Featured Post

MAZOEZI NI LISHE YA UBONGO HUUONGEZEA KUMBUKUMBU



NA ALOYCE NDELEIO
WATAALAM mbalimbali wa masuala ya afya mara kwa mara wanashauri watu wawe wanafanya mazoezi ikiwa ni njia ya kuweka afya zao sawa, pia hushauri kuwa mazoezi ni tiba kwa baadhi ya dosari zinazotokeza mwilini.
Hata  hivyo fikra nyingine ni kuwa mazoezi husaidia kunyoosha viungo na kutoa jasho pamoja na kupunguza uzito lakini wataalamu wanabainisha kuwa mazoezi ni lishe kwa ubongo kwani huuongezea kumbukumbu.
Mara nyingi baadhi ya watu hufikiria jinsi ubongo wa mwanadamu utakavyokuwa pindi atakapofikia uzeeni katika dhana kuwa atasahau baadhi ya mambo na hususani yale ambayo yatakuwa hakuyaandika kwenye vitabu vya kumbukumbu za kila siku ili aweze kuyarejea.

Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa uwezo wa ubongo wa binadamu unapungua kadri mtu mwenyewe anavyozeeka na hivyo kupoteza kumbukumbu au kuwa msahaulifu.
Hali hiyo inasababisha ashindwe kufanya maamuzi sahihi na mara nyingi hufikia hatua ya kushindwa kuzungumza na baadhi huzungumza kwa kurudia rudia baadhi ya maneno.
Hali ya aina hiyo imekuwa inawaogopesha baadhi ya watu na hivyo kuwafanya  wawe wanakuwa makini kwa kuchukua tahadhari za mara kwa mara.
Hilo linawezekana kwa kuandika kumbukumbu zao kwenye vitabu vya kumbukumbu, jambo ambalo ni zuri, na linaweza kuwanufaisha watu walio karibu nao iwapo kwa bahati mbaya watakuwa hawawezi kuzungumza au kutambua baadhi ya mambo.
Mara nyingine hutumika kama ushahidi wa kuondoa utata unaoweza kutokeza miongoni mwa ndugu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni iliyochapishwa kwenye gazeti la Washington Post nchini Marekani inadokezwa kuwa zipo njia ambazo mtu anaweza kutumia ili aweze kulinda uwezo wa ubongo wake, hali kadhalika kuulinda dhidi ya magonjwa.
Gazeti hilo linaarifu kuwa njia pekee itakayowezesha hali hiyo kuwepo ni kutoa changamoto kwa ubongo kwa kufanya mazoezi mara kwa mara.
Kwa mujibu wa utafiti mkubwa ulioendeshwa kwa mwezi mmoja kupitia takwimu za kisayansi zilizochapishwa kwenye mtandao zilibainisha kuwa kufanya mazoezi kwa wingi kunapunguza hatari ya kukabiliwa na magonjwa ya moyo, pia ni miongoni mwa njia maridhawa za kuuweka ubongo katika hali nzuri ya kiafya.
Aidha, kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Marekani inabainishwa kuwa shughuli nyingi zinazotumia ubongo katika maisha ya mtu huufanya ubongo ushindwe kuhifadhi uwezo wake wa kumbukumbu.
Kutokana na utafiti huo mwandishi wa Uingereza, Margaret McCartney ambaye anauunga mkono anadokeza hali ya aina hiyo kufuatana na utafiti uliofanywa na Profesa Ian Robertson wa Idara ya Saikolojia katika Chuo cha Trinity mjini Dublin.
Akihadhiri katika tamasha la sayansi la Chama cha Maendeleo ya Sayansi nchini Uingereza, Profesa Robertson alisema kuwa hali hiyo sio tu kwamba mazoezi yanaboresha umri wa ubongo lakini mlo anaotumia mtu, mazoezi,  chemsha bongo na majaribio ya kuushughulisha ni miongoni mwa vigezo vinavyochangia.
Hali hiyo inawezesha kutambua kuwa ubongo unaweza ukawa na afya nzuri na hivyo kumwezesha mtu kufurahia maisha katika ngwe inayoanzia miaka 50 hadi 80.
McCathney anasema kuwa watafiti wapo kwenye harakati za utafiti unaohusu tiba ya kuzeeka, lakini habari nzuri ni kuwa kama mtu amebahatika kupata elimu, na anafanya kazi zinazomfanya awajibike kwa kutumia ubongo zaidi katika kufikiria masuala ya kazi, basi anakuwa kwenye nafasi nzuri ya kurefusha uwezo wa ubongo wake katika kuhifadhi kumbukumbu.
Anasema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa Profesa Robertson upo uthibitisho wa kuwepo uhusiano kati ya kiwango cha elimu na kushuka kwa uwezo wa ubongo katika kuhifadhi kumbukumbu.
