Featured Post

POLISI KENYA WAVAMIA OFISI ZA SHIRIKA LA HABARI LA CHINA



NAIROBI, KENYA
MAOFISA waliojihami wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi wa Kenya wamevamia ofisi za chombo cha habari cha Uchina China Global Television Network mjini Nairobi na kuwakamata wafanyikazi wa kigeni.

Mfanyikazi mmoja wa chombo hicho Saddique Shaban anasema kuwa takriban maafisa kumi ambao hawakujitambulisha walivamia makao hayo makuu ya runinga hiyo barani Afrika na kutaka kupewa vibali vya kufanyia kazi na wageni hao.
Kanda za video zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii ziliwaonyesha maafisa hao wa usalama wakiwakamata na kuwatoa wafanyikazi wa Kichina nje ya kituo hicho cha habari ambacho pia kina runinga.
Uvamizi huo umeharibu matangazo ya shirika hilo nje ya bara Afrika.
Waziri wa maswala ya ndani nchini Kenya, Fred Matiangi, amekuwa akiongeza msako huo dhidi ya wafanyikazi wa kigeni wasio na vibali vya kufanya kazi nchini.
Inspekata Jenerali Mkuu wa Polisi, Joseph Boinet, aliambia kituo cha habari cha Nation kwamba maofisa wake walifanya uvamizi huo baada ya kupata habari kwamba baadhi ya wafanyikazi katika kituo hicho cha Runinga hawakuwa na vibali vya kufanya kazi nchini humo.
Ofisa huyo anasema kuwa raia 13 wa China waliokuwa wamekamatwa waliachiliwa mara moja baada ya vibali vyao vya kufanya kazi nchini kuthibitishwa.
Ubalozi wa China ulitoa taarifa ukishutumu kukamatwa kwa raia wake na maafisa wa Polisi wa Kenya.
Ubalozi huo umesema kuwa raia wa Uchina ambao wanaishi nchini humu na kufanya kazi kihalali hawafai kuzuiliwa.
Idara ya uhamiaji ilianza msako dhidi ya wageni wanaofanya kazi kinyume na sheria kuanzia mwezi Mei.
Zaidi ya wageni 100,000 wanalengwa katika msako huo.

Comments