Featured Post

MAARIFA ASILIA HAZINA YA ELIMU ILIYOJIFICHA



NA ALOYCE NDELEIO
Maeneo yanayohesabika kuwa yapo nyuma katika nyanja ya maendeleo ni  vijijini ambako licha ya kukosa nyenzo za kisasa za kuharakisha maendeleo  bado maeneo hayo yanabakia kuwa na hazina ambayo ama inadharauliwa au kuwekwa pembezoni ambayo ni maarifa asilia.
Bila kutumia maarifa ya jumuia za vijijini nchi nyingi zinazoendelea hazitaweza kupiga hatua kwani maeneo hayo ndiyo yaliyo na idadi kubwa ya watu.
Kutokana na hali hiyo hazina kubwa ya maarifa asilia waliyo nayo inaweza kutumika kujiletea maendeleo kama kutakuwepo na kipaumbele kitakachotolewa katika dhima nzima ya kuifanya jamii iondokane na  umaskini na kukuza uchumi wake.

Nchi nyingi zinazohesabika kuwa ni maskini zina hazina za ziada ambazo ni  watu wake wenyewe wanazielewa jinsi gani zilivyo.
Inapoelezwa hazina mara nyingine inaweza kuhesabika kuwa ni hazina ya mafuta (petroli) au hazina ya rasilimali ya madini.
Lakini hazina iliyojificha miongoni mwa jamii za vijijini sio hiyo bali ni maarifa asilia na iwapo ni kuelezea ni wapi imefichika ni dhahiri maktaba ya hazina hiyo itakuwa ni wakulima.
Ukichukuliwa mfano wa jumuia za vijijini ambazo zinaotesha matunda ya asili na kulima bustani za mboga za majani katika makazi yao ni wazi kwamba mbali na kuwa hali hiyo ina umuhimu wake kiekolojia.
Utamaduni wa aina hiyo unachangia pia katika suala zima la uhakika wa chakula kwa kuufanya uhakika huo kuwa karibu na kupatikana kwa urahisi.
Katika mazingira ya aina hiyo ni wazi kuwa kinachojengeka ni dhana ya  “kulisha kaya” jambo ambalo limekuwa likifanyika kwa miaka mingi.
Hali hiyo inawezesha kuondokana na dhana kuwa mazingira ya nyumba yanatakiwa kuwa maua tu kwa ajili ya kujifurahisha lakini pia yanaweza kuwa ni chanzo kizuri cha mboga za majani na mazao machache ya msingi ya  chakula.

Elimu ya mazingira huanzia nyumbani
Chukulia mazingira ya nyumba yako kwa mfano kwamba umeotesha miche 100 mchanganyiko ya mimea inayotoa mboga mboga za majani au matunda kama ndizi, parachichi, nanasi n.k, pamoja na mimea ambayo ni dawa na ambayo sio rahisi kuipata sokoni.
Hatua kama hiyo moja kwa moja itakuwa ni kivutio kwa watu watakaotembelea nyumbani kwako. Kutokana na hali hiyo ni kwamba elimu kuhusu mazingira na mapambano kuhusu uhakika wa chakula ni muhimu yakaanzia nyumbani.
Mfano wa maarifa asilia kwenye uhifadhi wa chakula ni pamoja na kukausha kwa kutumia moshi bidhaa kama nyama na ambayo inaweza kutumiwa wakati kuna uhaba wa  nyama.
Hali kadhalika ni jamii hizi za vijijini zinazoelewa aina mbalimbali za mboga za majini ambazo ni tofauti na spishu za kigeni na ambazo zina virutubisho vingi vikilinganishwa na mboga kama kabeji, spinachi n.k.
Jamii hizi za vijijini ndizo zimekuwa zinafahamu aina ya  maua ambayo nyuki hupendelea na yapo sehemu gani ndani ya msitu hali inayofanya ufugaji wa kisasa wa nyuki kuwa rahisi kwani ni kuboresha mbinu wanazotumia wakazi wengi walio na maarifa asilia vijijini.
Jamii za vijijini zinafahamu pia kujenga vihenge ambavyo vimekuwa vinatumika kuhifadhi mazao au chakula cha akiba, vikiwa ni maghala kongwe kihistoria.
Wajasiriamali wadogo wamekuwa wanatumia  teknolojia asilia kuboresha  mbinu zao za kusindika na kuhifadhi mazao mbali mbali ambayo yanaweza kutumiwa baadaye wakati kuna uhaba wa chakula.
Kwa mfano ni jambo rahisi kwa wakazi wa vijijini kupata siagi au mafuta kutoka kwenye  maziwa kwa  kutumia njia za asili na hivyo kuwa  hawatumii mafuta ya kupikia kutoka  viwandani.
Jamii pia zinaweza kuhifadhi  aina hiyo ya mafuta kwa muda mrefu na hata kukabiliana na uhaba wa mazao ya wanyama pindi  kunapotokea ukame.

Kupiga vita ujinga kwa pamoja
Inaweza kuelezwa kuwa ndani ya jamii unakuwepo usindikaji wa mazao mbalimbali  kwa kutumia mbinu tofauti za asili na hali hiyo pia ipo kwenye  sekta nyingine kama za dawa za asili na ufugaji wa wanyama.
Katika dhana hiyo kuzitambua na kuziboresha aina hizo za maarifa  ni muhimu katika utamaduni na hata kwenye sababu za kijamii na kiuchumi. Aidha hiyo  inakuwa ni njia ya kuhifadhi bioanuai, kuhimiza uzalishaji wa ndani na kujihakikishia uhakika au usalama wa chakula.
Kutambua maarifa asilia na kuyatumia vizuri ni muhimu kutokana na sababu kuwa uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea unabakia ukisukumwa na masoko ya nje na hivyo watu hususani wanaoishi mijini huwa hawana njia ya kumudu kujilisha wenyewe.
Mara nyingi bidhaa kama nyama na mchele ambazo huagizwa kutoka nje zimekuwa zikionekana au kuelezwa kuwa hazina virutubisho kwa kulinganisha na bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.
Kwenye maeneo mbalimbali miongoni mwa jamii mazao kama ulezi na mtama yameanza kutoweka wakati ni mazao muhimu yanayochangia katika kudhibiti njaa wakati uzalishaji wa mazao ya kilimo unapokumbwa na ukame au mavuno kuwa haba.
Hoja inayoibuka hapa ni kwamba ni kwa namna gani hali hii inaweza kurudishwa? Hii inawezekana kwa kupiga vita ujinga wa pamoja. Katika hali hiyo Serikali, taasisi za kitaifa na kimataifa na asasi za kiraia, watafiti  na waandishi wa habari wana mchango mkubwa wa kutoa katika kuhakikisha maarifa asilia yanatumiwa ipasavyo.
Kila mmoja anatakiwa kuchangia katika hili kwani hiyo ndio thamani ya maendeleo kwa kutumia hazina iliyojificha ndani ya jamii vijijini.
Katika kuviona vitu kama hivi walio karibu navyo huvipuuza lakini wanaotoka mbali huvipa kipaumbele katika tafiti zao na walio wengi wamejipatia shahada zao kupitia tafiti walizozifanya ndani ya mfumo ulio na hazina ya maarifa asilia.

Comments