- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MWANDISHI WETU
Inatolewa chemsha bongo ya Jiografia-uchumi, “Zao gani
linalopatikana Afrika linalozaa mara mbili zaidi ya mahindi, mara tatu zaidi ya
mtama au uwele, ndiyo inayoongoza, nusu ya uzalishaji duniani inapatikana
Nigeria, uzalishaji umekuwa unaongezeka mara tatu kwa miaka 50 iliyopita na
huchangia theluthi moja ya mahitaji ya chakula ya idadi ya watu wake?”
Jibu la swali hilo ni mhogo; na taswira inaweza kukupeleka
kwenye ulaji wa mihogo mibichi ambao ni jambo la kawaida miongoni mwa jamii za
mijini pia, iliyochemshwa au kukaangwa, na ni maarufu kama chipsi dume.
Takwimu za mwaka 2004 za Shirika la Kilimo na Chakula la
Umoja wa Mataifa (FAO), inaonesha Afrika inazalisha mihogo kwenye eneo la
hektari milioni 18 kwa mwaka.
Miongo kadhaa iliyopita, mihogo imekuwa inalimwa kwenye
maelfu ya hektari na imekuwa chakula kikuu cha zaidi ya watu milioni 200 ambayo
ni sawa na robo ya idadi ya wa Afrika.
Mihogo inastawi vizuri katika nchi kadhaa mfano Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo ambayo kwa muda mrefu imekuwa inaongoza kwa uzalishaji,
imeenea hadi kusini mwa Afrika nchini Malawi na Zambia na mara nyingine hupiku
kilimo cha mahindi.
Hali kadhalika kutokana na ongezeko la VVU/Ukimwi ambao
umeua wakulima wengi, familia nyingi zimeingia kwenye kilimo cha mihogo kwani
kinahitaji nguvu kazi kidogo.
Uhakika wa kupambana
na njaa
Kwa wakulima wanaoishi maeneo ya karibu na miji ni zao zuri
la biashara na soko lake linapanuka.
Aidha, Ushirikiano wa Kiuchumi wa nchi za Afrika (NEPAD) kwa
kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo ya nchi za Tropiki (IITA)
ilizindua mkakati wa mihogo kwa Afrika ili kutoa msukumo kwa miradi ‘inayotumia
mihogo kama zao la uhakika wa chakula na silaha dhidi ya umaskini’.
Majani ya mhogo ni mboga maarufu ‘kisamvu’ ikiwa na protini
na unga wa mihogo hutumika kupika ugali ambao umepewa majina tofauti kulingana
na eneo kama bada, gari, attieke, foufou, chikwangue.
Hata hivyo kwa mujibu wa IITA takriban theluthi moja ya
mihogo yote huliwa ikiwa mibichi.
Utafiti Shirikishi wa Mihogo Afrika (COSCA) wa miaka ya 1990
ulibainika asilimia 20 ya mihogo inayozalishwa vijijini hutumiwa mijini.
Hata hivyo zao hilo linakabiliwa na magonjwa ambayo
yanahatarisha mazingira ya uhakika wa chakula na hali hiyo ilijionyesha
liliposhambuliwa na virusi nchini Uganda miaka ya 1990.
Kudhibiti magonjwa
Wanasayansi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Tropiki
(IITA) wakishirikiana na wataalamu wa Mfumo wa Taifa wa Utafiti wa Kilimo
nchini Tanzania hivi karibuni walitangaza aina ya miche ya mihogo
isiyoshambuliwa na ugonjwa wa mihogo Cassava Brown Streak (CBSD).
Ugonjwa huo hatari huozesha mizizi na umekuwa ukisumbua
katika maeneo yanayolima mihogo katika eneo la nchi za Maziwa Makuu.
Virusi wa ugonjwa huo Cassava Brown Streak (CBSV)
wamesababisha uzalishaji kushuka kuanzia asilimia 20 hadi 80 hivyo kuathiri
maisha ya watu wengi wa eneo la Afrika Mashariki.
Umekuwa kikwazo kikubwa katika juhudi za kujihakikishia
uhakika wa chakula nchini Tanzania ambako takribani watu milioni 50 wanategemea
mihogo katika lishe zao na kiuchumi, CBSD imesababisha hasara ya dola za
Marekani milioni 50 kwa wakulima wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Dkt. Caroline Herron, ambaye ni mtaalamu wa
magonjwa ya mimea kwenye utafiti wake juu ya mabadiliko ya virusi hao katika
Afrika Mashariki anasema: “Katika kipindi cha 15 iliyopita CBSD ulionekana
nchini Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Zambia, Malawi na Msumbiji.”
Aidha, Dkt. Edward Kanju, mtaalamu wa kukuza mihogo wa IITA
na Haji Saleh kutoka Wizara ya Kilimo, Kizimbani Zanzibar, wanaarifu kuwa
wakulima waliohusishwa kwenye mradi shirikishi wa kukuza miche ya mihogo
walitoa msukumo kwa serikali kutoa miche hiyo ambayo haishambuliwi na CBSD na
changamoto iliyopo ni kuotesha mimea hiyo kuchukua nafasi ya mimea
iliyoathirika.
Mihogo kwa kipindi cha miaka mingi imekuwa inadharauliwa na
tafiti ambazo zimekuwa zinatoa kipaumbele kwa nafaka nyingine lakini hivi
karibuni imeonyesha mafanikio kwamba ni lishe ya watu kwenye maeneo mengi na hivyo
kuonyesha umuhimu wa kufurahia ustawi wake.
