau – Lalanne, wakati wa Mkutano wa 18 wa
Baraza la Mawaziri wa Umoja huo, uliofanyika Mjini Mahe, nchini Seychelles na
kushuhudiwa na Rais wa Nchi hiyo, Mhe. Danny Faure.
Miongoni
mwa mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, ni kufanyika
kwa tathimini ya mifumo ya kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili
wa ugaidi wa nchi tatu wanachama wa umoja huo za Mauritius, Madagascar na
Seychelles, na kwamba zoezi la kuzitathmini nchi nyingine mbili za Zambia na
Malawi, linaendelea.
"Rasilimali
za nchi zetu zinahitaji kutumika vizuri, kwa sababu zinapotumika vibaya
zinapunguza uwezo wa nchi zetu kuchochea maendeleo haraka, pale zinapo
hatarisha sekta yetu ya fedha, matumizi adili ya rasilimali hizi na usalama wa
nchi zetu" alisema Dkt. Mpango.
Aidha,
Dkt. Mpango amesema kuwa utakasishaji wa fedha haramu unazuiwa kwa sababu
unamadhara makubwa kiuchumi, kijamii na kiusalama kwa nchi wanachama.
"Fedha
ambazo zinakuja kuja tu hivi! Hujui kama zinakwenda kugharamia ugaidi, au ni
fedha za wananchi wetu lakini wanazitorosha ambapo badala ya kuzitumia ipasavyo
wanazitumia kufanya mambo haramu" aliongeza Dkt. Mpango.
Kwa
upande wake, Katibu Mtendaji wa Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini Mwa Afrika
ESAAMLG, Dkt. Elliawony Kisanga amesema kuwa tangu umoja huo uanzishwe
miaka 19 iliyopita, yamekuwepo mafanikio makubwa na kazi iliyopo mbele ya
uongozi mpya ni kuanza na kuendelea kufanyika kwa tathmini ya mifumo ya udhibiti
ya nchi za Zambia, Malawi na Tanzania.
Mwenyekiti
Mpya wa ESAAMLG, Waziri wa Fedha, Biashara, Uwekezaji na Mipango ya Kiuchumi wa
Seychelles Balozi Maurice Lousteau – Lalanne, ameipongeza Tanzania chini
ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, kwa uongozi wake mahili na
kuuwezesha umoja huo kutekeleza majukumu yake ipasavyo na msukumo wake utakuwa
kuwezesha nchi wanachama kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria.
Aidha
Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa ESAAMLG ulitanguliwa na Mkutano wa 36 wa
Kikosi Kazi cha Maafisa waandamizi wa ESAAMLG, ambapo ndugu Onesmo Makombe
alikabidhi kwa niaba ya Tanzania Uenyekiti wa Kikosi Kazi cha Maafisa
Waandamizi wa ESAAMLG kwa ndugu Philip Moustache wa Jamhuri ya Seychelles.
Tanzania
ilipokea uongozi wa Umoja huo Septemba 7 mwaka jana wakati wa Mkutano wa 17 wa
Baraza la Mawaziri wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika uliofanyika
Zanzibar, ikipokea majukumu ya uongozi huo kutoka nchi ya Zimbabwe.
Comments
Post a Comment