Kiwango cha elimu kina uhusiano na kuongezeka kwa muunganiko wa mawasiliano katika seli za ubongo.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, Chama cha Wataalamu wa Masuala ya Ubongo cha Marekani kinadai kuwa watu ambao mara kwa mara huwa wanafanya shughuli zinazohusisha kufikiri kama vile kusoma magazeti kila siku, au kutembelea sehemu za makumbusho, pamoja na sehemu nyingine ambazo ni tofauti na mazingira yake ambayo yanakuwa yamemjengea mtu taswira mgando kwenye ubongo huchangamka kimawazo.
Kutokana na hali hiyo ni kwamba kubadilisha mazingira au kusoma mambo au matukio mapya katika magazeti huingiza jambo jipya katika ubongo na hivyo kulazimika kufikiri au kutambua hali ambayo humfanya mtu awe na afya njema.
Gazeti hilo linaripoti kuwa hali hiyo imekuwepo baada ya utafiti  wa Profesa Robertson kuendeshwa au kufanyika miongoni mwa watu 1700 kwa kipindi cha miaka sita.
Hali kadhalika watafiti walibaini kuwa watu wanaofanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki ni mara chache sana wanaweza kukumbwa na tatizo la kiharusi.
Katika nadharia moja ambayo ililenga utafiti wa wanyama uliweza kuleta matokeo yaliyobainisha kuwa mazoezi ya mwili yanaboresha mtiririko wa damu mwilini na kiwango cha hewa ya oksijeni kinachopokelewa kwenye ubongo.
Hali kadhalika mazoezi hayo yanaweza kuuongezea ubongo uwezo mwingine wa ziada ambao ni kuboresha kukua kwa tishu na chembe chembe za damu katika sehemu ya ubongo inayohusika na kuhifadhi kumbukumbu.
Kuhusu changamoto ambayo inatolewa kwa ubongo kwa mtu ambaye anafanya mazoezi, kwa mujibu wa majaribio yaliyofanywa nchini Marekani katika Chuo Kikuu cha John Hopkins cha Baltmore unaonesha kuwa hali hiyo inaweza kuboresha maisha ya watu walio na umri mkubwa na hususani wastaafu.
Watafiti hao ambao walilifanyia majaribio kundi moja la  wazee ambao mara nyingi huwa wanaonekana kama watu waliotengwa kijamii hususani kwa utamaduni wa nchi za magharibi ambako familia hazina mshikamano kama zilivyo familia za nchi maskini hasa Afrika.
Waliwafanyia mazoezi katika suala zima la kusoma ili kuushughulisha ubongo ambapo baadaye walizinduka na kuwa wasaidizi wa kujitolea kwa kufanya shughuli mbalimbali za kujitolea katika mashule.
Aidha, watafiti walipofuatilia ili kuangalia maendeleo yao baada ya kipindi cha miezi sita walibaini kuwa si tu kwamba uwezo wao wa kufikiri ulikuwa umeongezeka bali pia walikuwa wanaweza kutembea kwa haraka, na walikuwa tayari wameshapanua mawasiliano na jamii iliyokuwa inawazunguka.
Kutokana na hali hiyo inakuwa ni vigumu kupingana na wataalamu ambao kwa kiasi kikubwa wameweza kubaini kuwa sayansi si suluhisho la mwisho bali ni sehemu ya chachu ya kupanua uwanja wa kuelewa.
Hivyo ni muhimu na ni wazo mwafaka kufanya mazoezi ambayo kwa upande mmoja yanaboresha afya ya mwili na kwa upande mwingine yanakuwa ni lishe ya ubongo, hivyo kuboresha au kuufanya uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu kuwa mkubwa.
Katika mazingira ya jamii kama Tanzania wapo wanaoamini au wanaochukulia kuwa wanaofanya mazoezi ama ya mbio nyepesi au yoyote yale ambayo hayako kwenye orodha ya mashindano kuwa wanapoteza muda.
Hali kadhalika imejengeka dhana kuwa kutembelea maeneo mbalimbali tofauti na mazingira waliyozoea kama vile kutalii hilo linaonekana kuwa ni kwa ajili ya watalii kutoka nje.
Dhana potovu hiyo kwa kuwa yanayoonekana kwa kufanya utalii huo wa ndani huondoa mgando wa uelewa na kupata taswira mpya ndani ya ubongo.
Hata hivyo, ukweli unabakia kuwa kufanya hivyo ni kuutafutia ubongo lishe ambayo itauwezesha kukuza uwezo wake wa kumbukumbu.
Hali hiyo pia hupunguza kwa kiwango kikubwa utegemezi na upweke ambao unaweza kumkumba mtu anapofikia kwenye umri mkubwa na ndio maana inashauriwa na kuwepo kauli mbiu mara kwa mara ya ‘Fanya Mazoezi kwa Afya’.
CHANZO: TANZANIA

Comments