Featured Post

SERIKALI KUTEKELEZA MIRADI KWA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI YENYE THAMANI YA MABILIONI YA SHILINGI

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akifungua semina ya siku moja iliyowahusisha Mawaziri, Naibu Mawaziri na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Taasisi zake, kuhusu Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), iliyofanyika katika ukumbi wa  Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Walemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), akuzungumza wakati akiahirisha semina ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Jijini Dodoma.
Mshauri wa Masuala ya Kisheria katika mradi wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kutoka Benki ya Dunia, Philip Kelly akiwasilisha mada katika semina ya siku moja ya  PPP, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Lugola (Mb) (kulia) akiwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi -CCM (2015) wakati aliposhiriki semina ya Siku moja iliyohusisha Mawaziri, Naibu Mawaziri na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Taasisi zake, kuhusu Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), iliyofanyika katika ukumbi wa  Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
Baadhi ya Washiriki wa Semina ya siku moja iliyohusisha Mawaziri, Naibu Mawaziri na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Taasisi zake, wakifuatilia mada kuhusu Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), iliyofanyika katika ukumbi wa  Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Walemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), (kushoto) akisoma makabrasha kuhusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Jijini Dodoma. kushoto kwake ni Naibu Waziri Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Mhandisi Stella Manyaya (Mb) na anayefuatiwa ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Japhet Hasunga.
Mshauri wa Masuala ya Kisheria katika mradi wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) Bw. Philip Kelly (katikati) akifafanua jambo wakati wa semina ya siku moja ya  PPP, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma. Kushoto ni Mtaalamu wa Masuala ya PPP, Bw. Craig Sugden na kulia ni Bw. Abhijit Bhaumik, wote watatu wanatoka Benki ya Dunia.
Kamishna wa Idara ya Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. John Mboya, akieleza namna Serikali na Sekta Binafsi ilivyojipanga kutekeleza zaidi ya miradi 10 katika sekta za Afya, Barabara, Reli, Dawa za binadamu na elimu, wakati wa Semina ya siku moja ya Ubia kati ya pande hizo mbili iliyowashirikisha Mawaziri, Naibu Mawaziri na Maafisa waandamizi wa Serikali na baadhi ya Taasisi zake, Jijini Dodoma
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuahirishwa kwa Semina ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki ya Dunia,  yaliyohusisha Mawaziri na Manaibu waziri, Jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini-WFM)


Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuanzisha na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ubia kati ya Sekta ya Umma na  Binafsi (PPP) ambapo miradi  zaidi ya 11 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji lengo likiwa ni kufanikisha azma ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Idara ya  Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP),  Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. John Mboya  wakati akiwasilisha mada ya utekelezaji wa dhana ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo nchini kwenye semina iliyowashirikisha mawaziri, naibu mawaziri na baadhi ya watendaji wa serikali iliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Akiwasilisha mada hiyo, Dkt. John Mboya amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa  umakini mkubwa katika uandaaji na utekelezaji wa dhana hiyo ya ubia Sekta ya Umma na Binafsi kwa kuzingatia sheria, sera, miongozo, kanuni na taratibu mbalimbali zilizopo.
Aidha alizitaka taasisi na wadau wa utekelezaji kuwa tayari kujifunza kutoka katika nchi zilizoendelea kupitia dhana hii ya ushirikikishwaji wa sekta binafsi katika kuchochea ukuaji wa viwanda na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Dkt. Mboya aliitaja baadhi ya miradi iliyoko katika hatua mbalimbali ya utekelezwaji kwa Ubia kati  ya Sekta ya Umma na Binafsi kuwa ni  mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART), Ujenzi wa Viwanda vya dawa, mradi wa VETA utakaohusisha ujenzi wa vyuo 10 ambavyo vinatarajiwa kutoa ujuzi mbalimbali kwa wanafunzi wapatao 90,000 ili kukidhi mahitaji ya wataalamu watakao saidia kufanikisha uchumi wa viwanda.
"MIradi Mingine ni Ujenzi wa Bandari ya Mwambani, barabara ya Dar es salaam hadi Chalinze, Ujenzi wa Reli kwenye miradi ya Mchuchuma hadi Mbambabay mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara, Ujenzi wa Reli kuanzia Tanga, Arusha hadi Musoma, na  mradi wa umeme wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Akijibu swali la Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,   Josesph Kakunda, aliyetaka kujua kuhusu kuondolewa kwa sheria ya utekelezwaji  wa miradi kwa Ushirikishwaji wa Pamoja kati ya serikali na sekta binafsi (Joint Venture) ambayo haikufanikiwa kama ilivyokusudiwa hapo awali, Dkt. Mboya alisema kuwa sheria hiyo haijaondolewa bali  miradi hiyo itatekelezwa kupitia sheria ya Kampuni.
Akichangia katika mjadala wa semina hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya, alisema ni vema wakati wa kuchagua miradi wahusika wawe makini ili kuepuka kuanzisha miradi inayofanana na ambayo inaweza kuwa chanzo cha kufa kwa miradi iliyotangulia.
"Ninashauri kuwepo kwa fursa ya ushirikishwaji katika miradi midogo ambayo ina manufaa kwa wananchi ikiwemo ya ujenzi wa nyumba za waalimu" Alisema Mhandisi Manyanya
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alizitaka taasisi ambazo zinatekeleza miradi kwa ubia na sekta binafsi zielezee umma wa watanzania mafanikio yaliyopatikana ili kuhamasisha wadau wengine kufuata nyayo hizo huku akitolea mfano Shirika la Maendeleo ya Petroli  nchini (TPDC) ambalo nalo liko katika utekelezaji wa dhana hiyo.
Mwenyekiti wa semina hiyo  Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, alisema kuwa Serikali imepeleka Muswada Bungeni unaohusu PPP, ambao ukipitishwa na Bunge linalotarajiwa kuanza Septemba 4, 2018, utekelezaji wa ubia huo utakwenda kwa kasi zaidi ili kuiwezesha nchi kufikia malengo yake ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge , Kazi,Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama, akiahirisha mafunzo hayo, aliwataka wadau wa semina hiyo kuendelea kukutana na kuelimishana hadi hapo marekebisho ya sheria hiyo ya Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) yatakapofanyika.
"Utekelezwaji wa dhana hii ya Ubia Sekta ya Umma na Binafsi ndio njia rahisi itakayosaidia kukamilisha miradi mingi ambayo imeainishwa katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapainduzi (CCM) na kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, bila ushirikiano huu na sekta binafsi hatuwezi kufikia uchumi wa viwanda kwa kasi inayotakiwa’’ Alisema Waziri Mhagama.
Semina hiyo ya siku moja imeendeshwa na wataalamu wa masuala ya Ubia Sekta ya Umma na Binafsi kutoka Benki ya Dunia, ambapo Jumapili, kamati tatu za Bunge zitapatiwa elimu na kujengewa uwezo kuhusu dhana hiyo ya PPP. 




Comments