Featured Post

MAZUZU HUUPIGIA ZUMARI UBADHIRIFU



NA ALOYCE NDELEIO
MWANDISHI wa riwaya Nkem Nwankwo wa Nigeria alipoandika riwaya yake “My Mercedes is Bigger Than Yours” ambao kwa tafsiri  isiyo rasmi ni  “Benzi yangu ni kubwa kuliko ya kwako” ambayo leo hii tafsiri inaweza kuonekana katika mambo mengi kutokana na kukithiri kwa mambo ya ufisadi katika maeneo ya nchi nyingi za Afrika hususani katika kipindi cha miaka iliyofuata baada ya uhuru.

Kila mara kumekuwepo malalamiko ya mara kwa mara  kwamba “Nchi hii katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru bado imekuwa ombaomba. Baada ya miaka 50 ya uhuru tumekuwa wategemezi kwa misaada. Baada ya miaka 50 ya uhuru  bado kilimo ni cha jembe la mkono” ulinganisho huo umekuwa ni kibwagizo mara nyingi yanapozungumziwa masuala ya maendeleo.
Kwa kuwianisha na lugha picha aliyoitumia Nwanko zipo tafsiri nyingi  zinaoweza kuelezwa kutokana na kukithiri kwa wizi, ukwapuaji, uporaji, ujangili, ubadhirifu na ulaji rushwa ambako kunaweza kuelezwa kuwa kumekuwa kukifanya na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijiona kuwa ndio wanaostahili kuionja pepo peke yao.
Tambo zenyewe kama ni kuchukulia tafsiri ya moja kwa moja katika  Tanzania ya leo hii lazima itakuwa kutumia Benzi hakutakuwa na mvuto kwa kuwa Tanzania haikutumia sana aina hiyo ya gari na kama matumizi hayo yangekuwepo wangekuwepo wavuna jasho wanaofahamika kama Wabenzi.
Kwa maana hiyo  hapa tunaweza kusema Shangingi langu ni kubwa kuliko lako, lakini ukiweka mbali mashangingi hayo pamoja na ufahari wake, wanaweza wakatokeza  wengine wakasema, “Kasri langu ni kubwa kuliko lako’,  wanaweza kwenda mbali na kudai “Ukuta wa nyumba yangu mzuri kuliko wa kwako”.
Watakapohama hapo wanaweza kuhamia kwa ‘nyumba zao ndogo’ na kudai ni nzuri kuliko ya mwingine. Lakini haitashangaza kusikia “Shule anayosoma mwanangu ni nzuri kuliko anayosoma wa kwako. Au  “Shule anayosoma mwanangu ni gharama kubwa kuliko anayosoma wa kwako”.  Papo hapo usije ukasahau kuwa unaweza kusikia, “Simu yangu ni ya kisasa kuliko ya kwako.”
Kwa mvuja jasho ambaye  kibanda chake kimeezekwa kwa makuti na akiomba mvua isnyeshe anaposikia majigambo ya ina ahiyo mwili huchoka na maungo kulegea na papo hapo maumivu ya kichwa yakianza taratibu. Lakini basi ni pale mvua  itakaponyesha ndipo humlaumu  aliye juu kwamba anamtesa bila kuwaona wavuna jasho ambao waliamua kutafuna kwa meno yote keki ya taifa.
Hata hivyo, inapotokea kwamba zipo fedha zilizochotwa kutoka katika  mifuko ya umma na watu wanaosujudiwa kuwa ni wajanja kupitia zabuni  ambazo kwa uhakika zinaonesha kuwanyonga wavuja jasho  ndipo unapobaini kuwa tambo zinazoelezwa na walio wengi zimetokana na kuvuna jasho la mvuja jasho.
Hata hivyo, yanapotokea mambo ya kusikitisha umekuwepo utamaduni potofu wa kusujudia upuuzi unaofanyika mbele ya walala hoi  lakini  viongozi walio na nia nje ya wamekuwa wanakwazwa kwa kukosa nguvu ya umma kutoka chini katika jamii inayowazunguka na mara nyingine kutoka juu katika ngazi ya taifa.
