Featured Post

MAMA WA KAMBO 'AAMRISHA' MWANAYE WA MIAKA 9 KUBAKWA MBELE YAKE



KASHMIR, INDIA
MAOFISA wa Polisi wamewakamata watu sita kuhusiana na ubakaji wa kikundi na mauaji ya msichana wa miaka tisa nchini India katika jimbo la Kashmir.

Maofisa wanasema kuwa mama wa kambo wa msichana huyo alimwambia mwanaye wa kiume mwenye umri wa miaka 14 na wengine watatu kumbaka msichana huyo mbele yake.
Wanasema kuwa mwili wa msichana huyo ulipatikana siku ya Jumapili katika msitu wilayani Baramulla.
Aliteswa na mwili wake kuchomwa na tindi kali, waliongezea.
Mama huyo wa kambo anadaiwa kukasirishwa kwa kuwa msichana huyo alikua akipendwa sana na mumewe.
Maafisa wa polisi waliambia BBC Urdu kwamba msichana huyo alitoweka kwa siku kumi kabla ya mwili wake kupatikana.
Ilibainika kwamba mama huyo wa kambo alikuwa na chuki dhidi ya mke wa pili wa mumewe na watoto wake, mtandao wa kituo cha habari cha NDTV kilimnukuu afisa mmoja wa polisi Miir Imtiyaz Hussain akisema.
Bwana Hussein alisema kuwa msichana huyo aliuawa kwa shoka baada ya kubakwa na genge.

Mashambulio dhidi ya wanawake yameongezeka
Alisema kuwa mmoja ya washukiwa mwenye umri wa miaka 19 alimpiga na kumjeruhi vibaya mwilini.
Hii ni mara ya pili ubakaji mbaya wa aina hiyo umefanyika katika jimbo la Kashmir katika miezi ya hivi karibuni.
Mnamo mwezi Aprili, 2018 msichana Muislamu wa miaka minane kutoka Wilaya ya Kathua alibakwa na genge na kuuawa.
Hatua hiyo ilizua hisia kali baada ya mawaziri wawili kutoka chama cha Hindu Bharatiya BJP kuhudhuria mkutano kuwaunga mkono washukiwa ambao ni Wahindu.
Tatizo la unyanyasji wa kingono nchini India limeongezeka tangu ubakaji wa genge mwaka 2012 na mauaji ya mwanafunzi wa miaka 23 katika basi katika mji mkuu wa Delhi.
Uhalifu huo ulisababisha maandamano ya siku kadhaa na kuilazimu serikali kubuni sheria kali dhidi ya ubakaji ikiwemo hukumu ya kifo.
Hatahivyo mashambulio dhidi ya wanawake na watoto yanaendelea kuripotiwa nchini humo.
BBC

Comments