- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MWANDISHI WETU
Jumuia ya kimataifa hivi karibuni ilizitaka nchi jirani
kuunganisha nguvu ili kuokoa pamoja na kuwepo kwa usimamizi endelevu wa misitu
kwenye mfumo wa ikolojia wa Miombo/Mopane ndani ya Afrika kutokana na sababu
kuwa mfumo huo asilia ndio unaoonesha kufungamana kwa binadamu na misitu.
Kutokana na kutambua umuhimu na tishio linaloukabili mfumo
wa ikolojia wa Miombo Tanzania ilitoa angalizo kwa jumuia ya kimataifa kupitia Maendeleo ya
Ubia kwa kuunganisha juhudi zake kuokoa mfumo wa ikolojia kwa Tanzania,
Zambia na sehemu zote za Jumuia ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Makubaliano ya kuratibu uhifadhi na usimamizi wa mfumo wa
ikolojia wa Miombo/Mopane kati ya Serikali ya Zambia na Tanzania, ulisainiwa na
serikali kupitia Wizara ya maliasili na Utalii ambapo ilisema kuwa tishio
linaloukabili mfumo huo lisipodhibitiwa kutasababisha hasara kwa jamii kwa kuwa
ni mfumo unabeba sehemu kubwa ya maisha ya viumbe hai.
Ilielezwa kuwa katika kipindi cha miaka ya karibuni ujangili
wa maliasili na usafirishaji haramu
wa bidhaa za maliasili kutoka
Afrika umeongezeka kwa kasi na kwamba
hali hiyo inaleta tishio si tu kwa idadi
ya rasilimali hizo bali pia kwa mifumo ya uchumi, siasa na ikolojia.
Jambo lililo wazi ni kwamba uondoaji haramu wa
maliasili ndani au nje ya maeneo
yaliyohifadhiwa kama itaendelea bila kukomeshwa
kutasababisha madhara kwa sekta ya utalii si tu kwa Tanzania bali pia kwa mataifa mengine ya Afrika.
Ilibainishwa kuwa mitandao ya kuhamasisha na kuondoa
maliasili ndani na nje ya nchi
umeendeleza usafirishaji wa bidhaa za maliasili
na hivyo kufanya iwe vigumu kwa nchi moja peke yake kuingilia kati
kudhibiti. Hivyo kutokana na hali hiyo Tanzania ilitoa wito kwa nchi jirani na
jumuia ya kimataifa kuungwa mkono katika
kukabiliana na jukumu hili muhimu.
Iliarifiwa kuwa katika juhudi za kukabiliana na uhamishaji
haramu wa bidhaa za maliasili, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua kadhaa zikiwemo
kuongeza operesheni za kawaida na nyingine maalum pamoja na kampeni ya
kujenga uelewa katika ngazi za ndani na jumuia ya kimataifa.
Hivi karibuni serikali ilijikita kwenye uhifadhi wa wanyama pori na hususani
tembo ambapo ilikuwa mwenyeji wa mkutano uliobeba kauli mbiu ya “Acha uhalifu dhidi ya
wanyama pori Ongeza uhifadhi wa wanyama pori” uliofanyika jijini Dar es
Salaam.”
Ilibainishwa kuwa kwenye mkutano huo Serikali ya Tanzania na
Mfuko wa Kimataifa wa Kuhifadhi (ICCF)
kwa kushirikiana na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na wadau
wengine muhimu walianzisha miundombinu
sahihi na endelevu ya kupata fedha kwa
ajili ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa meno ya tembo.
Mfumo wa ikolojia wa msitu wa Tanzania na Zambia kwa kiwango
kikubwa kinajumuisha mfumo wa Miombo/Mopane ambao ni eneo muhimu
lililohifadhiwa kwa ajili ya rasilimali ya wanyama pori na misitu.
Kwa kuzingatia umuhimu huo ilibainika ni muhimu kujumuisha
aina hii ya msitu kwenye azimio la
mkutano wa kikanda wa kutokomeza uhalifu dhidi ya wanyama pori na kukuza
uhifadhi wa wanyama pori uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
Arusha (AICC) kuanzia Novemba 7 hadi 8, 2014 ukiwa na mtazamo wa kuanzisha
mtazamo shirikishi wa kudhibiti uondoaji
haramu wa bidhaa za maliasili.
