Featured Post

KUTUMIA RASILIMALI KWA BUSARA HUEPUSHA ‘UGONJWA WA KIDACHI’



NA ALOYCE NDELEIO
MWANDISHI maarufu wa Hispania wa karne ya 16, Miguel de Cervantes Saavedra, ambaye aliandika kitabu Don Quixote de la Mancha, aliwahi kusema, “Furaha ya utajiri haipatikani kwa kumiliki au kuwa na matumizi ya anasa bali hutokana na busara kwenye matumizi hayo”.
Maneno hayo aliyatoa kipindi ambacho Hispania ilikuwa ikifurahia utajiri wa maliasili ilioupata kutokana na kugundulika kwake ikiwemo dhahabu kwenye koloni lake huko Marekani.

Kwenye miaka ya 1960 Uholanzi ilijikuta ikiwa na utajiri mkubwa baada ya kugundulika kwa kiasi kikubwa hifadhi ya gesi asilia kwenye bahari ya kaskazini.
Bila kutarajia hatua hiyo chanya ya maendeleo ilikuwa na athari kubwa kwenye sehemu muhimu za uchumi wa nchi hiyo. Aidha sarafu yake (Guilder) iliimarika na kufanya bidhaa nyingine  zisizotokana na mafuta  kushindwa kuingia kwenye ushindani.
Hali hiyo ndio baadaye ilikuja kufahamika kama “Ugonjwa wa Kidachi’. Japo ugonjwa huo kwa ujumla unahusiana na ugunduzi wa rasilimali ya maliasili.
Aidha unaweza kutokea katika  aina yoyote ya maendeleo ambayo yatatokana na mtiririko mkubwa wa fedha za nje, ukiwemo kupanda kwa kasi kwa bei za rasilimali za maliasili, msaada kutoka nje na hata uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje.
Jambo muhimu katika ugonjwa wa Kidachi ni muda wa kati ya ugunduzi wa madini na wakati ambapo fedha zinaingia.
Hivi karibuni ilikuwepo kasi kubwa ya makampuni ya nje kuhusu kupata zabuni za kuchimba gesi asilia  iliyogundulika kuwepo kwa wingi hapa nchini.
Aidha mwenendo wa ushindani ulikuwa na taswira ya kugombea kwa kuwa yalikuwepo makampuni kutoka China na India yakishindana na makampuni ya kimataifa ya nchi za magharibi ili kupata uwekezaji wa kuvuna gesi hiyo.
Washiriki wakubwa walikuwa ni pamoja na kampuni ya kimataifa ya BG Group ya Uingereza, Statoil ya Norway, Shell ya Uholanzi, Total ya Ufaransa na Exxon Mobil Corp ya Marekani.
Hata hivyo India ilitangaza  kampuni yake inayomilikiwa na serikali ya kutafuta na kuchimba mafuta (ONGC) kwamba nayo ingeomba leseni ya kwa ajili ya kupata vitalu ya mafuta na gesi vilivyopo Tanzania.
Tanzania kwa upande wake ilitangaza kwamba Shirika la Taifa la Mafuta Baharini la China (CNOOC) nalo limetuma maombi ya leseni kwa ajili ya kutafuta mafuta na gesi nchini Tanzania.
Balozi wa China nchini Tanzania Lu Youqing, alitangaza kuwa mashirika makubwa ya China yatatuma zabuni zao kwa ajili  ya kupata vitalu  vya gesi na mafuta nchini Tanzania na kuongeza kuwa Beijing  inaiangalia hali ya baadaye ya mauzo ya gesi ya Tanzania nje.
“Kwa kuwa Tanzania na China ni marafiki wakubwa, China ni lazima kwanza ifungue soko la bidhaa za Tanzania zikiwemo bidhaa za mafuta na gesi,” Youqing aliwaambia waandishi wa habari.
Aliongeza, “Tunazishawishi kampuni kubwa na zinazoongoza kwa mafuta na gesi  kuja kwa ajili ya zabuni hiyo…Zitashiriki kwenye zabuni za mafuta na gesi na pia zitakubaliana na kanuni na sheria za Tanzania.”
Kwa mujibu wa makadirio ya serikali Tanzania ina zaidi ya futi za ujazo trilioni 40 za hifadhi ya gesi asilia  na kiwango hicho kinaweza kuongezeka mara tano ndani ya kipindi kifupi kijacho kama uchimbaji wa awali utaonesha kuwa na mafanikio.
