Featured Post

MAANDALIZI YA MASOKO YATUPIE MACHO MASKINI




NA ALOYCE NDELEIO
NDANI ya mwenendo wa kifedha uliopo hivi sasa itakuwa ni vigumu kwa nchi maskini au zinazoendelea kufanikisha malengo endelevu ya maendeleo kama hakutakuwepo njia ya kuifikia mitaji binafsi.
Katika mazingira hayo hoja inayoibuka ni kwamba serikali na taasisi za maendeleo ya kifedha zinaweza kuanzisha masoko ili kukuza uwekezaji binafsi?
Hilo litawezekana kwa kuangalia na kuelewa mambo ya msingi yanayounda masoko pamoja na michango yake muhimu.

Masoko yote yanaundwa na misingi kadhaa ambayo kwa ujumla inafanana. Kwa kuangalia nadharia za kiuchumi, serikali zinazotaka kuanzisha masoko ni lazima zijikite katika hatua ambazo zinakuza teknolojia mpya, taasisi nzuri, uwepo wa mawazo mengi na mtaji wa nguvu kazi.
Pia inaweza kuanzisha muundo kwa masoko mapya kupitia uungwaji mkono kwa njia ya motisha na usimamizi wake.
Kwa mfano nchi inayozalisha mazao mengi ya chakula inaweza kubuni njia za kusindika ambazo zitaendana na hali ya masoko ya nchi zinazoagiza vyakula hivyo hatua ambayo italifanya soko la mazao hayo kuwa la kisasa na hivyo kukuza mauzo ya nje.
Hali hiyo inaweza kutumika pia kwa mazao ya mifugo kama maziwa na nyama, hatua ambayo ni njia ya kuwa na mzunguko endelevu wa bidhaa.
Hapo inamaanisha kuwa taasisi za maendeleo zinaweza kutoa mchango mkubwa katika kujenga daraja kati ya serikali na sekta binafsi utakaokuwa na mchango mkubwa katika mabadiliko chanya ndani ya soko.
Katika mkakati wa kuanzisha masoko ni muhimu kuwa na dira iliyo wazi ya jinsi gani soko litakavyoendeshwa kwa kipindi fulani. Masoko endelevu ni mara chache hutokea kwa bahati mbaya au bahati nzuri. Haya huwa yanatokea kutokana na mikakati inayokuwa imepangwa.
Yapo mambo kadhaa ambayo yanatakiwa ili kufanikisha mchango wake katika maendeleo endelevu ambayo ni lazima masoko mapya yawe nayo.
Wigo wa masoko lazima ujumuishe na kunufaisha idadi kubwa ya watu na hivyo kujumuisha wale ambao hawakuwa wamelengwa katika uwekezaji wa mwanzo.
Juhudi za maendeleo ya soko ni lazima ziwe endelevu na ni lazima ziboreshe mabadiliko ya kimfumo ya soko uliojikita ndani yake mbali na uwekezaji wa mwisho unaofanywa na serikali au taasisi ya maendeleo ya kifedha. Hali hiyo inamaanisha kuwa kufanyike bila kuwepo mizigo ya kifedha isiyo endelevu kwa serikali. Hivyo masoko ni lazima yawe endelevu kimazingira na kijamii.
Aidha, soko linatakiwa liwe linabadilika. Washiriki katika soko lazima waridhie njia na taasisi ambazo zinaweza kuendelea kutoka bidhaa na huduma hata kama mazingira ya nje yatabadilika.
Jambo la nyongeza katika kuyafikia Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG’s), masoko ni lazima yawe jumuishi na yafanye kazi kwa ajili ya maskini. Kwa mfano taasisi za fedha na benki za maendeleo zimeshawekeza katika huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi hatua ambayo ni ya mwanzo na ya mfano katika kuanzisha masoko.
