Featured Post

MISAADA INAUMIZA, SI NEEMA BALI BALAA



NA ALOYCE NDELEIO
“Lazima tufange kazi kwa maendeleo yetu badala ya kusbiri fedha kutoka nje, inashangaza  wananchi wanasubiri kumwagiwa fedha, utasikia, neema yaja, heshima ya nchi ni kujitambua, kujitegemea.”
Hivyo ni kauli y Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu , Benjamin William Mkapa wakati akizindua  kitabu, Global Poverty  (The Case for sub-Sahara Africa), kilichoandikwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Marten Lumbanga na kuongeza, “Hakuna wa kutumwagia  kwa ajili ya maendeleo yetu bali yataletwa kwa watu kufanya kazi kwani heshima ya nchi ni kujitegemea.”
Aidha Balozi  Lumbanga alisema “Kwa bahati nzuri  nchi nyingi za Afrika zinajitambua  kuwa ni maskini na kazi inayoendelea  ni kuondokana na umaskini, maendeleo yanaonekana.”

Hivyo si mara ya kwanza kwa Rais Mstaafu Mkapa kutoa  maoni yake hayo kwani  hivi karibuni alisema nchi za Afrika hazitajikomboa kiuchumi kama zitaendelea kutegemea na kushabikia misaada kutoka kwa nchi wahisani na badala yake zitumie rasilimali na biashara zao wenyewe ili zifike mbali zaidi ya zinavyodhani.
Kauli hiyo aliitoa kwenye kongamano la lililowashirikisha pia Marais Wastaafu Olusegun Obasanjo wa Nigeria na Festus Mogae wa Botswana likiwa lilikuwa limeandaliwa na Taasisi ya Uongozi jijini Dar es Salaam.
Hoja inayojitokeza katika maoni hayo yanathibitisha kile kinachoelezwa kuwa misaada inayotolewa  na nchi zilizoendelea  ipo katika mifumo kadhaa, kiuchumi, kijamii  na kibinadamu na imekuwa ndio kipaumbele cha nchi hizo tangu kipindi kilichofuata baada ya uhuru  wa nchi nyingi za Afrika  miaka ya 1960.
Asasi zisizo za serikali  kwa mamia elfu  zimekuwa zikijaribu kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi zikiwa zinapambana na magonjwa ya kutisha, kutoa misaada ya chakula na maji, kutoa walimu na mambo mengine mengi.
Misaada inayotolewa kwa ajili ya waathirika wa janga la asili huwa na ufanisi katika kupunguza maumivu ambayo yanakuwepo kwa wakati huo wa tukio na hata hivyo huwa sio suluhisho la kudumu na haisaidii kutoa jukwaa imara kwa nchi iliyokumbwa na janga  katika mazingira  endelevu.
Hivyo nchi tajiri zimekuwa zinatoa misaada, sawa, na hali kadhalika kuwepo kwa watu wanaoendelea kukampeni kuhusu upatikanaji wa misaada, lakini misaada hiyo kutoka nje  haioneshi kuchangia katika hatua za maana za kupambana na umaskini miongoni mwa nchi maskini.
Tangu miaka ya 1950 utamaduni wa maendeleo ya kiuchumi umekuwa unahodhiwa na wazo kuwa kiwango kikubwa cha misaada ni suluhisho la kuziba pengo lililopo miongoni mwa nchi zinazoendelea, lakini kiuhalisia  umekuwepo uthibitisho unaoonesha kuwa mtiririko mkubwa wa misaada hiyo huishia kuleta madhara zaidi kuliko kuneemesha.
Uchambuzi wa kukua kwa uchumi katika nchi za Asia katika miongo kadhaa iliyopita ambazo zimekuwa zikipokea kiwango kidogo cha misaada ikilinganishwa na Afrika ni kielelezo kizuri kwamba misaada haisaidii.
Ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia inaonesha kuwa miongoni mwa watu milioni 700 waliondolewa kutoka kwenye lindi la umaskini kati ya mwaka 1980 na 2010, watu milioni 627 kati ya hao ni kutoka China. Hiyo inamaanisha kuwa watu milioni 73 ni kutoka  sehemu nyingine duniani.
Kwa maneno mengine ni kwamba asilimia 89.6 walitoka China, hivyo  kutoa kiashiria kilicho wazi kwamba misaada kutoka nje si suluhisho dhidi ya umaskini.
Kimsingi utoaji wa misaada ulionekana kama njia ya kutokomeza umaskini uliokithiri lakini kuanzia miaka ya 2000 nadharia ya msukumo mkubwa  imekuwa ndio mada inayozua mjadala ikihusu matokeo hasi ya misaada ambayo inaonekana kuziacha nchi zinazoendelea katika hali mbaya kuliko zilivyokuwa.
Kwa kuliangalia eneo la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, juhudi zote zilizokwishafanyika zinajionesha wazi, lakini kwa kuangalia takwimu za misaada ya nje katika bajeti kwa nchi nyingi, kiwango cha kupiga hatua kimebadilika ghafla na kuonekana kuwa ni cha chini ikilinganishwa na  fedha nyingi ambazo zimeshapokea.
Kwa ujumla Afrika inapokea takribani dola bilioni 50 za misaada ya kimataifa kwa mwaka.
Hata hivyo, badala ya kuboresha kwa kasi hali ya maisha ya watu milioni 600 wanaoishi chini ya mstari wa umaskini, misaada hiyo imewafanya walio matajiri kuwa matajiri zaidi.
Taswirahiyo inaonesha kuwa walio maskini kuwa maskini zaidi na hivyo kukwamisha ukuaji wa uchumi, na hali kadhalika kuchochea  mzunguko wa rushwa.
Misaada Rasmi ya Maendeleo (ODA) ni utoaji rasmi wa fedha ambazo zinagawiwa miongoni mwa nchi zinazoendelea zikilenga kukuza maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa nchi hizo.
Fedha hizo ambazo humwagwa kwa nchi hizo zinatoka si tu kwa serikali moja kwenda kwa serikali nyingine ikiwa ni programu ya msaada, bali pia  hutoka katika  programu za maendeleo kimataifa zinazoratibiwa na Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambao huwa ni wawezeshaji kati ya serikali zinazotoa na zile zinazopokea.
Misaada ya nje haina tofauti na kushamirisha rushwa na utegemezi. Hii inamaanisha kuwa misaada inaimarisha wigo wa rushwa miongoni mwa nchi zinazopokea na ambako tayari rushwa imesambaa.
Kwa mujibu wa Transparency International (TI) ni kwamba kwa bahati mbaya  hali hiyo ndiyo iliyotamalaki miongoni mwa nchi nyingi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zinapokea kiwango kikubwa cha misaada.
Nchi hizo zina kiwango kidogo cha ufanisi katika maeneo mengi ya utawala bora  hususani katika suala la rushwa.
Hali hiyo inaonesha kwamba  misaada ya nje inasukuma kiasi cha rasilimali zilizopo kuwa mikononi mwa makundi maalumu ya viongozi, ambao wanakuwa maswahiba wa watendaji wa serikali. Hili liko wazi kwani wapo viongozi ambao ni wadokozi na ambao hufumbia mcho vimelea vya rushwa.
Hakuna uwiano sawa katika usambazaji wa misaada miongoni mwa idadi ya watu au matumizi yake katika kukuza uchumi na kusaidia watu maskini badala yake zimekuwa zikitumika kununulia vifaa vya kijeshi, kuanzisha au kuendesha miradi ya anasa isiyo na faida, manunuzi ya uongo au kughushi katika manunuzi hayo n.k. 
