Featured Post

MASOKO YA KISASA YANAWAPA KISOGO WAKULIMA WA NDANI



NA ALOYCE NDELEIO
MARA nyingi siku za mwisho wa wiki huwa ni fursa ya wanajamii walio wengi katika maeneo ya mijini kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali watakazotumia kwa ajili ya wiki inayofuata.
Baadhi hununua bidhaa hizo kwenye masoko ya kisasa maarufu kama “Super markets” lakini waliowengi  hununua bidhaa hizo ambazo nyingi huwa ni vyakula kwenye masoko ya kawaida.

Kwa jiji kama  Dar es Salaam  wamezoea kufanya ununuzi huo kwenye  soko maarufu la Kariakoo na mengine kama Tandika na vivyo hivyo katika majiji na miji mingine.
Hata hivyo wengine bado wanategemea ununuzi wa bidhaa hizo kwenye magenge  kwa kuwa  vipato vyao haviruhusu kununua bidhaa nyingi kwa ajili ya wiki inayofuata na badala yake wamekuwa tegemezi kwa magenge hayo, mara nyingine huitwa ‘duka wala’.
Kwa waliobahatika kutembelea masoko haya ya kisasa katika siku hizo za mwishoni mwa wiki na hata kama bado, unaweza kutembelea kujionea jinsi wateja wanavyofanya  ununuzi wao ndani yake wakishehenesha bidhaa mbalimbali  kwenye vitoroli maalumu vinavyotumika  ndani ya masoko hayo.
Hata hivyo baadhi ya bidhaa hizo zinaweza kupatikana katika masoko ya kawaida kama vile Kariakoo, Tandika na mengine mengi tu kama si kwenye maduka ya kawaida.
Taswira ya haraka  ambayo mtu anaweza kuipata katika ununuzi wa aina hiyo ni kwamba huwa ni wa haraka zaidi kuliko ambavyo unaweza kufanyika  kwenye masoko ya kawaida. Hata hivyo hiyo si hoja, hoja ni aina ya bidhaa zinazopatikana ndani ya masoko hayo ya kisasa.
Aidha ni ukweli usiopingika kuwa wanaofanya ununuzi kwenye ‘super markets’ hizo ni wanajamii walio na ajira nzuri.
Kwa kuangalia namna wanavyoshehenesha bidhaa mbalimbali  kwenye  vitoroli  ndani ya masoko hayo  kuanzia vyakula hadi vinywaji  kwa mtu asiye na mazoea au uwezo wa kufanya ununuzi wa aina hiyo ataingiwa na hofu ya gharama atakayolipa  sehemu ya kutokea na ambapo hukaguliwa na kulipia kwa  kuwa pato lake ni dogo.
Hali  hiyo inazifanya familia zilizo na pato la chini kufanya  ununuzi wa bidhaa nyingi hugeukia maduka yanayokuwa kwenye sehemu wanazoishi (duka-wala) au magenge ili waweze kupata mahitaji hayo na mara nyingi huweza hata kukopa hususani kwa bidhaa kama unga wa ngano, mchele,  au maharagwe ambayo hutumiwa kwa ajili ya biashara ya vitafunwa  au mama lishe.
“Supermarkets” hizi zimepenyeza kwa wingi miongoni mwa nchi zinazoendelea  hususani katika nyanja ya soko la vyakula hali ambayo imeleta mabadiliko kwenye soko la mazao ya vyakula  na hata tabia ya mamilioni ya walaji wa vyakula hivyo hususani kwa jamii zinazoishi mijini.
Hata hivyo mabadiliko ya haraka ya  mfumo wa soko la reja reja kwa vyakula kumekuwa kunatoa changamoto kubwa kwa wazalishaji wa mazao hayo.
Wakulima wadogo wa kawaida wamekuwa hawana uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya uzalishaji wa vyakula, usindikaji na hata kuyafikisha kwa walengwa  hali ambayo inaweza kusababisha watupwe nje ya uchumi wa aina hiyo kama hawatamudu kukabiliana na mabadiliko hayo.
Mtiririko huo unamaanisha kuwa wakulima wadogo ndani ya nchi watakuwa wanaelea kwenye bahari ambayo ama watamudu kuogelea na kupiga mbizi au kuzama ndani yake.
Jambo kama hilo linamfanya  Mchumi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Kostas Stamoulis atahadharishe, “Wakulima wadogo wapo kwenye hatari ya kuwekwa pembezoni kama hawatapewa msaada wa kiteknolojia, mitaji ya kuanzia  na mambo mengine ambayo yanahitajika katika kuingia kwenye soko la vyakula.
“Wanahitaji  msaada katika jambo hili ili waweze kusindika na hata kuhifadhi vyakula, wanahitaji mbegu nzuri na bora, hali kadhalika wanahitaji uelewa wa kemikali salama za kuhifadhia ili waweze kupata soko na hata kutambuliwa”.
Super markets hizo nchini Tanzania   zimepanuka haraka  baada ya kufunguliwa kwa milango ya uwekezaji ambapo wawekezaji kutoka Afrika Kusini ndio wamekuwa wanahodhi  sekta  hiyo wakiwa na milolongo ya masoko Shoprite and Scores.
Maduka hayo pia yameuzwa kwa makampuni mengine kama Nakumat na mengine yameibukia sehemu mbalimbali katikati ya miji mbalimbali.
Ukiwemo mfumo thabiti na ulio kwenye usimamizi mzuri faida inaweza kupatikana kwa bidhaa zenye viwango na ubora na hivyo masoko hayo kuchochea mikakati ya wazalishaji ambao wanayauzia mazao mbalimbali.
Hata  hivyo wazalishaji ni lazima wawe na uwezo wa kuzalisha bidhaa ambazo zitadumu kwa muda mrefu au zitakazokuwa zinapatikana kwa msimu mrefu au kwa muda wote wa siku 365 za mwaka zikiwa na viwango visivyobadilika katika dhana ya ladha, muonekano, uhakika na hata  usalama.
Mchumi huyo anasema, “Ukiziangalia nyanya na matunda mengine  ni lazima yawe na sura inayovutia, lakini pia suala la ladha linapewa kipaumbele… hali kadhalika ni lazima yawe na kiwango kidogo sana cha viuatilifu, yafikishwe sokoni kwa wakati mwafaka, na uzalishaji wake uwe endelevu na usioyumba … rafu (mashelfu) za masoko zisiwe tupu … ziwe zimejaa muda wote.”