Mihogo ya Tanzania
kuuzwa China
Katika hotuba yake wakati wa kufungua kikao cha Bunge la
bajeti kilichomalizika Juni 29, mwaka huu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Kassim Majaliwa alisema kuwa
mihogo imepata soko nchini China.
China na Thailand zina miradi kadhaa inayohusisha
kutengeneza nishati mbadala ya mihogo kwa ajili ya viwanda. Hiyo ni sehemu tu
lakini ni malighafi katika sekta nyingine na itajibainisha kadri soko lake litakavyokuwa linakua.
Mihogo inaweza kutumiwa kuzalisha nishati mbadala kwa
kiwango cha asilimia kumi hadi 25 kwa magari yenye injini za kawaida
zinazotumia petroli, hadi asilimia 100 kwa magari ambayo injini zake
zimefanyiwa marekebisho.
Mfano Brazil inaongoza duniani kwa matumizi ya nishati ya
mimea ambapo hutengeneza kiasi cha hektolita milioni 120 kwa mwaka kutoka
kwenye miwa na mihogo.
Hiyo ni taswira kuwa zao hilo limeingia katika uwanja wa zao
la biashara na kuwa ni fursa ya aina yake katika sekta ya kilimo.
Hatua hiyo inamaanisha kuwa zao hilo linaingia katika
malighafi inayozalisha bidhaa za biashara jambo ambalo limo miongoni mwa nchi
zinazozalisha zao hilo.
Mfano wa bidhaa za zao hilo upo nchini Brazil ambako kuna
maduka yanayouza mikate ya mihogo na unga wa mihogo umekuwa ni mbadala wa unga
wa ngano katika kutengeneza mikate.
Mwaka 2002 Brazil ilipitisha sheria kuwa mikate
inayotengenezwa nchini humo iwe na asilimia 20 ya unga wa mihogo na asilimia 40
kwa maandazi au keki. Lengo la sheria hiyo ni kupunguza gharama za kuagiza
ngano kutoka nje na kuyawezesha mazao ya ndani kuwa na nguvu katika biashara.
Waokaji wa mikate nchini Nigeria hivi sasa wametakiwa kuoka
mikate yenye asilimia kumi ya unga wa mihogo.
Katika nyanja ya chakula cha mifugo, mihogo inatumika kama
mbadala kwa vyakula vinavyochanganywa na mifupa. Afrika hutumia mihogo chini ya
asilimia mbili kwa lishe ya wanyama ikilinganishwa na asilimia 30 inayotumika
Amerika ya Kusini.
Profesa Faustine Lekule wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine
(SUA) alishabainisha hilo la matumizi ya mihogo kama chakula cha mifugo katika
utafiti alioufanya kuhusu matumizi ya mihogo kama chakula cha mifugo.
Matumizi mengi ya viwandani hutumia mihogo kama malighafi
ili kupata wanga unaotumika kwenye viwanda vya vyakula, nguo, dawa na mipira.
Soko kubwa
Mtazamo wa soko la mihogo umekuwa mkubwa japo soko lenyewe
halijafikiwa na wakulima wa Afrika, kwani wengi huwa na wakati mgumu wa kuuza
mazao yao na wanahitaji kujitosheleza kwa chakula wakati bidhaa za viwandani
zinahitaji malighafi hiyo.
Teknolojia za usindikaji ni muhimu kwani gharama za
uzalishaji zikiwa nafuu wazalishaji na wasindikaji watapata mapato ya kutosha.
Katika soko la dunia wanga wa mihogo unapata ushindani kutoka wanga wa mahindi
ambao si ghali.
Kwa mfano, mwaka 2002 wanga wa mahindi ulioagizwa nchini
Nigeria kutoka Ulaya gharama ilikuwa chini mara tatu kuliko wanga wa mihogo
iliyolimwa nchini humo.
Maendeleo makubwa katika teknolojia na masoko ni muhimu kwa
mihogo kuingia katika masoko ya ndani na ya kimataifa.
Hutengeneza bia
Wakati viwanda vya kutengeneza bia vikihangaika na
upatikanaji wa shayiri zipo baadhi ya nchi ambazo hutumia mihogo kutengeneza
aina hiyo ya kinywaji.
Msumbiji inatengeneza bia inayotokana na mihogo, hivyo ni
moja ya malighafi inayotumiwa na viwanda vya bia.
Mwandishi wa makala haya alibahatika kufika Msumbiji miaka
ya hivi karibuni na kushuhudia bia inayotengenezwa kwa zao hilo.
Hata hivyo, alipobahatika kutembelea Kiwanda cha Bia
Tanzania (TBL) aliuliza iwapo kuna mpango wa kutumia mihogo kutengeneza
kinywaji hicho kama ilivyo nchini Msumbiji.
Jibu lililotolewa ni kwamba kilimo cha zao hilo hakiendeshwi
kibiashara na hivyo itakuwa ni vigumu kupata malighafi ya kutosha kutengeneza
kinywaji hicho.
Kwa mwanya huo wa kupata soko nchini China inamaanisha
kufungua mwanya pia kwa zao hilo kuzalishwa kibiashara na kufungua mwanya kwa
mahitaji ya malighafi kwa masoko ya ndani.
Inamaanisha pia mihogo si tu itatoa mchango katika uhakika
wa chakula bali kusukuma maendeleo kiuchumi na hivyo kuliibua tumaini hilo la
kiuchumi lililojificha.
Comments
Post a Comment