Featured Post

KWA NINI SAFARI ZA KUTALII TANZANIA ZINAKIDHI UBORA



NA ALOYCE NDELEIO
SAFARI za utalii zinahitaji maandalizi kabla ya kuzianza hali ambayo imekuwa inaonekana kuwa ni changamoto ambayo mtu anakumbana nayo pindi anapojipangia safari yake kuhusu ni sehemu gani atakayotembelea.
Kwa nchi za Afrika mathalani Zimbabwe kuna maporomoko ya maji ya Victoria ambayo yako kwenye mto Zambezi, Afrika Kusini kuna mbuga nzuri za wanyama, Kenya nao wana kivutio cha simba wakubwa na Botswana inaongoza kwa utalii ulio rafiki kiikolojia.

Lakini kwa mujibu wa matokeo ya kura zilizopigwa kwenye mtandao wa tovuti ya safaribooking.com hivi karibuni inabainisha kuwa kwa mtu anayepanga safari zake sehemu nzuri ya kuchagua ni Tanzania.
Mtandao huo ambao una makao yake makuu nchini Uholanzi ulifikia hatua hiyo kutokana na kura zilizopigwa na watalii 1000 na wataalamu wengine 756 wakiwemo waandishi wa vitabu vya miongozi ya safari kutoka kampuni za Lonely Planet, Rough Guides, Frommer's, Bradt na Footprint kwa kipindi cha miaka miwili.
Matokeo ya kura hizo ni kwamba Tanzania ni pendeleo la wazi kwa watu wanaofanya safari za utalii  ambapo mwandishi Tim Bewer  ambaye ni mwandishi wa miongozo ya safari na mmoja wa wataalamu waliopiga kura  kutoka kampuni ya Lonely Planet.
Anasema, “Tanzania ndiko iliko Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Kreta ya Ngorongoro” na kuongeza, “Hili pekee linaifanya kuwa sababu ya msingi ya kuamua nchi nzuri kwa ajili ya safari barani Afrika”.
Tanzania ina maeneo ambayo yanatambuliwa na Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kama urithi wa dunia yakiwemo maeneo mawili ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambako ni makazi ya mamilioni ya nyumbu ambao wanaunda moja ya taswira ya ajabu duniani kwa kuhama kutoka eneo kwenda eneo jingine katika sehemu ya kipindi kimoja cha mwaka.
Aidha, inaelezwa kuwa maeneo mengine ni Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko milima mingine barani Afrika. Aidha inafahamishwa kuwa kivutio kimoja kilichopo kwa mujibu wa Safari Bookings ni kuwepo kwa vidokezo vingi mno ambavyo vinaweza kukidhi safari moja.
Taarifa hiyo kuhusu hali hiyo imekuja na kukaribisha kama uthibitisho kuwa Tanzania bado ni kivutio cha utalii hususan baada ya milipuko ya mabomu ambayo yalitokea kwenye mkutano mjini Arusha na kusababisha vifo vya watu wawili.
Tukio hilo lilisababisha taharuki miongoni mwa wageni wanaotembelea vivutio vilivyopo kwenye jiji hilo.
Viwango kwa mujibu wa kura zilizopigwa na watalii na wataalam wa masuala ya safari kwa nchi tano ambazo zinaongoza kuwa  sehemu nzuri ya kwenda kwa safari na alama zake katika mabano ni Tanzania (4.84), Botswana (4.75), Kenya (4.66), Zambia (4.58), Afrika Kusini  (4.55), Namibia (4.54), Uganda (4.16) na Zimbabwe (4.14). 
Tanzania ni eneo kubwa kwa ajili ya likizo pamoja na safari za kitalii, ina fukwe nzuri na maumbo ya nchi yanayovutia. Lakini jambo jingine muhimu mno ni kwamba bado Tanzania ni makazi mazuri kwa ajili ya safari za utalii barani Afrika. 
Wakati hali ikiwa hivyo kama vile kichocheo cha kuipaisha Tanzania katika nyanja ya utalii ilikuwa ni ziara ya Rais wa Marekani Barack Obama alipotembelea Tanzania.
Ziara hiyo iliacha kumbukumbu miongoni mwa sekta zilizojipambanua kunufaika na ujio wa Rais Obama ni pamoja na sekta ya utalii ambapo serikali imekuwa inapata mapato makubwa.
Kwa kuangalia baadhi ya mapato kwa miaka iliyopita kama mwaka wa fedha wa 2012/13 yalifikia dola za Marekani  bilioni 1.5 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 2.8 ikilinganishwa na dola milioni  950 sawa na shilingi  trilioni  1.2 ambazo zilipatikana kwa mwaka wa fedha 2011/12.  
Kuwepo kwa ziara za viongozi mbalimbali wa mataifa makubwa katika kuitembelea Tanzania ni jambo ambalo linahuisha uchumi wa kidiplomasia.
Mfano wakati wa ziara ya Obama Tanzania ilijikuta wakati huo huo ikimpokea mtangulizi wa rais huyo George W. Bush kwa kwati mmoja lakini wakiwa katika mikakati tofauti.
Licha ya kwamba Bush alikuwa ameshafika Tanzania mwaka 2008 alipokuwa madarakani kiuhalisia ni kwamba ujio wa Marais hao wa 44 na 43 wa Marekani kwa wakati mmoja jambo ambalo lilishangaza katika ngazi za kidiplomasia. 
Viongozi wakubwa duniani hutembelea Afrika kwa nadra, lakini Tanzania ilimpokea Obama ikiwa ni miezi mitatu tu tangu Rais wa China Xi Jinping afanye ziara yake.
Kwa dhana ya kuichagua Tanzania wachambuzi wa mambo wanaona ni mwafaka kusema kuwa kuna mambo mengine mengi ukichana na ushindani wa moja kwa moja kati ya Washington na Beijing kutokana na ziara hiyo.
Marekani ni mshirika mkubwa na pekee wa maendeleo katika kutoa fedha kwa ajili ya miundombinu, anasema J. Peter  Pham wa Kituo cha Afrika Baraza la Atlantiki na kuongeza kuwa Washington ni lazima iwianishe kanda kijiografia na hali kadhalika kidini na lugha katika kuchagua mataifa ya kutembelea.
Hata hivyo, ni dhahiri kuwa ziara za viongozi mbalimbali duniani vinaipaisha Tanzania katika nyanja ya Utalii na kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Marekani inashika nafasi ya pili baada ya Uingereza kwenye soko rasmi la watalii kwenye promosheni za taasisi za umma, watalii na watu wanaoenda likizo za kitalii.
Takribani watalii wa Marekani 60,000 hutembelea Tanzania kila mwaka  ikilinganishwa na watalii 65,000 kutoka Uingereza ambao hutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.
Watalii kutoka Marekani wanahesabika kuwa ni miongoni mwa watalii bora na kwamba wanafanya matumizi makubwa ya kitalii pindi wanapotembelea Tanzania ambayo ni pamoja na kufanya utalii wa uwindaji.
Lakini pamoja na hali hiyo yote ni kwamba inakolezwa na na kuwepo kwa mazingira salama ya amani na utulivu.

Comments