Ufanisi na utekelezaji
Kama ilivyo kwenye sheria zinazotawala shughuli mbalimbali na hususani bidhaa ambazo ni vyakula  ili uwepo ufanisi katika utekelezaji,  bidhaa zinazoingia katika soko ni muhimu kuingia kwenye mkondo wa kusindikwa, kuhifadhiwa na kusafirishwa hivyo hatua hizo zinahitaji uwekezaji na utendaji mpya kwa wazalishaji wadogo.
Asilimia 90 ya mazao yanaingia kwenye super market yanatakiwa yawe yameoshwa, yamesindikwa, kuthibitishwa kwa kupewa nembo na  hata kuhakikiwa sehemu yanakotoka.
Ili uwepo uwezekano wa kuwa na bidhaa zinazofaa ni dhahiri kwamba wazalishaji ni lazima wasafirishe bidhaa zao kutoka sehemu  zinakozalishwa ambako ni  mbali na soko ndani ya magari yenye majokofu.
Matakwa ya kimataifa yanaweza kuwa kikwazo katika  uhakiki wa bidhaa  yanajikita  kuanzia viwango vya kuotesha  ambavyo ni  vigumu kuliko vikwazo  vinavyokuwa vimewekwa kwenye ngazi ya kitaifa.
Athari za super market nchini Tanzania zimekuwa wazi hali ambayo imewahi kupingwa na  wakulima wa matunda nchini wakipinga  uingizaji wa matunda kutoka Afrika Kusini matunda ambayo yanalimwa hapa nchini.
Lakini kwa wanajamii ambao wanaweza kufikia viwango hivyo vya mahitaji  faida yake huwa ya kuvutia kutokana na ujio wa masoko hayo kuwa unatoa soko la uhakika na imara, ambalo kwa wakulima wanaoweza kuuza bidhaa zao humo huwa linalipa.
Faida nyingine ambayo ni pamoja na kuboreshwa kwa ubora na usalama wa chakula  kinachouzwa ndani kwani wakulima watajitahidi kuvifikia viwango vya hali ya juu vinavyotakiwa kwa bidhaa za masoko hayo.
Matokeo ya hali kama hiyo yanawezesha kuwa na aina nzuri na bora za vyakula ndani ya nchi sanjari na kuwafanya wazalishaji kuingia kwenye ushindani wa kutafuta soko la nje.

