Featured Post

KUWAJIBIKA, KUKATAA RUSHWA NDIO UTAWALA BORA



NA ALOYCE NDELEIO
"Tunataka kiongozi ambaye anachukia rushwa, na hata tukimwangalia usoni tunaamini anachukia rushwa, Si ambaye hata ukimuangalia unajiuliza, mmh, huyu!"
Hiyo ni kauli iliyotolewa na hayati  Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  akilenga kwenye namna ya kupata viongozi waadilifu na wasafi ambao wataweza kulitegemeza taIfa  badala ya kulididimiza.

Lakini katika mazingira ya leo hii  na kwa mwenendo wa siasa zilizopo ndani ya jamii  ya sasa hao ambao alisema ukiwaangalia  na kuleta mshangao wapo wengi.
Hali hiyo inatokana na sababu kuwa katika nchi nyingi zinazoendelea kuna matukio mengi ya watu kujiingiza katika siasa kwa lengo la kujitajirisha au kuficha maovu yao mengi.
Wasomi mahiri na wafanyabiashara maarufu wameshajiingiza katika siasa na kupata nafasi za juu za uongozi kwa kuuza sera za kutetea wanyonge, lakini ni wachache sana waliotekeleza sera hizo.
Wanasiasa wengi wakishapata madaraka wanasahau wanyonge waliowapigia kura na kuanza kujinufaisha wao binafsi, ndugu, jamaa na marafiki zao.
Katika kuonesha hali ilivyo miongoni mwa nchi hizo zipo rejea chache ambapo hadi  mwishoni mwa mwaka 2007 yalikuwepo matukio ya wanasiasa maarufu na viongozi wakuu kadhaa ambao walipoteza nafasi zao za uongozi kwa kulazimika kujiuzulu, kufukuzwa na kufungwa kwa ufisadi.
Mifano hii hai inaanzia huko Manila, Ufilipino ambako Septemba 12, 2007 rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Estrada alipatikana na hatia ya kuhusika na vitendo vya rushwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Estrada alipatikana na hatia hiyo iliyothibitishwa na Mahakama Kuu kuwa aliiba fedha za serikali zinazofikia 100bn/- wakati akiwa rais. Rais huyo wa zamani ambaye alikuwa mcheza sinema na mfanyabiashara maarufu kabla ya kuingia katika siasa, baada ya hukumu hiyo alilalamikia utaratibu wa vyombo vya sheria nchini humo kwa kudai  kuwa vinatumiwa kisiasa na uongozi uliokuwa madarakani wa Rais  Gloria Arroyo.
“Najua hukumu hii imeshinikizwa na serikali, ili kwamba nionekane mtu wa hovyo, ingawa ukweli wenyewe wanautambua,” alilalamika Estrada.
Rais huyo wa zamani aliikimbia Ikulu ya nchi hiyo mwaka 2001 baada ya wananchi kuandamana wakimshinikiza ajiuzulu kwa tuhuma za ufisadi na uongozi mbovu.
Baada ya kuikimbia Ikulu uchaguzi uliiitishwa na yeye mwenyewe hakushiriki. Kufuatia hukumu hiyo, Estrada pia aliamuriwa kulipa 17bn/- na kukabidhi jumba lake la kifahari ambalo inaelezwa alilijenga kutokana na vitendo vya rushwa akiwa madarakani.
Estrada hata hivyo, ilielezwa kuwa  alitumikia kifungo hicho akiwa katika nyumba yake nyingine jijini Manila na hakuruhusiwa kutoka ndani, na alilazimika kuomba kibali alipotaka kutoka nje ya eneo la nyumba yake. 
Mtoto wake Jinggoy, ambaye aliunganishwa katika kesi hiyo, aliachiwa huru na kufutiwa kosa la wizi lililokuwa linamkabili kwa kushirikiana na baba yake. Msemaji wa Rais Gloria Arroyo aliwaomba wananchi kuwa na utulivu, kwani sheria imechukua mkondo wake na kuwa hakuna aliye juu ya sheria.
Kesi dhidi ya Estrada ilianza siku chache baada ya kuikimbia Ikulu kufuatia maandamano ya wananchi wenye hasira mwaka 2001 na tangu wakati huo alikuwa katika kifungo cha ndani ya jumba lake la kifahari ambalo baadaye alitakiwa kulikabidhi kwa serikali. Hukumu hiyo ilihitimisha mahabusu ya ndani kwake ambamo alikaa kwa miaka sita na miezi minne kabla ya hukumu yake.
