Featured Post

KWANINI TAFITI ZA SAYANSI HAZIFAHAMIKI MAPEMA?



NA ALOYCE NDELEIO
Mara nyingi tafiti za kisayansi zinapofanywa na wataalamu mbalimbali hulenga kutatua vikwazo vinavyojitokeza ndani ya jamii, lakini ili tafiti hizo ziweze kuwa ni ufumbuzi wa vikwazo ni muhimu zikawafikia walengwa hususani maskini.
Hali hiyo inamaanisha kuwa kiwango cha sayansi kilicho na uwiano na mwitiko kinahitajika kwa jamii zilizoko pembezoni.

Katika maeneo ambayo tafiti haziwafikii walengwa huwa inatokana na kuwepo kwa uhamaji wa wasomi kimataifa kutoka nchi zinazoendelea kwenda zilizoendelea.
Hata hivyo uhamaji huo wa wasomi upo pia kitaifa kutoka jumuiya za vijijini kwenda mijini, tukio ambalo linazifanya tafiti kuwa mbali na mahitaji ya jumuia za ndani ya nchi.
Pale ambapo hali hiyo inakuwepo inakuwa vigumu kuzielewa kazi za wanasayansi au tafiti zao kwa kuwa zinakuwa hazijapewa kipaumbele cha kufikishwa katika jamii hizo.
Wakati hivi sasa fainali za Kombe la Dunia ambazo zinafanyika Urusi yapo mazingira yaliyofanya kueleweka uwepo wa mechi hizo. Hali hiyo inamfanya kila mmoja kuelewa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na kwamba linashughulika na jambo gani.
Hali kama hiyo itakuwepo na imeshakuwepo pindi yanapotokea mashindano ya Olimpiki na wengi kufahamu Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na inashughulikia mambo gani.
Hata hivyo zinaweza kuwepo taasisi nyingi zikiwa na malengo yake  mazuri tu lakini hayaelewiki au si mara zote malengo yake yanaeleweka, kwa maana hiyo hata kwa tafiti nyingi inakuwa hivyo.
Kwa mtu aliyejijengea mazoea ya kusoma mambo mbalimbali katika maktaba ni lazima atakuwa anakumbana na kazi nyingi za wasomi  zinazohusu tafiti zikiwa zimesheheni kwenye rafu za maktaba hizo na baadhi zikiwa na tandabui.
Hali kadhalika unaporambaza (surf) kwenye baadhi ya kurasa za tovuti za intaneti tafiti za aina hiyo pia zinatiririka. Majarida ya tafiti nayo yanakuwa yamebeba tafiti za wasomi, maofisa wengi ndani ya maofisi  nao hawakosi kuwa na tafiti za wasomi mbalimbali.
Hata hivyo wataalamu wengi kila kukicha wanaendelea kufanya tafiti mpya na  kuchapisha nakala nyingi za matokeo.
Swali  linaibuka kuwa hivi kweli watu wanazisoma tafiti au kazi hizi? Kama wapo wanaozisoma wanazielewa na zinaleta au kutoa mwangwi wa mabadiliko yoyote hivyo kwamba ujumbe au matokeo yake yanazifikia jamii au walengwa ambao ni maskini?
Louise Tickcle wa Idara ya Maendeleo ya Uingereza (DFID) anabainisha kuwa lipo lundo kubwa la tafiti zinazohusu mambo ya maendeleo na hasa yanayozihusu nchi zinazoendelea na hata zilizo katika kipindi cha mpito.
Hata hivyo anasema kuwa changamoto inayowakabili wasomi na wataalamu waliobobea katika baadhi ya sekta na wataalamu wa fani mbalimbali na hasa asasi zisizo za serikali ni namna ya kuwa mwaminifu kwa njia ambazo zitawezesha matokeo ya tafiti zao kupenya katika midahalo ya jamii.
Hali hiyo ndiyo inayowezesha utaalamu au maarifa hayo yachupe kutoka taswira ya nadharia na kuingia kwenye utekelezaji kwa vitendo na  kubadilisha maisha ya watu.
Kutokana na hali hiyo anahoji kuwa ni vipi watafiti hao wanaweza kuhakikisha kuwa kazi zao hazibaki kulundukana kwenye meza za wapanga sera kwenye makasha yaliyobandikwa majina kuwa ni “mapya” au “zilizoingia”?
