Featured Post

MBEGU BORA HULETA TIJA, KUWAKOMBOA WAKULIMA




NA ALOYCE NDELEIO
Kamati ya Taifa ya kupitisha aina mpya za mbegu za mazao hivi karibuni  iliidhinisha matumizi ya mbegu mpya 22 za mazao ya biashara na chakula na mbegu nne za mazao ya biashara ambayo ni kahawa za Arabika na Robusta zilipitishwa.
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ilisema kuwa mbegu nyingine zilizopitishwa ni pamoja na aina mbili za viazi vitamu, aina moja ya mbegu ya mahindi na aina nne za dengu.

Mbegu nyingine za mazao ya chakula ilielezwa kuwa ni aina moja ya soya, aina mbili za nyanya, mbili za figiri, mbili za mnavu aina moja ya ngogwe na aina mbili za mchicha.
Ilielezwa kwamba aina hizo za mbegu ni mpya kabisa na zimeshaidhinishwa na baada ya kufanyiwa utafiti na taasisi za umma na binafsi na za Uyole, Mbeya, Kibaha, Pwani, Hoti Tengeru na TaCRI mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wa taasisi binafsi ilifahamishwa kuwa utafiti huo umefanywa na kampuni binafsi ya Pioneer Hybrid Seeds ambapo kupitia tafiti za taasisi hizo mbegu hizo zimegundulika kuwa na sifa ya kutoa mavuno mengi, kustahimili ukame na ukinzani dhidi ya magonjwa.
Pamoja na hali hizo imebainika kuwa mbegu hizo hukomaa haraka na  na zinapendwa na walaji. Hatua hiyo inaonekana kuwa ni faraja kwa wakulima ambao kwa kiwango kikubwa wamekuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi za uzalishaji.
Mbegu nzuri ni muhimu kwenye uzalishaji wa kilimo na miongoni mwa nchi zinazoendelea kwani wakulima wanashindwa kuzipata mbegu hizo kutokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wake pamoja na bei.
Kimsingi mbegu ndiyo kianzio cha uzalishaji wa mazao na hata hivyo umuhimu wake umekuwa unaelezwa juu juu. Mbegu zisizo na ubora zinaathiri uzalishaji na hata kusababisha kuenea kwa maradhi.
Wakulima wanahitaji kuendana na hali pamoja na mahitaji ya uzalishaji na kumudu kuzikabili changamoto za mfumo wa kuhama kwa mifumo ya kilimo -jiolojia ambayo inasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Hata hivyo  miongoni mwa nchi nyingi zinazoendelea wakulima hujikuta wakiwa kwenye upande wa hasara ikiwa ni pamoja na kukosa kiasi cha kutosha cha mbegu bora kwa bei wanayoimudu. Kikwazo kingine kwa wakulima wadogo katika kupata mbegu nzuri unajumuisha mfumo duni wa uzalishaji, kuhifadhi na mgawanyo bila kusahau miundombinu duni ya kudhibiti ubora.
Mbegu bandia ni tatizo kubwa miongoni mwa nchi za Afrika kutokana na kuwepo wakala wanaosambaza mbegu duni zisizo na ubora kwa wakulima  na hili huwagharimu pindi mavuno yanapokuwa kidogo au kutovuna kabisa.
Lakini jambo jingine muhimu ni kukosekana kwa taarifa na sera za kutosha za zinazohusu mbegu kitaifa.

Tishio kwa baioanuai
Kwa mujibu wa Ofisa Kilimo wa Masuala ya Uhakika na Usalama wa Mbegu wa Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Tom Osborn, bei za juu ya vyakula na mabadiliko ya tabianchi kunafanya kuwepo kwa seti ya mkanganyiko katika mfumo mzima wa mbegu na hususani kwa wakulima wadogo.
Anasema, “Mifumo ya mbegu inahitaji kuimarishwa ili kuiwezesha iwe ya hamasa hivyo kwamba wakulima wanaweza kuifikia na kupata aina tofauti za mbegu ambazo zitakidhi mahitaji.”
Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) katika mkutano wa Oktoba 2009 uliokuwa ni mkutano mkubwa kuhusu mbegu ulisisitizia kuhusu  mchango muhimu wa sekta rasmi na zisizo zinazojishughulisha na mbegu  katika kukabiliana na changamoto zilizokuwa mbele yake.
Hivi sasa wakulima wengi wadogo bado wanatumia sekta isiyo rasmi kupata mbegu ambazo wamekuwa wakizihifadhi kwa kipindi kuanzia mwaka mmoja hadi mwaka mwingine na hata kubadilishana kienyeji.
Mfumo rasmi wa kibiashara ambao masoko huboresha mbegu zilizothibitishwa na mamlaka za usimamizi si kila mara zinakuwa zipo na wakulima maskini  na zinakabiliwa na ukosoaji mkubwa katika maeneo mengine.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Sera za Mbegu na Haki duniani imehodhiwa na kanuni kumi na inadaiwa aina za biashara zimekuwa zinahodhi soko.
Hata hivyo wanasayansi wa Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo na Mazingira wanaonya kuwa  kuongezeka kwa udhibiti wa mbegu kunakofanywa na kampuni kunatishia bioanuai, jambo ambalo limekuwa ni kubwa katika maeneo mbalimbali hususani kwenye visiwa vya Pasifiki ikiwa ni changamoto kubwa inayoyakabili maisha yao, utamaduni na mbinu zao za kienyeji za kilimo.
Hali hiyo imesababisha nchi nyingi zilizo kwenye eneo hilo  kuagiza aina zote za mbegu kutoka nje ukiondoa mbegu za mazao machache.
Wataalamu hao wanabainisha kuwa mbegu za kisasa ambazo zinajumuisha aina chache zimekuwa mbadala wa mbegu za asili na zimekuwa zinapigiwa debe na kampuni zinazohusika na hata kupewa ruzuku na serikali.
Hata hivyo, wanasema kuwa uoteshaji wa mbegu za aina hiyo hugharimu kwani zinahitaji mitaji mikubwa na zinashambuliwa kwa urahisi na magugu na magonjwa.