Vyanzo vya ndani
Stamoulis anaarifu, “Lipo tishio, lakini pia ni fursa”. Kuitumia fursa hiyo kunaweza kuchukua muda na hata hivyo mipango ya FAO ipo njiani kuanzisha mawasiliano yatakayounganisha wazalishaji, Asasi Zisizo za Serikali, na super markets zenyewe.
Katika kuhakikisha kuwa masoko haya yanalinda hadhi yaliyojijengea miongoni mwa jamii na hata kujenga jina lake kibiashara hufanya jitihada za kuhakikisha kuwa vyanzo vya bidhaa zake ni ndani ya eneo husika.
Nchini Namibia kwa mfano misaada ya kiufundi hutolewa kwa wakulima wadogo ambayo ni kama mbegu, uelewa na hata uthibitishaji.
Hata hivyo nchini Tanzania kutokana na kelele zilizopigwa na wakulima kupinga uingizwaji wa mazao au bidhaa nyingine kutoka nje kwenye masoko hayo Shoprite kwenye soko lake la Arusha ilikubali kuwa asilimia 90 ya bidhaa zake ziwe zinatoka kwenye vyanzo vya ndani.
Wazalishaji wa nchi zinazoendelea wameingizwa kwenye hatari ya kuendeshwa na mkondo ambao bidhaa inamwendesha mnunuzi hivyo kwamba kama wakiteleza soko nalo linateleza lakini pamoja na hali hiyo uzalishaji wao mdogo hauwezi kuwafanya watengwe.
Hii inamaanisha kuwa vyakula vingi hupotea kutokana na uhifadhi duni baada ya mavuno, ukosefu wa vifaa vya kuhifadhia na kukosekana kwa teknolojia sahihi ya usindikaji vijijini.
Jambo hili ni dhahiri hususani kwa mazao ambayo huharibika haraka kama matunda na mboga mboga ambayo kiasi kikubwa huharibika hata kabla ya kuvuna au kufikishwa sokoni.
Lakini katika kukabiliana na hali hiyo mafunzo ya mbinu za usindikaji yanaweza kusaidia wakulima walio maeneo ya vijijini ili waweze kujiongezea kipato na kuboresha hali ya lishe miongoni mwa familia zao.
Hoja hapa inaibuka ni wangapi wanakuwa radhi kununua bidhaa inayozalishwa hapa nchini wakati bidhaa ya aina hiyo   kutoka nje ipo kwenye maeneo hayo?
Kasumba ya kuthamini mazao yanayotoka nje kuliko yanayozalishwa hapa nchini imekomaa lakini mtazamo huo umekuwa ni kinyume kwa wageni kutoka nje ya nchi ambao huzivamia bidhaa zinazozalishwa au kutengenezwa nchini kuanzia vyakula hadi bidhaa nyingine kama nguo.
Ukiwepo uzalendo wa kununua bidhaa zinazozalishwa nchini ni msukumo tosha unaowezesha kukuza uchumi na hata kupunguza umasikini lakini inapotokea kuwa hata wale wa nyumbani hawathamini hali hiyo basi ni dhahiri kuwa lipo pengo kubwa kati ya walio nacho na wasio nacho na dhana hiyo inaweza kuwa kikwazo katika mkakati mzima wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Lakini pamoja na hali hiyo chanzo cha mazao mengi ni vijijini, na iwapo teknolojia, nishati, miundombinu ya usafirishaji na masoko yakisogezwa  karibu vikiwepo basi wakulima watakuwa wanasogezwa kwenye duara la ndani la uchumi na kuepushwa na dhana ya kutopea kwenye duru la pembezoni.
CHANZO: TANZANITE 

Comments