- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
TANZANIA YA YAIBAKIDHI SEYCHELLES UONGOZI WA MAPAMBANO DHIDI YA UTAKASISHAJI FEDHA HARAMU NA UFADHILI WA UGAIDI MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mwenyekiti wa Umoja wa Udhibiti wa Fedha Haramu wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG), aliyemaliza muda wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (wa pili kulia), akipongezana na Mwenyekiti mpya wa umoja huo, Waziri wa Fedha, Biashara, Uwekezaji na Mipango ya Kiuchumi wa Seychelles, Balozi Maurice Lousteau – Lalanne, wakati wa Mkutano wa 18 wa Umoja huo uliofanyika, Mahe-Seychelles. Kulia ni Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Maafisa Waandamizi wa ESAAMLG aliyemaliza pia muda wake kutoka Tanzania, Onesmo Makombe.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango, Seychelles).
Na Benny Mwaipaja, WFM, Mahe, Seychelles
TANZANIA imekabidhi uongozi wa
mwaka mmoja wa Umoja wa Udhibiti wa Fedha Haramu wa Nchi za Mashariki na Kusini
mwa Afrika (ESAAMLG) kwa nchi ya Seychelles, huku ikijivunia mafanikio makubwa
ya kuhakikisha kuwa nchi wanachama wa umoja huo zinakuwa na sera, sheria,
taasisi na mifumo imara inayowezesha mapambano dhidi ya vitendo vya
utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, amekabidhi uongozi huo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kwa
Waziri wa Fedha, Biashara, Uwekezaji na Mipango ya Kiuchumi wa Seychelles
Balozi Maurice Lousteau – Lalanne,wakati wa Mkutano wa 18 wa Baraza
la Mawaziri wa Umoja huo, uliofanyika Mjini Mahe, nchini Seychelles na
kushuhudiwa na Rais wa Nchi hiyo, Mhe. Danny Faure.
Miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa
katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, ni kufanyika kwa tathimini ya mifumo ya
kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi wa nchi tatu
wanachama wa umoja huo za Mauritius, Madagascar na Seychelles, na kwamba zoezi
la kuzitathmini nchi nyingine mbili za Zambia na Malawi, linaendelea.
"Rasilimali za nchi zetu
zinahitaji kutumika vizuri, kwa sababu zinapotumika vibaya
zinapunguza uwezo wa nchi zetu kuchochea maendeleo haraka, pale zinapo
hatarisha sekta yetu ya fedha, matumizi adili ya rasilimali hizi na usalama wa
nchi zetu" alisema Dkt. Mpango
Aidha, Dkt. Mpango amesema kuwa
utakasishaji wa fedha haramu unazuiwa kwa sababu unamadhara makubwa kiuchumi,
kijamii na kiusalama kwa nchi wanachama..
"Fedha ambazo zinakuja kuja tu
hivi! Hujui kama zinakwenda kugharamia ugaidi, au ni fedha za wananchi wetu
lakini wanazitorosha ambapo badala ya kuzitumia ipasavyo wanazitumia kufanya
mambo haramu" aliongeza Dkt. Mpango
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa
Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini Mwa Afrika ESAAMLG, Dkt.
Elliawony Kisanga amesema kuwa tangu umoja huo uanzishwe miaka 19
iliyopita, yamekuwepo mafanikio makubwa na kazi iliyopo mbele ya uongozi mpya
ni kuanza na kuendelea kufanyika kwa tathmini ya mifumo ya udhibiti ya nchi za
Zambia, Malawi na Tanzania.
Mwenyekiti Mpya wa ESAAMLG, Waziri
wa Fedha, Biashara, Uwekezaji na Mipango ya Kiuchumi wa Seychelles BaloziMaurice
Lousteau – Lalanne, ameipongeza Tanzania chini ya Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, kwa uongozi wake mahili na kuuwezesha umoja huo
kutekeleza majukumu yake ipasavyo na msukumo wake utakuwa kuwezesha nchi
wanachama kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria.
Aidha Mkutano wa Baraza
la Mawaziri wa ESAAMLG ulitanguliwa na Mkutano wa 36 wa Kikosi Kazi cha Maafisa
waandamizi wa ESAAMLG, ambapo Bw. Onesmo Makombe alikabidhi kwa niaba ya
Tanzania Uenyekiti wa Kikosi Kazi hicho kwa Bw. Philip Moustache wa Jamhuri ya
Seychelles.
Tanzania ilipokea uongozi wa Umoja
huo Septemba 7 mwaka jana wakati wa Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi
za Mashariki na Kusini mwa Afrika uliofanyika Zanzibar, ikipokea majukumu ya
uongozi huo kutoka nchi ya Zimbabwe ambapo Umoja huo unaundwa na nchi 18 ambazo
ni Angola, Botswana, Eswatini, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Madagascar, Malawi,
Mauritius, Mozambique, Namibia, Rwanda, Seychelles, South Africa, Tanzania,
Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Comments
Post a Comment