Featured Post

KWA WALA RUSHWA NDIKO KODI HAILIPWI


NA MWANDISHI WETU
Kati ya mambo ya msingi yaliyoibuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni suala la kodi ambalo linaenda bega kwa bega na hazina ya mafunzo aliyokuwa anayatoa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwalimu alisema, “Nazungumza habari za kutokusanya kodi. Kutokusanya kodi ni sifa moja ya viserikali corrupt popote pale. Popote, wala usifikiri ni Tanzania peke yake...Serikali corrupt popote pale, haitozi kodi.
“Serikali corrupt inatumwa na wenye mali. Inawafanyia kazi wenye mali. Serikali corrupt itamwambieje mwenye mali, kwamba ‘utalipa, usipolipa utakiona!’ Atacheka tu huyu. Atakwambia ‘unaniambia hivyo wewe? kesho siji basi!’”
Wakati serikali ilipoanza kukusanya kodi kutoka kwa wafanya biashara na hususani waliokuwa wanapitisha bidhaa zao katika bandari ya Dar es Salaam  na ambao walikuwa hawalipii kodi bidhaa zao  hapo ndipo ilionyesha ni kwa jinsi gani jamii ilikuwa imekengeuka.
Ilikuwa ni dhahiri kuwa Tanzania hii ilikuwa imechepuka  na kuondoka katika mstari kwa kulipuuza somo lililohusu kodi ambalo alilitoa Mwalimu Nyerere.
Modno mnyoofu wa kukusanya kodi ambao alikuwa anauelezea Baba wa Taifa ulikuwa umepigwa kisogo na baadhi ya wanajamii ambao hawakuwa wanyoofu pia.
Katika mazingira hayo jambo lililowezesha kukithiri kwa hali hiyo ni kutamalaki wa rushwa jambo ambalo liliikosesha serikali haki yake ya  kupata nyenzo za kupelekea wananchi  maendeleo.
Katika mazingira kama hayo pia inaweza kuelezwa kwamba serikali ilikuwa imeingizwa katika mchepuko hatari kwani waliokuwa wamepewa dhamana ya uongozi au usimamizi wa amana za nchi walifanya mambo kwa kuipa kisogo dhana ya vyeo ni dhamana na vitumike kwa faida ya wote na kwa maslahi ya wote.
Aidha vyeo vilionekana ndio nyenzo ya kuvuna jasho la walala hoi kwani badala ya kuwajibika kwa ajili ya umma  ikawa ni kuwajibika kwa ajili yao na wana wao.
Katika mtazamo wa kauli za Mwalimu aliona kuwa baadhi ya viongozi walikuwa wameshapandikiza mazingira ya kupuuza  hisia za utaifa za uzalendo, ujasiri, kujituma, kuwajibika na kwamba walikuwa wamejibadili kitaswira kama watu wanaohama kesho na hivyo kuwa na haja ya kukusanya  kila walichokiona ili wakafaidi mbele ya safari.
Taswira hiyo ilionesha kuwa  wao ndio waliokuwa na meno  na wanajua kutafuna  ndio maana leo hii lilipotajwa  suala kuwepo  kwa wafanyakazi hewa ndani ya taasisi za umma  na kwamba hata marehemu walikuwa wakilipwa malipo  hiyo ilikuwa ni fedheha ambayo Mwalimu hakuwa ameisahau katika masomo yake.
Wakati serikali ya Awamu ya Tano ilipoanza mkakati wa kupambana na kuangalia namna ya kudhibiti hali hiyo  na hususani kwa kuhakikisha kuwa kodi inalipwa katika kila sekta hilo lilikuwa ni mwiba kwa walioona kuwa wanaweza kuishi kwa mwenendo wa mazoea.
Katika kuchepuka  huko  ambako nchi iliingia  ni dhahiri waliokuwa na dhamana  walikuwa wakihanikiza uendelevu wa kuvuna jasho na kuwaacha walala hoi  ndani ya umaskini  ujinga na maradhi na wakishamirisha dhuluma na kuibua adui mwingine ambaye ni rushwa.
Walioona kuneemeka huko kuna tija waliiweka kando kanuni njema katika masomo mema ya kushirikiana na jamii kwa ujumla  kuijenga nchi, badala yake wakaunda mtandao wao wa kushirikiana kuitafuna nchi.
Kwa ujumla yote hayo yalishamirishwa na kumea  kwa kupuuza kipengele muhimu katika masomo na kauli za Mwalimu  ya kusema kweli na kustawisha kusema uongo.
Ukweli unabakia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikijipambanua kwamba haina mchezo katika suala zima la kukusanya mapato yake, zikiwamo kodi mbalimbali ambazo zinatakiwa kulipwa na kila raia.
Katika kutekeleza hilo, ndiyo maana jamii imekuwa ikisikia na kuona serikali ikichukua hatua mbalimbali za kukusanya mapato yake, ikiwamo kutumia nguvu kuwabana watu ambao hawalipi kodi, hivyo kuathiri uendeshaji wake pamoja na utoaji wake wa huduma za msingi kwa wananchi.
Kwa mfano, jamii imeshuhudia jinsi wafanyabiashara waliokuwa wakipitisha makontena ya mizigo bandarini walivyoshughulikiwa kwa kukamatwa na kufunguliwa kesi za kukwepa kulipa mapato ya serikali, wengine kupewa muda kulipa, wengine kushtakiwa.
Katika maeneo mbalimbali  jamii pia imeshuhudia wafanyabiashara wakifungiwa biashara zao zikiwamo za maduka, baa, hoteli na zingine kutokana na kudaiwa kodi. Kimsingi, katika suala la kodi serikali haina utani wala mchezo na mtu yeyote.
Kutokna ana kutokuwa na utani katika jambo hilo  ndio maana serikali imekomalia kudai kodi kwa makontena 20 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda  ambayo yamewekwa bayana kuwa yameliiinia bandarini hapo kama mali binafsi na si ya taasisi.
 Kutokana na hali hiyo kwamba hayakuchukuliwa  kulingana na maagizo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuyapiga mnada kwa kuzingatia kanuni za kisheria.
Hali hiyo imeibua mijadala  lakini sheria inabakia pale pale na kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango,  mnada huo utaendelea hadi kieleweke kwamba kodi ya serikali inapatikana.
Dhana ya malalamiko na madai kwamba watapata laana wanaofanya au wanaoyanadi wapata laana  dhana hiyo haiwezi kua na mashiko kwani inakwenda tofauti na ile dhana inayosema, ‘Mpe Kaisari yaliyo yake na Mungu yaliyo yake.’
Jambo lililo dhahiri ni kwamba Serikali inarejesha heshima ya nchi, kutokana na hali ambayo Watanzania waliokuwa wamefikia, ya kuchuma fedha kwa njia za mkato na kuzitumia katika anasa na matumizi ya kujirusha. Waliokuwa wakifanya hayo ni watumishi wa umma kwa kutumia nafasi zao za utumishi, wafanyabiashara na  wapambe wao.
Kuziba mianya dhahiri kunaonekana sasa na  umuhimu wa kulipa kodi iwe kwa serikali yenyewe, taasisi zake, watu binafsi, asasi zisizo za kiserikali na kampuni binafsi hilo haliwezi kukwepeka. Hakuna anayetaka kutoa huduma bila kulipwa stahiki yake.

Comments