Kwa mujibu wa Dkt. James Putzel, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha LSE Crisis States katika Asasi ya Maendeleo ya Mitala (DESTIN) ni kwamba jambo ambalo wasomi watafiti hawalifanyi ni kufanya utafiti ulionuia kuzikabili sera au mtazamo wa kisiasa.
Anasema, “Jambo  muhimu ni kuelewa kitu kinachofanya kazi ulimwenguni na jinsi kinavyoleta mabadiliko, njia gani za baadaye ambazo ni  mbadala … hivi ndivyo wataalamu watafiti wanatakiwa kufanya mahali popote wanapokuwa wana dondoo za tafiti zenye ukweli.
Anadokeza, “Katika utafiti wowote unaweza kupiga hatua au ukafika kwenye hitimisho iwapo aina ya uchaguzi ambao idara ya serikali au asasi zisizo za serikali inayofanywa hupimwa na mahitaji ya papo hapo na matokeo yake huwa ni ya papo hapo.”
 Dk. Putzel anaarifu, “Utafiti wa kisomi unaingia ndani zaidi ya hapo na kutoa uwanja mpana zaidi wa ubunifu na ugunduzi usitegemewa.”
Wakati inakubalika kwamba ni vigumu kuipelekea jamii matokeo ya tafiti hususani katika uwanja wa sera; Dk. Putzel na timu yake ya ubunifu imeibuka na mbinu mpya ambazo zinafanya kazi.
Anasema kuwa jambo alilojifunza kwa  zaidi ya mwaka mmoja ni kwamba ni watu wachache walio tayari kusoma kitu chochote ambacho kinakuwa kimeelezewa au kufafanuliwa kwa urefu.
Kutokana na hali hiyo anasema kuwa ni vizuri kwa tafiti kufikisha ujumbe au maudhui ya kazi kwa ujumla na hilo linawezekana kwa kutumia  njia mwafaka ya kufanya kazi na wahusika.
Anaendelea kusema, “Tumepeleka watu wetu kwa marejeo katika DFID, ambako wataalamu wake wanaweza kuwa na hadhira nzuri na hili linawezekana… tumejaribu kuzungumza na wawakilishi  katika nchi tunamofanyia tafiti.”
Anabainisha kuwa kituo chake cha Crisis  States  pia kimetoa kipaumbele  kwa kuwa na hifadhi za maktaba  zenye muhtasari wa tafiti katika tovuti zake  ili kuwezesha kufikiwa  kwa vyanzo hivyo na wapanga sera wote wa nchi za Kaskazini na Kusini.
Aidha Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Ushirika na Usalama  katika Chuo Kikuu cha Bradford wa Idara ya Maendeleo ya Mitala ya Amani, Dkt. Greene anadokeza kuwa ni muhimu kwa watafiti  wasomi  kutawanya kile wanachokuwa nacho kwenye vichwa vyao na njia mojawapo ya kufanikisha hilo ni lazima kuwa pamoja  na wapanga sera.
Dkt. Greene anasema, “Mara zote huwa ninaangalia tafiti ambazo zinalandana na sera kwa njia ambayo itafanya jamii inufaike na sera kutoka mwanzo hadi mwisho.
“Kwangu mimi iwapo  kuna watu wanataka kuchangia katika midahalo ya utekelezaji  au maamuzi, hawawezi kutegemea ushawishi wao kukubalika bila kuwa pamoja katika kujihusisha na sera za jamii.”
“Wapo maofisa ambao wamekanganyikiwa wanaopenda kufanya utekelezaji wa jambo katika maeneo au nyanja ambazo wasomi wanafanyia” anasema, na kuongeza kuwa kukanganyikiwa kwa maofisa hawa kunatokana na sababu kuwa wapo karibu na watafiti wenyewe.
Kwa jumla  watu wanaotakiwa kujishughulisha nao ili kutoa ushawishi wa sera ni maofisa, lakini jambo la kuelewesha umma zaidi ni kuwepo upeo wa kisiasa miongoni mwa wabunge na mawaziri katika mipango ya sera.
CHANZO: TANZANITE

Comments