Hali hiyo inamaanisha kuwa kunaweza kuwepo kulindana ndio maana wavuja jasho katika jamii wanakosa nafasi kwa vile muda mwingi wanautumia kuhangaikia maisha yao na wana wao na mara nyingi huweza  kujawa na hofu kutokana na nguvu za kifedha wanazokuwa nazo wavuna jasho kwamba wanaweza kukumbana na misuguano ya ana kwa ana.
Dhana iliyopo hapo ni kwamba jamii imepitia katika kipindi cha kulima na kupalilia uoza, kupigia zumari na vigelegele unyang’anyi, kusujudia ubadhirifu na kuwapuuza wavuja jasho waliopo katika msongamano huku wavuna jasho wakipitia katika barabara ya mwendo kasi. 
Hali hiyo inamaanisha tambo  zinazotolewa na kupigiwa zumari na vigelegele zimekuwa zinatokana na mbinu za kihafidhina za kujikusanyia mali binafsi kupitia rushwa na mbaya zaidi katika mitindo ya ki-Machiavelian.
Lakini kwa mazuzu inasadifu kupigia zeze, zumari, vifijo na vigelegele tambo  hizo kwa ajili ya kuwapamba wabadhirifu  ilhali wanyonge  wakiumia.
Hali inakuwa hivyo kutokana na viongozi walio wengi kukumbatia  dhana nzima ya utandawazi kijuu juu  kumbatio ambalo limesababisha  ujenzi wa matabaka  na hivyo kuwepo kwa tabaka la walionacho na la wasionacho na hata hivyo kwa wale walio nacho kuendelea kuneemeka na wasio nacho wakitopea kwenye kudhoofu.
Tangu miaka ya mwanzoni ya kujitawala, wamekuwepo watendaji  waliolitia hasara kwa kuingia mikataba na kampuni au serikali za nje bila umakini au kwa kuhongwa. Matokeo ya mikataba hiyo ni umaskini kuendelea kushamiri kwa wengi huku wachache wakiishi kwa raha. Hawa ndio walio ambao wamekuwa wakitamba Benzi langu ni kubwa kuliko la kwako.
 Kuwepo au kugundulika kwa baadhi ya rasilimali au maliasili muhimu kumekuwa kunasababisha matumizi yake kuwa mabaya.
Aidha, wingi huo umekuwa unasababisha baadhi ya wazawa kutofaidika na mirahaba inayotokana nazo. Kisa kinabakia ni kujineemesha kwa wachache kwa kutumia mikataba mibovu.
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya mazingira wamekuwa wanaliona hilo na lililo wazi ni kwamba baada ya wawekezaji kufaidika kutokana na maliasili kama madini, wazawa wamekuwa wanabakia na mashimo matupu kama sio mahandaki pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira.
Katika jitihada za kutokomeza umaskini hatua zinazochukuliwa zinaridhisha na kwamba zinaweza kuhesabika kuwa ndio zitakazochangia  kuziba pengo la umaskini kutokana na miundombinu kuwezesha watu kuzifikia baadhi ya huduma muhimu.
Hata hivyo kumudu kuzifikia huduma hizo kutakuwa na maana kama watakuwa na kipato cha kuwawezesha kuzipata kwa kuwa umaskini wa kipato bado ni tatizo linalohitaji kufumbuliwa.
Hilo linawezekana kwa kuwa na nguvu ya kuyafikia masoko ya uhakika  yatakayowawezesha kuuza malighafi wanazozalisha kwa kuzingatia kwamba asilimia kubwa ya jamii inayokumbwa na kadhia ya umaskini ni inayoishi vijijini na ni wakulima wa mazao mbalimbali.
Haiyumkini dhana ya uchumi wa viwanda inaweza kuwa suluhisho la hilo na kwamba  inaweza kutumika kama nyenzo ya kupunguza umaskini wa kipato kwani itakuwa sio tu soko la malighafi bali soko la ajira pia.
Sasa basi wakati mikakati ya kupambana ili kunyanyua maisha ya wachovu ikiwa inahimizwa sio ajabu  ikakutana na vikwazo ambavyo vitatoka kwa mazuzu ambao watakuwa wakipigia zeze mambo ya kukwamisha mikakati hiyo.

Comments