Hatua hiyo imewezesha kukua kwa makampuni kufuatia uwekezaji ambao  umesaidia kuwaleta watu wengi ambao hawafikiwi na huduma za kibenki ambao awali walikuwa wakitumia fedha taslimu na hivyo kuokoa muda  uliokuwa unapotea kwa kufuata mfumo wa kawaida wa kifedha ili kuhudumiwa.
Uanzishaji wa masoko una njia kadhaa muhimu na mojawapo ni kuwepo jukwaa pamoja na mabadiliko yatakayowezesha masoko kufanya kazi.
Utekelezaji wa mabadiliko ya sera katika sekta kama vile nishati au kilimo kunaondoa vikwazo na vizuizi kwa wawekezaji binafsi na kuwawezesha kuingia katika masoko hayo. Uwajibikaji katika hili kimsingi upo ndani ya serikali na mara nyingine ukiwepo ushauri au msaada kutoka taasisi za maendeleo ya kifedha.
Njia nyingine ni kuboresha ushindani ambao utasababisha wachangiaji wengine katika soko kukuza ushiriki wao. Kwa mfano kuwekeza katika namna mpya ya rejareja ambayo itaboresha huduma na kupunguza bei kutawafanya washindani katika soko hilo kuridhia kuenenda na maboresho ya kibiashara kama hayo.
Kuonesha mafanikio na kuboresha michango ya mawazo ni njia nyinge ya kujenga masoko. Mafanikio huzaa uigaji na hii ndio dhana ya msingi ya kuonesha mafanikio. Kwa mfano muundo mpya wa kibiashara ambao  utavutia mtaji na kuonesha kufikiwa kwake na soko kutatoa msukumo kwa taasisi nyingine binafsi kuwa na muundo kama huo. Hivyo uigaji kama huo unahimizwa.
Mfano wa kuigana upo dhahiri katika makampuni ya simu ambapo  zimekuwa zikinadi bidhaa zao kwa kuigana. Kampuni ya Tigo kwa mfano ina vifurushi vya ‘Halichachi’ na wakati huo huo Vodacom ina vifurushi vya ‘Haliishi’ na Airtel wana ‘Hatupimi’. Kilichopo hapo ni tofauti ya majina lakini bidhaa ni ile ile.
Kujenga stadi zinazofungua fursa mpya za soko ni njia nyingine mwafaka. Mfano unaweza kuwa ni kufundisha wasimamizi wa kuiga masoko  na kuboresha uwekezaji katika taasisi za kifedha kunaweza kuunda soko la bidhaa zinazoweza kuyumba ambazo ni nyenzo ya kifedha inayosaidia wateja wa makampuni kudhibiti athari za kifedha.
Kuanzisha shughuli za soko katika sekta na sehemu ya idadi ya watu ambao  hawakuunganisha moja kwa moja katika uwekezaji wa awali, njia hizi zinaweza kuboresha mabadiliko ya soko ambayo yataenda mbali kupitia matokeo ya moja kwa moja  ya mradi husika wa maendeleo au uwekezaji.
Kwa taasisi za maendeleo ya kifedha changamoto inayozikabili ni kuingiza  njia za uendeshaji wa biashara zikiwa na mtazamo huu wa masoko, kuliko ilivyo kwa  mtazamo wa kawaida  katika uwekezaji binafsi.
Hii inamaanisha kuna haja ya kubadili mtazamo kutoka katika kuangalia njia moja katika kipindi ambacho inatakiwa kuangalia kwa mapana jinsi aina kadhaa za uwekezaji unavyoweza kuchangia au kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo.
Wakati hali ikiwa hivyo inatakiwa pia mtazamo unaojikita kuangalia athari za mazingira dhidi ya watu maskini na walioko pembezoni ili kuhakikisha unakuwepo ujumuishwaji na uendelevu.
Katika kuangalia uundaji wa masoko yanaweza kuwepo mazingira magumu hususaai katika maeneo ambayo yana migogoro na ambako uwekezaji binafsi ni muhimu katika kufikia malengo ya kutokomeza umaskini yaliyomo katika Malengo Endelevu ya Maendeleo.

Comments