Huko Japan, moja ya nchi zilizoendelea sana kwa viwanda, Waziri Mkuu  Shinzo Abe alijiuzulu, Septemba 12, 2007.
Abe alitangaza kujiuzulu wadhifa huo kufuatia kushindwa kwa chama chake katika uchaguzi uliofanyika nchini humo Julai 2007. Waziri Mkuu huyo ndiye anatajwa kuwa na umri mdogo zaidi kushika nafasi hiyo mwaka 2006, akiwa na umri wa miaka 52.   Viongozi wengi waliomtangulia walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 55 na kuendelea.
Tangu kushindwa kwa chama chake, Abe alikuwa akishinikizwa kuachia ngazi ili kutoa nafasi kwa viongozi wengine kuiongoza Japan, ambayo ni  miongoni mwa nchi tajiri zaidi duniani.
Akitangaza uamuzi huo kwenye televisheni ya taifa, Abe alisema alilazimika kuachia ngazi ili kuwapa nafasi watu wengine kuiongoza Japan. Kiongozi huyo alisema anaamini kiongozi atakayechukua nafasi yake atatumia nguvu zake zote kwa kushirikiana na wengine kuhakikisha kuwa ugaidi unatokomezwa.
Septemba 09, 2007, Abe alieleza kuwa Japan inahitaji kiongozi mwenye mtazamo chanya ambaye atahakikisha nchi hiyo inaendelea kuwa na nguvu kubwa ya uchumi na hata kijeshi. Alisema kiongozi wa namna hiyo atawaweka Wajapan katika misingi iliyopo sasa ya hali bora ya uchumi kwa kila mwananchi.
Alisisitiza, "Nchi inahitaji kiongozi imara ambaye anaweza kuwasaidia katika shughuli zao, lazima awe ni mtu ambaye wanamwamini na kumpenda.”
Kiongozi wa chama cha upinzani cha SD, Mizuho Fukushima alisema kujiuzulu kwa Abe muda huo kunaonesha jinsi asivyojali muda na masuala muhimu ya Japan.
Mnamo Julai 09, 2007 Rais wa zamani wa Indonesia, Jenerali Muhammad  Suharto alifikishwa mahakamani kwa madai ya kujinufaisha na fedha za wahisani  kutoka katika mfuko wa elimu uliojulikana Supersemar mwaka 1974.
Kwa mujibu mwa mwendesha mashtaka, Dachmer Munthe, "Kesi ilifunguliwa baada ya kupatikana kwa ushahidi kwamba fedha za mfuko ambao Suharto alikuwa mwenyekiti na hazikutumika kwa ajili ya kusomesha wanafunzi kama ilivyokusudiwa bali kwa manufaa ya kibinafsi ya Suharto, jamaa na marafiki zake.
Mwendesha mashtaka alisema toka mwaka 1978 na kuendelea  Suharto alitumia asilimia 85  ya fedha za mfuko huo kwa mambo yake binafsi.  Kesi ilianza Agosti 09, 2007. Suharto alifariki mwaka 2008.
Hata hivyo hivi karibuni Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma naye aliingia katika matata baada ya kufunguliwa mashtaka kutokana na ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Zote hizi ni rejea ambazo zinaonesha kuwepo madarakani kwa baadhi ya wanasiasa kunawafanya wawe na vichwa ngumu na kugeuka kuwa mafisadi kwa kuwapora wananchi kile ambacho ni chao na kujinufaisha wao wenyewe.
Rejea hizi zinasadifu kwa Tanzania ya leo ambako viongozi wengi wamekuwa wanaziona nafasi zao kama ni za kinabii na hazihitaji kuguswa au matendo yao hayapaswi kuelezwa  au kufahamika mbele ya jamii.
Matukio ya kifisadi ambayo yanatokana na kuchota fedha kwenye akaunti za umma  na kuziingiza kwenye mifuko yao binafsi badala ya mifuko ya maendeleo  kwa manufaa ya jamii ndicho kinachoshuhudiwa leo.
Hata hivyo  linapokuja suala la kuwajibika kutokana na kushindwa kwao kuwajibika kwa masuala nyeti yakiwemo ya kula rushwa ndipo wanapoonekana kuwa wakali kama mbogo aliyekoswa na risasi.
Ukali huo upo kwenye kauli zao nyingine nyingi za majigambo ambazo kwa walala hoi ni kero na karaha.  

Comments