Suluhisho kuzalisha mbegu ndani ya nchi
Kuhusu suala la upatikanaji wa mbegu bora serikali ilisema imejenga uwezo wake wa ndani wa kuzalisha mbegu kwa kufufua mashamba ya mbegu yake ili yaweze kuzalisha mbegu bora kama yalivyokusudiwa.
Aidha, ilifahamishwa kuwa hatua za dhati zimechukuliwa za kuhusisha wadau wengine katika kuzalisha mbegu ikiwa ni pamoja na kutumia mashamba ya Jeshi la Kujenga Taifa na ya Idara ya Magereza. Hadi mwaka 2009  uzalishaji wa mbegu nchini ulikuwa umefikia tani 16,144.79 ikilinganishwa na mwaka 2005 ambapo ilikuwa ni tani 10,477.17.
Ili kuhakikisha kuwa uzalishaji wa mbegu bora nchini unafanikiwa serikali ililazimika kuimarisha Wakala wa Serikali wa Mbegu ili aweze kufanya kazi ya kuongoza, kuratibu na kusimamia shughuli za uzalishaji wa mbegu bora nchini.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wakulima miongoni mwa nchi zinazoendelea wamekuwa wanaanzisha njia mbadala kwa kuunda mfumo wa mbegu wa jumuia ambao unatoa aina bora zinazoendana na mahitaji ya ndani na kutoa fursa muhimu kwa wazalishaji kupata kipato.
Uzalishaji wa mbegu unaweza kuwa ni shughuli iliyo na faida na hivyo kuwepo kwa sekta ndogo ya ujasiriamali ambayo unatoa mtazamo mzuri kama  kuunganishwa na masoko kunakuwa kwa uhakika.

Ufahamu na udhibiti wa ubora
Mafunzo na elimu ni muhimu katika kuwasaidia wakulima kuingia kwenye teknolojia mpya na mbinu za kuzalisha mbegu.
Aidha, ni muhimu uwepo mfumo wa usimamizi wa uwazi ambao ni muhimu katika kuhakikisha kwamba wakulima wanamudu kuzifikia mbegu bora. Katika kanda nyingi barani Afrika biashara ya mbegu kwenye mipaka imekuwa inazuiwa na kuwepo kwa tofauti kati ya sheria na usimamizi kitaifa.
Hata hivyo, imekuwepo mikakati katika kulipatia suala hili ufumbuzi ikiwa ni pamoja na mkakati wa Programu ya Afrika ya Bioteknolojia na Mbegu  na mikakati kadhaa ya usimamizi iliyoanzishwa na Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuia ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Katika nchi kama Senegal na Tanzania kuondoa kuhodhi udhibiti wa ubora yamekuwepo mafanikio kwenye kupatikana kwa mbegu ya mpunga. Mfumo huo unaegemea kwenye kutangaza ubora wa mbegu mtazamo ambao umeanzishwa na FAO katika kuboresha uzalishaji wa mbegu ndani ya nchi na kuzidhibiti. Katika mfumo huo wakulima wamekuwa wakipewa mafunzo kuhusu uzalishaji wa mbegu na usimamizi wake.
Pamoja na hali hiyo kulinda haki miliki ni muhimu ili uwepo uzalishaji endelevu wa mbegu ikiwa ni pamoja na kuwa na wataalamu wa uzalishaji. Ni mara chache wakulima hunufaika wakati kampuni zinazozalisha mbegu hutumia mbegu zao za asili kuzalisha aina mpya za mbegu.
Miradi mizuri ni ile ambayo wakulima wanahusishwa kwa ukaribu na jambo hili limewahi kuifanyika Kusini Magharibi mwa China na kuwa na ufanisi mkubwa kutokana na kufanyika kwa utafiti shirikishi ukiwahusisha wakulima na wazalishaji wa mbegu.
Mazingira kama hayo huwezesha wazalishaji wa mbegu kupata faida kwa uwiano sawa kwa wakulima kutokana na michango ya pamoja ya mbegu na uelewa katika uzalishaji.
Kuidhinishwa kwa  mbege hizo nchini ni matarajio kuwa wakulima ambao walikuwa wanakatishwa tamaa na mavuno kidogo waliyokuwa wanayapata  watakuwa na fursa ya kuongeza kipato na hiyo kuondokana na umaskini na kwa upande mwingine wakiwa wanajihakikishia usalama na uhakika  wa chakula.

Comments