Hatua ya kufikia maamuzi hayo serikali mbili za Zambia na
Tanzania zilikubaliana kuhakikisha kuwa
watu wake kuwa wanajikita kuhifadhina
kusimamia ipasavyo mfumo wa ikolojia wa
Miombo/Mopane.
Japo sera za taifa za misitu na wanyamapori pamoja na sheria
zinaunga mkono uhifadhi na usimamizi wa miombo aina hiyo ya misitu imeendelea
kupunguzwa kwa kukata miti hovyo. Hali
hiyo kwa upande mmoja inaweza kuwa ni kwa sababu taasisi zinazoshughulikia
mfumo huu wa ikolojia zinakuwa hazina uwezo wa kifedha na nguvu kazi.
Kutokana na Tanzania kutambua umuhimu wa kukuza usimamizi
endelevu wa mfumo ikolojia wa Miombo
iliamua kuchukua nafasi hiyo kudokeza mambo kadhaa yanayohusiana na
suala hilo.
Serikali ilisema, “Tumeshawishika na kuunga mkono usimamizi
endelevu wa mfumo wa ikolojia wa Miombo kwa kuwa unasaidia uwezeshaji wa maisha
ya idadi kubwa ya watu wake kwa
kuwapatia aina mbalimbali za bidhaa na huduma kama vile chakula, nishati ya kupikia
(kuni), makazi, malighafi za ujenzi wa nyumba zao na dawa zikiwa ni baadhi tu
miongoni mwa bidhaa na huduma nyingi.
“Kama nyongeza mfumo wa Miombo unajumuisha fursa za kipekee kwa jumuia za vijijini nchini Tanzania za kukuza
maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ulinzi wa mazingira kwenye ukanda wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na umekuwa ukizuia matokeo
hasi ya mabadiliko ya tabianchi. Ni
muhimu kwamba kupunguza mabadiliko ya tabianchi na kuridhia hatua ambazo
zitakuwa sehemu ya utekelezaji makubaliano yaliyosainiwa.”
Kwa kuzingatia masuala ya mabadiliko ya tabianchi na misitu,
imekuwepo haja ya kuweka kipaumbele
katika kudhibiti vichocheo vya ukataji miti na kuteketeza misitu pamoja na
uharibifu wa ardhi. Masuala mengine kama kilimo, nishati, ufugaji na matumizi mengine ya ardhi yanahitaji
kutupiwa macho pia.
Aidha serikali iliwataka wadau wote kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha kwamba utekelezaji wa
usimamizi endelevu wa misitu kupitia makubaliano juu ya mfumo wa ikolojia wa
Miombo kwa manufaa ya watu wake ambapo kimsingi kutaharakishwa na kuungwa mkono
kwa kutumia rasilimali za kutosha.
Serikali ya Zambia kwa upande wake ilisema kuwa changamoto
kwenye usimamizi dhidi ya uhalifu unaofanywa kwenye misitu ikiwemo ukataji wa
miti uchomaji haramu wa mkaa na kiwango kikubwa cha uvunaji haramu wa miti kwa
ajili ya mbao kwa spishu adimu haziwezi kufanikiwa bila kuwepo juhudi za pamoja
miongoni mwa nchi husika.
Ushirikiano kwenye shughuli mpakani utakuwa ni msingi wa
kupata ufumbuzi kwenye usimamizi na uhifadhi wa mfumo ikolojia kwa ajili ya
uendelevu wake ambapo Serikali ya Zambia iliamua kujikita kwenye makubaliano na
kuhakikisha unakuwepo uhifadhi na usimamizi wa mfumo wa ikolojia.
Serikali ya Ujerumani
kupitia ubalozi wake nchini Tanzania, ilipongeza juhudi za Tanzania na
Zambia kwa hatua ilizochukua kuhifadhi
mfumo huo ili kuisaidia jamii katika
mahitaji yake pamoja na maendeleo kupitia matumizi endelevu ya maliasili.
Hata hivyo ilibainishwa kuwa njia mbadala za kujipatia
kipato kama ufugaji nyuki, ufugaji wa samaki na uwindaji kwenye mapori
unahitaji kuungwa mkono.
Comments
Post a Comment