Hali kadhalika fedha hizo za misaada zinatumiwa na viongozi ambao wanakuwa na sera chache na wanataka kufikia malengo yao ya kisera kwa kasi, ikiwa ni pamoja na kuongeza ukubwa wa serikali kwa kuajiri watumishi (ambao hawachangii chochote katika mfumo au maendeleo na mara nyingine kuajiri watumishi hewa) ikiwa ni njia ya kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira.
Madhara kwa upande wa utegemezi ni kwamba nchi ambazo zimekuwa zikipokea kiwango kikubwa cha fedha zimekuwa hazikuzi biashara za ndani  kwa sababu zinakuwa na fedha za ‘bure’ mikononi mwao. Hali hiyo inazuia  aina yoyote ya kuboresha maendeleo ya binadamu na hata pato la nchi.
Hoja inayoibuka ni kwamba kwanini misaada inaendelea kutolewa? Kimsingi inaonesha kama vile wanasiasa wa nchi zilizoendelea wapo kama wanaangalia na kuwalinda wenzao wa nchi zinazopokea misaada.
Mkakati wa kimaslahi na kisiasa wa wahisani unaonesha kuwa hatua za kutoa misaada ni muhimu zaidi kuliko kujali suala la utawala bora  miongoni mwa mataifa yanayopokea.
Hali hiyo inazifanya nchi za Afrika kutopiga hatua ya maendeleo huku zikiwa zinaongozwa na viongozi wadokozi. Historia ya ukoloni nayo inachangia kwa kiwango kikubwa katika mchakato wa misaada.
Ufaransa kwa mfano huwa inatoa kiwango kikubwa cha misaada kwa nchi zilizokuwa makoloni yake ikiwa ni kama kufuta madhara ya mambo waliyoyafanya hapo zamani.
Australia na nchi za Nordic huwa zinawatenga, tofauti na Ufaransa au Uingereza nchi hizo hutoa misaada yake tu kwa nchi zilizo na kiwango kidogo cha rushwa. Hii inatokana na sababu kuwa hazikuwa na makoloni hivyo zinakuwa huru dhidi ya mashinikizo ya kisiasa.
Kama rejea ni kwamba Kamisheni ya Uchumi ya Ulaya (EEC) ambayo hivi sasa ni Umoja wa Ulaya (EU) iliwahi kuzitenga nchi za Ureno, Ugiriki na Hispania kabla ya kuwa wanachama wake na hivyo kuwaruhusu  kuwa wanachama wake baada ya kuwa na serikali za kidemokrasia.
Hilo lilionekana ni sawa na huenda IMF na WB wanaweza kufanya jambo kama hilo kwa sababu hadi sasa hawajazitenga nchi zinazopokea misaada na ambazo rushwa miongoni mwake imetamalaki.
Hata hivyo hoja nyingine ni kwamba je, uchumi wa nchi za Afrika unaweza kurudi katika mkondo sahihi? Kama misaada inakuwa haifanyi kazi basi kuna haja ya kufanya marekebisho.
Kama watendaji hao wa dunia hataweza kusaidia basi angalau wasiache mambo yakazidi kuharibika. Sera mpya na hamasa zinaweza kuwekwa pamoja kuonesha hatua kuliko kushindwa. Misaada inatakiwa ibadilishwe  iwe ni biashara. Ikimaanisha kuwa misaada hiyo itolewe katika mfumo wa biashara.
Wananchi wa Afrika wanatakiwa kujengewa uwezo hivyo kwamba wanakuwa waundaji wa ujasiriamali unaostawi, ili wamudu kuishi  kwa kutumia shughuli zao. Sera sahihi na zilizokamilika pamoja na usimamizi mzuri wa masuala ya uchumi  ni muhimu zaidi kuliko misaada kwa nchi zinazoendelea.
Taasisi thabiti na imara  zinaepuka misaada kwa kuwa inageuka kuwa laana. Hivyo lazima iwepo misaada katika kuboresha utawala bora  kabla ya kutolewa msaada wa kifedha kwa sababu bila serikali thabiti, misaada ya kifedha haitaweza kufanikisha matamanio ya malengo.

Comments