Wakati huo huo ulikuwepo mjadala wa ndani  ulioendeshwa na Mfuko wa Sekta Binafsi  ambao umekuwa unataka kuhakikisha kuwa Watanzania wanashirikishwa na hawatengwi kwenye shughuli za mafuta na gesi na ulipamba moto na hadi mwafaka wa kushiriki kwenye uvunaji wa rasilimali hiyo ulipopatikana.
Hiyo ilikuwa ni gesi lakini baadaye  likaibuka suala la makinikia  ambalo lilifumbu macho jinsi ambavyo nchi tajiri zimekuwa zikimufaika na madini kutoka  nchini na mengi yakiwa yanasafirishwa  nje bila kuwepo ulipaji wa kodi.
Pamoja na ukwepaji huo wa kodi ikaonekana pia kwamba mikataba mibovu ilikuwa imeingiwa na hivyo kuifanya  serikali kupata hasara kubwa.
Taswira iliyotokeza ni kwmaba ulikuwepo ufujaji mkubwa wa rasilimali hizo hususani katika suala la mapato ya serikali. Ufujaji huo ndio vimelea vya ugonjwa wa kidachi.
Hali inakuwa hivyo kwa sababu mara nyingi watendaji  wa nchi zilizojaliwa rasilimali kama hizo wamekuwa wanakengeuka kutokana na fedha lukuki zinazoingia bila ya daftari.
Hapo ndipo wanajamii hujikuta wakiwa hawanufaiki na rasilimali na utajiri ama uwe mpya au ambao umekuwepo.
Muhimu ni ugawaji wa mapato yanayotokana na mauzo ya rasilimali, yawekwe wazi kabisa, ni kiasi gani cha mapato, serikali inaweza kutumia na kwa ajili gani.
Kwa mfano inaweza kuwepo sera ya mapato yanayotokana na rasilimali  yanawekezwa katika sekta za uchumi na katika maeneo yaliyopewa kipaumbele. Kwa kufanya hivyo kutauepusha uchumi wa nchi kunasa katika mtego wa kuitegemea sana sekta moja na kuzisahau sekta nyingine za uchumi.
Mfano sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania ni lazima iendelezwe. Kinyume na hali hiyo ni dhahiri kutakuwa na njama za kifisadi na kushamirisha kimelea cha Ugonjwa Kidachi.
Katika mazingira hayo ili kuepuka Ugonjwa wa Kidachi tiba yake ni wapanga sera ambao wanatakiwa kuangalia iwapo utajiri mpya unaogunduliwa ni wa muda mfupi au ni wa kudumu.
Katika nchi ambazo zinatarajia rasilimali mpya kumalizika kwa haraka, mitiririko ya misaada huwa ya muda  na faida inayotokana na biashara huwa ya mpito wafanya biashara wanatakiwa kulinda sekta nyingine zitakazokuwa taabani kwa kutumia fedha za nje.
Lakini zinakuwepo changamoto za kuhakikisha kwamba hifadhi itakayokuwapo haitaingia kwenye kushuka thamani na kwamba utajiri wa ziada  unaokuwepo nchini unatumika ipasavyo na kusimamiwa kwa uwazi kupitia vyombo husika mfano benki kuu au mifuko ya udhamini.
Katika nchi ambazo ugunduzi wa utajiri kama huo unaelekea kuwa ni wa kudumu wapanga sera wanahitaji kusimamia mabadiliko ya kimuundo ambayo huwa hayaepukiki ndani ya uchumi  ili kuhakikisha  uchumi unakuwa imara.
Wanaweza kuchukua hatua kwa kuboresha ufanisi kwenye sekta ya bidhaa zisizo za biashara  ikiwezekana kupitia sekta binafsi na kuziunda upya na kuwekeza kwenye mafunzo mapya kwa mfanyakazi.
Kadhalika wanaweza kutaka kuendelea kubadilisha mauzo ya nje ili  kupunguza utegemezi  kwenye sekta inayokua kwa kuifanya isidhurike na mitikisiko ya nje kama vile kushuka kwa  bei ya bidhaa.
Ukiwepo utendaji makini katika kusimamia utajiri wa nchi au kubadilisha mkondo wa uchumi  ili kuendana na mazingira mapya na hivyo utajiri huo kutumika kwa busara bila shaka itakuwa ni thibitisho ya kile  alichokisema Cervantes.
CHANZO: TANZANITE 

Comments